Isaya 63

Siku Ya Mungu Ya Kisasi Na Ukombozi

1 Ni nani huyu anayekuja kutoka Edomu,

kutoka Bosra, mwenye mavazi

yaliyotiwa madoa mekundu?

Ni nani huyu, aliyevikwa joho la kifahari,

anayetembea kwa ukuu wa nguvu zake?

“Mimi ndimi, nisemaye katika haki,

mwenye nguvu wa kuokoa.”

2 Kwa nini mavazi yako ni mekundu,

kama ya yule akanyagaye shinikizo la zabibu?

3 “Nimekanyaga shinikizo la zabibu peke yangu;

kutoka katika mataifa

hakuna mtu awaye yote

aliyekuwa pamoja nami.

Nimewaponda mataifa kwa miguu katika hasira yangu

na kuwakanyaga chini

katika ghadhabu yangu;

damu yao ilitia matone matone kwenye mavazi yangu

na kutia madoa nguo zangu zote.

4 Kwa kuwa siku ya kisasi ilikuwa moyoni mwangu,

mwaka wa ukombozi wangu umefika.

5 Nilitazama, lakini hakuwepo ye yote wa kunisaidia,

nilishangaa kwa kuwa hakuwepo

ye yote aliyetoa msaada;

hivyo mkono wangu wenyewe ndio ulionifanyia wokovu,

na ghadhabu yangu mwenyewe

ndiyo iliyonitegemeza.

6 Nilikanyaga mataifa kwa miguu katika hasira yangu,

katika ghadhabu yangu niliwalewesha

na kumwaga damu yao juu ya ardhi.”

Kusifu Na Kuomba

7 Nitasimulia juu ya wema waBwana,

kwa ajili ya matendo ambayo

kwayo apaswa kusifiwa,

sawasawa na yote ambayoBwana

ametenda kwa ajili yetu:

naam, mambo mengi mema aliyoyatenda

kwa ajili ya nyumba ya Israeli,

sawasawa na huruma zake

na wema wake mwingi.

8 Alisema, “Hakika wao ni watu wangu,

wana ambao hawatanidanganya”;

kisha akawa Mwokozi wao.

9 Katika taabu zao zote naye alitaabika

na malaika wa uso wake akawaokoa.

Katika upendo wake na rehema zake aliwakomboa,

akawainua na kuwachukua siku zote zilizopita.

10 Lakini waliasi

na kumhuzunisha Roho Mtakatifu wake.

Hivyo aligeuka na kuwa adui yao

na yeye mwenyewe akapigana dhidi yao.

11 Ndipo watu wake wakazikumbuka siku zilizopita,

siku za Mose na watu wake:

yuko wapi yeye aliyewaleta kupitia katikati ya bahari,

pamoja na wachungaji wa kundi lake?

Yuko wapi yule aliyeweka

Roho wake Mtakatifu katikati yao,

12 aliyetuma mkono wake uliotukuka wenye nguvu

kuwa katika mkono wa kuume wa Mose,

aliyegawa maji ya bahari mbele yao,

ili kujipatia jina milele,

13 aliyewaongoza kupitia kwenye vilindi?

Kama farasi katika nchi iliyo wazi,

wao hawakujikwaa,

14 kama ng’ombe washukao bondeni kwenye malisho,

walipewa pumziko na Roho waBwana.

Hivi ndivyo ulivyowaongoza watu wako

ili kujipatia mwenyewe jina tukufu.

15 Tazama chini kutoka mbinguni ukaone

kutoka katika kiti chako cha enzi

kilichoinuliwa juu, kitakatifu na kitukufu.

Uko wapi wivu wako na uweza wako?

Umetuzuilia wema wako na huruma zako.

16 Lakini wewe ni Baba yetu,

ingawa Abrahamu hatufahamu sisi

wala Israeli hatutambui;

wewe, EeBwana, ni Baba yetu,

Mkombozi wetu tangu zamani za kale

ndilo jina lako.

17 EeBwana, kwa nini unatuacha tuende mbali na njia zako

na kuifanya mioyo yetu migumu

hata hatukukuheshimu?

Rudi kwa ajili ya watumishi wako,

yale makabila ambayo ni urithi wako.

18 Kwa maana kwa muda mfupi watu wako walimiliki

mahali pako patakatifu,

lakini sasa adui zetu wamepakanyaga

mahali patakatifu pako.

19 Sisi ni watu wako tangu zamani;

lakini tumekuwa kama wale ambao

hujawatawala kamwe,

kama wale ambao

hawajaitwa kwa jina lako.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/63-f03a29f94e7239bcc6f2674f5b9a1265.mp3?version_id=1627—