Luka 6

Bwana Wa Sabato

1 Ikawa siku moja ya Sabato Yesu alikuwa akipita katika mashamba ya nafaka, wanafunzi wake wakawa wakivunja masuke ya nafaka, wakayafikicha kwa mikono yao na kula punje zake.

2 Baadhi ya Mafarisayo wakawauliza, “Mbona mnafanya mambo ambayo ni kinyume na sheria siku ya Sabato?”

3 Yesu akawajibu, “Je, ninyi hamkusoma jinsi alivyofanya Daudi wakati yeye na wenzake walipokuwa na njaa?

4 Aliingia ndani ya nyumba ya Mungu, akaichukua ile mikate mitakatifu ambayo huliwa na makuhani peke yao. Naye pia akawapa wenzake wakala!”

5 Yesu akawaambia, “Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa Sabato.”

6 Ikawa siku nyingine ya Sabato Yesu aliingia ndani ya sinagogi akawa anafundisha, huko palikuwa na mtu ambaye mkono wake wa kuume ulikuwa umepooza.

7 Mafarisayo na walimu wa sheria walikuwa wakitafuta sababu ya kumshtaki Yesu, hivyo wakawa wanamwangalia kwa karibu ili waone kama ataponya katika siku ya Sabato.

8 Lakini Yesu alijua mawazo yao, hivyo akamwambia yule mwenye mkono uliopooza, “Inuka.” Hivyo yule mtu akainuka, akasimama mbele yao wote.

9 Ndipo Yesu akawaambia wale walimu wa sheria na Mafarisayo, akisema, “Nawauliza ninyi, ni lipi lililo halali siku ya Sabato, kutenda mema au kutenda mabaya? Kuokoa maisha au kuyaangamiza?”

10 Akawatazama watu wote waliokuwepo, kisha akamwambia yule aliyepooza mkono, “Nyosha mkono wako!” Akaunyosha na mkono wake ukawa tena mzima kabisa.

11 Wale wakuu wakakasirika sana, wakashauriana wao kwa wao, ni nini watakachomtendea Yesu.

Yesu Achagua Mitume Kumi Na Wawili

12 Ikawa katika siku hizo Yesu alikwenda mlimani kuomba, akakesha usiku kucha akimwomba Mungu.

13 Kulipopambazuka akawaita wanafunzi wake, naye akachagua kumi na wawili, ambao pia aliwaita mitume:

14 Simoni aliyemwita Petro, Andrea nduguye, Yakobo, Yohana, Filipo, Bartolomayo,

15 Mathayo, Tomasi. Yakobo mwana wa Alfayo, Simoni aliyeitwa Zelote,

16 Yuda mwana wa Yakobo na Yuda Iskariote, ambaye ndiye aliyemsaliti Yesu.

Yesu Aponya Wengi

17 Akashuka pamoja nao akasimama mahali penye uwanja tambarare. Hapo palikuwa na idadi kubwa ya wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu kutoka sehemu zote za Uyahudi, Yerusalemu na kutoka pwani ya Tiro na Sidoni,

18 waliokuwa wamekuja kumsikiliza na kuponywa magonjwa yao. Wale waliokuwa wakiteswa na pepo wachafu akawaponya.

19 Watu wote walikuwa wanajitahidi kumgusa kwa sababu nguvu zilikuwa zikimtoka na kuwaponya wote.

Baraka Na Ole

20 Akawatazama wanafunzi wake, akasema:

“Mmebarikiwa ninyi mlio maskini,

kwa sababu Ufalme wa Mbinguni ni wenu.

21 Mmebarikiwa ninyi mlio na njaa sasa,

kwa sababu mtashibishwa.

Mmebarikiwa ninyi mnaolia sasa,

kwa sababu mtacheka.

22 Mmebarikiwa ninyi, watu watakapowachukia,

watakapowatenga na kuwatukana

na kulikataa jina lenu kama neno ovu,

kwa ajili ya Mwana wa Adamu.

23 “Furahini na kurukaruka kwa shangwe kwa sababu thawabu yenu ni kubwa mbinguni, kwa kuwa hivyo ndivyo baba zao walivyowatenda manabii.

24 “Lakini ole wenu ninyi mlio matajiri,

kwa sababu mmekwisha kupokea faraja yenu.

25 Ole wenu ninyi mlioshiba sasa,

maana mtaona njaa.

Ole wenu ninyi mnaocheka sasa,

maana mtaomboleza na kulia.

26 Ole wenu watu watakapowasifu,

kwani ndivyo baba zao walivyowasifu

manabii wa uongo.

Wapendeni Adui Zenu

27 “Lakini nawaambia wale wanaonisikia, wapendeni adui zenu. Watendeeni mema wanaowachukia.

28 Wabarikini wale wanaowalaani, waombeeni wale wanaowatendea mabaya.

29 Kama mtu akikupiga shavu moja mgeuzie na la pili. Mtu akikunyang’anya koti lako, usimzuie kuchukua joho pia.

30 Mpe kila akuombaye na kama mtu akichukua mali yako usitake akurudishie.

31 Watendeeni wengine kama ambavyo mngetaka wawatendee ninyi.

32 “Kama mkiwapenda tu wale wanaowapenda, mwapata sifa gani? Hata wenye dhambi huwapenda wale wawapendao.

33 Tena mkiwatendea mema wale tu wanaowatendea ninyi mema mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ hufanya vivyo hivyo.

34 Tena mnapowakopesha wale tu mnaotegemea wawalipe, mwapata sifa gani? Hata ‘wenye dhambi’ huwakopesha wenye dhambi wenzao wakitarajia kulipwa mali yao yote.

35 Lakini wapendeni adui zenu, watendeeni mema, wakopesheni bila kutegemea kurudishiwa mlichokopesha. Ndipo thawabu yenu itakapokuwa kubwa, nanyi mtakuwa wana wa Aliye Juu Sana, kwa sababu yeye ni mwema kwa watu wasio na shukrani na waovu.

36 Iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.

Kuwahukumu Wengine

37 “Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa. Msilaumu, nanyi hamtalaumiwa. Sameheni, nanyi mtasamehewa.

38 Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.”

39 Pia akawapa mfano akasema, “Je, kipofu aweza kumwongoza kipofu? Je, wote wawili hawatatumbukia shimoni?

40 Mwanafunzi hamzidi mwalimu wake, ila yule aliyehitimu aweza kuwa kama mwalimu wake.

41 “Mbona unatazama kibanzi kilichoko ndani ya jicho la mwenzako nawe huoni boriti iliyoko ndani ya jicho lako?

42 Utawezaje kumwambia ndugu yako, ‘Ndugu yangu, niache nikitoe hicho kibanzi kilichoko ndani ya jicho lako’, wakati wewe mwenyewe huoni boriti iliyoko ndani ya jicho lako? Ewe mnafiki, ondoa kwanza boriti ndani ya jicho lako, ndipo utakapoweza kuona dhahiri jinsi ya kuondoa kibanzi kilichoko ndani ya jicho la ndugu yako.

Mti Na Mazao Yake

43 “Hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya wala hakuna mti mbaya uzaao matunda mazuri.

44 Kila mti hujulikana kwa matunda yake. Kwa maana watu hawachumi tini kwenye miiba wala zabibu kwenye michongoma.

45 Vivyo hivyo mtu mwema hutoa mambo mema kutoka kwenye hazina ya moyo wake, naye mtu mwovu hutoa mambo mabaya kutoka kwenye hazina ya moyo wake. Kwa kuwa mtu hunena kwa kinywa chake yale yaliyoujaza moyo wake.

Mjenzi Mwenye Busara Na Mjenzi Mpumbavu

46 “Kwa nini mnaniita, ‘Bwana, Bwana,’ nanyi hamfanyi ninayowaambia?

47 Nitawaonyesha jinsi alivyo mtu yule anayekuja kwangu na kusikia maneno yangu na kuyatenda.

48 Yeye ni kama mtu anayejenga nyumba, akachimba chini sana na kuweka msingi kwenye mwamba. Mafuriko yalipokuja, maji ya ghafula yakaipiga ile nyumba lakini haikutikisika, kwa sababu ilikuwa imejengwa vizuri juu ya mwamba.

49 Lakini yeye ayasikiaye maneno yangu na asiyatende ni kama mtu aliyejenga nyumba juu ya mchanga bila kuweka msingi. Mafuriko yalipoikumba nyumba ile, ikaanguka mara na kubomoka kabisa.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/6-e7ebcbfbee6a8349555d7a0f68c211ea.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

13 + fourteen =