Habakuki 3

Maombi Ya Habakuki

1 Sala ya nabii Habakuki iliyoimbwa kwa shigionothi.

2 Bwana, nimezisikia sifa zako,

nami naogopa, EeBwana.

Fufua kazi yako katikati ya miaka,

katikati ya miaka tangaza habari yako;

katika ghadhabu kumbuka rehema.

3 Mungu alitoka Temani,

yeye aliye Mtakatifu kutoka Mlima Parani.

Utukufu wake ulifunika mbingu

na sifa zake zikaifunika dunia.

4 Mng’ao wake ulikuwa kama jua lichomozalo,

mionzi ilimulika kutoka mkononi mwake,

ambako nguvu zake zilifichwa.

5 Tauni ilimtangulia;

maradhi ya kuambukiza

yalifuata nyayo zake.

6 Alisimama, akaitikisa dunia;

alitazama, na kuyafanya mataifa yatetemeke.

Milima ya zamani iligeuka mavumbi

na vilima vilivyozeeka vikaanguka.

Njia zake ni za milele.

7 Niliona watu wa Kushani katika dhiki,

na makazi ya Midiani katika maumivu makali.

8 EeBwana, uliikasirikia mito?

Je, ghadhabu yako ilikuwa dhidi ya vijito?

Je, ulighadhibikia bahari ulipoendesha farasi

wako na magari yako ya ushindi?

9 Uliufunua upindi wako

na kuita mishale mingi.

Uliigawa dunia kwa mito;

10 milima ilikuona ikatetemeka.

Mafuriko ya maji yakapita huko;

vilindi vilinguruma

na kuinua mawimbi yake juu.

11 Jua na mwezi vilisimama kimya mbinguni

katika mng’ao wa mishale yako inayoruka,

na katika mng’ao wa mkuki wako umeremetao.

12 Kwa ghadhabu ulipita juu ya dunia

na katika hasira ulikanyaga mataifa.

13 Ulikuja kuwaokoa watu wako,

kumwokoa masiya wako.

Ulimponda kiongozi wa nchi ya uovu,

ukamvua toka kichwani hadi wayo.

14 Kwa mkuki wake mwenyewe ulitoboa kichwa chake

wakati mashujaa wake

walipofurika nje kwa kishindo kututawanya,

wakifurahi kama waliokaribu kutafuna

wale wanyonge waliokuwa mafichoni.

15 Ulikanyaga bahari kwa farasi wako,

ukisukasuka maji makuu.

16 Nilisikia na moyo wangu ukagonga kwa nguvu,

midomo yangu ikatetemeka kwa hofu

niliposikia sauti;

uchakavu ukanyemelea mifupa yangu,

na miguu yangu ikatetemeka.

Hata hivyo nitasubiri kwa uvumilivu siku ya maafa

kuyajilia mataifa yaliyotuvamia.

17 Ingawa mtini hauchanui maua

na hakuna zabibu juu ya mizabibu,

ingawaje mzeituni hauzai,

na hata mashamba hayatoi chakula,

iwapo hakuna kondoo katika banda

wala ng’ombe katika zizi,

18 hata hivyo nitashangilia katikaBwana,

nitamfurahia Mungu Mwokozi wangu.

19 BwanaMwenyezi ni nguvu yangu;

huifanya miguu yangu kama miguu ya paa,

huniwezesha kupita juu ya vilima.

(Kwa kiongozi wa uimbaji. Kwa vinanda vyangu vya nyuzi.)

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HAB/3-bec1d4175c363e1dfe8d2d3391793194.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

eight − 5 =