Waamuzi 6

Gideoni

1 Waisraeli wakafanya tena yaliyo maovu mbele zaBwana, naye kwa miaka sabaBwanaakawatia mikononi mwa Wamidiani.

2 Mkono wa Midiani ukawa na nguvu dhidi ya Israeli na kwa ajili ya Wamidiani, Waisraeli wakajitengenezea mahali pa kujificha milimani, kwenye mapango na ngome.

3 Kila wakati Waisraeli walipopanda mazao mashambani, Wamidiani, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki walivamia nchi yao.

4 Wakapiga kambi katika mashamba yao na kuharibu mazao ya nchi yote hadi kufikia Gaza, wala hawakuacha kiumbe cho chote kilicho hai kwa Waisraeli, iwe kondoo au ng’ombe au punda.

5 Walipanda na mifugo yao na mahema yao, mfano wa makundi ya nzige. Ilikuwa haiwezekani kuwahesabu watu na ngamia zao; wakavamia nchi ili kuiharibu.

6 Waisraeli wakafanywa kuwa maskini sana na Wamidiani, hata Israeli wakamliliaBwanakuomba msaada.

7 Waisraeli walipomliliaBwanakwa sababu ya Wamidiani,

8 Bwanaakawapelekea nabii, ambaye aliwaambia, “Hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli, asemalo: Niliwapandisha mtoke Misri, toka nchi ya utumwa.

9 Nikawanyakua kutoka mikononi mwa Wamisri na kutoka mikononi mwa watesi wenu wote. Nikawafukuza watoke mbele yenu nami nikawapa ninyi nchi yao.

10 Nikawaambia, ‘Mimi ndimiBwanaMungu wenu; msiiabudu miungu ya Waamori, ambayo mnakaa katika nchi yao!’ Lakini ninyi hamkuitii sauti yangu.”

11 Malaika waBwanaakaja akaketi chini ya mti wa mwaloni huko Ofra, ambao ulikuwa mali ya Yoashi Mwebiezeri, ambako Gideoni mwanawe alikuwa akipepeta ngano penye shinikizo la kukamulia zabibu, ili kuificha Wamidiani wasiione.

12 Malaika waBwanaalipomtokea Gideoni, akamwambia, “Bwanayu pamoja nawe, Ewe shujaa mwenye nguvu.”

13 Gideoni akajibu, “Ee Bwana wangu, kamaBwanayu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametutokea? Yako wapi basi yale matendo yake makuu baba zetu waliyotusimulia juu yake waliposema, ‘Je,Bwanahakutupandisha kutoka Misri?’ Lakini sasaBwanaametuacha na kututia katika mkono wa Midiani.”

14 Bwanaakamgeukia na kusema “Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli kutoka mikononi mwa Wamidiani. Je, si mimi ninayekutuma wewe?”

15 Gideoni akauliza, “Ee Bwana wangu, nitawezaje kuwaokoa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu kuliko zote katika Manase, nami ndiye mdogo wa wote katika jamaa yangu.”

16 Bwanaakamjibu, “Nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kana kwamba walikuwa ni mtu mmoja.”

17 Gideoni akajibu, “Kama basi nimepata kibali machoni pako, nipe ishara kuonyesha kweli kwamba ni wewe unayesema nami.

18 Tafadhali ninakuomba usiondoke hapa mpaka nitakaporudi na kukuletea sadaka yangu na kuiweka mbele yako.”

NayeBwanaakamwambia, “Nitangoja mpaka utakaporudi.”

19 Gideoni akaingia ndani ya nyumba yake na kuandaa mwana-mbuzi pamoja na kuoka mikate isiyotiwa chachu kutokana na efa mojaya unga. Akaweka nyama kwenye kikapu na mchuzi kwenye chungu, akamletea huyo malaika hapo nje chini ya mti wa mwaloni na kumpa.

20 Malaika wa Mungu akamwambia, “Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uviweke juu ya mwamba huu na umimine huo mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo.

21 Malaika waBwanaakainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika waBwanaakatoweka kutoka machoni pake.

22 Gideoni alipotambua kuwa ni malaika waBwana, akapiga kelele kwa mshangao, akasema, “Ole wangu,BwanaMwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika waBwanauso kwa uso!”

23 LakiniBwanaakamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope. Hutakufa.”

24 Hivyo Gideoni akamjengeaBwanamadhabahu mahali pale na kupaita, Yehova-Shalom. Mpaka leo ingalipo imesimama huko Ofra ya Waabiezeri.

25 Usiku ule uleBwanaakamwambia, “Mchukue ng’ombe dume wa baba yako, yaani, yule wa pili mwenye miaka saba, na ubomoe ile madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako, na ukaikate ile Ashera iliyo karibu nayo.

26 Kisha mjengeeBwanaMungu wako, madhabahu halisi, kwa taratibu zake, juu ya huu mwamba. Kwa kutumia kuni za hiyo nguzo ya Ashera uliyoikatakata, mtoe sadaka huyo dume wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa.”

27 Basi Gideoni akawachukua watumishi wake kumi na kufanya kamaBwanaalivyomwambia. Lakini kwa kuwa aliwaogopa jamaa yake na watu wa mji, akafanya haya usiku badala ya mchana.

28 Watu wa mji walipoamka asubuhi, tazama madhabahu ya Baali imebomolewa na nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwakatwa na yule ng’ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya madhabahu iliyojengwa upya!

29 Wakaulizana, “Ni nani aliyetenda mambo haya?”

Walipochunguza kwa makini, wakaambiwa, “Ni Gideoni mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda hivi.”

30 Watu wa mji wakamwambia Yoashi, “Mlete mwanao hapa. Ni lazima afe, kwa sababu amebomoa madhabahu ya Baali na kukatakata nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.”

31 Lakini Yoashi akauambia ule umati uliokuwa umezunguka ukiwa kinyume naye, “Je, ninyi mtamtetea Baali? Mnajaribu kumwokoa? Ye yote mwenye kumpigania atauawa kufikia kesho asubuhi! Kama Baali ni mungu kweli, anaweza kujitetea mwenyewe wakati mtu anapobomoa madhabahu yake.”

32 Basi siku ile wakamwita Gideoni “Yerub-Baali,” yaani, “Baali na ashindane naye,” kwa sababu alibomoa madhabahu yake.

33 Basi Wamidiani wote, Waamaleki na mataifa mengine ya mashariki wakaunganisha majeshi yao, wakavuka ng’ambo ya Yordani na kupiga kambi katika Bonde la Yezreeli.

34 Ndipo Roho waBwanaakamjia Gideoni, akapiga tarumbeta, akiwaita Waabiezeri ili wamfuate.

35 Akatuma wajumbe waende katika Manase yote, akiwataka wachukue silaha na pia katika Asheri, Zabuloni na Naftali, nao wakakwea ili kukutana nao.

36 Gideoni akamwambia Mungu, “Kama utawaokoa Waisraeli kwa mkono wangu, kama ulivyoahidi:

37 tazama, nitaweka ngozi ya kondoo kwenye kiwanja cha kupuria nafaka, na kama utakuwepo umande juu ya ngozi tu, nayo ardhi yote ikiwa kavu, ndipo nitakapojua kuwa utaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.”

38 Hivyo ndivyo ilivyotokea. Gideoni akaamka asubuhi na mapema kesho yake, akaikamua ile ngozi, umande ukatoka, maji ya kujaa bakuli.

39 Kisha Gideoni akamwambiaBwana, “Usinikasirikie. Ninaomba nifanye ombi moja lingine. Niruhusu nifanye jaribio jingine moja kwa ngozi hii. Wakati huu uifanye ngozi hii kavu na ardhi yote ifunikwe na umande.”

40 Usiku ule Mungu akafanya hivyo. Ngozi ile ilikuwa kavu, nayo ardhi yote ikafunikwa na umande.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JDG/6-2b4effce819ff9f4eabfd4b77b6bef3a.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

five × 2 =