Waebrania 6

Hatari Ya Kuanguka

1 Kwa hiyo, tukiachana na mafundisho yale ya awali kuhusu Kristo na tusonge mbele ili tufikie utimilifu, si kuweka tena msingi wa mafundisho ya kuzitubia kazi zisizo na uhai na imani katika Mungu, yaani,

2 mafundisho kuhusu aina za ubatizo, kuwekea watu mikono, ufufuo wa wafu na hukumu ya milele.

3 Mungu akitujalia tutafanya hivyo.

4 Kwa kuwa ni vigumu kuwarejeza tena katika toba wale ambao wakati fulani walishapata nuru, ambao walishaonja kipawa cha mbinguni, ambao wamekwisha kushiriki katika Roho Mtakatifu,

5 wale ambao wameonja uzuri wa Neno la Mungu na nguvu za wakati ujao,

6 kisha wakaanguka, kwa kuwa kwa nafsi zao wanamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili na kumdhalilisha hadharani.

7 Ardhi ile ipokeayo mvua inyeshayo juu yake mara kwa mara hutoa mazao yanayowanufaisha wale ambao kwa ajili yao yalimwa, nayo nchi hiyo hupokea baraka kutoka kwa Mungu.

8 Lakini ardhi ile ikizaa miiba na mibaruti haina thamani na iko hatarini kulaaniwa. Mwisho wake ni kuchomwa moto.

9 Ingawa tunasema hivi, ndugu zangu wapendwa, kwa upande wenu tuna hakika ya mambo mema zaidi, mambo yale yahusuyo wokovu.

10 Mungu si dhalimu, hataisahau kazi yenu na upendo ule mlioonyesha kwa ajili yake katika kuwahudumia watakatifu na kama vile mnavyoendelea kuwahudumia.

11 Nasi twataka kila mmoja wenu aonyeshe bidii iyo hiyo ili mpate kujua uhakika kamili wa lile tumaini mpaka mwisho,

12 ili msije mkawa wavivu, bali mpate kuwaiga wale ambao kwa imani na saburi hurithi zile ahadi.

Uhakika Wa Ahadi Ya Mungu

13 Mungu alipompa Abrahamu ahadi yake, kwa kuwa hakuwepo mwingine aliyekuwa mkuu kuliko yeye ambaye angeweza kuapa kwa jina lake, aliapa kwa nafsi yake,

14 akisema, “Hakika nitakubariki na kukupa wazao wengi.”

15 Naye baada ya kungoja kwa saburi, Abrahamu alipokea kile kilichoahidiwa.

16 Wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao, nacho kiapo hicho huthibitisha kile kilichosemwa na kumaliza mabishano yote.

17 Kwa njia hii, Mungu alipotaka kuonyesha kwa udhahiri zaidi kwa warithi wa ile ahadi ile asili ya kutokubadilika kwa ahadi yake, aliithitibisha kwa kiapo.

18 Mungu alifanya hivyo, ili kwa vitu viwili visivyobadilika, yaani ahadi yake na kiapo chake, ambavyo kwa hivyo Mungu hawezi kusema uongo, sisi ambao tumemkimbilia, tuwe na moyo mkuu kulishika lile tumaini lililowekwa mbele yetu.

19 Tunalo tumaini hili lililo kama nanga ya roho, lililo imara na thabiti. Tumaini hili huingia katika patakatifu palipo nyuma ya pazia,

20 mahali ambapo Yesu mtangulizi wetu aliingia kwa niaba yetu. Yeye amekuwa Kuhani Mkuu milele, kwa mfano wa Melkizedeki.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/6-9c32152f6ae0491e330bc3ac47a5d53b.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

1 × four =