Isaya 5

Wimbo Wa Shamba La Mizabibu

1 Nitaimba wimbo kwa ajili ya mmoja nimpendaye

kuhusu shamba lake la mizabibu:

Mpendwa wangu alikuwa na shamba la mizabibu

kwenye kilima chenye rutuba.

2 Alililima na kuondoa mawe

na akaliotesha mizabibu bora sana.

Akajenga mnara wa ulinzi ndani yake

na kutengeneza shinikizo la kukamulia divai pia.

Kisha akatazamia kupata mazao ya zabibu nzuri,

lakini lilizaa matunda mabaya tu.

3 “Basi enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda,

hukumuni kati yangu na shamba langu la mizabibu.

4 Ni nini zaidi ambacho kingeweza kufanyika

kwa ajili ya shamba langu la mizabibu

kuliko yale niliyofanya?

Nilipotazamia kupata zabibu nzuri,

kwa nini lilizaa zabibu mbaya tu?

5 Sasa nitawaambia lile nitakalolitendea

shamba langu la mizabibu:

Nitaondoa uzio wake,

nalo litaharibiwa,

nitabomoa ukuta wake,

nalo litakanyagwa.

6 Nitalifanya nchi ya ukiwa isiyokaliwa na watu,

halitakatiwa matawi wala kulimwa,

nayo michongoma na miiba itamea huko,

nitaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.”

7 Shamba la mzabibu laBwanaMwenye Nguvu Zote

ni nyumba ya Israeli,

na watu wa Yuda

ni bustani yake ya kumpendeza.

Alitazamia haki, lakini akaona umwagaji damu,

alitazamia uadilifu,

lakini akasikia vilio vya taabu.

8 Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba

na kuunganisha mashamba baada ya mashamba

hadi hakuna nafasi iliyobaki

nanyi mnaishi peke yenu katika nchi.

9 BwanaMwenye Nguvu Zote amesema nikisikia:

“Hakika nyumba kubwa zitakuwa ukiwa,

nayo majumba ya fahari yatabaki bila kukaliwa.

10 Shamba la mizabibu la eka kumi

# litatoa bathimoja ya divai,

# na homeriya mbegu zilizopandwa

# itatoa efamoja tu ya nafaka.”

11 Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema

wakikimbilia kunywa vileo,

wale wakawiao sana mpaka usiku,

mpaka wamewaka kwa mvinyo.

12 Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao,

matari, filimbi na mvinyo,

lakini hawayajali matendo yaBwana,

wala hawana heshima

kwa ajili ya kazi ya mikono yake.

13 Kwa hiyo watu wangu watakwenda uhamishoni

kwa sababu ya kukosa ufahamu,

watu wao wenye vyeo watakufa kwa njaa

na watu wao wengi watakauka kwa kiu.

14 Kwa hiyo kaburilimeongeza hamu yake

na kupanua mdomo wake bila kikomo,

ndani mwake watashuka wakuu wao na wingi wa watu

pamoja na wagomvi wao

na wafanyao sherehe wote.

15 Hivyo mwanadamu atashushwa

na binadamu atanyenyekezwa,

macho ya wenye majivuno yatanyenyekezwa.

16 LakiniBwanaMwenye Nguvu Zote atatukuzwa

kwa ajili ya haki yake,

naye Mungu Mtakatifu atajionyesha mwenyewe

kuwa mtakatifu kwa haki yake.

17 Kondoo watajilisha kwenye malisho yao wenyewe,

wana-kondoo na wageni watajilisha

katika magofu ya matajiri.

18 Ole wao wanaovuta dhambi kwa kamba za udanganyifu

na uovu kama kwa kamba za mkokoteni,

19 kwa wale wanaosema, “Mungu na afanye haraka,

aharakishe kazi yake

ili tupate kuiona.

Huo mpango wa Aliye Mtakatifu wa Israeli na ukamilike,

tena udhihirike ili tupate kuujua.”

20 Ole wao wanaoita ubaya ni wema

na wema ni ubaya,

wawekao giza badala ya nuru

na nuru badala ya giza,

wawekao uchungu badala ya utamu

na utamu badala ya uchungu.

21 Ole wao walio na hekima machoni pao wenyewe

na kujiona wenye akili machoni pao wenyewe.

22 Ole wao walio mashujaa kwa kunywa mvinyo

nao walio hodari katika kuchanganya vileo,

23 wale wanaoachilia wenye hatia kwa kupokea hongo,

lakini huwanyima haki wasio na hatia.

24 Kwa hiyo, kama ndimi za moto zirambavyo nyasi

na kama vile majani makavu

yazamavyo katika miali ya moto,

ndivyo mizizi yao itakavyooza

na maua yao yatakavyopeperushwa

kama mavumbi;

kwa kuwa wameikataa sheria yaBwanaMwenye Nguvu Zote

na kulisukumia mbali

neno la Aliye Mtakatifu wa Israeli.

25 Kwa hiyo hasira yaBwanainawaka dhidi ya watu wake,

mkono wake umeinuliwa na anawapiga.

Milima inatetemeka,

maiti ni kama takataka kwenye barabara.

Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali,

mkono wake bado umeinuliwa juu.

26 Yeye anainua bendera kwa ajili ya mataifa yaliyo mbali,

anapiga filimbi kwa ajili ya wale walio kwenye miisho ya dunia.

Tazama wamekuja,

kwa kasi na kwa haraka!

27 Hakuna hata mmoja wao anayechoka wala kujikwaa,

hakuna hata mmoja anayesinzia wala kulala,

hakuna mkanda uliolegezwa kiunoni,

hakuna gidamu ya kiatu iliyokatika.

28 Mishale yao ni mikali,

pinde zao zote zimevutwa,

kwato za farasi wao ziko kama jiwe la gumegume,

magurudumu ya magari yao ya vita ni kama upepo wa kisulisuli.

29 Ngurumo yao ni kama ile ya simba,

wananguruma kama wana simba,

wanakoroma wanapokamata mawindo yao

na kuondoka nayo pasipo ye yote wa kuokoa.

30 Katika siku ile watanguruma juu yake

kama ngurumo za bahari.

Kama mtu akiitazama nchi,

ataona giza na dhiki;

hata nuru itatiwa giza kwa mawingu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/5-9bfcdfb609100a4924e8bba32be4ad0b.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

19 + 14 =