Waebrania 8

Kuhani Mkuu Wa Agano Jipya

1 Basi jambo tunalotaka kulisema ni hili: Tunaye Kuhani Mkuu ambaye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni,

2 yeye ahudumuye katika patakatifu, pa hema la kweli lililowekwa na Bwana, wala si mwanadamu.

3 Kila Kuhani Mkuu huwekwa ili atoe sadaka na dhabihu. Vivyo hivyo ilikuwa jambo muhimu kwa huyu Kuhani naye awe na kitu cha kutoa.

4 Kama angelikuwa duniani, hangelikuwa kuhani, kwa sababu tayari wapo watu watoao sadaka kama ilivyoelekezwa na sheria.

5 Wanahudumu katika patakatifu palipo mfano na kivuli cha mambo ya mbinguni. Hii ndiyo sababu Mose alionywa alipokaribia kujenga hema, akiambiwa: “Hakikisha kuwa unafanya kila kitu sawasawa na kile kielelezo ulichoonyeshwa kule mlimani.”

6 Lakini huduma aliyopewa Yesu ni bora zaidi kuliko yao kama vile lile Agano ambalo yeye ni mjumbe wake lilivyo bora zaidi kuliko lile la zamani, nalo limewekewa misingi juu ya ahadi zilizo bora zaidi.

7 Kwa maana kama hapakuwa na kasoro katika lile Agano la kwanza, pasingekuwa na haja ya kutafuta nafasi kwa ajili ya jingine.

8 Lakini Mungu aliona kosa kwa watu, naye akasema:

“Siku zinakuja, asema Bwana,

nitakapofanya Agano jipya

na nyumba ya Israeli

na nyumba ya Yuda.

9 Agano langu halitakuwa kama lile

nililofanya na baba zao

nilipowashika mkono

ili kuwatoa katika nchi ya Misri,

kwa kuwa hawakuendelea kuwa waaminifu katika Agano langu,

nami nikawaacha,

asema Bwana.

10 Baada ya siku zile, hili ndilo Agano nitakalofanya

na nyumba ya Israeli, asema Bwana.

Nitaweka sheria zangu katika nia zao

na kuziandika katika mioyo yao.

Nitakuwa Mungu wao,

nao watakuwa watu wangu.

11 Mtu hatamfundisha tena jirani yake,

wala mtu hatamfundisha ndugu yake akisema, ‘Mjue Bwana,’

kwa sababu wote watanijua mimi,

tangu aliye mdogo wa wote hadi aliye mkuu sana.

12 Kwa kuwa nitasamehe uovu wao,

wala sitazikumbuka dhambi zao tena!”

13 Kwa kuliita Agano hili “jipya” Mungu amefanya lile Agano la kwanza kuwa kuukuu; nacho kitu kinachoanza kuchakaa na kuwa kikuukuu kiko karibu kutoweka.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/8-da391403df16dc980a95b56a1ce4abd0.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

three × 4 =