Yeremia 52

Anguko La Yerusalemu

1 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na mmoja. Jina la mama yake aliitwa Hamutali binti Yeremia, kutoka Libna.

2 Alifanya maovu machoni paBwana, kama vile alivyokuwa amefanya Yehoyakimu.

3 Ilikuwa ni kwa sababu ya hasira yaBwanakwamba haya yote yalitokea Yerusalemu na Yuda, naye mwishoni akawaondoa mbele zake.

Basi Sedekia aliasi dhidi ya mfalme wa Babeli.

4 Kwa hiyo katika mwaka wa tisa wa kutawala kwake Sedekia, katika siku ya kumi ya mwezi wa kumi, Nebukadneza mfalme wa Babeli alifanya vita dhidi ya Yerusalemu na jeshi lake lote. Wakapiga kambi nje ya mji na kuuzunguka mji pande zote.

5 Mji ulizungukwa kwa jeshi mpaka mwaka wa kumi na moja wa kutawala kwake Mfalme Sedekia.

6 Ilipowadia siku ya tisa katika mwezi wa nne njaa ilikuwa kali sana ndani ya mji kiasi kwamba hapakuwa na chakula kwa ajili ya watu.

7 Kisha ukuta wa mji ulivunjwa na jeshi lote likakimbia. Wakaondoka mjini usiku kupitia mlango ulioko kati ya kuta mbili karibu na bustani ya mfalme, ingawa Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji. Walikimbia kuelekea Araba,

8 lakini jeshi la Wakaldayo lilimfuatia Mfalme Sedekia na kumpata katika tambarare za Yeriko. Askari wake wote walitengwa naye na kutawanyika,

9 naye akakamatwa.

Alipelekwa kwa mfalme wa Babeli huko Ribla katika nchi ya Hamathi, mahali ambapo alimtangazia hukumu.

10 Huko Ribla mfalme wa Babeli aliwachinja wana wa Sedekia mbele ya macho yake, pia akawaua maafisa wote wa Yuda.

11 Kisha akayang’oa macho ya Sedekia, akamfunga kwa pingu za shaba na kumpeleka Babeli alipomweka gerezani mpaka siku ya kifo chake.

12 Mnamo siku ya kumi ya mwezi wa tano, katika mwaka wa kumi na tisa wa kutawala kwake Nebukadneza mfalme wa Babeli, Nebuzaradani jemadari wa askari walinzi wa mfalme, aliyemtumikia mfalme wa Babeli, alikuja Yerusalemu.

13 Alichoma moto Hekalu laBwana, jumba la kifalme na nyumba zote za Yerusalemu. Aliteketeza kila jengo muhimu.

14 Jeshi lote la Wakaldayo chini ya uongozi wa jemadari wa askari walinzi wa mfalme lilivunja kuta zote kuzunguka Yerusalemu.

15 Nebuzaradani jemadari wa walinzi akawachukua uhamishoni baadhi ya watu maskini sana na wale waliobaki katika mji, pamoja na mabaki ya watu wa hivi hivi na wale waliokuwa wamemwendea mfalme wa Babeli.

16 Lakini Nebuzaradani akaacha yale mabaki ya wale watu maskini sana wa nchi ili kufanya kazi katika mashamba ya mzabibu na mashamba mengine.

17 Wakaldayo walivunja nguzo za shaba, vile vibanio vinavyohamishika na ile Bahari ya Shaba ambavyo vyote vilikuwa katika Hekalu laBwana, wakachukua shaba yote na kuipeleka Babeli.

18 Walichukua pia zile sufuria, yale masepetu, ile mikasi ya kusawazishia tambi, yale mabakuli ya kunyunyizia, sahani pamoja na vyombo vyote vya shaba vilivyotumika ndani ya Hekalu.

19 Jemadari wa askari walinzi wa mfalme akachukua yale masinia, vile vyetezo, yale mabakuli ya kunyunyizia, zile sufuria, vile vinara vya taa, zile sahani na yale mabakuli yanayotumika kwa sadaka za kinywaji, vyote vile vilivyokuwa vimetengenezwa kwa dhahabu safi au fedha.

20 Shaba iliyotokana na zile nguzo mbili, ile Bahari na wale mafahali kumi na mawili wa shaba waliokuwa chini yake, pamoja na vile vibanio vinavyohamishika, ambavyo Mfalme Solomoni alikuwa ametengeneza kwa ajili ya Hekalu laBwana, vilikuwa na uzito usioweza kupimika.

21 Kila nguzo ilikuwa na urefu wa dhiraa kumi na nane kimo chake na mzunguko dhiraa kumi na mbili zikiwa na unene wa nyanda nne na zote zilikuwa wazi ndani.

22 Sehemu ya juu ya nguzo moja ilikuwa na urefu wa dhiraa tano na ilipambwa kwa wavu na makomamanga ya shaba kuizunguka kote. Nguzo nyingine, pamoja na makomamanga yake vyote vilifanana na hiyo ya kwanza.

23 Kulikuwa na makomamanga tisini na sita pembeni, jumla ya makomamanga juu ya wavu uliokuwa umezunguka yalikuwa mia moja.

24 Waliochukuliwa na jemadari wa askari walinzi ni Seraya Kuhani Mkuu, kuhani Sefania aliyefuata kwa cheo na mabawabu watatu.

25 Miongoni mwa wale watu waliokuwa wamesalia katika mji, alimchukua afisa kiongozi wa wapiganaji na washauri saba wa kifalme. Akamchukua pia mwandishi aliyekuwa afisa mkuu wa kuandika watu wa nchi na watu wake sitini waliokutwa katika mji.

26 Nebuzaradani jemadari akawachukua wote na kuwapeleka kwa mfalme wa Babeli huko Ribla.

27 Huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, mfalme akaamuru wote wanyongwe.

Hivyo Yuda alitekwa, akaenda mbali na nchi yake.

28 Hii ndiyo hesabu ya watu ambao Nebukadneza aliwachukua kwenda uhamishoni:

katika mwaka wa saba Wayahudi 3,023;

29 katika mwaka wa kumi na nane wa kutawala kwake Nebukadneza,

watu 832 kutoka Yerusalemu;

30 katika mwaka wa ishirini na tatu wa kutawala kwake,

Wayahudi 745 walichukuliwa kwenda uhamishoni na Nebuzaradani, jemadari wa askari walinzi wa mfalme.

Jumla ya watu wote walikuwa 4,600.

Yehoyakini Anaachiwa Huru

31 Katika mwaka wa thelathini na saba tangu Yehoyakini mfalme wa Yuda apelekwe uhamishoni, mwaka ambao Evil-Merodakialifanyika mfalme wa Babeli, akamwacha huru Yehoyakini mfalme wa Yuda na kumfungua kutoka gerezani katika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa kumi na mbili.

32 Alizungumza naye kwa upole na kumpa kiti cha heshima kilicho juu kuliko vya wale wafalme wengine aliokuwa nao huko Babeli.

33 Hivyo Yehoyakini akayavua mavazi yake ya gerezani na siku zote za maisha yake zilizobaki alikula katika meza ya mfalme.

34 Siku kwa siku mfalme wa Babeli alimpa Yehoyakini posho wakati wote wa uhai wake, mpaka siku ya kifo chake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/52-c2b86b923a92dc454bdb791d63c04e8c.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

4 × 5 =