Mwanzo 32

Yakobo Ajiandaa Kukutana Na Esau

1 Yakobo pia akaondoka akaenda zake, malaika wa Mungu wakakutana naye.

2 Yakobo alipowaona, akasema, “Hii ni kambi ya Mungu!” Kwa hiyo akapaita mahali pale Mahanaimu.

3 Yakobo akatuma wajumbe kumtangulia kwa Esau ndugu yake huko Seiri, katika nchi ya Edomu.

4 Akawaagiza akisema: “Hili ndilo mtakalomwambia bwana wangu Esau: ‘Mtumishi wako Yakobo anasema, nimekuwa nikiishi pamoja na Labani na nimekuwako huko mpaka sasa.

5 Ninao ng’ombe na punda, kondoo na mbuzi, watumishi wa kiume na wa kike. Sasa ninatuma ujumbe huu kwa bwana wangu, ili nipate kibali machoni pako.’ ”

6 Wajumbe waliporudi kwa Yakobo, wakamwambia, “Tulikwenda kuonana na ndugu yako Esau, naye sasa anakuja kukulaki akifuatana na wanaume 400.”

7 Kwa hofu kuu na huzuni, Yakobo akagawanya watu aliokuwa nao katika makundi mawili, pia akagawanya makundi ya kondoo na mbuzi, na vile vile ng’ombe na ngamia.

8 Yakobo alifikiri, “Kama Esau akija na kushambulia kundi moja, kundi lililobaki litaweza likanusurika.”

9 Ndipo Yakobo akaomba, “Ee Mungu wa baba yangu Abrahamu, Mungu wa baba yangu Isaki, EeBwana, ambaye uliniambia, ‘Rudi katika nchi yako na jamaa yako, nami nitakufanya ustawi,’

10 mimi sistahili fadhili na uaminifu wako wote ulionitendea mimi mtumishi wako. Nilikuwa na fimbo tu mkononi mwangu nilipovuka mto huu wa Yordani, lakini sasa ninayo makundi mawili.

11 Nakuomba, uniokoe na mkono wa ndugu yangu Esau, kwa maana ninaogopa kuwa atakuja kunishambulia, pia mama pamoja na watoto wao.

12 Lakini umeshasema, ‘Hakika nitakufanya ustawi na kuufanya uzao wako kuwa mwingi kama mchanga wa baharini ambao hauwezi kuhesabika!’ ”

13 Akalala pale usiku ule, miongoni mwa vitu alivyokuwa navyo, akachagua zawadi kwa ajili ya Esau ndugu yake:

14 Mbuzi waume ishirini na mbuzi wake 200, kondoo waume ishirini na kondoo wake 200.

15 Ngamia wake thelathini pamoja na ndama zao, ng’ombe wake arobaini na mafahali kumi, punda wake ishirini na punda waume kumi.

16 Akaviweka chini ya uangalizi wa watumishi wake, kila kundi peke yake na kuwaambia, “Nitangulieni na kuacha nafasi kati ya makundi.”

17 Akamwagiza yule aliyetangulia kuwa, “Ndugu yangu Esau atakapokutana nawe na kukuuliza, ‘Wewe ni wa nani? Unakwenda wapi? Wanyama hawa wote mbele yako ni mali ya nani?’

18 Ndipo utakaposema, ‘Ni mali ya mtumishi wako Yakobo. Ni zawadi ambazo zimetumwa kwa bwana wangu Esau, naye anakuja nyuma yetu.’ ”

19 Akamwagiza pia yule mtumishi wa kundi la pili, la tatu na yale mengine yote yaliyofuata akiwaambia, “Mtamwambia Esau maneno hayo hayo mtakapokutana naye.

20 Hakikisheni mmesema, ‘Mtumishi wako Yakobo anakuja nyuma yetu.’ ” Kwa kuwa alifikiri, “Nitaweza kumtuliza kwa zawadi hizi ninazotanguliza, hatimaye, nitakapomwona, huenda atanikubali.”

21 Kwa hiyo zawadi za Yakobo zilitangulia mbele yake, lakini yeye mwenyewe alilala kambini usiku ule.

Yakobo Ashindana Mweleka Na Mungu

22 Usiku ule Yakobo akaamka akawachukua wake zake wawili, watumishi wake wawili wa kike na wanawe kumi na mmoja na akavuka kivuko cha Yaboki.

23 Baada ya kuwavusha ng’ambo ya kijito, alivusha pia mali zake zote.

24 Kwa hiyo Yakobo akaachwa peke yake na mtu mmoja akashikana naye mweleka mpaka mapambazuko.

25 Yule mtu alipoona kuwa hawezi kumshinda, aligusa kiungio cha nyonga ya Yakobo kwa hiyo nyonga yake ikateguka wakati alipokuwa akishikana mweleka na yule mtu.

26 Ndipo yule mtu akasema, “Niache niende, kwa kuwa ni mapambazuko.”

Lakini Yakobo akajibu, “Sitakuacha uende usiponibariki.”

27 Yule mtu akamwuliza, “Jina lako nani?”

Akajibu, “Yakobo.”

28 Ndipo yule mtu akasema, “Jina lako halitakuwa tena Yakobo, bali Israeli, kwa sababu umeshindana na Mungu na watu pia, nawe umeshinda.”

29 Yakobo akasema, “Tafadhali niambie jina lako.”

Lakini akajibu, “Kwa nini kuniuliza Jina langu?” Ndipo akambariki huko.

30 Kwa hiyo Yakobo akapaita mahali pale Penieli, akasema, “Ni kwa sababu nimemwona Mungu uso kwa uso na bado maisha yangu yameokoka.”

31 Jua lilikuwa linachomoza Yakobo alipoondoka Penueli, naye alikuwa akichechemea kwa sababu ya nyonga yake.

32 Kwa hiyo mpaka leo Waisraeli hawali mshipa ulioungana na kiungio cha nyonga, kwa sababu kiungio cha nyonga ya Yakobo kiliteguliwa karibu na mshipa huo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/32-9e30cac4943bbcb2650af7802393d885.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 33

Yakobo Akutana Na Esau

1 Yakobo akainua macho akamwona Esau akija na watu wake 400, kwa hiyo akawagawanya watoto kati ya Lea, Raheli na wale watumishi wake wawili wa kike.

2 Akawaweka wale watumishi wa kike na watoto wao mbele, Lea na watoto wake wakafuata, Raheli na Yosefu wakaja nyuma.

3 Yeye mwenyewe akatangulia mbele na kusujudu mara saba alipomkaribia ndugu yake.

4 Lakini Esau akamkimbilia Yakobo kumlaki na kumkumbatia, akamwangukia shingoni na kumbusu. Nao wakalia.

5 Esau akainua macho akawaona wale wanawake na watoto. Akauliza, “Hawa uliofuatana nao ni nani?”

Yakobo akamjibu, “Ni watoto ambao Mungu amempa mtumishi wako kwa neema.”

6 Kisha wale watumishi wa kike na watoto wao wakakaribia na kusujudu.

7 Kisha Lea na watoto wake wakaja na kusujudu. Mwisho wa wote wakaja Yosefu na Raheli, nao pia wakasujudu.

8 Esau akauliza, “Una maana gani kuhusu makundi hayo yote niliyokutana nayo?”

Akasema, “Ni ili kupata kibali machoni pako, bwana wangu.”

9 Lakini Esau akamwambia, “Ndugu yangu, tayari nina wingi wa mali. Ulivyo navyo viwe vyako mwenyewe.”

10 Yakobo akasema, “La hasha! Tafadhali, kama nimepata kibali machoni pako, upokee zawadi hii kutoka kwangu. Kwa maana kuuona uso wako, ni kama kuuona uso wa Mungu, kwa kuwa umenipokea kwa takabali kubwa.

11 Tafadhali ukubali zawadi iliyoletwa kwako, kwa kuwa Mungu amenineemesha na ninavyo vyote ninavyohitaji.” Kwa sababu Yakobo alisisitiza, Esau akapokea.

12 Ndipo Esau akasema, “Na tuendelee na safari, nitakuwa pamoja nawe.”

13 Lakini Yakobo akamwambia, “Bwana wangu unajua kwamba watoto ni wachanga na kwamba ni lazima nitunze hawa kondoo wake na ng’ombe wanaonyonyesha. Wakipelekwa kwa haraka hata kama ni kwa siku moja tu, wanyama wote watakufa.

14 Hivyo bwana wangu umtangulie mtumishi wako, wakati mimi nikija polepole kwa mwendo wa makundi yaliyo mbele yangu na mwendo wa watoto, mpaka nifike kwa bwana wangu huko Seiri.”

15 Esau akamwambia, “Basi na niwaache baadhi ya watu wangu pamoja nawe.”

Yakobo akauliza, “Lakini kwa nini ufanye hivyo, niache tu nipate kibali machoni pa bwana wangu.”

16 Hivyo siku hiyo Esau akashika njia akarudi Seiri.

17 Pamoja na hayo, Yakobo akaenda Sukothi, mahali alipojijengea makazi kwa ajili yake na mabanda kwa ajili ya mifugo yake. Hii ndiyo sababu sehemu ile inaitwa Sukothi.

18 Baada ya Yakobo kutoka Padan-Aramu, alifika salama katika mji wa Shekemu huko Kanaani na kuweka kambi yake karibu na mji.

19 Akanunua kiwanja kutoka kwa wana wa Hamori, baba wa Shekemu, kwa bei ya vipande mia vya fedha, ambapo alipiga hema lake.

20 Pale akajenga madhabahu na kupaita El-Elohe-Israeli.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/33-6452315bd46aef6827c859c7500164b2.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 34

Dina Na Washekemu

1 Basi Dina, binti wa Yakobo aliyezaliwa na Lea, akatoka nje kuwatembelea wanawake wa nchi ile.

2 Ikawa Shekemu mwana wa Hamori Mhivi, mtawala wa eneo lile alipomwona, akamchukua na kumnajisi.

3 Moyo wake ukavutwa sana kwa Dina binti Yakobo, akampenda huyu msichana na akazungumza naye kwa kumbembeleza.

4 Shekemu akamwambia baba yake Hamori, “Nipatie msichana huyu awe mke wangu.”

5 Yakobo aliposikia kwamba binti yake Dina amenajisiwa, wanawe walikuwa mashambani wakichunga mifugo yake, kwa hiyo akalinyamazia jambo hilo mpaka waliporudi nyumbani.

6 Kisha Hamori baba yake Shekemu akaenda kuzungumza na Yakobo.

7 Basi wana wa Yakobo walikuwa wamerudi kutoka mashambani mara tu waliposikia kilichotokea. Walikuwa wamejawa na huzuni na ghadhabu, kwa sababu Shekemu alikuwa amefanya jambo la aibu katika Israeli kwa kukutana kimwili na binti wa Yakobo, kitu ambacho hakingepasa kufanyika.

8 Lakini Hamori akawaambia, “Moyo wa mwanangu Shekemu umeelekea kwa binti yenu. Tafadhali mpeni awe mke wake.

9 Oaneni na sisi, tupeni binti zenu nanyi mchukue binti zetu.

10 Mwaweza kuishi katikati yetu, nchi ni wazi kwenu. Ishini ndani yake, fanyeni biashara humu na mjipatie mali.”

11 Kisha Shekemu akamwambia baba yake Dina pamoja na ndugu zake, “Na nipate kibali machoni penu, nami nitawapa cho chote mtakachosema.

12 Niambieni kiasi cha mahari na zawadi nitakayoileta, hata iwe kubwa kiasi gani, nami nitawalipa cho chote mtakachodai. Nipeni tu huyu msichana awe mke wangu.”

13 Kwa sababu ndugu yao Dina alikuwa amenajisiwa, wana wa Yakobo wakajibu kwa udanganyifu walipozungumza na Shekemu pamoja na baba yake Hamori.

14 Wakawaambia, “Hatuwezi kufanya jambo kama hili, hatuwezi kumtoa dada yetu kwa mtu ambaye hakutahiriwa. Hiyo itakuwa aibu kwetu.

15 Tutakuruhusu kwa sharti moja tu, kwamba mtakuwa kama sisi kwa kuwatahiri wanaume wenu wote.

16 Kisha tutawapa binti zetu na sisi tutawachukua binti zenu. Tutaishi kwenu na tutakuwa watu wamoja nanyi.

17 Lakini mkikataa kutahiriwa, tutamchukua ndugu yetu na kuondoka.”

18 Pendekezo lao likawa jema kwa Hamori na Shekemu mwanawe.

19 Kijana mdogo, ambaye alikuwa ameheshimiwa kati ya wote walioishi nyumbani mwa baba yake, hakupoteza muda kufanya waliyoyasema, kwa sababu alikuwa amependezwa sana na binti Yakobo.

20 Kwa hiyo Hamori na Shekemu mwanawe walikwenda kwenye lango la mji kuzungumza na wenzao wa mjini.

21 Wakasema, “Hawa watu ni marafiki kwetu, tuwaruhusu waishi katika nchi yetu na kufanya biashara ndani yake, nchi ina nafasi tele kwa ajili yao. Tunaweza kuoa binti zao. Nao wanaweza kuoa binti zetu.

22 Lakini watu hao watakuwa tayari kukubali kuishi nasi kama watu wamoja nao kwa sharti kwamba wanaume wetu watahiriwe, kama wao.

23 Je, si mifugo yao, mali zao na wanyama wao wengine wote watakuwa wetu? Basi na tuwape kibali, nao wataishi miongoni mwetu.”

24 Wanaume wote waliotoka nje ya lango la mji walikubaliana na Hamori na Shekemu mwanawe na kila mwanaume katika mji ule akatahiriwa.

25 Baada ya siku tatu, wakati wote wakiwa wangali katika maumivu, wana wawili wa Yakobo, yaani Simeoni na Lawi, ndugu zake Dina, wakachukua panga zao nakuvamia mji ambao haukutazamia vita, wakaua kila mwanaume.

26 Wakawaua Hamori na Shekemu mwanawe kwa upanga kisha wakamchukua Dina kutoka nyumba ya Shekemu na kuondoka.

27 Wana wa Yakobo walipita juu ya maiti katika kuteka nyara mji ule ambamo dada yao alikuwa amenajisiwa.

28 Wakachukua kondoo na mbuzi, ng’ombe, punda na kila kitu kilichokuwa chao ndani ya mji ule na mashambani.

29 Walichukua utajiri wao wote pamoja na wanawake na watoto wao, wakachukua nyara kila kitu ndani ya nyumba zao.

30 Kisha Yakobo akawaambia Simeoni na Lawi, “Mmeleta taabu kwangu kwa kunifanya ninuke kama uvundo kwa Wakanaani na Waperizi, watu waishio katika nchi hii. Sisi ni wachache, kama wakiunganisha nguvu zao dhidi yangu na kunishambulia, mimi na nyumba yangu tutaangamizwa.”

31 Lakini wakamjibu, “Je, ilikuwa vyema kumtendea dada yetu kama kahaba?”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/34-5739f8e58f375adcb67498908a88b68a.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 35

Yakobo Arudi Betheli

1 Kisha Mungu akamwambia Yakobo, “Panda uende Betheli ukakae huko na ukamjengee Mungu madhabahu huko, Yeye aliyekutokea ulipokuwa unamkimbia Esau ndugu yako.”

2 Hivyo Yakobo akawaambia watu wa nyumbani mwake pamoja na wote waliokuwa naye, “Iondoeni miungu ya kigeni ile iliyoko katikati yenu, jitakaseni na mkabadilishe nguo zenu.

3 Kisha njoni, twende Betheli, mahali nitakapomjengea Mungu madhabahu, aliyenijibu katika siku ya shida yangu, ambaye amekuwa pamoja nami po pote nilipokwenda.”

4 Kwa hiyo wakampa Yakobo miungu yote ya kigeni waliyokuwa nayo pamoja na pete zilizokuwa masikioni mwao, Yakobo akavizika chini ya mti wa mwaloni huko Shekemu.

5 Kisha wakaondoka na hofu ya Mungu ikawapata miji yote iliyowazunguka kwa hiyo hakuna aliyewafuatia.

6 Yakobo na watu wote waliokuwa pamoja naye wakafika Luzu (ndio Betheli), katika nchi ya Kanaani.

7 Huko akajenga madhabahu na akapaita mahali pale El-Betheli, kwa sababu mahali pale ndipo Mungu alipojifunua kwake alipokuwa akimkimbia ndugu yake.

8 Wakati huu Debora, mlezi wa Rebeka, akafa na akazikwa chini ya mti wa mwaloni ulioko chini ya Betheli. Kwa hiyo pakaitwa Alon-Bakuthi.

9 Baada ya Yakobo kurudi kutoka Padan-Aramu, Mungu alimtokea tena na kumbariki.

10 Mungu akamwambia, “Jina lako ni Yakobo, lakini hutaitwa tena Yakobo, jina lako utakuwa Israeli.” Kwa hiyo akamwita Israeli.

11 Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi, ukazae na kuongezeka. Taifa na jamii ya mataifa itatoka kwako, nao wafalme watatoka viunoni mwako.

12 Nchi niliyowapa Abrahamu na Isaki nakupa wewe pia, nami nitawapa wazao wako baada yako.”

13 Kisha Mungu akapanda juu kutoka kwake mahali pale alipozungumza naye.

14 Yakobo akasimamisha nguzo ya jiwe mahali pale Mungu alipozungumza naye, akamimina sadaka ya kinywaji juu yake, pia akamimina mafuta juu yake.

15 Yakobo akapaita mahali pale Mungu alipozungumza naye Betheli.

Vifo Vya Raheli Na Isaki

16 Kisha wakaondoka Betheli. Walipokuwa umbali fulani kabla ya kufika Efrathi, Raheli akaanza kusikia uchungu na alipata shida kuu.

17 Alipokuwa katika shida hii katika kujifungua, mkunga akamwambia, “Usiogope, kwa sababu umempata mwana mwingine.”

18 Hapo alipopumua pumzi yake ya mwisho, kwa maana alikuwa akifa, akamwita mwanawe Benoni. Lakini babaye akamwita Benyamini.

19 Kwa hiyo Raheli akafa, akazikwa kando ya njia iendayo Efrathi (ndio Bethlehemu).

20 Juu ya kaburi lake, Yakobo akasimamisha nguzo, ambayo mpaka leo inatambulisha kaburi la Raheli.

21 Israeli akaendelea tena na safari yake na kupiga hema mbele ya Ederi.

22 Wakati Israeli alipokuwa akiishi katika nchi ile, Reubeni mwanawe alikutana kimwili na suria wa baba yake aitwaye Bilha, naye Israeli akasikia jambo hili.

Yakobo alikuwa na wana kumi na wawili:

23 Wana wa Lea walikuwa:

Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo,

Simeoni, Lawi, Yuda, Isikari na Zabuloni.

24 Wana wa Raheli walikuwa:

Yosefu na Benyamini.

25 Wana waliozaliwa na Bilha mtumishi wa kike wa Raheli walikuwa:

Dani na Naftali.

26 Wana waliozaliwa na Zilpa mtumishi wa kike wa Lea walikuwa:

Gadi na Asheri.

Hawa walikuwa wana wa Yakobo, waliozaliwa kwake akiwa Padan-Aramu.

27 Yakobo akarudi nyumbani kwa baba yake Isaki huko Mamre, karibu na Kiriath-Arba (yaani Hebroni), ambapo walikuwa wameishi Abrahamu na Isaki.

28 Isaki aliishi miaka 180.

29 Kisha Isaki akapumua pumzi yake ya mwisho akafa, akakusanywa pamoja na watu wake akiwa mzee wa miaka mingi. Nao wanawe Esau na Yakobo wakamzika.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/35-bef0a453cbf819b0eaf4d4632d30171d.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 36

Wazao Wa Esau

1 Hivi ndivyo vizazi vya Esau (yaani Edomu).

2 Esau akaoa wake kutoka miongoni mwa wanawake wa Kanaani: Ada binti wa Eloni Mhiti, Oholibama binti wa Ana, mjukuu wa kike wa Sibeoni Mhivi,

3 pia akaoa Basemathi binti wa Ishmaeli, dada yake Nebayothi.

4 Ada akamzalia Esau Elifazi, Basemathi akamzaa Reueli,

5 Oholibama akamzaa Yeushi, Yalamu na Kora. Hawa ndio wana wa Esau waliozaliwa kwake huko Kanaani.

6 Esau akawachukua wake zake, watoto wake wa kiume na wa kike na wote wa nyumbani mwake, mifugo yake pamoja na wanyama wake wengine wote na mali yake yote ambayo alikuwa ameipata akiwa Kanaani, akahamia katika nchi iliyo mbali na Yakobo ndugu yake.

7 Mali zao zilikuwa nyingi sana kiasi kwamba haikuwa rahisi wao kuishi pamoja, nchi waliyokuwa wakiishi isingewatosha wote kwa ajili ya mifugo yao.

8 Kwa hiyo Esau (ambaye ni Edomu) aliishi katika nchi ya kilima huko Seiri.

9 Hawa ndio wazao wa Esau, baba wa Waedomu, katika nchi ya kilima cha Seiri.

10 Haya ndiyo majina ya wana wa Esau:

Elifazi, mwana wa Esau ambaye mkewe Ada alimzalia; na Reueli, mwana wa Esau ambaye mkewe Basemathi alimzalia.

11 Wana wa Elifazi ni:

Temani, Omari, Sefo, Gatamu na Kenazi.

12 Elifazi mwana wa Esau alikuwa pia na suria aliyeitwa Timna, ambaye alimzalia Amaleki. Hawa ndio waliokuwa wajukuu wa Ada mke wa Esau.

13 Wana wa Reueli ni:

Nahathi, Zera, Shama na Miza. Hawa ndio waliokuwa wajukuu wa Basemathi mkewe Esau.

14 Wana wa Oholibama binti Ana, mkewe Esau, aliyekuwa mjukuu wa Sibeoni, aliomzalia Esau ni:

Yeushi, Yalamu na Kora.

15 Hawa ndio waliokuwa wakuu miongoni mwa wazao wa Esau:

Wakuu wa wana wa Elifazi, mzaliwa wa kwanza wa Esau ni:

Temani, Omari, Sefo, Kenazi,

16 Kora, Gatamu na Amaleki. Hawa ndio waliokuwa wakuu waliotoka kwa Elifazi huko Edomu, waliokuwa wajukuu wa kiume wa Ada.

17 Wakuu wa wana wa Reueli, mwana wa Esau ni:

Nathani, Zera, Shama na Miza. Hawa ndio wakuu waliotoka kwa Reueli huko Edomu, waliokuwa wajukuu wa kiume wa Basemathi mkewe Esau.

18 Wakuu wa wana wa Esau ambao mkewe Oholibama alimzalia ni:

Yeushi, Yalamu na Kora. Hawa ndio wakuu waliotoka kwa mke wa Esau, Oholibama binti Ana.

19 Hawa ndio waliokuwa wana wa Esau (ndiye Edomu), na hawa ndio waliokuwa wakuu wao.

20 Hawa ndio walikuwa wana wa Seiri, Mhori, waliokuwa wakiishi katika nchi ile:

Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana,

21 Dishoni, Eseri na Dishani. Hawa ndio wana wa Seiri huko Edomu waliokuwa wakuu kwa Wahori.

22 Wana wa Lotani walikuwa:

Hori na Homamu. Timna alikuwa dada yake Lotani.

23 Wana wa Shobali walikuwa:

Alvani, Manahathi, Ebali, Shefo na Onamu.

24 Wana wa Sibeoni walikuwa:

Aiya na Ana. Huyu Ana ndiye aliyegundua chemchemi ya maji moto jangwani alipokuwa akichunga punda za Sibeoni baba yake.

25 Watoto wa Ana walikuwa:

Dishoni na Oholibama binti wa Ana.

26 Wana wa Dishoni walikuwa:

Hemdani, Eshbani, Ithrani na Kerani.

27 Wana wa Ezeri walikuwa:

Bilhani, Zaavani na Akani.

28 Wana wa Dishani walikuwa:

Usi na Arani.

29 Hawa ndio waliokuwa wakuu wa Wahori:

Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana,

30 Dishoni, Ezeri na Dishani. Hawa ndio walikuwa wakuu wa Wahori, kufuatana na makundi yao, katika nchi ya Seiri.

Watawala Wa Edomu

31 Wafuatao ni wafalme waliotawala Edomu kabla ya mfalme ye yote wa Israeli kutawala:

32 Bela mwana wa Beiri alikuwa mfalme wa Edomu. Mji wake uliitwa Dinhaba.

33 Bela alipokufa, nafasi yake ya ufalme ikashikwa na Yobabu mwanawe Zera kutoka Bosra.

34 Yobabu alipokufa, Hushamu kutoka nchi ya Watemani akatawala baada yake.

35 Hushamu alipokufa, Hadadi mwana wa Bedadi, ambaye alikuwa ameshinda Midiani katika nchi ya Moabu, akatawala baada yake. Mji wake uliitwa Avithi.

36 Hadadi alipokufa, Samla kutoka Masreka akawa mfalme baada yake.

37 Samla alipokufa, Shauli kutoka Rehobothi ng’ambo ya Mto Eufrati akatawala baada yake.

38 Shauli alipokufa, Baal-Hanani mwana wa Akbori alitawala badala yake.

39 Baal-Hanani mwana wa Akbori alipokufa, Hadadi akatawala baada yake. Mji wake uliitwa Pau, naye mke wake aliitwa Mehetabeli binti Matredi, binti Me-Zahabu.

40 Hawa ndio wakuu waliotokana na Esau, kwa majina, kufuatana na koo zao na nchi zao:

Timna, Alva, Yethethi,

41 Oholibama, Ela, Pinoni,

42 Kenazi, Femani, Mibsari,

43 Magdieli na Iramu. Hawa ndio walikuwa wakuu wa Edomu, kufuatana na makazi yao katika nchi waliyoimiliki.

Huyu ndiye aliyekuwa Esau, baba wa Waedomu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/36-3b2cde05d94227532eeeb3958cc5e1eb.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 37

Ndoto Za Yosefu

1 Yakobo akaishi Kanaani katika nchi ambayo baba yake alikuwa ameishi.

2 Zifuatazo ni habari za Yakobo.

Yosefu, kijana wa miaka kumi na saba, alikuwa akichunga makundi ya kondoo na mbuzi pamoja na ndugu zake wa mama wengine, yaani wana wa Bilha na wana wa Zilpa wake za baba yake, naye akawa akimletea baba yake taarifa mbaya kuhusu hao ndugu zake.

3 Basi, Israeli akampenda Yosefu kuliko ye yote miongoni mwa kaka zake, kwani ni mwanawe wa uzeeni, akamshonea joho lililorembwa vizuri sana.

4 Ndugu zake walipoona kwamba baba yao anampenda Yosefu kuliko ye yote mwingine miongoni mwao, walimchukia na hawakusema naye neno lo lote jema.

5 Yosefu akaota ndoto, naye alipowaeleza ndugu zake, wakamchukia zaidi.

6 Akawaambia, “Sikilizeni ndoto niliyoota:

7 Tulikuwa tukifunga miganda ya nafaka shambani, ghafula mganda wangu ukasimama wima, wakati miganda yenu ikiuzunguka na kuuinamia.”

8 Ndugu zake wakamwambia, “Wewe unakusudia kututawala? Hivi kweli wewe utatutawala sisi?” Wakaongeza kumchukia zaidi kwa sababu ya ndoto yake pamoja na yale aliyowaambia.

9 Kisha akaota ndoto nyingine, akawaambia ndugu zake akisema, “Sikilizeni, nimeota ndoto nyingine, wakati huu jua, mwezi na nyota kumi na moja zilikuwa zinanisujudia.”

10 Alipomwambia baba yake pamoja na ndugu zake, baba yake akamkemea akisema, “Ni ndoto gani hii uliyoota? Hivi kweli mama yako na mimi na ndugu zako tutakuja kukusujudia wewe hadi nchi?”

11 Ndugu zake wakamwonea wivu, lakini baba yake akaliweka jambo hilo moyoni.

Yosefu Anauzwa Na Ndugu Zake

12 Basi, ndugu zake walikuwa wamekwenda kuchunga makundi ya baba yao karibu na Shekemu,

13 naye Israeli akamwambia Yosefu, “Kama ujuavyo, ndugu zako wanachunga makundi huko karibu na Shekemu. Njoo, nitakutuma kwao.”

Yosefu akajibu, “Vema sana niko tayari.”

14 Kwa hiyo akamwambia, “Nenda uone kama mambo yote ni salama kwa ndugu zako na makundi, kisha uniletee habari.” Ndipo akamtuma Yosefu kutoka Bonde la Hebroni.

Yosefu alipofika Shekemu,

15 mtu mmoja akamkuta akizungukazunguka mashambani na akamwuliza, “Unatafuta nini?”

16 Akajibu, “Ninawatafuta ndugu zangu. Unaweza kuniambia wanachunga wapi makundi yao?”

17 Yule mtu akajibu, “Wamehama hapa. Nimesikia wakisema, ‘Twende Dothani.’ ”

Kwa hiyo Yosefu akawafuatilia ndugu zake na kuwakuta karibu na Dothani.

18 Ndugu zake walipomwona akiwa mbali, kabla hajawafikia, wakapanga shauri baya la kumwua.

19 Wakaambiana, “Yule mwota ndoto anakuja!

20 Njoni sasa, tumwue na kumtupa katika shimo mojawapo na tuseme kwamba mnyama mkali amemrarua. Kisha tutaona matokeo ya ndoto zake.”

21 Reubeni aliposikia jambo hili, akajaribu kumwokoa kutoka mikononi mwao akasema, “Tusiutoe uhai wake.

22 Tusimwage damu yo yote. Mtupeni katika shimo lililoko hapa jangwani, lakini msimguse.” Reubeni alisema hivyo ili amwokoe kutoka mikononi mwao, kisha amrudishe nyumbani kwa baba yake.

23 Kwa hiyo Yosefu alipowafikia ndugu zake, walimvua lile joho lake, lile joho lililorembwa vizuri alilokuwa amevaa.

24 Kisha wakamchukua wakamtupa katika shimo. Wakati huo shimo lilikuwa tupu, halikuwa na maji ndani yake.

25 Walipokaa ili wale chakula chao, wakainua macho wakaona msafara wa Waishmaeli ukija kutoka Gileadi. Ngamia wao walikuwa wamepakizwa mizigo ya vikolezo, uvumba na manemane, nao walikuwa njiani kuvipeleka Misri.

26 Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutafaidi nini ikiwa tutamwua ndugu yetu na kuificha damu yake?

27 Njoni, tumwuze kwa hawa Waishmaeli, tusimguse kwa kuwa hata hivyo, yeye ni ndugu yetu, nyama yetu na damu yetu wenyewe.” Ndugu zake wakakubali.

28 Kwa hiyo wale wafanyabiashara Wamidiani walipofika pale, ndugu zake wakamtoa Yosefu kutoka kwenye lile shimo na kumwuza kwa shekeli ishiriniza fedha kwa wale Waishimaeli, ambao walimpeleka Misri.

29 Reubeni aliporudi kutazama kwenye lile shimo na kuona kwamba Yosefu hayupo, alirarua nguo zake.

30 Akawarudia ndugu zake na kusema, “Kijana hayuko mle! Nielekee wapi sasa?”

31 Kisha wakalichukua lile joho la Yosefu, wakachinja mbuzi na kulichovya katika damu.

32 Wakalichukua lile joho lililorembwa vizuri na kulipeleka kwa baba yao na kusema, “Tumeliokota hili joho. Uchunguze uone kama ni la mwanao.”

33 Baba yao akalitambua akasema, “Hili ni joho la mwanangu! Mnyama mkali amemrarua. Hakika Yosefu ameraruliwa vipande vipande.”

34 Kisha Yakobo akararua nguo zake, akavaa nguo ya gunia na kumwombolezea mwanawe kwa siku nyingi.

35 Wanawe wote na binti zake wakaja kumfariji, lakini hakukubali kufarijiwa. Akasema, “Hapana, nitamwombolezea mwanangu mpaka nimfikie kaburini.” Kwa hiyo baba yake akaendelea kumlilia.

36 Wakati ule ule, Wamidiani wakamwuza Yosefu huko Misri kwa Potifa, mmojawapo wa maafisa wa Farao, aliyekuwa mkuu wa ulinzi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/37-7377bc119f8c5847bfc9b3118dbd2088.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 38

Yuda Na Tamari

1 Wakati ule, Yuda akawaacha ndugu zake akaenda kuishi na Hira Mwadulami.

2 Huko Yuda akakutana na binti wa Kikanaani aitwaye Shua akamwoa na akakutana naye kimwili,

3 akapata mimba akamzaa mwana, ambaye alimwita Eri.

4 Akapata mimba tena, akamzaa mwana na kumwita Onani.

5 Akamzaa mwana mwingine tena, akamwita Shela. Huyu alimzalia mahali paitwapo Kezibu.

6 Yuda akampatia Eri, mzaliwa wake wa kwanza mke, aitwaye Tamari.

7 Lakini Eri, mzaliwa wa kwanza wa Yuda alikuwa mwovu machoni paBwana, kwa hiyoBwanaakamwua.

8 Kisha Yuda akamwambia Onani, “Kutana kimwili na mke wa ndugu yako na utimize wajibu wako kwake kama mke wa ndugu yako ili umpatie ndugu yako uzao.”

9 Lakini Onani alijua kwamba uzao haungekuwa wake, kwa hiyo kila alipokutana kimwili na mke wa ndugu yake, alimwaga chini mbegu za kiume ili asimpatie ndugu yake uzao.

10 Alichofanya kilikuwa kiovu machoni paBwana, hivyo, piaBwanaakamwua Onani.

11 Kisha Yuda akamwambia Tamari mkwewe, “Ishi kama mjane nyumbani mwa baba yako mpaka mwanangu Shela atakapokua.” Kwa maana alifikiri, “Angeweza kufa pia kama ndugu zake.” Kwa hiyo Tamari alikwenda kuishi nyumbani kwa baba yake.

12 Baada ya muda mrefu mke wa Yuda binti wa Shua akafariki. Baada ya msiba, Yuda alikwenda Timna, kwa watu waliokuwa wakikata kondoo wake manyoya, naye alifuatana na rafiki yake Hira Mwadulami.

13 Tamari alipoambiwa, “Baba mkwe wako yuko njiani kwenda Timna kukata kondoo wake manyoya,”

14 alivua mavazi yake ya ujane, akajifunika kwa shela ili asifahamike, akaketi kwenye mlango wa Enaimu, ambao upo njiani kuelekea Timna. Akafanya hivyo kwa sababu aliona kwamba, ingawa Shela amekua, lakini alikuwa hajakabidhiwa kwake kuwa mkewe.

15 Yuda alipomwona alifikiri ni kahaba, kwa sababu alikuwa amefunika uso wake.

16 Pasipo kutambua kwamba alikuwa mkwe wake, akamwendea kando ya njia na kumwambia, “Njoo sasa, nikutane na wewe kimwili.”

Yule mkwewe akamwuliza, “Utanipa nini nikikutana nawe kimwili?”

17 Akamwambia, “Nitakutumia mwana-mbuzi kutoka kundi langu.”

Akamwuliza, “Utanipa kitu cho chote kama amana mpaka utakapompeleka?”

18 Akamwuliza, “Nikupe amana gani?”

Akamjibu, “Pete yako na kamba yake pamoja na fimbo iliyo mkononi mwako.” Kwa hiyo akampa vitu hivyo kisha akakutana naye kimwili, naye akapata mimba yake.

19 Tamari akaondoka, akavua shela yake akavaa tena nguo zake za ujane.

20 Wakati ule ule, Yuda akamtuma rafiki yake Mwadulami apeleke yule mwana-mbuzi ili arudishiwe amana yake kutoka kwa yule mwanamke, lakini yule rafiki yake hakumkuta yule mwanamke.

21 Akawauliza watu wanaoishi mahali pale, “Yuko wapi yule kahaba wa mahali pa kuabudia miungu aliyekuwa kando ya barabara hapa Enaimu?”

Wakamjibu, “Hajawahi kuwepo mwanamke ye yote kahaba wa mahali pa kuabudia miungu hapa.”

22 Kwa hiyo akamrudia Yuda na kumwambia, “Sikumpata. Zaidi ya hayo, watu wanaoishi mahali pale walisema ‘Hapakuwahi kuwepo mwanamke ye yote kahaba wa mahali pa kuabudia miungu hapa.’ ”

23 Kisha Yuda akasema, “Mwache avichukue vitu hivyo, ama sivyo tutakuwa kichekesho. Hata hivyo, nilimpelekea mwana-mbuzi, lakini hukumkuta.”

24 Baada ya miezi mitatu Yuda akaambiwa, “Tamari mkweo ana hatia ya kuwa kahaba, na matokeo yake ana mimba.”

Yuda akasema, “Mtoeni nje na achomwe moto hadi afe!”

25 Alipokuwa akitolewa nje, akatuma ujumbe kwa baba mkwe wake kusema, “Nina mimba ya mtu mwenye vitu hivi.” Akaongeza kusema, “Angalia kama utatambua kwamba pete hii na kamba yake pamoja na fimbo hii ni vya nani.”

26 Yuda akavitambua na kusema, “Yeye ana haki kuliko mimi, kwa kuwa sikumkabidhi kwa mwanangu Shela ili awe mkewe.” Tangu hapo hakukutana naye kimwili tena.

27 Wakati ulipofika wa kujifungua, kukawa na wana mapacha tumboni mwake.

28 Alipokuwa akijifungua, mmoja akatoa mkono wake nje, kwa hiyo muuguzi akachukua uzi mwekundu na kuufunga mkononi mwa yule mtoto akasema, “Huyu ametoka kwanza.”

29 Lakini alipourudisha mkono wake ndugu yake akaanza kutoka naye akasema, “Hivi ndivyo ulivyotoka kwa nguvu!” Akaitwa Peresi.

30 Kisha ndugu yake, aliyekuwa na uzi mwekundu mkononi, akatoka naye akaitwa Zera.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/38-500dfeb3411bbd2a3b1fcf5503e0d91c.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 39

Yosefu Na Mke Wa Potifa

1 Wakati huu Yosefu alikuwa amechukuliwa mpaka Misri. Mmisri aliyeitwa Potifa aliyekuwa mmojawapo wa maafisa wa Farao, mkuu wa ulinzi, akamnunua Yosefu kutoka kwa Waishimaeli waliomleta Misri.

2 Bwanaalikuwa pamoja na Yosefu, naye akastawi, Yosefu akaishi nyumbani kwa bwana wake Mmisri.

3 Potifa alipoona kuwaBwanaalikuwa pamoja na Yosefu na kwambaBwanaalimfanikisha kwa kila kitu alichokifanya,

4 Yosefu alipata kibali machoni pa Potifa, akamfanya mhudumu wake. Potifa akamweka kuwa msimamizi wa nyumba yake, naye akamkabidhi kuwa mwangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho.

5 Kuanzia wakati huo Potifa alipomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nyumba na mali zake zote alizokuwa nazo,Bwanaaliibariki nyumba ya Potifa kwa sababu ya Yosefu. Baraka yaBwanailikuwa juu ya kila kitu alichokuwa nacho Potifa, nyumbani na shambani.

6 Kwa hiyo Potifa akamwachia Yosefu uangalizi wa kila kitu alichokuwa nacho, Yosefu alipokuwa katika uongozi, Potifa hakuwa na sababu ya kujishughulisha na kitu cho chote isipokuwa chakula alichokula.

Yosefu alikuwa mwenye umbo zuri na sura ya kuvutia;

7 baada ya kitambo mke wa Potifa akamtamani Yosefu, akamwambia, “Njoo, ukutane nami kimwili!”

8 Lakini Yosefu akakataa. Akamwambia yule mwanamke, “Mimi nikiwa katika uongozi, bwana wangu hahusiki na kitu cho chote katika nyumba hii, kila kitu alicho nacho amenikabidhi.

9 Hapa nyumbani hakuna aliye mkuu kuliko mimi. Bwana wangu hakunizuilia kitu cho chote isipokuwa wewe, kwa kuwa wewe ni mke wake. Nitawezaje basi kufanya uovu huu na kutenda dhambi dhidi ya Mungu?”

10 Ingawa yule mwanamke aliendelea kumshawishi Yosefu siku baada ya siku, Yosefu alikataa kukutana naye kimwili wala kukaa karibu naye.

11 Siku moja Yosefu akaingia ndani ya nyumba kufanya kazi zake, wala hapakuwepo na mfanyakazi ye yote ndani ya nyumba.

12 Mke wa Potifa akashika vazi Yosefu alilokuwa amevaa, akamwambia, “Njoo tukutane kimwili!” Lakini Yosefu akaacha vazi lake mkononi mwa huyo mwanamke, akatoka nje ya nyumba akikimbia.

13 Yule mwanamke alipoona kwamba Yosefu amemwachia vazi lake mkononi na kukimbilia nje ya nyumba,

14 akawaita watumishi wake wa nyumbani, akawaambia, “Tazameni! Huyu Mwebrania ameletwa hapa kutudhihaki! Aliingia hapa ndani ili akutane nami kimwili, lakini nikapiga kelele.

15 Aliposikia kelele za kuomba msaada, akaacha vazi lake kando yangu akakimbilia nje.”

16 Yule mwanamke akaliweka lile vazi karibu naye mpaka Potifa aliporudi nyumbani.

17 Ndipo akamweleza kisa hiki, akisema: “Yule mtumwa wa Kiebrania uliyetuletea alinijia ili kunidhihaki.

18 Lakini mara nilipopiga kelele kuomba msaada, akaliacha vazi lake kando yangu akakimbia nje ya nyumba.”

19 Potifa aliposikia kisa hiki mkewe alichomweleza, akisema, “Hivi ndivyo mtumwa wako alivyonitenda.” Hasira ya Potifa ikawaka.

20 Potifa akamchukua Yosefu na kumweka gerezani, mahali ambapo wahalifu wa mfalme walikuwa wamefungwa.

Lakini wakati Yosefu alipokuwa huko gerezani,

21 Bwanaalikuwa pamoja naye, akamhurumia na kumpa kibali mbele ya msimamizi wa gereza.

22 Kwa hiyo msimamizi wa gereza akamweka Yosefu awe mkuu wa wafungwa pamoja na kusimamia yote ambayo yalitendeka mle gerezani.

23 Msimamizi wa gereza hakujishughulisha tena na kitu cho chote kilichokuwa chini ya uangalizi wa Yosefu, kwa sababuBwanaalikuwa pamoja na Yosefu akimfanikisha kwa kila alichofanya.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/39-ee7c1009eac9f887c6ba4734ba611dad.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 40

Mnyweshaji Na Mwokaji

1 Baada ya muda, mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, wakamkosea bwana wao, mfalme wa Misri.

2 Farao akawakasirikia hawa maafisa wake wawili, mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu,

3 akawaweka chini ya ulinzi katika nyumba ya mkuu wa kikosi cha ulinzi katika gereza lile lile alimofungwa Yosefu.

4 Mkuu wa kikosi cha ulinzi akawakabidhi kwa Yosefu, naye akawahudumia.

Walipokuwa wamekaa chini ya ulinzi kwa muda,

5 kila mmoja wa hao wawili waliokuwa wamewekwa gerezani, yaani mnyweshaji na mwokaji wa mfalme wa Misri, waliota ndoto usiku mmoja, na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti.

6 Yosefu alipowajia asubuhi yake, akawaona kwamba walikuwa na huzuni.

7 Ndipo Yosefu akawauliza maafisa hao wa Farao waliokuwa chini ya ulinzi pamoja naye nyumbani mwa bwana wake, akasema, “Mbona nyuso zenu zimejaa huzuni leo?”

8 Wakamjibu, “Sisi sote tuliota ndoto, lakini hapakuwa na mtu ye yote wa kuzifasiri.”

Ndipo Yosefu akawaambia, “Je, kufasiri ndoto si kazi ya Mungu? Niambieni ndoto zenu.”

9 Basi mkuu wa wanyweshaji akamweleza Yosefu ndoto yake. Akamwambia, “Katika ndoto yangu niliona mzabibu mbele yangu,

10 nao mzabibu ulikuwa na matawi matatu. Mara tu ulipoanza kuchipua, maua yalichanua na vishada vyake vikawa zabibu zilizoiva.

11 Kikombe cha Farao kilikuwa mkononi mwangu, nikazitwaa zabibu, nikazikamua katika kikombe cha Farao, na nikaweka kikombe mkononi mwake.”

12 Yosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Matawi matatu ni siku tatu.

13 Katika siku hizi tatu, Farao atakutoa gerezani na kukuweka tena kwenye nafasi yako, nawe utaweka kikombe cha Farao mikononi mwake, kama vile ulivyokuwa unafanya ulipokuwa mnyweshaji wake.

14 Lakini wakati mambo yatakapokuwia mazuri, unikumbuke, unifanyie wema, useme mema juu yangu kwa Farao ili niondoke huku gerezani.

15 Kwa maana nilichukuliwa kwa nguvu kutoka nchi ya Waebrania, na hata hapa nilipo sikufanya lo lote linalostahili niwekwe gerezani.”

16 Yule mwokaji mkuu alipoona kuwa Yosefu amefasiri ikiwa na maana nzuri, akamwambia Yosefu, “Mimi pia niliota ndoto: Kichwani mwangu kulikuwepo vikapu vitatu vya mikate.

17 Katika kikapu cha juu kulikuwa na aina zote za vyakula vilivyookwa kwa ajili ya Farao, lakini ndege walikuwa wakivila kutoka kwenye kikapu nilichokuwa nimebeba kichwani.”

18 Yosefu akamwambia, “Hii ndiyo maana yake: Vikapu vitatu ni siku tatu.

19 Katika siku hizi tatu, Farao atakata kichwa chako na kukutundika juu ya mti. Nao ndege watakula nyama ya mwili wako.”

20 Mnamo siku ya tatu, ilikuwa kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Farao, naye akawaandalia maafisa wake wote karamu. Akawatoa gerezani mnyweshaji mkuu na mwokaji mkuu, akawaweka mbele ya maafisa wake:

21 Ndipo akamrudisha mnyweshaji kwenye nafasi yake, ili aweke kikombe mikononi mwa Farao tena,

22 lakini akamwangika yule mwokaji mkuu, sawasawa na jinsi Yosefu alivyowaambia katika tafsiri yake.

23 Pamoja na hayo, mnyweshaji mkuu hakumkumbuka Yosefu, bali alimsahau.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/40-a5e9d052d77b9d867c41aac0b2b0138f.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 41

Ndoto Za Farao

1 Baada ya miaka miwili kamili kupita, Farao aliota ndoto: Tazama alikuwa amesimama kando ya Mto Nile,

2 wakati ng’ombe saba, wazuri na wanono, walitokea mtoni wakajilisha kwenye manyasi.

3 Baada yao ng’ombe wengine saba, wabaya na waliokonda, wakatokea mtoni Nile wakasimama kando ya wale wanono ukingoni mwa mto.

4 Wale ng’ombe wabaya na waliokonda wakawala wale saba wazuri na wanono. Kisha Farao akaamka.

5 Farao akaingia usingizini tena akaota ndoto ya pili: Akaona masuke saba ya nafaka, yenye afya na mazuri, yanakua katika bua moja.

6 Baadaye, masuke mengine saba yakachipua, yakiwa membamba yaliyonyaushwa na upepo wa mashariki.

7 Masuke yale membamba yakameza yale masuke saba yenye afya na yaliyojaa. Basi Farao akaamka kutoka usingizini, kumbe ilikuwa ndoto.

8 Asubuhi yake, alifadhaika akilini, hivyo akawaita waaguzi wote pamoja na watu wenye busara wa Misri. Walipokuja, Farao akawaeleza ndoto zake, lakini hakuna hata mmoja aliyeweza kumfasiria.

9 Ndipo mnyweshaji mkuu alipomwambia Farao, “Leo nimekumbushwa kuhusu kosa langu.

10 Wakati fulani Farao aliwakasirikia watumishi wake, akanifunga mimi na mwokaji mkuu katika nyumba ya mkuu wa ulinzi.

11 Kila mmoja wetu aliota ndoto katika usiku mmoja na kila ndoto ilikuwa na maana yake tofauti.

12 Basi kijana wa Kiebrania aliyekuwa pamoja nasi huko, alikuwa mtumishi wa mkuu wa kikosi cha ulinzi. Tulimweleza ndoto zetu, naye akatufasiria, akitupa kila mtu tafsiri ya ndoto yake.

13 Nayo mambo yakawa sawa kabisa na jinsi alivyotufasiria ndoto zetu: Mimi nilirudishwa kazini mwangu na huyo mtu mwingine akaangikwa.”

14 Basi, Farao akatuma Yosefu aitwe, naye akatolewa kifungoni haraka. Baada ya kunyoa na kubadilisha nguo zake akaenda mbele ya Farao.

15 Farao akamwambia Yosefu, “Nimeota ndoto, wala hakuna mtu hata mmoja anayeweza kuifasiri. Lakini nimesikia ikisemwa kwa habari yako kwamba unapoelezwa ndoto waweza kuifasiri.”

16 Yosefu akamjibu Farao, “Siwezi kuifasiri, lakini Mungu atampa Farao jibu analolihitaji.”

17 Kisha Farao akamwambia Yosefu, “Katika ndoto yangu nilikuwa nimesimama ukingoni mwa Mto Nile,

18 nikawaona ng’ombe saba, wazuri na wanono, wakijitokeza kutoka mtoni wakaja kujilisha kwenye manyasi.

19 Baada ya hao, ng’ombe wengine saba wadhaifu wakatokea, wabaya sana na waliokonda. Kamwe sikuwahi kuona ng’ombe wabaya jinsi hiyo katika nchi yote ya Misri.

20 Hao ng’ombe waliokonda na wabaya sana wakawala wale ng’ombe saba walionona waliojitokeza kwanza.

21 Lakini hata baada ya kuwala, hakuna mtu ambaye angeweza kusema kwamba wamekula, bado walionekana wabaya kama mwanzoni. Kisha nikaamka kutoka usingizini.

22 “Pia katika ndoto zangu niliona masuke saba ya nafaka, yamejaa na mazuri, yanakua katika bua moja.

23 Baada ya hayo masuke mengine saba yakachipua, yaliyonyauka, membamba na yamekaushwa na upepo wa mashariki.

24 Yale masuke membamba ya nafaka yakayameza yale masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka. Nimewaeleza waaguzi, wala hakuna ye yote aliyeweza kunifasiria.”

25 Ndipo Yosefu akamwambia Farao, “Ndoto za Farao ni ndoto iyo hiyo moja. Mungu amemfunulia Farao jambo analokusudia kufanya karibuni.

26 Ng’ombe saba wazuri ni miaka saba, nayo masuke saba mazuri yaliyojaa nafaka ni miaka saba, ni ndoto iyo hiyo moja.

27 Ng’ombe saba waliokonda na wabaya wale waliojitokeza baadaye ni miaka saba, vivyo hivyo masuke saba ya ngano yaliyodhoofika na kukaushwa na upepo wa mashariki, ni miaka saba ya njaa.

28 “Ni kama vile nilivyomwambia Farao: Mungu amemwonyesha Farao jambo analokusudia kufanya karibuni.

29 Miaka saba ya neema inakuja katika nchi yote ya Misri,

30 lakini itafuata miaka saba ya njaa. Ndipo neema yote ya Misri itasahaulika na njaa itaikumba nchi.

31 “Neema iliyokuwa katika nchi haitakumbukwa, kwa sababu njaa itakayofuata itakuwa kali mno.

32 Sababu ya ndoto kumjia Farao kwa namna mbili ni kwamba jambo hilo Mungu ameshaamua kwa hakika, naye Mungu atalifanya karibuni.

33 “Basi sasa Farao na atafute mtu mwenye akili na hekima ili amweke kuwa msimamizi wa nchi ya Misri.

34 Farao na aweke wenye amri nchini kote wakusanye sehemu ya tano ya mavuno ya Misri katika miaka hii saba ya neema.

35 Wakusanye chakula chote katika miaka hii saba ya neema inayokuja na kuhifadhi nafaka chini ya mamlaka ya Farao, iwe akiba ya chakula katika miji.

36 Chakula hiki kitakuwa akiba ya tahadhari kwa ajili ya nchi, ili kitumike katika ile miaka saba ya njaa itakayokuja Misri, ili nchi isiharibiwe na njaa.”

37 Mpango huu ulionekana mzuri kwa Farao na kwa maafisa wake wote.

38 Hivyo Farao akawauliza, “Je tunaweza kumpata ye yote kama mtu huyu, ambaye Roho wa Mungu yumo ndani yake?”

39 Ndipo Farao akamwambia Yosefu, “Maadamu Mungu amekufunulia yote haya, hakuna mwingine ye yote mwenye akili na hekima kama wewe.

40 Wewe utakuwa msimamizi wa jumba langu la kifalme, na watu wangu wote watatii amri zako. Ni kuhusu kiti cha ufalme tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.”

Yosefu Msimamizi Wa Misri

41 Kwa hiyo Farao akamwambia Yosefu, “Sasa nakuweka uwe msimamizi wa nchi yote ya Misri.”

42 Ndipo Farao akaivua pete yake ya muhuri kutoka kidoleni mwake na kuivalisha katika kidole cha Yosefu. Akamvika majoho mazuri ya kitani safi na mkufu wa dhahabu shingoni mwake.

43 Akampandisha katika gari lake la farasi kama msaidizi wake, watu wakatangulia wakishangilia, wakisema, “Achieni njia!” Ndivyo Farao alivyomweka Yosefu kuwa msimamizi wa nchi yote ya Misri.

44 Kisha Farao akamwambia Yosefu, “Mimi ni Farao, lakini pasipo neno lako, hakuna mtu mwenye ruhusa kuinua mkono au mguu katika nchi yote ya Misri.”

45 Farao akamwita Yosefu Safenath-Panea, pia akampa Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, kuwa mke wake. Ndipo Yosefu akaitembelea nchi yote ya Misri.

46 Yosefu alikuwa na miaka thelathini alipoingia katika utumishi wa Farao mfalme wa Misri. Naye Yosefu akatoka mbele ya Farao akasafiri katika nchi yote ya Misri.

47 Katika ile miaka saba ya neema nchi ilizaa mazao kwa wingi sana.

48 Yosefu akakusanya chakula chote kilichozalishwa katika ile miaka saba ya neema nchini Misri, akakihifadhi katika ghala za miji. Katika kila mji kulihifadhiwa chakula kilichozalishwa katika mashamba yaliyouzunguka mji huo.

49 Yosefu alihifadhi nafaka nyingi, mfano wa mchanga wa bahari, ilikuwa nyingi mno kiasi kwamba walishindwa kuweka kumbukumbu kwa sababu akiba ilizidi sana kupita kipimo.

50 Kabla ya miaka ya njaa kuanza, Asenathi binti Potifera, kuhani wa mji wa Oni, alikuwa amemzalia Yosefu wana wawili wa kiume.

51 Yosefu akamwita mzaliwa wake wa kwanza Manase, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenifanya nisahau taabu zangu zote pamoja na jamaa yote ya nyumba ya baba yangu.”

52 Mwana wa pili akamwita Efraimu, akisema, “Ni kwa sababu Mungu amenistawisha katika nchi ya mateso yangu.”

53 Ile miaka saba ya neema huko Misri ikaisha,

54 nayo miaka ile saba ya njaa ikaanza, sawasawa na alivyosema Yosefu. Kulikuwa na njaa katika nchi nyingine zote, bali katika nchi yote ya Misri kulikuwa na chakula.

55 Wakati nchi yote ya Misri ilipopatwa na njaa, watu wakamlilia Farao ili awape chakula. Ndipo Farao alipowaagiza Wamisri wote, akisema, “Nendeni kwa Yosefu, nanyi mfanye anachowaambia.”

56 Wakati njaa ilipokuwa imeenea katika nchi yote, Yosefu akafungua ghala za vyakula na kuwauzia Wamisri nafaka, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno katika nchi yote ya Misri.

57 Pia nchi nyingine zote zilikuja Misri kununua nafaka kutoka kwa Yosefu, kwa sababu njaa ilikuwa kali mno duniani kote.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/41-36eacdccb6e11fd311395303eebe2a45.mp3?version_id=1627—