Yakobo 5

Onyo Kwa Matajiri

1 Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia.

2 Utajiri wenu umeoza na mavazi yenu yameliwa na nondo.

3 Dhahabu yenu na fedha yenu vimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho.

4 Angalieni! Ule ujira wa vibarua waliolima mashamba yenu mliouzuia kwa hila unapiga kelele dhidi yenu na vilio vya wavunaji vimefika masikioni mwa Bwana Mwenye Nguvu Zote.

5 Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe, mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa.

6 Mmewahukumu na kuwaua watu wenye haki, ambao walikuwa hawapingani nanyi.

Uvumilivu Katika Mateso

7 Kwa hiyo, ndugu zangu, vumilieni hadi kuja kwake Bwana. Angalieni jinsi mkulima angojavyo ardhi itoe mavuno yake yaliyo ya thamani na jinsi anavyovumilia kwa ajili ya kupata mvua za kwanza na za mwisho.

8 Ninyi nanyi vumilieni tena simameni imara, kwa sababu kuja kwa Bwana kumekaribia.

9 Ndugu zangu, msinung’unikiane msije mkahukumiwa. Hakimu amesimama mlangoni!

10 Ndugu zangu, waangalieni manabii walionena kwa Jina la Bwana, ili kuwa mfano wa uvumilivu katika kukabiliana na mateso.

11 Kama mnavyojua, tunawahesabu kuwa wamebarikiwa wale waliovumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu na mmeona kile ambacho hatimaye Bwana alimtendea. Bwana ni mwingi wa huruma naye amejaa rehema.

12 Zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, ama kwa mbingu, au kwa dunia au kwa kitu kingine cho chote. “Ndiyo” yenu na iwe ndiyo, na “Hapana” yenu iwe hapana, la sivyo mtahukumiwa.

Maombi Ya Imani

13 Je, mtu ye yote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna ye yote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu.

14 Je, kuna ye yote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kanisa wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana.

15 Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana atamwinua na kama ametenda dhambi, atasamehewa.

16 Kwa hiyo ungamianeni makosa yenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.

17 Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi. Akaomba kwa bidii kwamba mvua isinyeshe nayo haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita.

18 Kisha akaomba tena, mbingu zikatoa mvua nayo ardhi ikatoa mazao yake.

19 Ndugu zangu, ye yote miongoni mwenu akipotoka na kuicha kweli, naye akarejezwa na mtu mwingine,

20 hamna budi kujua kwamba ye yote amrejezaye mwenye dhambi kutoka katika upotovu wake, ataiokoa roho ya huyo mwenye dhambi kutoka katika mauti na kusitiri wingi wa dhambi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JAS/5-7b59a2129497051ac52f034f89beaa71.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

five + 9 =