Ayubu 24

Ayubu Analalamikia Jeuri Duniani

1 “Kwa nini Mwenyezi asiweke nyakati kwa ajili ya hukumu?

Kwa nini wale wamjuao wazitafute

siku kama hizo bila mafanikio?

2 Watu husogeza mawe ya mpaka;

huchunga makundi ya wanyama

waliyonyang’anya kwa nguvu.

3 Huwanyang’anya yatima punda wao

na kumchukua rehani fahali wa mjane.

4 Humsukuma mhitaji kutoka katika njia

na kuwafanya maskini wote wa nchi

kulazimika kujificha.

5 Kama punda-mwitu jangwani,

maskini huzunguka katika kazi zao

wakitafuta chakula;

mahali pasipokaliwa na watu wala kulimika

hupata chakula cha watoto wao.

6 Hukusanya chakula mashambani

na kuokota masazo

katika mashamba ya mizabibu ya waovu.

7 Kwa kukosa nguo, usiku kucha hukaa bila nguo,

hawana cho chote cha kujifunika baridi.

8 Hutota kwa mvua za mlimani,

nao huikumbatia miamba kwa ajili ya kukosa pa kujisitiri.

9 Watoto wasio na baba hupokonywa matitini;

watoto wachanga wa maskini hukamatwa kwa nguvu

kwa ajili ya deni.

10 Kwa kukosa nguo, hutembea uchi;

hubeba miganda ya ngano, lakini huwa na njaa.

11 Hukamua zeituni katika mawe ya kusagia,

hukanyaga mashinikizo,

lakini wanaona kiu.

12 Kilio cha huzuni cha wanaokufa kinapaa kutoka mjini,

nazo nafsi za waliojeruhiwa zinalilia msaada.

Lakini Mungu hamlaumu mtu ye yote

kwa kutenda mabaya.

13 “Wako wale wanaoiasi nuru,

wasiofahamu njia zake

wala hawakai katika mapito yake.

14 Wakati mwanga wa mchana unapotoweka,

mwuaji huinuka naye huwaua maskini na mhitaji,

wakati wa usiku huiba kama mwivi.

15 Jicho la mzinzi hungojea wakati wa giza,

naye hufikiri, ‘Hakuna jicho litakaloniona,’

naye huuficha uso wake.

16 Katika giza, huvunja majumba,

lakini wakati wa mchana hujifungia ndani,

hawataki kufanya lo lote nuruni.

17 Kwa wote hawa, giza nene ndiyo asubuhi yao,

hujifanya rafiki na vitisho vya gizani.

18 “Lakini wao ni povu juu ya maji;

sehemu yao juu ya nchi imelaaniwa,

hivyo hakuna hata mmoja

aendaye kwenye shamba la mizabibu.

19 Kama vile joto na hari vikaushavyo theluji iliyoyeyuka,

ndivyo kuzimu kuwanyakuavyo

wale waliotenda dhambi.

20 Tumbo lililowazaa huwasahau,

nao huwa karamu ya mabuu;

watu waovu hawakumbukwi tena,

lakini huvunjika kama mti.

21 Huwafanya mawindo wanawake walio tasa

na wale wasio na watoto,

nao hawaonyeshi huruma kwa wajane.

22 Lakini Mungu huwakokota wenye nguvu kwa uwezo wake,

ingawa wamestawi, hawana hakika ya maisha.

23 Aweza akawaacha wakapumzika wakijihisi salama,

lakini macho yake yanaona njia zao.

24 Kwa kitambo kidogo hutukuka, hatimaye hutoweka,

hushushwa na kukusanywa kama wengine wote,

hukatwa kama masuke ya nafaka.

25 “Kama hili sivyo, ni nani awezaye

kuthibitisha kuwa mimi ni mwongo

na kuyafanya maneno yangu kuwa si kitu?”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JOB/24-371672903050fe2165c24e426b3d26df.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

four × four =