Warumi 9

Kuteuliwa Kwa Israeli Na Mungu

1 Ninasema kweli katika Kristo, wala sisemi uongo, dhamiri yangu inanishuhudia katika Roho Mtakatifu.

2 Nina huzuni kuu na uchungu usiokoma moyoni mwangu.

3 Kwa maana ningetamani hata mimi nilaaniwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu hasa, wale walio wa kabila langu kwa jinsi ya mwili,

4 yaani, watu wa Israeli, ambao ndio wenye kule kufanywa wana, ule utukufu wa Mungu, yale maagano, kule kupokea sheria, ibada ya kwenye Hekalu na zile ahadi.

5 Wao ni wa uzao wa mababa wakuu wa kwanza, ambao kutoka kwao Kristo alikuja kwa jinsi ya mwili kama mwanadamu, yeye ambaye ni Mungu aliye juu ya vyote, mwenye kuhimidiwa milele! Amen.

6 Si kwamba Neno la Mungu limeshindwa. Kwa maana si kila Mwisraeli ambaye ni wa uzao utokanao na Israeli ni Mwisraeli halisi.

7 Wala si tu kwamba kwa sababu wamezaliwa na wazao wa Abrahamu ni watoto wake, lakini ahadi ya Mungu kwa Abrahamu ilikuwa: “Watoto wako watahesabiwa katika uzao wa Isaki.”

8 Hii ina maana kwamba, si watoto waliozaliwa kimwili walio watoto wa Mungu, bali ni watoto wa ahadi wanaohesabiwa kuwa uzao wa Abrahamu.

9 Kwa maana ahadi yenyewe ilisema, “Nitakurudia tena wakati kama huu, naye Sara atapata mtoto wa kiume.”

10 Wala si hivyo tu, bali pia watoto aliowazaa Rebeka walikuwa na baba huyo huyo mmoja, yaani, baba yetu Isaki.

11 Lakini, hata kabla hao mapacha hawajazaliwa au kufanya jambo lo lote jema au baya, ili kwamba kusudi la Mungu la kuchagua lipate kusimama,

12 si kwa matendo, bali kwa yeye mwenye kuita, Rebeka aliambiwa, “Mkubwa atamtumikia mdogo.”

13 Kama vile ilivyoandikwa, “Nimempenda Yakobo, lakini Esau nimemchukia.”

Mungu Hana Upendeleo

14 Tuseme nini basi? Je, Mungu ni dhalimu? La, hasha!

15 Kwa maana Mungu alimwambia Mose,

“Nitamrehemu yeye nimrehemuye,

nami nitamhurumia yeye nimhurumiaye.”

16 Kwa hiyo haitegemei kutaka kwa mwanadamu au jitihada, bali hutegemea huruma ya Mungu.

17 Kwa maana Maandiko yamwambia Farao, “Nilikuinua kwa kusudi hili, ili kwamba nipate kuonyesha uweza wangu juu yako na ili Jina langu lipate kutangazwa duniani pote.”

18 Kwa hiyo basi, Mungu humhurumia yeye atakaye kumhurumia na humfanya mgumu yeye atakaye kumfanya mgumu.

19 Basi mtaniambia, “Kama ni hivyo, kwa nini basi bado Mungu anatulaumu? Kwa maana ni nani awezaye kupinga mapenzi yake?”

20 Lakini, Ewe mwanadamu, u nani wewe ushindane na Mungu? “Je, kilichoumbwa chaweza kumwambia yeye aliyekiumba, ‘Kwa nini umeniumba hivi?’ ”

21 Je, mfinyanzi hana haki ya kufinyanga kutoka katika bonge moja vyombo vya udongo, vingine kwa matumizi ya heshima na vingine kwa matumizi ya kawaida?

22 Iweje basi, kama Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake na kufanya uweza wake ujulikane, amevumilia kwa uvumilivu mwingi vile vyombo vya ghadhabu vilivyoandaliwa kwa uharibifu?

23 Iweje basi, kama yeye alitenda hivi ili kufanya wingi wa utukufu wake ujulikane kwa vile vyombo vya rehema yake, alivyotangulia kuvitengeneza kwa ajili ya utukufu wake,

24 yaani pamoja na sisi, ambao pia alituita, si kutoka kwa Wayahudi peke yao, bali pia kutoka kwa watu Mataifa?

Yote Yalitabiriwa Katika Maandiko

25 Kama vile Mungu asemavyo katika Hosea:

“Nitawaita ‘watu wangu’

wale ambao si watu wangu;

nami nitamwita ‘mpenzi wangu’

yeye ambaye si mpenzi wangu,”

26 tena,

“Itakuwa hasa mahali pale walipoambiwa,

‘Ninyi si watu wangu,’

wao wataitwa ‘wana wa Mungu aliye hai.’ ”

27 Isaya anapiga kelele kuhusu Israeli:

“Ingawa idadi ya wana wa Israeli ni wengi kama mchanga

ulioko pwani ya bahari,

ni mabaki yao tu watakaookolewa.

28 Kwa kuwa Bwana ataitekeleza

hukumu yake duniani kwa haraka

na kwa ukamilifu.”

29 Ni kama vile alivyotabiri Isaya akisema:

# “Kama Bwana Mwenye Nguvu Zote

asingetuachia uzao,

tungalikuwa kama Sodoma,

tungalikuwa kama Gomora.”

Kutokuamini Kwa Israeli

30 Kwa hiyo tuseme nini basi? Kwamba watu Mataifa ambao hawakutafuta haki, wamepata haki ile iliyo kwa njia ya imani.

31 Lakini Israeli, ambao walijitahidi kupata haki kwa njia ya sheria, hawakuipata.

32 Kwa nini? Kwa sababu hawakuitafuta kwa njia ya imani bali kwa njia ya matendo. Wakajikwaa kwenye lile “jiwe la kukwaza.”

33 Kama ilivyoandikwa:

“Tazama naweka katika Sayuni jiwe la kukwaza

na mwamba wa kuwaangusha,

ye yote atakayemwamini

hataaibika kamwe.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ROM/9-2ac804dd6f26958769ce19bdf4b29bcb.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

1 × five =