Habakuki 1

1 Neno alilopokea nabii Habakuki.

Lalamiko La Habakuki

2 EeBwana, hata lini nitakuomba msaada,

lakini wewe husikilizi?

Au kukulilia, “Udhalimu!”

Lakini hutaki kuokoa?

3 Kwa nini unanifanya nitazame dhuluma?

Kwa nini unavumilia makosa?

Uharibifu na udhalimu viko mbele yangu;

kuna mabishano na mapambano kwa wingi.

4 Kwa hiyo sheria imepotoshwa,

nayo haki haipo kabisa.

Waovu wanawazunguka wenye haki,

kwa hiyo haki imepotoshwa.

Jibu La Bwana

5 “Yatazame mataifa,

uangalie na ushangae kabisa.

Kwa sababu katika siku zako nitafanya kitu

ambacho hungeamini,

hata kama ungeambiwa.

6 Nitawainua Wababeli,

watu hao wakatili na wenye haraka,

ambao hupita dunia yote

kuteka mahali pa kuishi

pasipo pao wenyewe.

7 Ni watu wanoogopwa na wanaotisha;

wenyewe ndio sheria yao

na huinua heshima yao wenyewe.

8 Farasi wao ni wepesi kuliko chui,

na wakali kuliko mbwa mwitu

wakati wa machweo.

Askari wapanda farasi wao huenda mbio;

waendesha farasi wao wanatoka mbali.

Wanaruka kasi kama tai ili kunyafua;

9 wote wanakuja tayari kwa fujo.

Makundi yao ya wajeuri yanasonga mbele

kama upepo wa jangwani

na kukusanya wafungwa

kama mchanga.

10 Wanawabeza wafalme

na kuwadhihaki watawala.

Wanaicheka miji yote,

iliyozungushiwa maboma;

wanafanya malundo ya udongo

na kuiteka hiyo miji.

11 Kisha wanapita kasi kama upepo na kusonga mbele:

watu wenye hatia,

ambao nguvu zao ndio mungu wao.”

Lalamiko La Pili La Habakuki

12 EeBwana, je, wewe sio wa tangu milele?

Mungu wangu, Mtakatifu wangu, hatutakufa.

EeBwana, umewachagua wao ili watekeleze hukumu;

Ee Mwamba, umewaamuru watuadhibu.

13 Macho yako ni safi mno hata yasiweze kutazama uovu,

wala huwezi kuvumilia makosa.

Kwa nini basi unawavumilia wadanganyifu?

Kwa nini unakuwa kimya wakati waovu

wakiwameza wale wenye haki

kuliko wao wenyewe?

14 Umewafanya watu kama samaki baharini,

kama viumbe wa bahari wasio na mtawala.

15 Adui mwovu anawavuta wote kwa ndoana,

anawakamata katika wavu wake,

anawakusanya katika juya lake,

kwa hiyo anashangilia na anafurahi.

16 Kwa hiyo anatoa kafara kwa wavu wake

na kuchoma uvumba kwa juya lake,

kwa kuwa kwa wavu wake anaishi kwa starehe

na anafurahia chakula kizuri.

17 Je, aendelee kuwatoa walio katika wavu wake,

akiangamiza mataifa bila huruma?

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HAB/1-2499ca2309f069f88b812cf56b5f222e.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

17 − 15 =