Isaya 3

Hukumu Juu Ya Yerusalemu Na Yuda.

1 Tazama sasa, Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote,

yu karibu kuwaondolea Yerusalemu na Yuda

upatikanaji wa mahitaji na misaada,

upatikanaji wote wa chakula na maji,

2 shujaa na mtu wa vita,

mwamuzi na nabii,

mwaguzi na mzee,

3 jemadari wa kikosi cha watu hamsini

na mtu mwenye cheo, mshauri,

fundi stadi na mlozi mjanja.

4 Nitawafanya wavulana wawe maafisa wao,

watoto ndio watakaowatawala.

5 Watu wataoneana wao kwa wao

mtu dhidi ya mtu,

jirani dhidi ya jirani yake.

Kijana atainuka dhidi ya mzee,

mtu mnyonge dhidi ya mtu mwenye heshima.

6 Mtu atamkamata mmoja wa ndugu zake

katika nyumba ya baba yake na kusema,

“Unalo joho, wewe uwe kiongozi wetu,

tawala lundo hili la magofu!”

7 Lakini siku hiyo atapiga kelele akisema,

“Sina uponyaji.

Sina chakula wala mavazi katika nyumba yangu,

msinifanye niwe kiongozi wa watu.”

8 Yerusalemu inapepesuka,

Yuda inaanguka;

maneno yao na matendo yao ni kinyume naBwana,

wakiudharau uwepo wake uliotukuka.

9 Nyuso zao zinavyoonekana zinashuhudia dhidi yao,

hujivunia dhambi yao kama Sodoma,

wala hawaifichi.

Ole wao!

Wamejiletea maafa juu yao wenyewe.

10 Waambie wanyofu itakuwa heri kwao,

kwa kuwa watafurahia tunda la matendo yao.

11 Ole wa watu waovu! Maafa yapo juu yao!

Watalipwa kwa ajili ya yale mikono yao iliyotenda.

12 Vijana wanawatesa watu wangu,

wanawake wanawatawala.

Enyi watu wangu, viongozi wenu wanawapotosha,

wanawapoteza njia.

13 Bwanaanachukua nafasi yake mahakamani,

anasimama kuhukumu watu.

14 Bwanaanaingia katika hukumu

dhidi ya wazee na viongozi wa watu wake:

“Ninyi ndio mlioharibu shamba langu la mizabibu,

mali zilizonyang’anywa kutoka kwa maskini

zimo nyumbani mwenu.

15 Mnamaanisha nini kuwaponda watu wangu

na kuzisaga nyuso za maskini?”

asema Bwana,BwanaMwenye Nguvu Zote.

16 Bwanaasema,

“Wanawake wa Sayuni wana kiburi,

wanatembea na shingo ndefu,

wakikonyeza kwa macho yao,

wakitembea kwa hatua fupi fupi za madaha,

wakiwa na mapambo yanayotoa mlio kwenye vifundo vya miguu yao.

17 Kwa hiyo Bwana ataleta majipu kwenye vichwa vya wanawake wa Sayuni;

Bwanaatazifanya ngozi za vichwa vyao kuwa vipara.”

18 Katika siku ile Bwana atawanyang’anya uzuri wao: bangili, tepe za kichwani, mikufu yenye alama za mwezi mwandamo,

19 vipuli, vikuku, shela,

20 vilemba, mikufu ya kwenye vifundo vya miguu, mshipi, chupa za manukato na hirizi,

21 pete zenye muhuri, pete za puani,

22 majoho mazuri, mitandio, mavazi, kifuko cha kutilia fedha,

23 vioo, mavazi ya kitani, taji na shali.

24 Badala ya harufu ya manukato kutakuwa na uvundo;

badala ya mishipi, kamba;

badala ya nywele zilizotengenezwa vizuri, upara;

badala ya mavazi mazuri, nguo za magunia;

badala ya uzuri, alama ya aibu kwa chuma cha moto.

25 Wanaume wako watauawa kwa upanga,

mashujaa wako watauawa vitani.

26 Malango ya Sayuni yataomboleza na kulia,

akiwa maskini, ataketi mavumbini.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/3-97337bf7bbab98858f9a6194f2663a83.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

ten − 6 =