Luka 5

Kuitwa Kwa Wanafunzi Wa Kwanza

1 Siku moja Yesu alipokuwa amesimama karibu na Ziwa la Genesareti, watu wengi wakiwa wanasongana kumzunguka ili wapate kusikia neno la Mungu,

2 akaona mashua mbili ukingoni mwa ziwa, zikiwa zimeachwa hapo na wavuvi waliokuwa wanaosha nyavu zao.

3 Akaingia katika mojawapo ya hizo mashua ambayo ilikuwa ya Simoni, akamwomba aisogeze ndani ya maji kidogo kutoka pwani. Kisha akaketi na kufundisha watu akiwa mle ndani ya mashua.

4 Alipomaliza kunena, akamwambia Simoni, “Sasa peleka mashua hadi kilindini kisha mshushe nyavu zenu mkavue samaki.”

5 Simoni akamjibu, “Bwana, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha na hatukuvua cho chote. Lakini, kwa neno lako nitazishusha nyavu.”

6 Nao walipozishusha nyavu zao, wakavua samaki wengi sana, nyavu zao zikajaa zikaanza kukatika.

7 Wakawaashiria wavuvi wenzao kwenye ile mashua nyingine ili waje kuwasaidia. Wakaja, wakajaza mashua zote mbili samaki hata zikaanza kuzama.

8 Simoni Petro alipoona haya yaliyotukia alianguka miguuni mwa Yesu na kumwambia, “Bwana, ondoka kwangu, mimi ni mtu mwenye dhambi!”

9 Kwa kuwa yeye na wavuvi wenzake walikuwa wameshangazwa sana na wingi wa samaki waliokuwa wamepata,

10 vivyo hivyo wenzake Simoni, yaani, Yakobo na Yohana, wana wa Zebedayo walishangazwa pia.

Ndipo Yesu akamwambia Simoni, “Usiogope, tangu sasa utakuwa mvuvi wa watu.”

11 Hivyo wakasogeza mashua zao mpaka ufuoni mwa bahari, wakaacha kila kitu na kumfuata Yesu.

Yesu Amtakasa Mtu Mwenye Ukoma

12 Ikawa siku moja Yesu alipokuwa katika mji fulani, mtu mmoja mwenye ukoma mwili mzima akamjia. Alipomwona Yesu, alianguka chini mpaka uso wake ukagusa ardhi na kumsihi akisema, “Bwana, ukitaka waweza kunitakasa.”

13 Yesu akanyosha mkono wake akamgusa yule mtu, akamwambia, “Nataka, takasika!” Naye mara ukoma ukapona.

14 Yesu akamwagiza akisema, “Usimwambie mtu ye yote, bali nenda ukajionyeshe kwa kuhani na ukatoe dhabihu alizoagiza Mose ili kuwa ushuhuda kwao.”

15 Lakini habari zake Yesu zikazidi sana kuenea kotekote kuliko wakati mwingine wo wote, makutano makubwa ya watu yalikuwa yakikusanyika ili kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao.

16 Lakini mara kwa mara Yesu alijitenga nao ili kwenda mahali pa faragha kuomba.

Yesu Amponya Mtu Mwenye Kupooza

17 Siku moja Yesu alipokuwa akifundisha, Mafarisayo na walimu wa sheria, waliokuwa wametoka kila kijiji cha Galilaya na kutoka Uyahudi na Yerusalemu, walikuwa wameketi huko. Nao uweza wa Bwana ulikuwa juu yake kuponya wagonjwa.

18 Wakaja watu wamembeba mgonjwa aliyepooza kwenye mkeka. Wakajaribu kumwingiza ndani ili wamweke mbele ya Yesu.

19 Walipokuwa hawawezi kufanya hivyo kwa sababu ya umati wa watu, wakapanda juu ya paa, wakaondoa baadhi ya vigae, wakapata nafasi ya kumtelemsha yule mgonjwa kwa mkeka wake katikati ya ule umati pale pale mbele ya Yesu.

20 Yesu alipoiona imani yao, akamwambia yule mgonjwa, “Rafiki, dhambi zako zimesamehewa.”

21 Mafarisayo na wale walimu wa sheria wakaanza kuuliza, “Ni nani mtu huyu anayesema maneno ya makufuru? Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa Mungu peke yake?”

22 Yesu akijua mawazo yao akawauliza, “Kwa nini mnawaza haya mioyoni mwenu?

23 Je, ni lipi lililo rahisi zaidi, kumwambia huyu, ‘Umesamehewa dhambi zako,’ au kusema, ‘Simama, uende?’

24 Lakini ili mpate kujua ya kuwa Mwana wa Adamu anayo mamlaka duniani ya kusamehe dhambi,” Akamwambia yule aliyepooza, “Nakuambia, Simama, chukua mkeka wako uende nyumbani kwako.”

25 Mara yule mtu aliyekuwa amepooza akasimama mbele yao wote, akachukua mkeka wake akaenda zake nyumbani, huku akimtukuza Mungu.

26 Kila mmoja akashangaa na kumtukuza Mungu. Wakajawa na hofu ya Mungu, wakasema, “Leo tumeona mambo ya ajabu.”

Yesu Amwita Lawi

27 Baada ya haya Yesu alitoka na kumwona mtoza ushuru mmoja jina lake Lawi akiwa amekaa forodhani, mahali pake pa kukusanyia kodi, akamwambia, “Nifuate.”

28 Naye Lawi akaacha kila kitu, akaondoka, akamfuata.

29 Kisha Lawi akamfanyia Yesu karamu kubwa nyumbani kwake, nao umati mkubwa wa watoza ushuru na watu wengine walikuwa wakila pamoja nao.

30 Lakini Mafarisayo na walimu wa sheria ambao walikuwa wa madhehebu yao wakawalalamikia wanafunzi wa Yesu, wakisema, “Mbona mnakula na kunywa pamoja na watoza ushuru na wenye dhambi?”

31 Yesu akawajibu, “Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio wagonjwa.

32 Sikuja kuwaita wenye haki bali wenye dhambi wapate kutubu.”

Yesu Aulizwa Kuhusu Kufunga

33 Wakamwambia Yesu, “Wanafunzi wa Yohana na wa Mafarisayo mara kwa mara hufunga na kuomba, lakini wanafunzi wako wanaendelea kula na kunywa.”

34 Yesu akawajibu, “Je, mnaweza kuwafanya wageni wa bwana arusi kufunga wakati akiwa pamoja nao?

35 Lakini wakati utafika ambapo bwana arusi ataondolewa kwao, ndipo watakapofunga.”

36 Yesu akawapa mfano huu, akawaambia: “Hakuna mtu achanaye kiraka kutoka kwenye nguo mpya na kukishonea kwenye nguo kuukuu. Akifanya hivyo atakuwa amechana nguo mpya na kile kiraka hakitaendana na ile nguo kuukuu.

37 Hakuna mtu awekaye divai mpya kwenye viriba vikuukuu. Akifanya hivyo, hiyo divai mpya itapasua hivyo viriba nayo yote itamwagika.

38 Divai mpya lazima iwekwe kwenye viriba vipya.

39 Wala hakuna mtu anayependelea divai mpya baada ya kunywa divai ya zamani, husema, ‘Ile ya zamani ni nzuri zaidi.’ ”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/5-6c2cb629135db07e54ef56e942dbd4a5.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

11 − eight =