Waebrania 3

Yesu Ni Mkuu Kuliko Mose

1 Kwa hiyo ndugu watakatifu, mnaoshiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini Yesu, mtume na Kuhani Mkuu wa ukiri wetu.

2 Alikuwa mwaminifu kwa yeye aliyemweka, kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu.

3 Yesu ameonekana anastahili heshima kubwa kuliko Mose, kama vile mjenzi wa nyumba alivyo wa heshima kubwa kuliko nyumba yenyewe.

4 Kwa kuwa kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ni mjenzi wa kila kitu.

5 Basi Mose kama mtumishi alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, akishuhudia kwa yale ambayo yangetamkwa baadaye.

6 Lakini Kristo yeye ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu, sisi ndio nyumba yake, kama tutashikamana sana na ujasiri wetu na katika tumaini tunalojivunia.

Onyo Dhidi Ya Kutokuamini

7 Kwa hiyo, kama Roho Mtakatifu asemavyo:

“Leo, kama mkiisikia sauti yake,

8 msifanye mioyo yenu migumu,

kama mlivyofanya katika uasi,

wakati ule wa kujaribiwa jangwani,

9 pale baba zenu waliponijaribu na kunipima

ingawa kwa miaka arobaini

walikuwa wameona matendo yangu.

10 Hiyo ndiyo sababu nilikikasirikia kizazi kile,

nami nikasema, ‘Siku zote mioyo yao hupotoka,

nao hawajazijua njia zangu.’

11 Hivyo nikaapa kwa hasira yangu,

‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ”

12 Ndugu zangu, angalieni, asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai.

13 Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu iitwapo Leo, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.

14 Kwa kuwa tumekuwa washiriki wa Kristo, kama tukishikamana tu kwa uthabiti na tumaini letu la kwanza hadi mwisho.

15 Kama ilivyonenwa:

“Leo, kama mtaisikia sauti yake,

msifanye mioyo yenu migumu

kama mlivyofanya wakati wa kuasi.”

16 Basi ni nani wale waliosikia lakini bado wakaasi? Je, si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Mose?

17 Lakini ni nani aliowakasirikia miaka arobaini? Je, si wale waliofanya dhambi ambao miili yao ilianguka jangwani?

18 Ni nani hao ambao Mungu aliapa kuwa kamwe hawataingia rahani mwake isipokuwa ni wale waliokataa kutii?

19 Hivyo tunaona kwamba hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/3-3c941f65ae9207abfe401f52a09facf3.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

1 × three =