Isaya 2

Mlima Wa Bwana

1 Hili ndilo aliloliona Isaya mwana wa Amozi kuhusu Yuda na Yerusalemu:

2 Katika siku za mwisho

mlima wa Hekalu laBwanautaimarishwa

kama mlima mkuu miongoni mwa milima,

utainuliwa juu kupita vilima

na mataifa yote yatamiminika huko.

3 Mataifa mengi yatakuja na kusema,

“Njoni na tuupande mlima waBwana,

kwenye nyumba ya Mungu wa Yakobo.

Atatufundisha njia zake,

ili tuweze kuenenda katika mapito yake.”

Sheria itatoka Sayuni,

neno laBwanakutoka Yerusalemu.

4 Atahukumu kati ya mataifa

na ataamua magomvi ya mataifa mengi.

Watafua panga zao kuwa majembe

na mikuki yao kuwa miundu ya kukata matawi.

Taifa halitainua upanga dhidi ya taifa jingine,

wala hayatafanya mazoezi ya vita tena.

5 Njoni, Enyi nyumba ya Yakobo,

sisi na tutembee katika nuru yaBwana

Siku Ya Bwana

6 Umewatelekeza watu wako,

nyumba ya Yakobo.

Wamejaa ushirikina utokao Mashariki,

wanapiga ramli kama Wafilisti

na wanashikana mikono na wapagani.

7 Nchi yao imejaa fedha na dhahabu,

hakuna mwisho wa hazina zao.

Nchi yao imejaa farasi,

hakuna mwisho wa magari yao.

8 Nchi yao imejaa sanamu,

wanasujudia kazi za mikono yao,

vitu vile ambavyo vidole vyao vimevitengeneza.

9 Kwa hiyo mwanadamu atashushwa

na binadamu atanyenyekezwa,

usiwasamehe.

10 Ingieni kwenye miamba,

jificheni ardhini

kutokana na utisho waBwana

na utukufu wa enzi yake!

11 Macho ya mtu mwenye majivuno yatanyenyekezwa

na kiburi cha wanadamu kitashushwa,

Bwanapeke yake ndiye atakayetukuzwa siku hiyo.

12 BwanaMwenye Nguvu Zote anayo siku aliyoiweka akiba

kwa wote wenye kujivuna na wenye kiburi,

kwa wote wanaojikweza

(nao watanyenyekezwa),

13 kwa mierezi yote ya Lebanoni,

iliyo mirefu sana,

nayo mialoni yote ya Bashani,

14 kwa milima yote mirefu

na vilima vyote vilivyoinuka,

15 kwa kila mnara ulio mrefu sana

na kila ukuta wenye ngome,

16 kwa kila meli ya biashara ya Tarshishi

na kila chombo cha baharini cha fahari.

17 Majivuno ya mwanadamu yatashushwa

na kiburi cha wanadamu kitanyenyekezwa,

Bwanapeke yake ndiye atatukuzwa siku hiyo,

18 nazo sanamu zitatoweka kabisa.

19 Watu watakimbilia kwenye mapango ndani ya miamba

na kwenye mahandaki ardhini

kutokana na utisho waBwana

na utukufu wa enzi yake,

ainukapo kuitikisa dunia.

20 Katika siku ile watu watawatupia

panya na popo

vinyago vyao vya fedha na vya dhahabu,

walivyovitengeneza ili waviabudu.

21 Watakimbilia kwenye mapango miambani

na kwenye nyufa za miamba

kutokana na utisho waBwana

na utukufu wa enzi yake,

ainukapo kuitikisa dunia.

22 Acheni kumtumainia mwanadamu,

ambaye hana kitu ila pumzi katika pua zake.

Yeye ana thamani gani?

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/2-fe1cc94206caa8ad1921991cf7dd89f7.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

one × 4 =