Yoeli 1

1 Neno laBwanaambalo lilimjia Yoeli mwana wa Pethueli.

Uvamizi Wa Nzige

2 Sikilizeni hili, enyi wazee;

sikilizeni, ninyi nyote mnaoishi katika nchi.

Je, jambo kama hili lilishawahi kutokea

katika siku zenu au katika siku za babu zenu?

3 Waelezeni watoto wenu,

na watoto wenu wawaambie watoto wao,

na watoto wao kwa kizazi kitakachofuata.

4 Kilichosazwa na kundi la tunutu

nzige wakubwa wamekula,

kilichosazwa na nzige wakubwa

parare wamekula,

kilichosazwa na parare

madumadu wamekula.

5 Amkeni, enyi walevi, mlie!

Pigeni yowe enyi wanywaji wote wa mvinyo,

pigeni yowe kwa sababu ya mvinyo mpya,

kwa kuwa mmenyang’anywa

kutoka midomoni mwenu.

6 Taifa limevamia nchi yangu,

lenye nguvu tena lisilo na idadi;

lina meno ya simba,

magego ya simba jike.

7 Limeharibu mizabibu yangu

na kuangamiza mitini yangu.

Limebambua magome yake

na kuyatupilia mbali,

likayaacha matawi yake yakiwa meupe.

8 Omboleza kama bikira aliyevaa nguo ya gunia

anayehuzunika kwa ajili ya mume wa ujana wake.

9 Sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji

zimekatiliwa mbali kutoka nyumba yaBwana.

Makuhani wanaomboleza,

wale wanaohudumu mbele zaBwana.

10 Mashamba yameharibiwa,

ardhi imekauka;

nafaka imeharibiwa,

mvinyo mpya umekauka,

mafuta yamekoma.

11 Kateni tamaa, enyi wakulima,

lieni, enyi mlimao mizabibu;

huzunikeni kwa ajili ya ngano na shayiri,

kwa sababu mavuno ya shambani yameharibiwa.

12 Mzabibu umekauka

na mtini umenyauka;

mkomamanga, mtende na mtofaa,

miti yote ya shambani, imekauka.

Hakika furaha yote ya mwanadamu

imeondoka.

Wito Wa Toba

13 Vaeni nguo ya gunia, Enyi makuhani, muomboleze;

pigeni yowe, enyi mnaohudumu madhabahuni.

Njoni, vaeni nguo ya gunia usiku kucha,

enyi mnaohudumu mbele za Mungu wangu;

kwa kuwa sadaka za nafaka na sadaka za kinywaji

zimezuiliwa kufika katika nyumba ya Mungu wenu.

14 Tangazeni saumu takatifu;

liiteni kusanyiko takatifu.

Iteni wazee

na wote waishio katika nchi

waende katika nyumba yaBwanaMungu wenu,

wakamlilieBwana.

15 Ole kwa siku hiyo!

Kwa kuwa siku yaBwanaiko karibu;

itakuja kama uharibifu

# kutoka kwa Mwenyezi.

16 Je, chakula hakikukatiliwa mbali

mbele ya macho yetu:

furaha na shangwe

kutoka katika nyumba ya Mungu wetu?

17 Mbegu zinakauka

chini ya mabonge ya udongo.

Ghala zimeachwa katika uharibifu,

ghala za nafaka zimebomolewa,

kwa maana hakuna nafaka.

18 Jinsi gani ng’ombe wanavyolia!

Makundi ya mifugo yanahangaika

kwa sababu hawana malisho;

hata makundi ya kondoo yanateseka.

19 Kwako, EeBwana, naita,

kwa kuwa moto umeteketeza

malisho ya mbugani

na miali ya moto imeunguza

miti yote ya shambani.

20 Hata wanyama wa porini wanakuonea shauku;

vijito vya maji vimekauka,

na moto umeteketeza

malisho yote ya mbugani.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOL/1-c143eaab6d0d73e6f8727b9d2499d297.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

20 − 2 =