Warumi 10

1 Ndugu zangu, shauku ya moyo wangu na maombi yangu kwa Mungu ni kwa ajili ya Waisraeli, kwamba waokolewe.

2 Kwa maana ninaweza nikashuhudia wazi kwamba wao wanajuhudi kubwa kwa ajili ya Mungu, lakini juhudi yao haina maarifa.

3 Kwa kuwa hawakuijua haki itokayo kwa Mungu, wakatafuta kuweka haki yao wenyewe, hawakujitia chini ya haki ya Mungu.

4 Kwa maana Kristo ni ukomo wa sheria ili kuwe na haki kwa kila mtu aaminiye.

Wokovu Ni Kwa Ajili Ya Wote

5 Mose anaandika kuhusu haki ile itokanayo na sheria, kwamba, “Mtu atendaye mambo hayo ataishi kwa hayo.”

6 Lakini ile haki itokanayo na imani husema hivi: “Usiseme moyoni mwako, ‘Ni nani atakayepanda mbinguni?’ ” (yaani ili kumleta Kristo chini)

7 “au ‘Ni nani atashuka kwenda kuzimu?’ ” (yaani ili kumleta Kristo kutoka kwa wafu.)

8 Lakini andiko lasemaje? “Lile neno li karibu nawe, li kinywani mwako na moyoni mwako,” yaani, ni lile neno la imani tunalolihubiri.

9 Kwa sababu kama ukikiri kwa kinywa chako kwamba “Yesu ni Bwana,” na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka.

10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini na hivyo kuhesabiwa haki, tena kwa kinywa mtu hukiri na hivyo kupata wokovu.

11 Kama yasemavyo Maandiko, “Ye yote amwaminiye hatatahayarika.”

12 Kwa maana hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani, yeye ni Bwana wa wote, mwenye utajiri kwa wote wamwitao.

13 Kwa maana, “Kila mtu atakayeliitia Jina la Bwana, ataokoka.”

14 Lakini watamwitaje yeye ambaye hawajamwamini? Nao watawezaje kumwamini yeye ambaye hawajamsikia? Tena watamsikiaje bila mtu kuwahubiria?

15 Nao watahubirije wasipopelekwa? Kama ilivyaoandikwa, “Ni mizuri mno miguu ya hao wanaohubiri Injili ya amani na kuleta habari ya mema!”

16 Lakini si wote waliotii Habari Njema. Kwa maana Isaya asema, “Bwana, ni nani aliyeamini ujumbe wetu?”

17 Basi, imani chanzo chake ni kusikia na kusikia huja kwa neno la Kristo.

18 Lakini nauliza, Je, wao hawakusikia? Naam, wamesikia, kwa maana:

“Sauti yao imeenea duniani kote,

nayo maneno yao yamefika

hadi miisho ya ulimwengu.”

19 Nami nauliza tena: Je, Waisraeli hawakuelewa? Kwanza, Mose asema,

“Nitawafanya mwe na wivu kwa watu wale

ambao si taifa.

Nitawakasirisha kwa taifa la watu

wasio na ufahamu.”

20 Naye Isaya kwa ujasiri mwingi anasema,

“Watu wale waliokuwa hawanitafuti, wamenipata;

nimejidhihirisha kwa watu

wale waliokuwa hawaniulizii.”

21 Lakini kuhusu Israeli anasema,

“Mchana kutwa nimewanyoshea

watu wakaidi na wasiotii mikono yangu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/10-0864d8898873b398cc4cf456076702ae.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

nineteen + 18 =