1 Wakorintho 2

Kumtangaza Kristo Aliyesulibiwa

1 Ndugu zangu nilipokuja kwenu, sikuja na maneno ya ushawishi wala hekima ya hali ya juu nilipowahubiria siri ya Mungu.

2 Kwa kuwa niliamua kutokujua kitu cho chote wakati nikiwa nanyi isipokuwa Yesu Kristo, naye amesulibiwa msalabani.

3 Mimi nilikuja kwenu nikiwa dhaifu na mwenye hofu na kwa kutetemeka sana.

4 Kuhubiri kwangu na ujumbe wangu haukuwa kwa hekima na maneno ya kuwashawishi watu, bali kwa madhihirisho ya nguvu za Roho Mtakatifu

5 ili imani yenu isiwe imejengwa katika hekima ya wanadamu bali katika nguvu za Mungu.

Hekima Ya Kweli Itokayo Kwa Mungu

6 Lakini miongoni mwa watu waliokomaa twanena hekima, wala si hekima ya ulimwengu huu au ya watawala wa dunia hii wanaobatilika.

7 Sisi tunanena hekima ya Mungu ambayo ni siri, tena iliyofichika kwa wanadamu, ambayo Mungu aliikusudia kabla ya ulimwengu kuwepo, kwa ajili ya utukufu wetu.

8 Hakuna hata mtawala mmoja wa nyakati zetu aliyeelewa jambo hili. Kwa maana kama wangelielewa, wasingemsulibisha Bwana wa utukufu.

9 Lakini ni kama ilivyoandikwa:

“Lile jambo ambalo jicho halijapata kuona,

sikio halijapata kusikia,

wala halikuingia moyoni,

lile ambalo Mungu aliwaandalia

wale wampendao”:

10 Lakini mambo haya Mungu ametufunulia kwa njia ya Roho wake.

Roho huchunguza kila kitu, hata mambo ya ndani sana ya Mungu.

11 Kwa maana ni nani anayejua mawazo ya mtu isipokuwa roho iliyo ndani ya huyo mtu? Vivyo hivyo hakuna mtu ajuaye mawazo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu.

12 Basi hatukupokea roho ya dunia bali Roho yule atokaye kwa Mungu, ili tuweze kuelewa kile kipawa ambacho Mungu ametupatia bure.

13 Haya ndiyo tusemayo, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya wanadamu bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua kweli za kiroho kwa wale watu wa kiroho.

14 Mtu ambaye hana Roho wa Mungu hawezi kupokea mambo yatokayo kwa Roho wa Mungu, kwa kuwa ni upuzi kwake, naye hawezi kuyaelewa kwa sababu hayo yanaeleweka tu kwa jinsi ya rohoni.

15 Mtu wa kiroho hutambua mambo yote, lakini yeye mwenyewe hatambuliwi na mtu ye yote.

16 “Kwa maana ni nani aliyejua nia ya Bwana

ili apate kumfundisha?”

Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1CO/2-019a5eb9aac018c4124ae9e76d9aafcf.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

nine + twelve =