Mwanzo 42

Ndugu Za Yosefu Waenda Misri

1 Wakati Yakobo alipofahamu kuwa kuna nafaka huko Misri, akawaambia wanawe, “Mbona mnakaa tu hapa mnatazamana?”

2 Akaendelea kuwaambia, “Nimesikia kuwa huko Misri kuna nafaka. Telemkeni huko mkanunue chakula kwa ajili yetu, ili tuweze kuishi wala tusife.”

3 Ndipo wale ndugu kumi wa Yosefu, wakatelemka huko Misri kununua nafaka.

4 Lakini Yakobo hakumtuma Benyamini, ndugu yake Yosefu, pamoja na wengine, kwa sababu aliogopa asije akapatwa na madhara.

5 Hivyo wana wa Israeli walikuwa miongoni mwa wale waliokwenda Misri kununua nafaka, kwani njaa ilikuwa katika nchi ya Kanaani pia.

6 Wakati huo Yosefu alikuwa mtawala wa nchi ya Misri, naye alikuwa ndiye aliyewauzia watu wote nafaka. Kwa hiyo wakati ndugu zake Yosefu walipofika, wakamsujudia hadi nyuso zao zikagusa ardhi.

7 Mara Yosefu alipowaona ndugu zake, akawatambua, lakini akajifanya mgeni na kuzungumza nao kwa ukali, akiwauliza, “Ninyi mnatoka wapi?”

Wakamjibu, “Tumetoka katika nchi ya Kanaani kuja kununua chakula.”

8 Ingawa Yosefu aliwatambua ndugu zake, wao hawakumtambua.

9 Ndipo Yosefu alipokumbuka ndoto zake kuwahusu wao, akawaambia, “Ninyi ni wapelelezi! Mmekuja kuangalia mahali ambapo nchi yetu haina ulinzi.”

10 Wakamjibu, “Sivyo bwana wangu. Watumishi wako wamekuja kununua chakula.

11 Sisi sote ni wana wa baba mmoja. Watumishi wako ni watu waaminifu, wala sio wapelelezi.”

12 Akawaambia, “La hasha! Mmekuja kuangalia mahali ambapo nchi yetu haina ulinzi.”

13 Lakini wakamjibu, “Watumishi wako walikuwa kumi na wawili, wana wa mtu mmoja ambaye anaishi katika nchi ya Kanaani. Sasa mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu na mwingine alikufa.”

14 Yosefu akawaambia, “Ni sawa kabisa kama nilivyowaambia: Ninyi ni wapelelezi!

15 Na hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Hakika kama Farao aishivyo, hamtaondoka mahali hapa mpaka ndugu yenu mdogo aje hapa.

16 Tumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu, wengine mtawekwa gerezani, ili maneno yenu yajaribiwe kuona kama mnasema kweli. La sivyo, hakika kama Farao aishivyo ninyi ni wapelelezi!”

17 Akawaweka wote chini ya ulinzi kwa siku tatu.

18 Siku ya tatu Yosefu akawaambia, “Fanyeni hili nanyi mtaishi, kwa maana namwogopa Mungu:

19 Ikiwa ninyi ni watu waaminifu, mmoja wa ndugu zenu na abaki kifungoni, nanyi wengine pelekeni nafaka kwa jamaa yenu wanaoteseka kwa njaa.

20 Lakini ni lazima mniletee ndugu yenu mdogo hapa, ili maneno yenu yathibitike na kwamba msife.” Wakakubali kufanya hivyo.

21 Wakaambiana wao kwa wao, “Hakika tunaadhibiwa kwa sababu ya ndugu yetu. Tuliona jinsi alivyohuzunika alipokuwa anatusihi kuponya maisha yake, lakini hatukumsikiliza, hiyo ndiyo sababu dhiki hii imetupata.”

22 Reubeni akawajibu, “Sikuwaambieni msitende dhambi dhidi ya kijana? Lakini hamkunisikiliza! Sasa ni lazima tuadhibiwe kwa ajili ya damu yake.”

23 Hawakujua kuwa Yosefu angewaelewa, kwa sababu alitumia mkalimani.

24 Yosefu akajitenga nao akaanza kulia, kisha akawarudia na kuzungumza nao tena. Akataka Simeoni akamatwe na kufungwa mbele yao.

25 Yosefu akatoa amri ya kujaza magunia yao nafaka na kuweka fedha ya kila mmoja ndani ya gunia lake, kisha wapewe mahitaji ya njiani. Baada ya kufanyiwa hayo yote,

26 wakapakiza nafaka juu ya punda zao, wakaondoka.

27 Walipofika mahali pa kulala huko njiani mmoja wao akafungua gunia lake ili amlishe punda wake, akakuta fedha yake kwenye mdomo wa gunia lake.

28 Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Iko ndani ya gunia langu.”

Mioyo yao ikazimia, na kila mmoja akamgeukia mwenzake wakitetemeka, wakaulizana, “Ni nini hiki Mungu alichotufanyia?”

29 Walipofika kwa Yakobo baba yao katika nchi ya Kanaani, wakamweleza mambo yote yaliyowapata. Wakasema,

30 “Huyo mtu ambaye ndiye bwana katika nchi hiyo alisema nasi kwa ukali, akatutendea kana kwamba sisi tulikuwa tunaipeleleza nchi.

31 Lakini tulimwambia, ‘Sisi ni watu waaminifu, sio wapelelezi.

32 Tulizaliwa ndugu kumi na wawili, wana wa baba mmoja. Mmoja alikufa, na mdogo wetu wa mwisho yupo na baba yetu huko Kanaani.’

33 “Ndipo huyo mtu aliye bwana katika nchi hiyo alipotuambia, ‘Hivi ndivyo nitafahamu kuwa ninyi ni watu waaminifu: Mwacheni mmoja wa ndugu zenu pamoja nami hapa, kisha nendeni mpeleke chakula kwa ajili ya jamaa yenu inayoteseka kwa njaa.

34 Lakini mleteni huyo ndugu yenu mdogo kwangu, ndipo nitajua kuwa ninyi sio wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Kisha nitamrudisha ndugu yenu, nanyi mtaweza kufanya biashara katika nchi hii.’ ”

35 Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka kwenye magunia yao, ndani ya gunia la kila mtu kulikuwa na mfuko wa fedha! Wakati wao na baba yao walipoona mifuko ya fedha, wakaogopa.

36 Yakobo baba yao akawaambia, “Ninyi mmenipokonya watoto wangu. Yosefu hayupo na Simeoni hayupo tena na sasa mnataka kumchukua Benyamini. Kila kitu ni kinyume nami!”

37 Ndipo Reubeni akamwambia baba yake, “Waweza kuwaua wanangu wote wawili, ikiwa sitamrudisha Benyamini kwako. Mkabidhi Benyamini katika uangalizi wangu, nami nitamrudisha.”

38 Lakini Yakobo akasema, “Mwanangu hatashuka huko pamoja nanyi; ndugu yake amekufa naye ndiye peke yake aliyebaki. Ikiwa atapatwa na madhara katika safari mnayoiendea, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini kwa masikitiko.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/42-f716cf5abefac26de8eab11c88302681.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 43

Safari Ya Pili Ya Kwenda Misri

1 Wakati huu njaa ilikuwa bado ni kali mno katika nchi.

2 Hivyo wakati walipokuwa wamemaliza kula nafaka yote waliyoileta kutoka Misri, Yakobo baba yao akawaambia, “Rudini Misri mkatununulie chakula kingine zaidi.”

3 Lakini Yuda akamwambia, “Mtu yule alituonya kwa msisitizo, ‘Hamtauona uso wangu tena mpaka mje na ndugu yenu.’

4 Kama utakubali ndugu yetu aende pamoja nasi, tutakwenda kuwanunulia chakula.

5 Lakini ikiwa hutamruhusu aende, hatutakwenda, kwa sababu mtu yule alituambia, ‘Hamtauona uso wangu tena mpaka mje pamoja na ndugu yenu.’ ”

6 Israeli akauliza, “Kwa nini mkaniletea taabu hii kwa kumwambia yule mtu mlikuwa na ndugu mwingine?”

7 Wakamjibu, “Yule mtu alituhoji kwa undani sana habari zetu na za jamaa yetu. Alituuliza, ‘Je, baba yenu bado yungali hai? Je mnaye ndugu mwingine?’ Sisi tulimjibu maswali yake tu. Tungewezaje kujua kwamba angesema, ‘Mleteni mdogo wenu hapa?’ ”

8 Ndipo Yuda akamwambia baba yake Israeli, “Mtume kijana pamoja nami, nasi tutaondoka mara, ili sisi na wewe pamoja na watoto wetu tuweze kuishi, wala tusife.

9 Mimi mwenyewe nitakuhakikishia usalama wake, mimi mwenyewe nitawajibika kumrudisha. Ikiwa sitamrudisha kwako na kumweka mbele yako, nitakuwa mwenye lawama mbele yako maisha yangu yote.

10 Hakika, kama hatukuchelewa kuondoka, tungekuwa tumekwenda na kurudi mara mbili.”

11 Basi baba yao Israeli akawaambia, “Kama ni lazima iwe hivyo, basi fanyeni hivi: Wekeni baadhi ya mazao bora ya nchi katika mifuko yenu na mpelekeeni yule mtu kama zawadi, zeri kidogo, asali kidogo, vikolezo, manemane, kungu na lozi.

12 Chukueni fedha mara mbili, kwa kuwa mtazirudisha zile fedha zilizowekwa midomoni mwa magunia yenu. Labda ziliwekwa kwa makosa.

13 Mchukueni ndugu yenu pia mrudi kwa huyo mtu mara moja.

14 Naye Mungu Mwenyeziawajalieni rehema mbele ya huyo mtu ili apate kumwachia yule ndugu yenu na Benyamini mweze kurudi pamoja. Kwangu mimi kama nikufiwa nimefiwa.”

15 Basi hao watu wakazichukua zile zawadi na zile fedha mara mbili pamoja na Benyamini. Wakafanya haraka kwenda Misri na walipofika wakajionyesha kwa Yosefu.

16 Yosefu alipomwona Benyamini pamoja nao, akamwambia msimamizi wa nyumba yake, “Wachukue watu hawa nyumbani kwangu, mchinje mnyama na kuandalia chakula kwa kuwa watakula chakula cha mchana pamoja nami.”

17 Yule Msimamizi akafanya kama Yosefu alivyomwambia na akawachukua wale watu nyumbani kwa Yosefu.

18 Basi watu hao wakaogopa walipopelekwa nyumbani kwa Yosefu. Wakafikiri, “Tumeletwa hapa kwa ajili ya zile fedha zilizorudishwa katika magunia yetu mara ile ya kwanza. Anataka kutushambulia na kutushinda, atuchukue sisi kama watumwa, na atwae hawa punda zetu.”

19 Hivyo wakamwendea msimamizi wa nyumba wa Yosefu na kuzungumza naye kwenye ingilio la nyumbani.

20 Wakasema, “Tafadhali bwana, tulikuja hapa mara ya kwanza kununua chakula.

21 Lakini mahali pale tulipotua wakati wa jioni tulifungua magunia yetu, na kila mmoja wetu akakuta fedha zake, kwenye mdomo wa gunia lake kiasi kile kile tulicholeta. Kwa hiyo tumezirudisha.

22 Pia tumeleta fedha nyingine kwa ajili ya kununulia chakula. Hatujui ni nani aliziweka fedha hizo katika magunia yetu.”

23 Akawaambia, “Vema msiogope. Mungu wenu, Mungu wa baba yenu, amewapa ninyi hazina katika magunia yenu; mimi nilipokea fedha yenu.” Ndipo akawaletea Simeoni.

24 Msimamizi akawapeleka wale watu katika nyumba ya Yosefu, akawapa maji ya kunawa miguu na kuwapa punda wao majani.

25 Wakaandaa zawadi zao ili wampe Yosefu wakati atakapofika adhuhuri, kwa kuwa walikuwa wamesikia kwamba watakula chakula huko.

26 Yosefu alipokuja nyumbani, walimkabidhi zile zawadi walizokuwa nazo, ambazo walikuwa wamezileta mle nyumbani, nao wakamsujudia hadi nchi.

27 Akawauliza kuhusu hali yao, kisha akawaambia, “Yule baba yenu mzee mliyeniambia habari zake, yu hali gani? Je, bado yu hai?”

28 Wakamjibu, “Mtumishi wako baba yetu bado anaishi na ni mzima.” Kisha wakainama chini kumpa heshima.

29 Alipotazama na kumwona Benyamini ndugu yake, mwana wa mama yake hasa, akauliza, “Je, huyu ndiye ndugu yenu wa mwisho, ambaye mlinieleza habari zake?” Ndipo akasema, “Mungu na akufadhili, mwanangu.”

30 Akiwa ameguswa sana kwa kumwona ndugu yake, Yosefu akatoka nje kwa haraka na kutafuta mahali pa kulilia. Akaingia kwenye chumba chake cha pekee na kulilia humo.

31 Baada ya kunawa uso wake, akatoka nje na huku akijizuia akasema, “Pakueni chakula.”

32 Wakampakulia Yosefu peke yake, ndugu zake peke yao na Wamisri waliokula pamoja naye peke yao, kwa sababu Wamisri wasingeweza kula pamoja na Waebrania, kwa maana ilikuwa ni chukizo kwa Wamisri.

33 Watu hao walikuwa wameketi mbele yake kwa mfuatano wa umri wao, kuanzia mzaliwa wa kwanza hadi mzaliwa wa mwisho, wakatazamana wao kwa wao kwa mshangao.

34 Wakati walipopelekewa sehemu ya chakula kutoka mezani mwa Yosefu, sehemu ya Benyamini ilikuwa mara tano zaidi ya sehemu ya wale wengine. Kwa hiyo wakanywa na kufurahi pamoja naye.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/43-91a8d71585b0d8808d6766c5d4a77508.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 44

Kikombe Cha Fedha Ndani Ya Gunia

1 Kisha Yosefu akampa yule msimamizi wa nyumbani mwake maagizo haya: “Jaza magunia ya watu hawa kiasi cha chakula ambacho wanaweza kuchukua, na uweke fedha ya kila mtu kwenye mdomo wa gunia lake.

2 Kisha weka kikombe changu kile cha fedha kwenye mdomo wa gunia la yule mdogo wa wote pamoja na fedha zake ambazo angenunulia nafaka yake.” Naye akafanya kama Yosefu alivyosema.

3 Kulipopambazuka, hao watu wakaruhusiwa kuondoka pamoja na punda zao.

4 Kabla hawajafika mbali kutoka mjini, Yosefu akamwambia mtumishi wake, “Wafuatilie wale watu mara moja, utakapowakuta, waambie, ‘Kwa nini mmelipiza wema kwa ubaya?

5 Je, kikombe hiki sicho anachonywea bwana wangu na pia hukitumia kwa kutabiri mambo yajayo? Hili ni jambo ovu mlilolitenda.’ ”

6 Alipowafikia, akarudia maneno haya kwao.

7 Lakini wakamwambia mtumishi, “Kwa nini bwana wangu anasema maneno kama haya? Liwe mbali na watumishi wako wasije wakafanya jambo kama hilo!

8 Hata hivyo tulikurudishia zile fedha kutoka nchi ya Kanaani ambazo tulizikuta kwenye midomo ya magunia yetu. Hivyo kwa nini tuibe fedha au dhahabu kutoka nyumbani kwa bwana wako?

9 Ikiwa ye yote miongoni mwa watumishi wako atapatikana nacho, auawe, na sisi wengine tutakuwa watumwa wa bwana wangu.”

10 Akajibu, “Vema sana; na iwe kama msemavyo. Ye yote atakayekutwa nacho atakuwa mtumwa wangu, lakini ninyi wengine mtakuwa hamna lawama.”

11 Kila mmoja wao akafanya haraka kushusha gunia lake chini na kulifungua.

12 Ndipo msimamizi akaendelea kutafuta, akianzia kwa mkubwa wa wote na akaishia kwa mdogo wa wote. Basi kikombe kikapatikana katika gunia la Benyamini.

13 Kwa jambo hili, wakararua nguo zao. Ndipo wote wakapakiza mizigo yao juu ya punda zao na kurudi mjini.

14 Yosefu alikuwa bado yuko nyumbani mwake wakati Yuda na kaka zake walipoingia, wote wakajitupa chini mbele yake.

15 Yosefu akawaambia, “Ni jambo gani hili mlilolifanya? Hamjui kuwa mtu kama mimi anaweza kufahamu mambo kwa njia ya kutabiri?”

16 Yuda akajibu, “Tutaweza kusema nini kwa bwana wangu? Tutaweza kuzungumza nini? Tutawezaje kuthibitisha kwamba hatuna hatia? Mungu amefunua hatia ya watumishi wako. Sasa sisi tu watumwa wa bwana wangu, sisi wenyewe pamoja na yule aliyepatikana na kikombe.”

17 Lakini Yosefu alisema, “Liwe mbali nami kufanya jambo kama hili! Mtu yule tu aliyekutwa na kikombe ndiye atakayekuwa mtumwa wangu. Ninyi wengine, rudini kwa baba yenu kwa amani.”

18 Ndipo Yuda akamwendea na kumwambia: “Tafadhali bwana wangu, mruhusu mtumishi wako aseme neno kwa bwana wangu. Usimkasirikie mtumishi wako, ingawa wewe ni sawa na Farao mwenyewe.

19 Bwana wangu aliwauliza watumishi wake, ‘Mnaye baba au ndugu?’

20 Nasi tukakujibu, ‘Tunaye baba yetu ambaye ni mzee; pia yupo mwanawe mdogo aliyezaliwa katika uzee wake. Ndugu yake amekufa, na huyu mdogo ndiye mwana pekee kwa mama yake aliyebaki, naye baba yake anampenda.’ ”

21 “Ndipo ulipowaambia watumishi wako, ‘Mleteni kwangu ili niweze kumwona kwa macho yangu mwenyewe.’

22 Nasi tukamwambia bwana wangu, ‘Kijana hawezi kumwacha baba yake; akimwacha, baba yake atakufa.’

23 Lakini ukawaambia watumishi wako, ‘Ndugu yenu mdogo asiposhuka pamoja nanyi, hamtauona uso wangu tena.’

24 Tuliporudi nyumbani kwa mtumwa wako baba yangu, tulimwambia lile bwana wangu alilokuwa amesema.

25 “Ndipo baba yetu aliposema, ‘Rudini Misri mkanunue chakula kingine.’

26 Lakini tukamwambia, ‘Hatuwezi kushuka Misri mpaka ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi ndipo tutakapokwenda. Hatutaweza kuuona uso wa yule mtu mpaka ndugu yetu mdogo awe pamoja nasi.’

27 “Mtumwa wako baba yangu alituambia, ‘Mnajua mke wangu alinizalia wana wawili.

28 Mmojawapo alipotea, nami nikasema, “Hakika ameraruliwa vipande vipande.” Nami sijamwona tangu wakati huo.

29 Ikiwa mtaniondolea huyu tena na akapatwa na madhara, mtashusha kichwa changu chenye mvi kaburini nikiwa mwenye huzuni.’

30 “Hivyo sasa, kama kijana hatakuwa pamoja nasi nitakaporudi kwa mtumishi wako baba yangu, na kama baba yangu, ambaye maisha yake yamefungamanishwa na uhai wa kijana huyu,

31 akiona kijana hayupo nasi, atakufa. Watumishi wako watashusha kichwa chenye mvi cha baba yetu kaburini kwa huzuni.

32 Mtumwa wako alimhakikishia baba yangu usalama wa kijana. Nikamwambia, ‘Kama sikumrudisha kwako nitakuwa mwenye lawama mbele yako, baba yangu, maisha yangu yote!’

33 “Sasa basi, tafadhali mruhusu mtumishi abaki hapa kama mtumwa wa bwana wangu badala ya kijana, naye kijana umruhusu arudi na ndugu zake.

34 Ninawezaje kurudi kwa baba yangu kama kijana hatakuwa pamoja nami? La hasha! Usiniache nikaone huzuni ile itakayompata baba yangu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/44-9d9241ff7da03cf65e7d3fade2a34a47.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 45

Yosefu Anajitambulisha

1 Hapo Yosefu hakuweza kujizuia zaidi mbele ya wote waliokuwa wamesimama karibu naye, akapaza sauti, akasema, “Mwondoeni kila mtu mbele yangu!” Kwa hiyo hapakuwepo mtu ye yote pamoja na Yosefu alipojitambulisha kwa ndugu zake.

2 Naye akalia kwa sauti kubwa kiasi kwamba Wamisri walimsikia, hata watu wa nyumbani mwa Farao wakapata hizo habari.

3 Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ni Yosefu! Je, baba yangu angali hai bado?” Lakini ndugu zake hawakuweza kumjibu, kwa sababu walipatwa na hofu kuu mbele yake.

4 Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Sogeeni karibu nami.” Waliposogea, akasema, “Mimi ni ndugu yenu Yosefu, yule ambaye mlimwuza Misri!

5 Sasa, msihuzunike wala msijichukie wenyewe kwa kuniuza huku, kwa sababu ilikuwa ni ili kuokoa maisha ya watu ndiyo sababu Mungu alinituma niwatangulie ninyi.

6 Kwa miaka miwili sasa imekuwepo njaa katika nchi, pia kwa miaka mitano ijayo hapatakuwepo kulima wala kuvuna.

7 Lakini Mungu alinitanguliza mbele yenu ili kuhifadhi mabaki kwa ajili yenu katika nchi, na kuokoa maisha yenu kwa wokovu mkuu.

8 “Kwa hiyo basi, si ninyi mlionileta huku, bali ni Mungu. Alinifanya kuwa baba kwa Farao, bwana wa watu wa nyumbani mwake wote, na mtawala wa Misri yote.

9 Sasa rudini haraka kwa baba yangu na mwambieni, ‘Hili ndilo mwanao Yosefu asemalo: Mungu amenifanya mimi kuwa bwana wa Misri yote. Shuka uje kwangu, wala usikawie.

10 Nawe utaishi katika nchi ya Gosheni na kuwa karibu nami, wewe, watoto wako na wajukuu wako, makundi yako ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, pamoja na vyote ulivyo navyo.

11 Nitawatunza huko, kwa sababu bado iko miaka mingine mitano inayokuja ya njaa. La sivyo, wewe na nyumba yako na wote ulionao mtakuwa fukara.’

12 “Mnaweza kujionea wenyewe, hata ndugu yangu Benyamini, kwamba hakika ni mimi ninayezungumza nanyi.

13 Mwambieni baba yangu juu ya heshima yote niliyopewa huku Misri, na kuhusu kila kitu mlichokiona. Mleteni baba yangu huku haraka.”

14 Ndipo akamkumbatia Benyamini ndugu yake na kulia, naye Benyamini akamkumbatia akilia.

15 Pia akawabusu ndugu zake wote, huku akilia. Baada ya hayo ndugu zake wakazungumza naye.

16 Habari zilipofika kwenye jumba la kifalme la Farao kwamba ndugu zake Yosefu wamefika, Farao na maafisa wake wote wakafurahi.

17 Farao akamwambia Yosefu, “Waambie ndugu zako, ‘Fanyeni hivi: Pakieni wanyama wenu mrudi mpaka nchi ya Kanaani,

18 mkamlete baba yenu na jamaa zenu kwangu. Nitawapa sehemu nzuri sana ya nchi ya Misri nanyi mtafurahia unono wa nchi.’

19 “Mnaagizwa pia kuwaambia, ‘Fanyeni hivi: Chukueni magari ya kukokotwa kutoka Misri, kwa ajili ya watoto wenu na wake zenu, mkamchukue baba yenu mje.

20 Msijali kamwe kuhusu mali zenu, kwa sababu mema yote ya Misri yatakuwa yenu.’ ”

21 Hivyo wana wa Israeli wakafanya hivyo. Yosefu akawapa magari ya kukokotwa, kama Farao alivyoagiza, pia akawapa mahitaji kwa ajili ya safari yao.

22 Kila mmoja mavazi mapya, lakini Benyamini akampa shekeli 300za fedha, na jozi tano za nguo.

23 Hivi ndivyo vitu alivyotuma kwa baba yake: punda kumi waliochukua vitu vizuri vya Misri, punda wake kumi waliobeba nafaka, mikate na mahitaji mengine ya safari.

24 Akaagana na ndugu zake walipokuwa wakiondoka, akawaambia, “Msigombane njiani!”

25 Basi wakatoka Misri na kufika kwa baba yao Yakobo katika nchi ya Kanaani.

26 Wakamwambia baba yao, “Yosefu angali hai! Ukweli ni kwamba yeye ndiye mtawala wa Misri yote.” Yakobo akapigwa na bumbuwazi; hakuwasadiki.

27 Lakini walipokwisha kumweleza kila kitu ambacho Yosefu alikuwa amewaambia, na alipoona magari ya kukokotwa Yosefu aliyokuwa amempelekea ya kumchukua aende Misri, roho ya baba yao Yakobo ikahuishwa.

28 Ndipo Israeli akasema, “Nimesadiki! Mwanangu Yosefu bado yu hai. Nitakwenda nikamwone kabla sijafa.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/45-bf3981daf189bdd4486645818240288e.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 46

Yakobo Aenda Misri

1 Hivyo Israeli akaondoka na vyote vilivyokuwa mali yake, naye alipofika Beer-Sheba, akamtolea dhabihu Mungu wa Isaki baba yake.

2 Mungu akanena na Israeli katika maono usiku na kusema, “Yakobo! Yakobo!”

Akajibu, “Mimi hapa.”

3 Mungu akamwambia, “Mimi ndimi Mungu wa baba yako, usiogope kushuka Misri, kwa maana huko nitakufanya taifa kubwa.

4 Nitashuka Misri pamoja nawe, nami hakika nitakurudisha tena Kanaani. Mikono ya Yosefu mwenyewe ndiyo itakayofunga macho yako.”

5 Ndipo Yakobo akaondoka Beer-Sheba nao wana wa Israeli wakamchukua baba yao Yakobo na watoto wao na wake zao katika magari ya kukokotwa yale Farao aliyokuwa amempelekea kumsafirisha.

6 Wakachukua pia mifugo yao na mali walizokuwa wamezipata Kanaani, Yakobo na uzao wake wote wakashuka Misri.

7 Akawachukua wanawe na binti zake, wajukuu wake wa kiume na wa kike, yaani uzao wake wote mpaka Misri.

8 Haya ndiyo majina ya wana wa Israeli (Yakobo na wazao wake), waliokwenda Misri:

Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Yakobo.

9 Wana wa Reubeni ni:

Hanoki, Palu, Hesroni na Karmi.

10 Wana wa Simeoni ni:

Yemueli, Yamini, Ohadi, Yakini, Sohari na Shauli mwana wa mwanamke Mkanaani.

11 Wana wa Lawi ni:

Gershoni, Kohathi na Merari.

12 Wana wa Yuda ni:

Eri, Onani, Shela, Peresi na Zera (lakini Eri na Onani walifariki katika nchi ya Kanaani).

Wana wa Peresi ni:

Hesroni na Hamuli.

13 Wana wa Isakari ni:

Tola, Puva, Yashubu na Shimroni.

14 Wana wa Zabuloni ni:

Seredi, Eloni na Yaleeli.

15 Hawa ndio wana wa Lea aliomzalia Yakobo huko Padan-Aramu pamoja na binti yake Dina. Jumla ya wanawe na binti zake walikuwa thelathini na watatu.

16 Wana wa Gadi ni:

Sefoni, Hagi, Shuni, Esboni, Eri, Arodi na Areli.

17 Wana wa Asheri ni:

Imna, Ishva, Ishvi na Beria.

Dada yao alikuwa Sera.

Wana wa Beria ni:

Heberi na Malkieli.

18 Hawa ndio watoto Zilpa aliomzalia Yakobo, ambao Labani alimpa binti yake Lea; jumla yao walikuwa kumi na sita.

19 Wana wa Raheli mke wa Yakobo ni:

Yosefu na Benyamini.

20 Huko Misri, Asenathi binti wa Potifera, aliyekuwa kuhani wa mji wa Oni, alimzalia Yosefu wana wawili, Manase na Efraimu.

21 Wana wa Benyamini ni:

Bela, Bekeri, Ashbeli, Gera, Naamani, Ehi, Roshi, Mupimu, Hupimu na Ardi.

22 Hawa ndio wana wa Raheli aliomzalia Yakobo; jumla yao ni kumi na wanne.

23 Mwana wa Dani ni:

Hushimu.

24 Wana wa Naftali ni:

Yasieli, Guni, Yeseri na Shilemu.

25 Hawa walikuwa wana wa Bilha aliomzalia Yakobo, ambaye Labani alikuwa amempa Raheli binti yake; jumla yao walikuwa saba.

26 Wote waliokwenda Misri pamoja na Yakobo, ambao walikuwa wazao wake hasa pasipo kuhesabu wakwe zake, walikuwa watu sitini na sita.

27 Pamoja na wana wawili waliozaliwa na Yosefu huko Misri, jumla yote ya jamaa ya Yakobo, waliokwenda Misri, walikuwa sabini.

28 Basi Yakobo akamtanguliza Yuda aende kwa Yosefu ili amwelekeze njia ya Gosheni. Walipofika nchi ya Gosheni,

29 gari kubwa zuri la Yosefu liliandaliwa, naye akaenda Gosheni kumlaki baba yake Israeli. Mara Yosefu alipofika mbele yake, alimkumbatia baba yake, akalia kwa muda mrefu.

30 Israeli akamwambia Yosefu, “Sasa niko tayari kufa, kwa kuwa nimejionea mwenyewe kwamba bado uko hai.”

31 Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake na watu wa nyumbani mwa baba yake, “Nitapanda kwa Farao na kumwambia, ‘Ndugu zangu na watu wa nyumbani mwa baba yangu, ambao walikuwa wakiishi katika nchi ya Kanaani, wamekuja kwangu.

32 Watu hao ni wachunga mifugo, huchunga mifugo, wamekuja na makundi ya kondoo, mbuzi na ng’ombe pamoja na kila kitu walichonacho.’

33 Farao atakapowaita na kuwaulizeni, ‘Kazi yenu ni nini?’

34 Mjibuni, ‘Watumwa wako wamekuwa wachunga mifugo tangu ujana wetu mpaka sasa, kama baba zetu walivyofanya.’ Ndipo mtakaporuhusiwa kukaa katika nchi ya Gosheni, kwa kuwa wachunga mifugo wote ni chukizo kwa Wamisri.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/46-21a533b50215b06d21d8790e80799cbc.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 47

Yakobo Ambariki Farao

1 Yosefu akaenda na kumwambia Farao, “Baba yangu na ndugu zangu wamekuja kutoka nchi ya Kanaani wakiwa na makundi yao ya kondoo, mbuzi na ng’ombe, pamoja na kila kitu walichonacho, nao sasa wapo huko Gosheni.”

2 Akachagua ndugu zake watano na kuwaonyesha kwa Farao.

3 Farao akawauliza hao ndugu zake, “Kazi yenu ni nini?”

Wakamjibu, “Watumishi wako ni wachunga mifugo, kama vile baba zetu walivyokuwa.”

4 Pia wakamwambia, “Tumekuja kukaa huku kwa muda mfupi, kwa sababu njaa ni kali huko Kanaani, na mifugo ya watumishi wako haina malisho. Kwa hiyo sasa, tafadhali uruhusu watumishi wako wakae huko Gosheni.”

5 Farao akamwambia Yosefu, “Baba yako na ndugu zako wamekuja kwako,

6 nayo nchi ya Misri ipo mbele yako, uwakalishe baba yako na ndugu zako katika sehemu iliyo bora kupita zote katika nchi. Na waishi Gosheni. Kama unamfahamu ye yote miongoni mwao mwenye uwezo maalum, waweke wawe wasimamizi wa mifugo yangu.”

7 Ndipo Yosefu akamleta Yakobo baba yake na kumtambulisha mbele ya Farao. Baada ya Yakobo kumbariki Farao,

8 Farao akamwuliza, “Je una umri gani?”

9 Naye Yakobo akamwambia Farao, “Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni miaka 130. Miaka yangu imekuwa michache na ya taabu, wala haikufikia miaka ya kusafiri ya baba zangu.”

10 Kisha Yakobo akambariki Farao, naye akaondoka mbele ya uso wake.

11 Ndipo Yosefu akawakalisha baba yake na ndugu zake katika nchi ya Misri na kuwapa milki katika sehemu bora sana ya nchi, wilaya ya Ramesesi, kama Farao alivyoelekeza.

12 Pia Yosefu akampa baba yake, na ndugu zake na wote wa nyumbani mwa baba yake vyakula, kwa kulingana na hesabu ya watoto wao.

Uongozi Wa Yosefu Wakati Wa Njaa

13 Hata hivyo, hapakuwepo chakula katika sehemu yote kwa kuwa njaa ilikuwa kali sana; Misri na Kanaani zote zikaharibiwa kwa sababu ya njaa.

14 Yosefu akakusanya fedha zote zilizopatikana kutoka katika mauzo ya nafaka huko Misri na Kanaani, akazileta kwenye jumba la kifalme la Farao.

15 Fedha za watu wa Misri na Kanaani zilipokwisha, Wamisri wote wakamjia Yosefu na kumwambia, “Tupatie chakula. Kwa nini tufe mbele ya macho yako? Fedha zetu zimekwisha.”

16 Yosefu akawaambia, “Basi leteni mifugo yenu, nitawauzia chakula kwa kubadilisha na mifugo yenu, kwa kuwa fedha zenu zimekwisha.”

17 Kwa hiyo wakaleta mifugo yao kwa Yosefu, naye akawapa chakula kwa kubadilishana na farasi zao, kondoo na mbuzi zao, ng’ombe na punda zao. Katika mwaka huo wote Yosefu akawapa chakula kwa kubadilishana na mifugo yao yote.

18 Mwaka ule ulipokwisha, wakamjia mwaka uliofuata na kumwambia, “Hatuwezi kuficha ukweli mbele za bwana wetu kwamba, kwa kuwa fedha zetu zimekwisha na wanyama wetu ni mali yako, sasa hakuna cho chote kilichosalia kwa ajili ya bwana wetu isipokuwa miili yetu na ardhi yetu.

19 Kwa nini tuangamie mbele ya macho yako, sisi pamoja na nchi yetu? Utununue sisi pamoja na ardhi yetu ili kubadilishana kwa chakula. Nasi pamoja na nchi yetu tutakuwa watumwa wa Farao. Tupe sisi mbegu ili tuweze kuishi wala tusife, nchi yetu isije ikawa ukiwa.”

20 Kwa hiyo Yosefu akamnunulia Farao nchi yote ya Misri. Wamisri, mmoja baada ya mwingine, waliuza mashamba yao, kwa sababu njaa ilikuwa kali sana kwao. Nchi ikawa mali ya Farao,

21 naye Yosefu akawafanya watu watumike kama watumwa, kuanzia upande mmoja wa Misri hadi upande mwingine.

22 Hata hivyo, hakununua nchi ya makuhani, kwa sababu walikuwa wanapata mgawo wao wa kawaida kutoka kwa Farao, nao walikuwa na chakula cha kuwatosha kutokana na mgawo waliopewa na Farao. Hii ndiyo sababu hawakuuza ardhi yao.

23 Yosefu akawaambia watu, “Kwa vile nimewanunua ninyi pamoja na nchi yenu leo kuwa mali ya Farao, hapa kuna mbegu kwa ajili yenu ili mweze kuziotesha.

24 Lakini wakati mazao yatakapokuwa tayari, mpeni Farao sehemu ya tano. Sehemu hizo nne zitakazobaki mtaziweka kama mbegu kwa ajili ya mashamba na kwa ajili ya chakula chenu wenyewe na cha watu wa nyumbani mwenu na watoto wenu.”

25 Wakamwambia, “Umeokoa maisha yetu. Basi na tupate kibali mbele ya macho ya bwana wetu; tutakuwa watumwa wa Farao.”

26 Basi Yosefu akaiweka iwe sheria kuhusu nchi ya Misri, ambayo inatumika mpaka leo, kwamba, sehemu ya tano ya mazao ni mali ya Farao. Ni nchi ya makuhani tu ambayo haikuwa ya Farao.

27 Basi Waisraeli wakaishi Misri katika nchi ya Gosheni. Wakapata mali huko wakastawi na kuongezeka kwa wingi sana.

28 Yakobo akaishi Misri miaka kumi na saba, nayo miaka ya maisha yake ilikuwa 147.

29 Wakati ulipokaribia wa Israeli kufa, akamwita mwanawe Yosefu na kumwambia, “Kama nimepata kibali machoni pake, weka mkono wako chini ya paja langu na uniahidi kuwa utanifanyia fadhili na uaminifu. Usinizike Misri,

30 lakini nitakapopumzika na baba zangu, unichukue kutoka Misri, ukanizike walipozikwa.”

Yosefu akamwambia, “Nitafanya kama unavyosema.”

31 Akamwambia, “Niapie.” Ndipo Yosefu akamwapia, naye Israeli akaabudu, akijiegemeza kwenye mchago wa kitanda chake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/47-fad0628644bf4a49c26704b5981feddd.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 48

Manase Na Efraimu

1 Baada ya muda Yosefu akaambiwa kwamba, “Baba yako ni mgonjwa.” Kwa hiyo akawachukua wanawe wawili Manase na Efraimu, pamoja naye.

2 Yakobo alipoambiwa, “Mwanao Yosefu amekujia kukuona,” Israeli akakusanya nguvu zake, akaketi kitandani.

3 Yakobo akamwambia Yosefu, “Mungu Mwenyezialinitokea huko Luzu katika nchi ya Kanaani, huko akanibariki,

4 naye akaniambia, ‘Nitakufanya ustawi na kuongezeka hesabu yako, nitakufanya kuwa jamii ya mataifa, nami nitakupa nchi hii uimiliki milele wewe na wazao wako baada yako.’

5 “Sasa basi, wanao wawili waliozaliwa kwako huku Misri kabla sijaja hapa kwako watahesabiwa kuwa ni wangu; Efraimu na Manase watakuwa wangu, kama vile Reubeni na Simeoni walivyo wangu.

6 Lakini watoto utakaowazaa baada yao watakuwa wako. Katika nchi watakayoirithi, watatambuliwa kwa jina la ndugu zao.

7 Nilipokuwa ninarudi kutoka Padani, katika huzuni yangu Raheli alifariki katika nchi ya Kanaani tulipokuwa tungali tukisafiri, tukiwa karibu kufika Efrathi. Kwa hiyo nilimzika huko, kando ya njia iendayo Efrathi” (yaani Bethlehemu).

8 Wakati Israeli alipowaona wana wa Yosefu, akauliza, “Hawa ni nani?”

9 Yosefu akamjibu baba yake, “Hawa ni wana ambao Mungu amenipa nikiwa huku.”

Ndipo Israeli akasema, “Walete kwangu ili niwabariki.”

10 Basi macho ya Israeli yalikuwa hayaoni vizuri kwa sababu ya uzee, naye aliona kwa shida. Kwa hiyo Yosefu akawaleta wanawe karibu na baba yake, Israeli akawabusu na akawakumbatia.

11 Israeli akamwambia Yosefu, “Kamwe sikutazamia kuuona uso wako tena, lakini sasa Mungu ameniruhusu kuwaona watoto wako pia.”

12 Ndipo Yosefu akawaondoa wanawe magotini mwa Israeli naye akasujudu hadi nchi.

13 Yosefu akachukua wale wana wawili, Efraimu kwenye mkono wake wa kuume akimwelekeza kwenye mkono wa kushoto wa Israeli, na Manase katika mkono wake wa kushoto akimwelekeza kwenye mkono wa kuume wa Israeli, akawaleta karibu na babu yao.

14 Lakini Israeli akaupeleka mkono wake wa kuume, akauweka juu ya kichwa cha Efraimu, ingawa alikuwa ndiye mdogo, na mkono wake wa kushoto akaukatisha, akauweka juu ya kichwa cha Manase, ingawa Manase alikuwa ndiye mzaliwa wa kwanza.

15 Ndipo akambariki Yosefu akisema,

“Mungu ambaye baba zangu

Abrahamu na Isaki walimtii,

Mungu ambaye amekuwa mchungaji

wa maisha yangu yote mpaka leo hii,

16 Malaika ambaye aliniokoa kutoka katika madhara yote,

yeye na awabariki vijana hawa.

Na waitwe kwa jina langu

na kwa majina ya baba zangu Abrahamu na Isaki,

wao na waongezeke kwa wingi

katika dunia.”

17 Yosefu alipoona baba yake akiweka mkono wa kuume juu ya kichwa cha Efraimu, hakupendezwa, kwa hiyo akauchukua mkono wa baba yake kutoka kichwa cha Efraimu na kuuweka juu ya kichwa cha Manase.

18 Yosefu akamwambia, “Hapana, baba yangu, huyu ndiye mzaliwa wa kwanza; uweke mkono wako wa kuume juu ya kichwa chake.”

19 Lakini baba yake akakataa, akasema, “Ninajua, mwanangu, ninajua. Yeye pia atakuwa taifa, naye pia atakuwa mkuu. Hata hivyo, ndugu yake mdogo atakuwa mkuu kuliko yeye, nao wazao wake watakuwa kundi la mataifa.”

20 Akawabarikia siku ile na kusema,

“Kwa jina lenu Israeli watatamka baraka hii:

‘Mungu na awafanye kama Efraimu na Manase.’ ”

Kwa hiyo akamtanguliza Efraimu mbele ya Manase.

21 Ndipo Israeli akamwambia Yosefu, “Mimi ninakaribia kufa, lakini Mungu atakuwa pamoja nanyi, na atawarudisha katika nchi ya baba zenu.

22 Kwako wewe, kama aliye juu ya ndugu zako, ninakupa sehemu moja zaidi ya ndugu zako, lile eneo nililoteka kwa Waamori kwa upanga wangu na upindi wangu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/48-bf9c02c702cb52f4b46a09b11ba9e675.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 49

Yakobo Abariki Wanawe

1 Ndipo Yakobo akawaita wanawe na kusema: “Kusanyikeni kunizunguka ili niweze kuwaambia lile litakalowatokea siku zijazo.

2 “Kusanyikeni na msikilize, enyi wana wa Yakobo,

msikilizeni baba yenu Israeli.

3 “Reubeni, wewe ni mzaliwa wangu wa kwanza,

nguvu zangu, tunda la kwanza la nguvu zangu,

umepita kwa heshima, umepita kwa uwezo.

4 Usiyezuiwa kama maji, basi hutakuwa mkuu tena,

kwa kuwa ulipanda kwenye kitanda cha baba yako,

kwenye kitanda changu na kukinajisi.

5 “Simeoni na Lawi ni wana ndugu:

panga zao ni silaha za jeuri.

6 Mimi na nisiingie katika baraza lao,

nami nisiunganike katika kusanyiko lao,

kwa kuwa wamewaua watu katika hasira yao,

walikata mishipa ya miguu ya mafahali

kama walivyopenda.

7 Hasira yao na ilaaniwe, kwa kuwa ni kali mno,

nayo ghadhabu yao ni ya ukatili!

Nitawatawanya katika Yakobo

Na kuwasambaza katika Israeli.

8 “Yuda, ndugu zako watakusifu;

mkono wako utakuwa shingoni mwa adui zako;

wana wa baba yako watakusujudia.

9 Ee Yuda, wewe ni mwana simba;

unarudi toka mawindoni, mwanangu.

Kama simba hunyemelea na kulala chini,

kama simba jike: nani athubutuye kumwamsha?

10 Fimbo ya ufalme haitaondoka kwa Yuda,

wala fimbo ya mtawala kati ya miguu yake,

hadi aje yeye ambaye milki ni yake,

ambaye utii wa mataifa ni wake.

11 Atamfunga punda wake katika mzabibu,

naye mwana punda wake kwenye tawi lililo bora zaidi;

atafua mavazi yake katika divai,

majoho yake katika damu ya mizabibu.

12 Macho yake yatakuwa mekundu kwa divai,

meno yake yatakuwa meupe kwa maziwa.

13 “Zabuloni ataishi pwani ya bahari

na kuwa bandari za kuegesha meli;

mpaka wake utapanuka kuelekea Sidoni.

14 “Isakari ni punda mwenye nguvu

ambaye amelala kati ya mizigo yake.

15 Aonapo palivyo pazuri mahali pake pa kupumzika

na jinsi nchi yake inavyopendeza,

atainamisha bega lake kwenye mzigo

na kujitolea kwa ajili ya kazi ngumu.

16 “Dani atahukumu watu wake kwa haki

kama mmoja wa makabila ya Israeli.

17 Dani atakuwa nyoka kando ya barabara,

nyoka mwenye sumu kando ya njia,

yule aumaye visigino vya farasi

ili yule ampandaye aanguke chali.

18 “EeBwana, nautafuta wokovu wako.

19 “Gadi atashambuliwa ghafula na kundi la washambuliaji,

lakini yeye atawageukia na kuwashinda kabisa.

20 “Chakula cha Asheri kitakuwa kinono,

naye atatoa chakula kitamu kimfaacho mfalme.

21 “Naftali ni kulungu jike aliyeachiwa huru

azaaye watoto wazuri.

22 “Yosefu ni mzabibu uzaao,

mzabibu uzaao ulio kando ya chemchemi,

ambao matawi yake hutanda ukutani.

23 Kwa uchungu wapiga mshale walimshambulia,

wakampiga mshale kwa ukatili.

24 Lakini upindi wake ulibaki imara,

mikono yake ikatiwa nguvu,

na mkono wa Mwenye Nguvu wa Yakobo,

kwa sababu ya Mchungaji, Mwamba wa Israeli,

25 kwa sababu ya Mungu wa baba yako, anayekusaidia,

# kwa sababu ya Mwenyezi, yeye anayekubariki

kwa baraka za mbinguni juu,

baraka za kilindi kilichoko chini,

baraka za matitini na za tumbo la uzazi.

26 Baraka za baba yako ni kubwa

kuliko baraka za milima ya kale,

nyingi kuliko vilima vya kale.

Baraka hizo zote na zikae juu ya kichwa cha Yosefu,

juu ya paji la mwana wa kifalme miongoni mwa ndugu zake.

27 “Benyamini ni mbwa mwitu mlafi mwenye njaa kuu;

asubuhi hurarua mawindo yake,

jioni hugawa nyara.”

28 Haya yote ndiyo makabila kumi na mawili ya Israeli, na hivi ndivyo baba yao alivyowaambia alipowabariki, akimpa kila mmoja baraka inayomfaa.

Kifo Cha Yakobo

29 Ndipo alipowapa maelekezo haya: “Mimi niko karibu kukusanywa kwa watu wangu. Mnizike pamoja na baba zangu kwenye pango katika shamba la Efroni, Mhiti,

30 pango lililoko katika shamba la Makpela, karibu na Mamre huko Kanaani, ambalo Abrahamu alinunua kwa ajili ya mahali pa kuzikia kutoka kwa Efroni, Mhiti, pamoja na shamba.

31 Huko ndiko Abrahamu na Sara mkewe walikozikwa, huko akazikwa Isaki na Rebeka mkewe, na huko nilimzika Lea.

32 Shamba hilo na pango lililoko ndani yake lilinunuliwa kutoka kwa Wahiti.”

33 Baada ya Yakobo kumaliza kutoa maelekezo hayo kwa wanawe, akarudisha miguu yake kitandani, akapumua pumzi ya mwisho, na akakusanywa kwa watu wake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/49-c4739edacb2ac23d2046668a930d780b.mp3?version_id=1627—

Mwanzo 50

1 Basi Yosefu akamwangukia baba yake, akalilia juu yake na akambusu.

2 Ndipo Yosefu akawaagiza matabibu waliokuwa wakimhudumia, wamtie baba yake Israeli dawa ili asioze. Hivyo matabibu wakamtia dawa asioze,

3 wakatumia siku arobaini, kwa maana ndio muda uliotakiwa wa kutia dawa ili asioze. Nao Wamisri wakamwombolezea Yakobo kwa siku sabini.

4 Siku za kumwombolezea zilipokwisha, Yosefu akawaambia washauri wa Farao, “Kama nimepata kibali machoni penu semeni na Farao kwa ajili yangu. Mwambieni,

5 ‘Baba yangu aliniapisha na kuniambia, “Mimi niko karibu kufa; unizike katika kaburi lile nililochimba kwa ajili yangu mwenyewe katika nchi ya Kanaani.” Sasa nakuomba uniruhusu niende kumzika baba yangu, nami nitarudi.’ ”

6 Farao akasema, “Panda, uende kumzika baba yako, kama alivyokuapiza kufanya.”

7 Hivyo Yosefu akapanda kwenda kumzika baba yake. Maafisa wote wa Farao wakaenda pamoja naye, watu mashuhuri wa baraza lake na watu mashuhuri wote wa Misri.

8 Hawa ni mbali na watu wote wa nyumbani kwa Yosefu, na ndugu zake, na wale wote wa nyumbani mwa baba yake. Ni watoto wao, makundi yao ya kondoo, mbuzi na ng’ombe tu waliobakia katika nchi ya Gosheni.

9 Magari makubwa na wapanda farasi pia walipanda pamoja naye. Likawa kundi kubwa sana.

10 Walipofika kwenye sakafu ya kupuria nafaka ya Atadi, karibu na Yordani, wakalia kwa sauti na kwa uchungu; Yosefu akapumzika huko kwa siku saba kumwombolezea baba yake.

11 Wakanaani walioishi huko walipoona maombolezo yaliyofanyika katika sakafu ile ya kupuria ya Atadi, wakasema, “Wamisri wanafanya maombolezo makubwa.” Kwa hiyo mahali pale karibu na Yordani pakaitwa Abel-Mizraimu.

12 Hivyo wana wa Yakobo wakafanya kama baba yao alivyowaagiza:

13 Wakamchukua mpaka nchi ya Kanaani, wakamzika kwenye pango katika shamba la Makpela, karibu na Mamre, ambalo Abrahamu alilinunua kutoka kwa Efroni, Mhiti, pamoja na shamba liwe mahali pa kuzikia.

14 Baada ya Yosefu kumzika baba yake, akarudi Misri pamoja na ndugu zake na wale wote waliokuwa wamekwenda naye kumzika baba yake.

Yosefu Awaondolea Ndugu Zake Mashaka

15 Ndugu zake Yosefu walipoona kwamba baba yao amekufa, wakasema, “Itakuwaje kama Yosefu ataweka kinyongo dhidi yetu na kutulipa mabaya yote tuliyomtendea?”

16 Kwa hiyo wakampelekea Yosefu ujumbe, wakasema, “Kabla baba yako hajafa aliacha maagizo haya:

17 ‘Hili ndilo mtakalomwambia Yosefu: Ninakuomba uwasamehe ndugu zako dhambi na mabaya kwa vile walivyokutenda vibaya.’ Sasa tafadhali samehe dhambi za watumishi wa Mungu wa baba yako.” Ujumbe huu ulipomfikia, Yosefu akalia.

18 Ndipo ndugu zake wakaja na kujitupa chini mbele yake. Wakasema, “Sisi ni watumwa wako.”

19 Lakini Yosefu akawaambia, “Msiogope. Je, mimi ni badala ya Mungu?

20 Mlikusudia kunidhuru, lakini Mungu alikusudia mema, ili litimie hili linalofanyika sasa, kuokoa maisha ya watu wengi.

21 Hivyo basi, msiogope. Mimi nitawatunza ninyi nyote pamoja na watoto wenu.” Akawahakikishia na kusema nao kwa wema.

Kifo Cha Yosefu

22 Yosefu akakaa katika nchi ya Misri, yeye pamoja na jamaa yote ya baba yake. Akaishi miaka 110,

23 naye akaona kizazi cha tatu cha watoto wa Efraimu. Pia akaona watoto wa Makiri mwana wa Manase, wakawekwa magotini mwa Yosefu walipozaliwa.

24 Ndipo Yosefu akawaambia ndugu zake, “Mimi ninakaribia kufa. Lakini kwa hakika Mungu atawasaidia na kuwachukueni kutoka nchi hii na kuwapeleka katika nchi aliyomwahidi kwa kiapo Abrahamu, Isaki na Yakobo.”

25 Naye Yosefu akawaapisha wana wa Israeli na kuwaambia, “Hakika Mungu atawasaidia, nanyi ni lazima mhakikishe mmepandisha mifupa yangu kutoka mahali hapa.”

26 Kwa hiyo Yosefu akafa akiwa na umri wa miaka 110. Baada ya kumtia dawa ili asioze, akawekwa kwenye jeneza huko Misri.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/GEN/50-667ade373a42969c43134e5046ee63bb.mp3?version_id=1627—