Isaya 6

Agizo Kwa Isaya

1 Katika mwaka ule Mfalme Uzia alipokufa, nilimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu na kilichotukuzwa sana, nalo pindo la joho lake likajaza Hekalu.

2 Juu yake walikuwepo maserafi, kila mmoja alikuwa na mabawa sita: Kwa mabawa mawili walifunika nyuso zao, kwa mengine mawili walifunika miguu yao na kwa mawili walikuwa wakiruka.

3 Nao walikuwa wakiitana kila mmoja na mwenzake:

“Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu

niBwanaMwenye Nguvu Zote;

dunia yote imejaa utukufu wake.”

4 Kwa kutoa kwao sauti miimo ya milango na vizingiti vilitikisika, nalo Hekalu likajaa moshi.

5 Ndipo nikalia, “Ole wangu mimi! Nimeangamia! Kwa kuwa mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninaishi katikati ya watu wenye midomo michafu, nayo macho yangu yamemwona Mfalme,BwanaMwenye Nguvu Zote.”

6 Ndipo mmoja wa wale maserafi akaruka kunijia akiwa na kaa la moto linalowaka mkononi mwake, ambalo alikuwa amelichukua kwa koleo kutoka madhabahuni.

7 Akanigusa nalo kinywa changu na kusema, “Tazama, hili limegusa midomo yako, uovu wako umeondolewa nayo dhambi yako imesamehewa.”

8 Kisha nikasikia sauti ya Bwana ikisema, “Nimtume nani? Ni nani atakayekwenda kwa ajili yetu?”

Nami nikasema, “Mimi hapa. Nitume mimi!”

9 Akasema, “Nenda ukawaambie watu hawa:

“ ‘Mtaendelea daima kusikia,

lakini kamwe hamtafahamu;

mtaendelea daima kuona,

lakini kamwe hamtatambua.’

10 Fanya mioyo ya watu hawa kuwa migumu,

fanya masikio yao yasisikie

na upofushe macho yao.

Ama sivyo wanaweza kuona kwa macho yao,

wakasikia kwa masikio yao,

wakatambua kwa mioyo yao,

nao wakageuka na kuponywa.”

11 Ndipo nikasema, “Hadi lini, Ee Bwana?”

Naye akanijibu:

“Hadi miji iwe imeachwa magofu

na bila wakazi,

hadi nyumba zitakapobaki bila watu,

na mashamba yatakapoharibiwa na kuangamizwa,

12 hadiBwanaatakapokuwa amekwisha kumpeleka kila mmoja mbali sana,

na nchi itakapokuwa imeachwa kabisa.

13 Hata kama sehemu ya kumi ya watu watabaki katika nchi,

itaharibiwa tena.

Lakini kama vile mvinje na mwaloni

ibakizavyo visiki inapokatwa,

ndivyo mbegu takatifu

itakavyokuwa kisiki katika nchi.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/6-477c55de37f264094758a353be047415.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

seven + 9 =