Isaya 14

Yuda Kufanywa Upya

1 Bwanaatamhurumia Yakobo,

kwa mara nyingine tena atamchagua Israeli

na kuwakalisha katika nchi yao wenyewe.

Wageni wataungana nao

na kujiunga na nyumba ya Yakobo.

2 Mataifa watawachukua

na kuwaleta mahali pao wenyewe.

Nayo nyumba ya Israeli itamiliki mataifa kama watumishi wa kiume na watumishi

wa kike katika nchi yaBwana.

Watawafanya watekaji wao kuwa mateka

na kutawala juu ya wale waliowaonea.

3 Katika sikuBwanaatakapokuondolea mateso, udhia na utumwa wa kikatili,

4 utaichukua dhihaka hii dhidi ya mfalme wa Babeli:

Tazama jinsi mtesi alivyofikia mwisho!

Tazama jinsi ghadhabu yake kali ilivyokoma!

5 Bwanaamevunja fimbo ya mwovu,

fimbo ya utawala ya watawala,

6 ambayo kwa hasira waliyapiga mataifa

kwa mapigo yasiyo na kikomo,

nao kwa ghadhabu kali waliwatiisha mataifa

kwa jeuri pasipo huruma.

7 Nchi zote ziko kwenye mapumziko na kwenye amani,

wanabubujika kwa kuimba.

8 Hata misonobari na mierezi ya Lebanoni inashangilia mbele yako na kusema,

“Basi kwa sababu umeangushwa chini,

hakuna mkata miti atakayekuja kutukata.”

9 Huko chini Kuzimu kote kumetaharuki

kukulaki unapokuja,

inaamsha roho za waliokufa ili kukupokea,

wote waliokuwa viongozi katika ulimwengu,

inawafanya wainuke kwenye viti vyao vya kifalme,

wale wote waliokuwa wafalme juu ya mataifa.

10 Wote wataitika,

watakuambia,

“Wewe pia umekuwa dhaifu, kama sisi tulivyo;

wewe umekuwa kama sisi.”

11 Majivuno yako yote yameshushwa mpaka kuzimu,

pamoja na kelele ya vinubi vyako,

mafunza yametanda chini yako

na minyoo imekufunika.

12 Tazama jinsi ulivyoanguka kutoka mbinguni,

Ewe nyota ya asubuhi,

mwana wa mapambazuko!

Umetupwa chini duniani,

wewe uliyepata kuangusha mataifa!

13 Ulisema moyoni mwako,

“Nitapanda juu hadi mbinguni,

nitakiinua kiti changu cha enzi

juu ya nyota za Mungu,

nitaketi nimetawazwa

juu ya mlima wa kusanyiko,

kwenye vimo vya juu sana vya Mlima Mtakatifu.

14 Nitapaa juu kupita mawingu,

nitajifanya kama Yeye Aliye Juu Sana.”

15 Lakini umeshushwa chini hadi kuzimu,

hadi kwenye vina vya shimo.

16 Wale wanaokuona wanakukazia macho,

wanatafakari hatima yako:

“Je, huyu ndiye yule aliyetikisa dunia

na kufanya falme zitetemeke,

17 yule aliyeifanya dunia kuwa jangwa,

aliyeipindua miji yake

na ambaye hakuwaachia

mateka wake waende nyumbani?”

18 Wafalme wote wa mataifa wamelala

kwa heshima kila mmoja katika kaburi lake mwenyewe.

19 Lakini wewe umetupwa nje ya kaburi lako

kama tawi lililokataliwa,

umefunikwa na waliouawa

pamoja na wale waliochomwa kwa upanga,

wale washukao mpaka

kwenye mawe ya shimo.

Kama mzoga uliokanyagwa chini ya nyayo,

20 Hutajumuika nao kwenye mazishi,

kwa kuwa umeharibu nchi yako

na kuwaua watu wako.

Mzao wa mwovu hatatajwa tena kamwe.

21 Andaa mahali pa kuwachinjia wanawe

kwa ajili ya dhambi za baba zao,

wasije wakainuka ili kuirithi nchi

na kuijaza dunia kwa miji yao.

22 BwanaMwenye Nguvu Zote asema,

“Nitainuka dhidi yao,

nitalikatilia mbali jina lake kutoka Babeli

pamoja na watu wake walionusurika,

watoto wake na wazao wake,”

asemaBwana.

23 “Nitaifanya kuwa mahali pa bundi,

na kuwa nchi ya matope;

nitaifagia kwa ufagio wa maangamizi,”

asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.

Unabii Dhidi Ya Ashuru

24 BwanaMwenye Nguvu Zote ameapa,

“Hakika, kama vile nilivyopanga, ndivyo itakavyokuwa,

nami kama nilivyokusudia, ndivyo itakavyosimama.

25 Nitamponda Mwashuru katika nchi yangu,

juu ya milima yangu nitawakanyagia chini.

Nira yake itaondolewa kutoka kwa watu wangu,

nao mzigo wake utaondolewa kutoka mabegani mwao.”

26 Huu ndio mpango uliokusudiwa kwa ajili ya ulimwengu wote,

huu ni mkono ulionyooshwa juu ya mataifa yote.

27 Kwa kuwaBwanaMwenye Nguvu Zote amekusudia,

ni nani awezaye kumzuia?

Mkono wake umenyooshwa,

ni nani awezaye kuurudisha?

Unabii Dhidi Ya Wafilisti

28 Neno hili lilikuja mwaka ule Mfalme Ahazi alipokufa:

29 Msifurahi, enyi Wafilisti wote,

kwamba fimbo iliyowapiga imevunjika;

kutoka katika mzizi wa huyo nyoka

atachipuka nyoka mwenye sumu kali,

uzao wake utakuwa joka lirukalo,

lenye sumu kali.

30 Maskini kuliko maskini wote watapata malisho,

nao wahitaji watalala salama.

Lakini mzizi wako nitauangamiza kwa njaa,

nayo njaa itawaua walionusurika.

31 Piga yowe, Ee lango! Bweka, Ee mji!

Yeyukeni, enyi Wafilisti wote!

Wingu la moshi linakuja toka kaskazini,

wala hakuna atakayechelewa katika safu zake.

32 Ni jibu gani litakalotolewa

kwa wajumbe wa taifa hilo?

“Bwanaameifanya imara Sayuni,

nako ndani yake watu wake walioonewa

watapata kimbilio.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/14-eae0592fce4bc6b4c99ed9ef6670f182.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

6 − four =