Isaya 1

1 Maono kuhusu Yuda na Yerusalemu ambayo Isaya mwana wa Amozi aliyaona wakati wa utawala wa Uzia, Yothamu, Ahazi na Hezekia, wafalme wa Yuda.

Taifa Asi

2 Sikieni, enyi mbingu! Sikilizeni, enyi dunia!

Kwa maanaBwanaamesema:

“Nimewalisha watoto na kuwalea,

lakini wameniasi mimi.

3 Ng’ombe anamjua bwana wake,

naye punda anajua hori la mmiliki wake,

lakini Israeli hajui,

watu wangu hawaelewi.”

4 Lo! Taifa lenye dhambi,

watu waliolemewa na uovu,

uzao wa watenda mabaya,

watoto waliozoelea upotovu!

WamemwachaBwana,

Wamemkataa kwa dharau

yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli

na kumgeuzia kisogo.

5 Kwa nini mzidi kupigwa?

Kwa nini kudumu katika uasi?

Kichwa chako chote kimejeruhiwa,

moyo wako wote ni mgonjwa.

6 Kutoka wayo wako wa mguu

hadi kwenye utosi wa kichwa chako

hakuna uzima:

ni majeraha matupu na makovu

na vidonda vitokavyo damu,

havikusafishwa au kufungwa

wala kulainishwa kwa mafuta.

7 Nchi yenu imekuwa ukiwa,

miji yenu imeteketezwa kwa moto;

nchi yenu imeachwa tupu na wageni

mbele ya macho yenu,

imeharibiwa kama vile imepinduliwa na wageni.

8 Binti Sayuni ameachwa kama kipenu

katika shamba la mizabibu,

kama kibanda katika shamba la matikitimaji,

kama mji uliohusuriwa.

9 KamaBwanaMungu Mwenye Nguvu Zote

asingelituachia walionusurika,

tungelikuwa kama Sodoma,

tungelifanana na Gomora.

10 Sikieni neno laBwana,

ninyi watawala wa Sodoma;

sikilizeni sheria ya Mungu wetu,

enyi watu wa Gomora!

11 Bwanaanasema, “Wingi wa sadaka zenu,

ni kitu gani kwangu?

Ninazo sadaka za kuteketezwa nyingi kupita kiasi,

za kondoo waume

na mafuta ya wanyama walionona,

Sipendezwi na damu za mafahali

wala za wana-kondoo na mbuzi.

12 Mnapokuja kujihudhurisha mbele zangu,

ni nani aliyewataka ninyi mfanye hivyo,

huku kuzikanyaga nyua zangu?

13 Acheni kuniletea sadaka zisizokuwa na maana!

Uvumba wenu ni chukizo kwangu.

Miandamo ya Mwezi, Sabato na makusanyiko ya ibada:

siwezi kuvumilia makusanyiko yenu maovu.

14 Sikukuu zenu za Miandamo ya Mwezi

na sikukuu zenu zilizoamriwa

moyo wangu unazichukia.

Zimekuwa mzigo kwangu,

nimechoka kuzivumilia.

15 Mnaponyosha mikono yenu katika kuomba,

nitaficha macho yangu nisiwaone;

hata mkiomba maombi mengi

sitasikiliza.

Mikono yenu imejaa damu;

16 jiosheni na mkajitakase.

Yaondoeni matendo yenu maovu

mbele zangu!

Acheni kutenda mabaya,

17 jifunzeni kutenda mema!

Tafuteni haki,

watieni moyo walioonewa.

Teteeni shauri la yatima,

wateteeni wajane.

18 “Njoni basi na tuhojiane,”

asemaBwana.

“Ingawa dhambi zenu ni kama rangi nyekundu,

zitakuwa nyeupe kama theluji;

ingawa ni nyekundu sana kama damu,

zitakuwa nyeupe kama sufu.

19 Kama mkikubali na kutii,

mtakula mema ya nchi,

20 lakini kama mkikataa na kuasi,

mtaangamizwa kwa upanga.”

Kwa kuwa kinywa chaBwanakimenena.

21 Tazama jinsi ambavyo mji uliokuwa mwaminifu

umekuwa kahaba!

Mwanzoni ulikuwa umejaa unyofu,

haki ilikuwa inakaa ndani yake,

lakini sasa ni wauaji!

22 Fedha yenu imekuwa takataka,

divai yenu nzuri imechanganywa na maji.

23 Watawala wenu ni waasi,

rafiki wa wevi,

wote wanapenda rushwa

na kukimbilia hongo.

Hawatetei yatima,

shauri la mjane haliletwi mbele yao likasikilizwa.

24 Kwa hiyo Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

Mwenye Nguvu wa Israeli, asema hivi:

“Lo, nitapata faraja kutoka kwa adui zangu

na kujilipizia kisasi juu ya watesi wangu.

25 Nitauelekeza mkono wangu dhidi yenu,

nitawasafisha takataka yenu yote

na kuwaondolea unajisi wenu wote.

26 Nitawarudishieni waamuzi wenu

kama ilivyokuwa siku za zamani,

nao washauri wenu kama ilivyokuwa mwanzoni.

Baadaye utaitwa,

Mji wa Haki,

Mji Mwaminifu.”

27 Sayuni itakombolewa kwa haki,

wale waliomo ndani yake waliotubu kwa uaminifu.

28 Lakini waasi na wenye dhambi wote wataangamizwa,

nao wanaomwachaBwanawataangamia.

29 “Mtaaibika kwa sababu ya hiyo mialoni mliyoipenda

mkaifanya mahali pa kuabudia sanamu,

mtafadhaika kwa sababu ya bustani

mlizozichagua.

30 Mtakuwa kama mwaloni wenye majani yanayonyauka,

kama bustani isiyokuwa na maji.

31 Mtu mwenye nguvu atatoweka

kama majani makavu yawakayo moto

na kazi yake kama cheche ya moto;

vyote vitaungua pamoja,

wala hakuna wa kuuzima huo moto.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/1-7f652a74bdea1a198249732ecbbf8fbe.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four × five =