Luka 9

Yesu Awatuma Wale Kumi Na Wawili

1 Yesu akiisha kuwaita wale kumi na wawili pamoja, aliwapa mamlaka na uwezo wa kutoa pepo wachafu wote na kuponya magonjwa yote,

2 kisha akawatuma waende wakahubiri Ufalme wa Mungu na kuponya wagonjwa.

3 Akawaagiza akisema, “Msichukue cho chote safarini, wala fimbo, wala mkoba, wala chakula, wala fedha, wala msichukue kanzu ya ziada.

4 Katika nyumba yo yote mwingiayo, kaeni humo hadi mtakapoondoka katika mji huo.

5 Kama watu wasipowakaribisha, mnapoondoka katika mji wao, kung’uteni mavumbi miguuni mwenu kuwa ushuhuda dhidi yao.”

6 Hivyo wale wanafunzi wakaondoka wakaenda kutoka kijiji hadi kijiji, wakihubiri habari njema na kuponya wagonjwa kila mahali.

7 Basi Herode mtawala wa Galilaya akasikia habari za yote yaliyotendeka, naye akafadhaika kwa kuwa baadhi ya watu walikuwa wakisema Yohana Mbatizaji amefufuka.

8 Wengine wakasema Eliya amewatokea, na wengine wakasema kwamba mmoja wa manabii wa kale amefufuka.

9 Herode akasema, “Yohana nilimkata kichwa. Lakini ni nani basi huyu ambaye ninasikia habari zake kuhusu mambo kama haya?” Akatamani sana kumwona.

Yesu Awalisha Watu 5,000

10 Wale mitume wake waliporudi, wakamweleza Yesu yote waliyofanya. Akawachukua akaenda nao faraghani mpaka mji mmoja uitwao Bethsaida.

11 Lakini umati wa watu ulipofahamu alikokwenda, ukamfuata. Akawakaribisha na kunena nao kuhusu Ufalme wa Mungu na kuwaponya wale wote waliokuwa wanahitaji uponyaji.

12 Ilipokaribia jioni, wale mitume kumi na wawili wakamjia Yesu na kumwambia, “Uage umati huu wa watu uondoke ili uweze kwenda kwenye vijiji vya karibu na sehemu za jirani, ili kupata chakula na mahali pa kulala, kwa maana hapa tuko nyikani.”

13 Yesu akawajibu, “Ninyi wapeni chakula.”

Wao wakasema, “Hatuna zaidi ya mikate mitano na samaki wawili, labda tuende tukanunue chakula cha kuwatosha watu wote hawa.”

14 Kwa kuwa walikuwako wanaume wapatao 5,000.

Yesu akawaambia wanafunzi wake, “waketisheni katika makundi ya watu hamsini hamsini.”

15 Wakafanya hivyo, wakawaketisha wote.

16 Yesu akaichukua ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama mbinguni, akavibariki na kuvimega, kisha akawapa wanafunzi wake waugawie ule umati wa watu.

17 Wote wakala, wakashiba. Nao wanafunzi wakakusanya vipande vilivyobaki, vikajaa vikapu kumi na viwili.

Petro Amkiri Bwana Yesu Kuwa Ndiye Kristo

18 Wakati mmoja, Yesu alipokuwa akiomba faraghani, nao wanafunzi wake wakiwa pamoja naye, akawauliza, “Watu husema mimi ni nani?”

19 Wakamjibu, “Wengine husema wewe ni Yohana Mbatizaji, wengine husema ni Eliya na wengine husema, wewe ni mmoja wa nabii wa kale aliyefufuka kutoka kwa wafu.”

20 Kisha akawauliza, “Je, ninyi mnasema mimi ni nani?”

# Petro akajibu, “Wewe ndiwe Kristowa Mungu.”

21 Yesu akawakataza wasimwambie mtu ye yote jambo hilo.

22 Yesu akasema, “Imempasa Mwana wa Adamu kupata mateso mengi na kukataliwa na wazee, viongozi wa makuhani na walimu wa sheria, naye atauawa na siku ya tatu atafufuka.”

23 Kisha akawaambia wote, “Ye yote anayetaka kunifuata ni lazima ajikane mwenyewe, achukue msalaba wake kila siku na anifuate.

24 Kwa maana ye yote atakayekuyaponya maisha yake atayapoteza, lakini ye yote atakayeyapoteza maisha yake kwa ajili yangu atayaokoa.

25 Je, itamfaidia nini mtu kuupata ulimwengu wote, lakini akayapoteza maisha yake?

26 Kama mtu ye yote akinionea aibu mimi na maneno yangu, Mwana wa Adamu atamwonea aibu mtu huyo atakapokuja katika utukufu wake na katika utukufu wa Baba na wa malaika watakatifu.

27 Amin, amin nawaambia, wako baadhi ya watu waliosimama hapa ambao hawataonja mauti mpaka watakapouona Ufalme wa Mungu.”

Bwana Yesu Abadilika Sura

28 Yapata siku nane baada ya Yesu kusema hayo, aliwachukua Petro, Yakobo na Yohana akaenda nao mlimani kuomba.

29 Alipokuwa akiomba, mwonekano wa sura yake ukabadilika, mavazi yake yakametameta kama mwanga wa umeme wa radi.

30 Ghafula wakawaona watu wawili, Mose na Eliya wakizungumza naye.

31 Walionekana katika utukufu wakizungumza na Yesu kuhusu kifo chake ambacho kingetokea huko Yerusalemu.

32 Petro na wenzake waliokuwa wamelala usingizi mzito walipoamka, wakaona utukufu wa Yesu na wale watu wawili waliokuwa wamesimama pamoja naye.

33 Mose na Eliya, walipokuwa wanaondoka, Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vizuri tukae hapa! Tutajenga vibanda vitatu, kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.” Lakini Petro alikuwa hajui asemacho.

34 Alipokuwa bado anazungumza, pakatokea wingu likawafunika, nao wakaogopa walipoingia mle kwenye wingu.

35 Sauti ikatoka kwenye lile wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa niliyemchagua, msikilizeni yeye.”

36 Baada ya sauti hiyo kusema, walimkuta Yesu akiwa peke yake. Wale wanafunzi wakalihifadhi jambo hili, wala kwa wakati huo hawakumwambia mtu ye yote yale waliyokuwa wameyaona.

Kuponywa Kwa Kijana Mwenye Pepo Mchafu

37 Kesho yake, waliposhuka kutoka mlimani, alikutana na umati mkubwa wa watu.

38 Mtu mmoja katika ule umati wa watu akapiga kelele, akasema, “Mwalimu, naomba umwangalie mwanangu, ndiye mtoto wangu wa pekee.

39 Mara kwa mara pepo mchafu humpagaa na kumfanya apige kelele, kisha humwangusha na kumtia kifafa akatokwa na povu kinywani. Huyo pepo mchafu anamtesa sana na hamwachi ila mara chache.

40 Niliwaomba wanafunzi wako wamtoe huyo pepo mchafu, lakini hawakuweza.”

41 Yesu akajibu akawaambia, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka, nitakaa nanyi na kuwavumilia mpaka lini? Mlete mwanao hapa.”

42 Hata yule mtoto alipokuwa akija, yule pepo mchafu akamwangusha, akamtia kifafa. Lakini Yesu akamkemea yule pepo mchafu amtoke, akamponya yule mtoto, akamrudisha kwa baba yake.

43 Watu wote wakastaajabia uweza mkuu wa Mungu. Wakati bado watu wanastaajabia hayo yote aliyokuwa akiyafanya Yesu, yeye akawaambia wanafunzi wake:

44 “Sikilizeni kwa makini haya nitakayowaambia sasa: Mwana wa Adamu atasalitiwa na kutiwa mikononi mwa watu.”

45 Lakini wao hawakuelewa alimaanisha nini. Maana ya maneno hayo ilifichika kwao, hivyo hawakuyaelewa, nao wakaogopa kumwuliza maana yake.

Ni Nani Atakayekuwa Mkubwa Kuliko Wote

46 Kukazuka mabishano miongoni mwa wanafunzi kuhusu ni nani miongoni mwao atakayekuwa mkuu kuliko wote.

47 Lakini Yesu akayatambua mawazo yao, akamchukua mtoto mdogo, akamsimamisha kando yake.

48 Kisha akawaambia, “Ye yote atakayemkaribisha mtoto huyu mdogo kwa Jina langu, atakuwa amenikaribisha mimi na ye yote atakayenikaribisha mimi, atakuwa amemkaribisha yeye aliyenituma, kwa maana yeye aliye mdogo miongoni mwenu, ndiye aliye mkuu kuliko wote.”

49 Yohana akasema, “Bwana, tumemwona mtu akitoa pepo wachafu kwa jina lako tukamzuia, kwa sababu yeye si mmoja wetu.”

50 Yesu akasema, “Msimzuie, kwa sababu ye yote ambaye si kinyume nanyi, yu upande wenu.”

Yesu Akataliwa Samaria

51 Wakati ulipokaribia wa yeye kuchukuliwa mbinguni, alikaza uso wake kwenda Yerusalemu.

52 Akatuma watu wamtangulie, nao wakaenda katika kijiji kimoja cha Samaria kumwandalia kila kitu,

53 lakini watu wa kijiji kile hawakumkaribisha kwa sababu alikuwa anakwenda zake Yerusalemu.

54 Wanafunzi wake, yaani, Yakobo na Yohana walipoona hayo, wakasema: “Bwana, unataka tuagize moto kutoka mbinguni ili uwaangamize?”

55 Yesu akageuka na kuwakemea,

56 nao wakaenda kijiji kingine.

Gharama Ya Kumfuata Yesu

57 Walipokuwa njiani wakienda, mtu mmoja akamwambia Yesu, “Nitakufuata ko kote uendako.”

58 Yesu akamjibu, “Mbweha wana mapango na ndege wa angani wana viota, lakini Mwana wa Adamu hana mahali pa kulaza kichwa chake.”

59 Yesu akamwambia mtu mwingine, “Nifuate.”

Mtu huyo akamjibu, “Bwana, niache kwanza nikamzike baba yangu.”

60 Yesu akamwambia, “Waache wafu wawazike wafu wao, bali wewe nenda ukautangaze Ufalme wa Mungu.”

61 Mtu mwingine akamwambia, “Bwana, nitakufuata lakini naomba kwanza nikaage jamaa yangu.”

62 Yesu akamwambia, “Mtu ye yote atiaye mkono wake kulima, kisha akatazama nyuma, hafai kwa Ufalme wa Mungu.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/9-d52862eaa4c999f7c98a7cdf165e1202.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

16 − 8 =