Waebrania 7

Kuhani Melkizedeki

1 Kwa kuwa huyu Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na Kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana, aliyekutana na Abrahamu akirudi katika kuwashinda hao wafalme, naye Melkizedeki akambariki,

2 ambaye Abrahamu alimpa sehemu ya kumiya kila kitu. Kwanza, jina hilo Melkizedeki maana yake “mfalme wa haki”; pia “mfalme wa Salemu,” maana yake “mfalme wa amani.”

3 Hana Baba wala mama, hana ukoo, hana mwanzo wala mwisho wa siku zake, kama Mwana wa Mungu, yeye adumu kuhani milele.

4 Tazama jinsi alivyokuwa mkuu: Hata Abrahamu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara zake.

5 Basi sheria inawaagiza wana wa Lawi wale ambao hufanyika makuhani hupokea sehemu ya kumi kutoka watu, ambao ni ndugu zao, ingawa wao ni wazao wa Abrahamu.

6 Huyu Melkizedeki, ingawa hakufuatia ukoo wake kutoka kwa Lawi, lakini alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu na kumbariki yeye aliyekuwa na zile ahadi.

7 Wala hakuna shaka kwamba mdogo hubarikiwa na aliye mkuu kuliko yeye.

8 Kwa upande mmoja, sehemu ya kumi hupokelewa na wale ambao hupatikana na kufa; lakini kwa upande mwingine hupokelewa na yeye ambaye hushuhudiwa kuwa yu hai.

9 Mtu anaweza hata kusema kwamba Lawi, ambaye hupokea sehemu ya kumi, alitoa hiyo sehemu ya kumi kupitia kwa Abrahamu,

10 kwa sababu Melkizedeki alipokutana na Abrahamu, Lawi alikuwa bado katika viuno vya baba yake wa zamani.

Yesu Mfano Wa Melkizedeki

11 Kama ukamilifu ungeweza kupatikana kwa njia ya ukuhani wa Walawi (kwa kuwa katika msingi huo sheria ilitolewa kwa watu) kwa nini basi imekuwapo haja ya kuja kuhani mwingine: kwa mfano wa Melkizedeki, wala si kwa mfano wa Aroni?

12 Kwa kuwa yanapotokea mabadiliko ya ukuhani, pia lazima yawepo mabadiliko ya sheria.

13 Yeye ambaye ndiye anayesemwa katika mambo haya, alikuwa wa kabila jingine na hakuna mtu wa kabila hilo aliyekuwa amehudumu katika madhabahu.

14 Kwa maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika uzao wa Yuda, tena kuhusu kabila hilo Mose hakusema lo lote kwa habari za ukuhani.

15 Tena hayo tuliyosema yako wazi zaidi kama akitokea kuhani mwingine kama Melkizedeki,

16 yeye ambaye amefanyika kuhani si kwa misingi ya sheria kama ilivyokuwa kwa baba zake, bali kwa misingi ya uwezo wa uzima usioharibika.

17 Kwa maana imeshuhudiwa kwamba:

“Wewe ndiye kuhani milele,

kwa mfano wa Melkizedeki.”

18 Kwa upande mmoja, kubatilishwa kwa ile amri ya mwanzo isiyofaa

19 (kwa maana sheria haikufanya kitu cho chote kuwa kikamilifu), kwa upande mwingine, tumeletewa tumaini lililo bora zaidi ambalo kwalo linatuleta karibu na Mungu.

20 Nalo tumaini hilo halikutolewa pasipo kiapo! Wengine walikuwa makuhani pasipo kiapo cho chote,

21 lakini Yesu alikuwa Kuhani kwa kiapo wakati Mungu alipomwambia:

“BWANA ameapa

naye hatabadili nia yake:

‘Wewe ndiwe Kuhani milele.’ ”

22 Kwa ajili ya kiapo hiki, Yesu amekuwa mdhamini wa Agano lililo bora zaidi.

23 Basi pamekuwepo na makuhani wengi wa aina hiyo, kwa kuwa kifo kiliwazuia kuendelea na huduma yao ya ukuhani,

24 lakini kwa sababu Yesu anaishi milele, anao ukuhani wa kudumu.

25 Kwa hiyo anaweza kuwaokoa kabisa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake, kwa sababu yeye adumu daima kuomba kwa ajili yao.

26 Kwa kuwa ilitupasa tuwe na Kuhani Mkuu wa namna hii, yaani, aliye mtakatifu, asiye na lawama, asiye na dosari, aliyetengwa na wenye dhambi na kuinuliwa juu ya mbingu.

27 Yeye hahitaji kutoa dhabihu siku kwa siku kwa ajili ya dhambi, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu kama wale makuhani wakuu wengine. Yeye alitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zao mara moja tu, alipojitoa mwenyewe.

28 Kwa kuwa sheria huwaweka makuhani wakuu watu ambao ni dhaifu, lakini lile neno la kiapo, lililokuja baada ya sheria, lilimweka Mwana, ambaye amefanywa kuwa mkamilifu milele.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/7-f144e85acd4bddbb9e7842805e3327e0.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

15 + two =