Nehemiah 5

Nehemia Anawasaidia Maskini

1 Wakati huu watu na wake zao wakalia kilio kikuu dhidi ya ndugu zao Wayahudi.

2 Baadhi yao walikuwa wakisema, “Sisi na wana wetu na binti zetu tu wengi, ili tuweze kula na kuishi, ni lazima tupate nafaka.”

3 Wengine walikuwa wakisema, “Tunaweka rehani mashamba yetu, mashamba ya mizabibu na nyumba zetu ili tupate nafaka wakati wa njaa.”

4 Bado kukawa na wengine waliokuwa wakisema, “Ilitubidi tukope fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa ajili ya mashamba yetu na mashamba yetu ya mizabibu.

5 Ingawa sisi ni mwili na damu moja sawa na watu wa nchi yetu, na ijapo wana wetu ni wazuri kama wana wao, bado inatupasa kuwatoa wana wetu na binti zetu kwenye utumwa. Baadhi ya binti zetu wameshakuwa watumwa tayari, lakini hatuna uwezo wa kuwakomboa, kwa sababu mashamba yetu na mashamba ya mizabibu yetu ni mali ya wengine.”

6 Niliposikia kilio chao na malalamiko haya, nilikasirika sana.

7 Nikayatafakari katika akili yangu, nikiwalaumu wakuu na maafisa. Nikawaambia, “Mnawaonea ndugu zenu kwa kuwatoza riba!” Basi nikaitisha mkutano mkubwa ili kuwashughulikia

8 na kusema: “Kulingana na uwezo wetu, tumewakomboa ndugu zetu Wayahudi waliokuwa wameuzwa kwa Mataifa. Sasa mnawauza ndugu zenu, ili wauzwe tena kwetu!” Walinyamaza kimya, kwa sababu hawakupata cho chote cha kusema.

9 Basi nikaendelea kusema, “Mnachokifanya si sawa. Je, haikuwapasa kutembea katika hofu ya Mungu wetu ili tuepukane na shutuma za adui zetu Mataifa?

10 Mimi na ndugu zangu na watu wangu tunawakopesha watu fedha na nafaka. Lakini jambo hili la kutoza riba likome!

11 Warudishieni mara moja mashamba yao, mashamba yao ya mizabibu, mashamba yao ya mizeituni na nyumba zao, pia riba yao mnayowatoza na sehemu ya fungu la mia la fedha, nafaka, divai mpya na mafuta.”

12 Wakasema, “Tutawarudishia na hatutataka kitu cho chote zaidi kutoka kwao. Tutafanya kama ulivyosema.”

Kisha nikawaita makuhani na kuwafanya wakuu na maafisa kuapa kufanya kile walichoahidi.

13 Pia nikakung’uta makunjo ya vazi langu na kusema, “Kila mtu ambaye hatatimiza ahadi hii, Mungu na amkung’ute hivi kutoka katika nyumba yake na katika mali zake. Basi mtu wa jinsi hiyo na akung’utiwe nje na aachwe bila kitu!”

Katika hili mkutano wote ukasema, “Amen” wakamtukuzaBwana. Nao watu wakafanya kama walivyokuwa wameahidi.

14 Zaidi ya hayo, kutoka mwaka wa ishirini wa Mfalme Artashasta, wakati nilipoteuliwa kuwa mtawala wao katika nchi ya Yuda, mpaka mwaka wake wa thelathini na mbili, yaani miaka kumi na miwili, mimi wala ndugu zangu hatukula chakula ambacho kwa kawaida hupewa watawala.

15 Lakini watawala wa mwanzoni, wale walionitangulia, waliwalemea watu na kuchukua kutoka kwao shekeli arobaini za fedhapamoja na chakula na mvinyo. Wasaidizi wao pia walipata nafasi ya kufaidi watu. Lakini kwa kumheshimu Mungu sikufanya hivyo.

16 Badala yake, nilijitoa kwa bidii katika kazi kwenye ukuta huu. Watu wangu wote walikutanika pale kwa ajili ya kazi, hatukujipatia shamba lo lote.

17 Zaidi ya hayo, Wayahudi 150 na maafisa walikula mezani pangu, pamoja na wale waliotujia kutoka mataifa jirani.

18 Kila siku niliandaliwa maksai mmoja, kondoo sita wazuri na kuku na mvinyo wa kila aina kwa wingi kila baada ya siku kumi. Licha ya mambo haya yote, sikudai chakula kilichokuwa fungu la mtawala, kwa sababu madai yalikuwa mazito sana kwa watu hawa.

19 Unikumbuke kwa fadhili, Ee Mungu wangu, kwa yote niliyofanya kwa ajili ya watu hawa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/NEH/5-2f6f42cbb00a68d11cc7cb243d8ff7c6.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four − 2 =