Yeremia 25

Miaka Sabini Ya Kuwa Mateka

1 Neno likamjia Yeremia kuhusu watu wote wa Yuda katika mwaka wa nne wa kutawala kwake Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, ambao ulikuwa mwaka wa kwanza wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babeli.

2 Hivyo nabii Yeremia akawaambia watu wote wa Yuda na wale wote waishio Yerusalemu:

3 Kwa miaka ishirini na mitatu, kuanzia mwaka wa kumi na tatu wa utawala wa Yosia mwana wa Amoni mfalme wa Yuda mpaka siku hii ya leo, neno laBwanalimekuwa likinijia nami nimesema nanyi mara kwa mara lakini hamkusikiliza.

4 IngawaBwanaamewatuma watumishi wake wote hao manabii kwenu mara kwa mara, hamkusikiliza wala hamkujali.

5 Wakasema, “Geukeni sasa, kila mmoja wenu kutoka katika njia yake mbaya na matendo yake maovu ndipo mtaweza kukaa katika nchi ambayoBwanaaliwapa ninyi na baba zenu milele.

6 Msiifuate miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu, msinikasirishe kwa vitu ambavyo mmevitengeneza kwa mikono yenu.”

7 “Lakini ninyi hamkunisikiliza mimi, tena mkanikasirisha kwa vitu mlivyovitengeneza kwa mikono yenu, nanyi mmejiletea madhara juu yenu wenyewe,” asemaBwana.

8 Kwa hiyoBwanaMwenye Nguvu Zote asema hivi: “Kwa sababu hamkuyasikiliza maneno yangu,

9 nitayaita mataifa yote ya kaskazini na mtumishi wangu Nebukadneza mfalme wa Babeli,” asemaBwana, “nitawaleta waishambulie nchi hii na wakazi wake wote na dhidi ya mataifa yote yanayowazunguka. Nitawaangamiza kabisa na kuwafanya kitu cha kuchukiwa na kudharauliwa na kuwa magofu daima.

10 Nitawaondolea sauti ya shangwe na furaha, sauti ya bibi na bwana arusi, sauti ya mawe ya kusagia na mwanga wa taa.

11 Nchi hii yote itakuwa ukiwa na isiyofaa kitu, nayo mataifa haya yatamtumikia mfalme wa Babeli kwa miaka sabini.”

12 “Lakini miaka sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli na taifa lake na nchi ya Wakaldayo kwa ajili ya hatia yao,” asemaBwana. “Nitaifanya kuwa ukiwa milele.

13 Nitaleta juu ya nchi hiyo mambo yote niliyosema dhidi yake, yote yaliyoandikwa katika kitabu hiki na kutolewa unabii na Yeremia dhidi ya mataifa yote.

14 Wao wenyewe watakuwa watumwa wa mataifa mengi na wafalme wakuu, nitawalipizia sawa sawa na matendo yao na kazi ya mikono yao.”

Kikombe Cha Ghadhabu Ya Mungu

15 Hili ndiloBwana, Mungu wa Israeli, aliloniambia: “Chukua kutoka mkononi mwangu kikombe hiki kilichojaa mvinyo ya ghadhabu yangu na kuyanywesha mataifa yote ambayo ninakutuma kwao.

16 Watakapoinywa watapepesuka na kukasirika sana kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka katikati yao.”

17 Hivyo nikakichukua kikombe kutoka mkononi mwaBwanana kuyafanya mataifa yote aliyonituma kwao kukinywa:

18 Yaani Yerusalemu na miji ya Yuda, wafalme wake na maafisa wake, kuwafanya magofu na kuwa kitu cha kuchukiza, cha dhihaka na laana, kama walivyo leo,

19 Farao mfalme wa Misri, watumishi wake, maafisa wake na watu wake wote,

20 pia wageni wote walioko huko, wafalme wote wa nchi ya Uzi, wafalme wote wa Wafilisti (wale wa Ashkeloni, Gaza, Ekroni na watu walioachwa huko Ashdodi),

21 Edomu, Moabu na Amoni,

22 wafalme wote wa Tiro na Sidoni, wafalme wa nchi za pwani ng’ambo ya bahari,

23 Dedani, Tema, Buzi na wote walio maeneo ya mbali,

24 wafalme wote wa Arabuni na wafalme wote wa watu wageni wanaoishi katika jangwa,

25 wafalme wote wa Zimri, Elamu na Umedi,

26 wafalme wote wa pande za kaskazini, wa karibu na wa mbali mmoja baada ya mwingine, yaani, falme zote juu ya uso wa dunia. Baada ya hao wote, mfalme wa Sheshakiatakunywa pia.

27 “Kisha uwaambie, ‘Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli asemalo: Kunyweni, mlewe na mtapike, angukeni wala msiinuke tena kwa sababu ya upanga nitakaotuma miongoni mwenu.’

28 Lakini kama wakikataa kupokea kikombe kutoka mikononi mwako na kunywa, waambie, ‘Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote: Ni lazima mnywe!

29 Tazama, nimeanza kuleta maafa juu ya mji ulio na Jina langu, je, kweli ninyi mtaepuka kuadhibiwa? Hamwezi kuepuka kuadhibiwa kwa maana nitaleta vita juu ya wote waishio duniani, asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.’

30 “Basi sasa toa unabii kwa maneno haya yote dhidi yao, uwaambie:

“ ‘Bwanaatanguruma kutoka juu;

atatoa sauti ya ngurumo

kutoka makao yake matakatifu

na kunguruma kwa nguvu sana

dhidi ya nchi yake.

Atapiga kelele kama wao wakanyagao mizabibu,

atapiga kelele dhidi ya wote waishio duniani.

31 Ghasia zitasikika hadi miisho ya dunia,

kwa maanaBwanaataleta mashtaka

dhidi ya mataifa;

ataleta hukumu juu ya wanadamu wote

na kuwaua waovu wote,’ ”

asemaBwana.

32 Hili ndiloBwanaMwenye Nguvu Zote asemalo:

“Tazama! Maafa yanaenea

kutoka taifa moja hadi jingine;

tufani kubwa inainuka

kutoka miisho ya dunia.”

33 Wakati huo, hao waliouawa naBwanawatatapakaa kila mahali, kuanzia mwisho mmoja wa dunia hadi mwisho mwingine. Hawataombolezewa wala kukusanywa au kuzikwa lakini watakuwa kama mavi yaliyoenea juu ya ardhi.

34 Lieni na kuomboleza, enyi wachungaji,

mgaegae mavumbini,

ninyi viongozi wa kundi.

Kwa maana wakati wenu wa kuchinjwa umewadia;

mtaanguka na kuvunjwavunjwa

kama vyombo vizuri vya udongo.

35 Wachungaji hawatakuwa na mahali pa kukimbilia,

viongozi wa kundi hawatapata

mahali pa kutorokea.

36 Sikia kilio cha wachungaji,

maombolezo ya viongozi wa kundi,

kwa maanaBwanaanayaharibu malisho yao.

37 Makao yao ya amani yataharibiwa

kwa sababu ya hasira kali yaBwana.

38 Kama simba ataacha pango lake,

nchi yao itakuwa ukiwa

kwa sababu ya upanga wa mdhalimu

na kwa sababu ya hasira kali

yaBwanaMungu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/25-5c30d2d0c9b69be6b39f63c913312dd4.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

1 × four =