Isaya 13

Unabii Dhidi Ya Babeli

1 Neno kuhusu Babeli ambalo Isaya mwana wa Amozi aliliona:

2 Twekeni bendera juu ya mlima usio na kitu,

wapazieni sauti,

wapungieni mkono waingie

katika malango ya wenye heshima.

3 Nimewaamuru watakatifu wangu;

nimewaita mashujaa wangu

waitimize hasira yangu:

wale wanaoshangilia ushindi wangu.

4 Sikilizeni kelele juu ya milima,

kama ile ya umati mkubwa wa watu!

Sikilizeni, makelele katikati ya falme,

kama mataifa yanayokusanyika pamoja!

BwanaMwenye Nguvu Zote anakusanya

jeshi kwa ajili ya vita.

5 Wanakuja kutoka nchi za mbali sana,

kutoka miisho ya mbingu,

Bwanana silaha za ghadhabu yake,

kuangamiza nchi yote.

6 Ombolezeni, kwa maana siku yaBwanai karibu,

# itakuja kama uharibifu kutoka kwa Mwenyezi.

7 Kwa sababu ya hili, mikono yote italegea,

moyo wa kila mtu utayeyuka.

8 Hofu itawakamata,

uchungu na maumivu makali yatawashika,

watajinyonganyonga kama mwanamke

aliye na utungu wa kuzaa.

Watatazamana kwa hofu kila mtu na mwenzake,

nyuso zao zikiwa katika hali

ya kuwaka kama moto.

9 Tazameni, siku yaBwanainakuja,

siku katili, yenye ghadhabu na hasira kali,

kuifanya nchi kuwa ukiwa

na kuwaangamiza wenye dhambi

waliomo ndani yake.

10 Nyota za mbinguni na makundi ya nyota

havitatoa mwanga wake.

Jua linalochomoza litatiwa giza

na mwezi hautatoa nuru yake.

11 Nitauadhibu ulimwengu kwa ajili ya uovu wake,

waovu kwa ajili ya dhambi zao.

Nitakomesha majivuno ya wenye kiburi

Na nitakishusha kiburi cha watu wakatili.

12 Nitawafanya wanadamu kuwa adimu

kuliko dhahabu safi,

watakuwa wachache sana

kuliko dhahabu ya Ofiri.

13 Kwa hiyo nitazifanya mbingu zitetemeke,

nayo dunia itatikisika kutoka mahali pake

katika ghadhabu yaBwanaMwenye Nguvu Zote,

katika siku ya hasira yake iwakayo.

14 Kama swala awindwaye,

kama kondoo wasio na mchungaji,

kila mmoja atarudi kwa watu wake mwenyewe,

kila mmoja atakimbilia nchi yake ya kuzaliwa.

15 Ye yote atakayetekwa atapasuliwa tumbo,

wote watakaokamatwa watauawa kwa upanga.

16 Watoto wao wachanga watavunjwa vipande vipande

mbele ya macho yao;

nyumba zao zitatekwa

na wake zao watatendwa jeuri.

17 Tazama, nitawachochea Wamedi dhidi yao,

ambao hawajali fedha

wala hawafurahii dhahabu.

18 Mishale yao itawaangusha vijana,

hawatakuwa na huruma kwa watoto wachanga

wala hawataangalia watoto kwa huruma.

19 Babeli, johari ya falme,

# utukufu wa kiburi cha Wababeli,

itaangushwa na Mungu

kama Sodoma na Gomora.

20 Hautakaliwa na watu kamwe

wala watu hawataishi humo kwa vizazi vyote,

hakuna Mwarabu atakayepiga hema lake huko,

hakuna mchungaji atakayepumzisha

makundi yake ya kondoo

na mbuzi huko.

21 Lakini viumbe wa jangwani watalala huko,

mbweha watajaza nyumba zake,

bundi wataishi humo

nao mbuzi-mwitu watarukaruka humo.

22 Fisi watalia ndani ya ngome zake,

mbweha ndani ya majumba yake

ya kifalme ya fahari.

Wakati wake umewadia,

na siku zake hazitaongezwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/13-151cf828900c0ae989de041b08c49078.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

2 × five =