Isaya 65

Hukumu Na Wokovu

1 “Nilijifunua kwa watu wale ambao hawakuniulizia,

nimeonekana kwa watu wale

ambao hawakunitafuta.

Kwa taifa lile ambalo halikuliita Jina langu,

nilisema, ‘Niko hapa, niko hapa.’

2 Mchana kutwa nimeinyosha mikono yangu

kwa watu wakaidi,

wanaokwenda katika njia ambazo si nzuri,

wafuatao mawazo yao wenyewe,

3 taifa ambalo daima hunikasirisha

machoni pangu,

wakitoa dhabihu katika bustani

na kufukiza uvumba juu

ya madhabahu za matofali;

4 watu waketio katikati ya makaburi

na kukesha mahali pa siri,

ili kuabudu mizimu,

walao nyama za nguruwe,

nazo sufuria zao zina mchuzi

wa nyama na mboga zilizonajisi,

5 wasemao, ‘Kaa mbali; usinikaribie,

kwa maana mimi

ni mtakatifu mno kwako!’

Watu wa aina hiyo ni moshi katika pua zangu,

ni moto uwakao mchana kutwa.

6 “Tazama, jambo hili hubakia limeandikwa mbele zangu:

sitanyamaza kimya

bali nitalipiza kwa ukamilifu;

nitalipiza mapajani mwao:

7 dhambi zenu na dhambi za baba zenu,”

asemaBwana.

“Kwa sababu walitoa dhabihu za kuteketezwa juu ya milima

na kunichokoza mimi juu ya vilima,

nitawapimia mapajani mwao

malipo makamilifu

kwa ajili ya matendo yao ya zamani.”

8 Hili ndilo asemaloBwana:

“Kama vile divai mpya ingali bado inapatikana

katika kishada cha zabibu,

nao watu husema, ‘Usikiharibu,

kwa kuwa bado kuna kitu kizuri ndani yake,’

hivyo ndivyo nitakavyofanya

kwa ajili ya watumishi wangu;

sitawaangamiza wote.

9 Nitawaleta wazao kutoka kwa Yakobo,

na kutoka kwa Yuda wale

watakaomiliki milima yangu,

watu wangu wateule watairithi,

nako huko wataishi watumishi wangu.

10 Sharoni itakuwa malisho

kwa ajili ya makundi ya kondoo na mbuzi,

na Bonde la Akori mahali pa kupumzikia

kwa makundi ya ng’ombe,

kwa ajili ya watu wangu wanaonitafuta.

11 “Bali kwenu ninyi mnaomwachaBwana

na kuusahau mlima wangu mtakatifu,

# ninyi mnaoandaa meza kwa ajili ya Bahati

na kujaza mabakuli ya mvinyo uliochanganywa

# kwa ajili ya Ajali,

12 nitawaagiza mfe kwa upanga,

nanyi nyote mtainama chini ili kuchinjwa;

kwa kuwa niliwaita lakini hamkuitika,

nilisema lakini hamkusikiliza.

Mlitenda maovu machoni pangu,

nanyi mkachagua mambo yale yanayonichukiza.”

13 Kwa hiyo hili ndilo asemaloBwanaMwenyezi:

“Watumishi wangu watakula,

lakini ninyi mtaona njaa;

watumishi wangu watakunywa

lakini ninyi mtaona kiu;

watumishi wangu watafurahi,

lakini ninyi mtaona haya.

14 Watumishi wangu wataimba

kwa furaha ya mioyo yao,

lakini ninyi mtalia

kutokana na uchungu wa moyoni

na kupiga yowe kwa sababu

ya uchungu wa roho zenu.

15 Mtaliacha jina lenu

kuwa laana kwa watu wangu waliochaguliwa;

BwanaMwenyezi atawaua ninyi,

lakini watumishi wake atawapa jina jingine.

16 Yeye aombaye baraka katika nchi

atafanya hivyo kwa Mungu wa kweli;

yeye aapaye katika nchi

ataapa kwa Mungu wa kweli.

Kwa kuwa taabu za zamani zitasahaulika

na kufichwa kutoka machoni pangu.

Mbingu Mpya Na Dunia Mpya

17 “Tazama, nitaumba

mbingu mpya na dunia mpya.

Mambo ya zamani hayatakumbukwa,

wala hayatakuja akilini.

18 Lakini furahini na kushangilia daima

katika hivi nitakavyoumba,

kwa kuwa nitaumba Yerusalemu uwe wa kupendeza,

nao watu wake wawe furaha.

19 Nami nitaifurahia Yerusalemu

na kuwafurahia watu wangu;

sauti ya maombolezo na ya kilio

haitasikika humo tena.

20 “Kamwe hatakuwepo tena ndani yake

mtoto mchanga atakayeishi siku chache tu,

au mzee ambaye hataishi akatimiza miaka yake.

Yeye atakayekufa akiwa na umri wa miaka mia moja

atahesabiwa kwamba ni kijana tu,

yeye ambaye hatafika miaka mia moja,

atahesabiwa kuwa amelaaniwa.

21 Watajenga nyumba na kuishi ndani yake;

watapanda mashamba ya mizabibu

na kula matunda yake.

22 Hawatajenga nyumba

na watu wengine waishi ndani yake,

au kupanda mazao na wengine wale.

Kwa kuwa kama zilivyo siku za mti,

ndivyo zitakavyokuwa

siku za watu wangu,

wateule wangu watafurahia kwa siku nyingi

kazi za mikono yao.

23 Hawatajitaabisha kwa kazi bure

wala hawatazaa watoto ili wapatwe na majanga,

kwa kuwa watakuwa taifa lililobarikiwa naBwana,

wao na wazao wao pamoja nao.

24 Kabla hawajaita nitajibu,

nao wakiwa katika kunena nitasikia.

25 Mbwa mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja,

naye simba atakula nyasi kama maksai,

lakini mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka.

Hawatadhuru wala kuharibu

katika mlima wangu mtakatifu wote,”

asemaBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/ISA/65-b96d6a2c779da3ede40e458f972ec0be.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

five × one =