Wakolosai 4

1 Ninyi mabwana, watendeeni watumwa wenu yaliyo haki na yanayostahili, mkitambua ya kwamba ninyi pia mnaye Bwana mbinguni.

Maagizo Zaidi

2 Dumuni sana katika maombi, mkikesha katika hayo pamoja na kushukuru.

3 Pia tuombeeni na sisi ili Mungu atufungulie mlango wa kunena, ili tupate kuitangaza siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake pia mimi nimefungwa.

4 Ombeni ili nipate kuitangaza Injili kwa udhahiri kama ipasavyo kunena.

5 Iweni na hekima jinsi mnavyoenenda mbele yao wale walio nje, mkiutumia vizuri wakati wenu.

6 Maneno yenu yawe yamejaa neema siku zote, yanayofaa, ili mjue jinsi iwapasavyo na inavyofaa kumjibu kila mtu.

Salamu Za Mwisho

7 Tikiko atawaambia habari zangu zote. Yeye ni ndugu mpendwa, mtenda kazi mwaminifu na mtumishi mwenzangu katika Bwana.

8 Nimemtuma kwenu kwa madhumuni haya ili kwamba mpate kufahamu hali yetu na pia awatie moyo.

9 Anakuja pamoja na Onesmo, ndugu yetu mpendwa na mwaminifu, ambaye ni mmoja wenu. Watawaambia mambo yote yanayotendeka hapa kwetu.

10 Aristarko aliye mfungwa pamoja nami anawasalimu, vivyo hivyo Marko, binamu yake Barnaba. (Mmeshapata maagizo yanayomhusu; akija kwenu, mpokeeni).

11 Yesu, yeye aitwaye Yusto, pia anawasalimu. Hawa peke yao, ndio Wayahudi miongoni mwa watenda kazi wenzangu kwa ajili ya Ufalme wa Mungu, nao wamekuwa faraja kwangu.

12 Epafra, ambaye ni mmoja wenu na mtumishi wa Kristo Yesu, anawasalimu. Yeye siku zote anawaombea kwa bidii kwamba msimame imara katika mapenzi yote ya Mungu mkiwa wakamilifu na thabiti.

13 Ninashuhudia kwa ajili yake kwamba anafanya kazi kwa bidii kwa ajili yenu na kwa ajili ya ndugu wa Laodikia na wale wa Hierapoli.

14 Rafiki yetu mpenzi Luka, yaani, yule tabibu, pamoja na Dema, wanawasalimu.

15 Wasalimuni ndugu wote wa Laodikia na pia Nimfa pamoja na kanisa linalokutana katika nyumba yake.

16 Baada ya barua hii kusomwa kwenu, hakikisheni kwamba inasomwa pia katika kanisa la Walaodikia. Nanyi pia msome barua inayotoka Laodikia.

17 Mwambieni Arkipo hivi: “Hakikisha kuwa unakamilisha ile huduma uliyopokea katika Bwana.”

18 Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe. Kumbukeni minyororo yangu. Neema iwe nanyi. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/COL/4-33abcd4fb0623743df664f1b62a3862c.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

3 × five =