Isaya 7

Ishara Ya Imanueli

1 Wakati Ahazi mwana wa Yothamu, mwana wa Uzia, alipokuwa mfalme wa Yuda, Mfalme Resini wa Aramuna Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli walipanda kupigana dhidi ya Yerusalemu, lakini hawakuweza kuushinda.

2 Wakati huu nyumba ya Daudi iliambiwa, “Aramu wameungana na Efraimu.” Kwa hiyo moyo wa Ahazi na ya watu wake ilitikiswa, kama miti ya msituni inavyotikiswa na upepo.

3 NdipoBwanaakamwambia Isaya, “Toka uende, wewe na mwanao Shear-Yashubu, mkutane na Ahazi huko mwisho wa mfereji wa Bwawa la Juu, kwenye barabara iendayo Shamba la Dobi.

4 Mwambie, ‘Uwe mwangalifu, utulie na usiogope. Usife moyo kwa ajili ya watu hawa wawili walio kama visiki vya kuni vifukavyo moshi, kwa ajili ya hasira kali ya Resini na Aramu na ya mwana wa Remalia.

5 Aramu, Efraimu na mwana wa Remalia wamepanga shauri baya ili wakuangamize, wakisema,

6 “Tuishambulie Yuda, naam na tuirarue vipande vipande na kuigawa miongoni mwetu na kumtawaza mwana wa Tabeeli awe mfalme juu yake.”

7 LakiniBwanaMwenyezi asema hivi:

“ ‘Jambo hili halitatendeka,

halitatokea,

8 kwa kuwa kichwa cha Aramu ni Dameski,

na kichwa cha Dameski ni Resini peke yake.

Katika muda wa miaka sitini na mitano

Efraimu atakuwa ameharibiwa

kiasi kwamba hataweza tena kuwa taifa.

9 Kichwa cha Efraimu ni Samaria,

na kichwa cha Samaria

ni mwana wa Remalia peke yake.

Kama hamtasimama thabiti katika imani yenu,

hamtaimarika kamwe.’ ”

10 Bwanaakasema na Ahazi tena,

11 “MwombeBwana, Mungu wako ishara, kama ni kwenye vina virefu sana au ni kwenye vimo virefu sana.”

12 Lakini Ahazi akasema, “Sitaomba; sitamjaribuBwana.”

13 Ndipo Isaya akasema, “Sikia sasa, Ewe nyumba ya Daudi! Je, haitoshi kujaribu uvumilivu wa wanadamu? Je, mtaujaribu uvumilivu wa Mungu wangu pia?

14 Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara: Bikira atachukua mimba, naye atamzaa mwana, na ataitwa Imanueli.

15 Atakula jibini na asali hapo atakapokuwa ameweza kukataa mabaya na kuchagua lililo jema.

16 Lakini kabla mtoto hajajua kukataa ubaya na kuchagua lililo jema, nchi ya wafalme hao wawili unaowaogopa itafanywa ukiwa.

17 Bwanaataleta juu yako, juu ya watu wako na juu ya nyumba ya baba yako wakati ambao haujawahi kuwako tangu Efraimu alipojitenga na Yuda, atawaleteeni mfalme wa Ashuru.”

18 Katika siku ileBwanaatawapigia filimbi mainzi kutoka kwenye vijito vya mbali vya Misri na nyuki kutoka nchi ya Ashuru.

19 Wote watakuja na kukaa kwenye mabonde yenye mitelemko na kwenye nyufa za miamba, kwenye vichaka vyote vyenye miiba na kwenye mashimo yote ya maji.

20 Katika siku ile Bwana atatumia wembe ulioajiriwa kutoka ng’ambo ya Mtoyaani mfalme wa Ashuru, kunyoa nywele za kichwa chako, malaika ya miguu yako na kuziondoa ndevu zako pia.

21 Katika siku ile, mtu atahifadhi hai ndama mmoja na kondoo wawili.

22 Kwa ajili ya wingi wa maziwa watakayotoa, atapata jibini ya kula. Wote watakaobakia katika nchi watakula jibini na asali.

23 Katika siku ile, kila mahali palipokuwa na mizabibu elfu moja yenye thamani ya shekeli 1,000za fedha, patakuwa na michongoma na miiba tu.

24 Watu watakwenda huko wakiwa na upinde na mshale, kwa maana nchi itafunikwa na michongoma na miiba.

25 Kuhusu vilima vyote vilivyokuwa vikilimwa kwa jembe, hamtakwenda huko tena kwa ajili ya hofu ya michongoma na miiba, patakuwa mahali ambapo ng’ombe wataachiwa huru na kondoo kukimbia-kimbia.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/7-788558f4b6838b26743b6aa0c4b84b55.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

one × two =