Luka 7

Yesu Amponya Mtumishi Wa Jemadari

1 Baada ya Yesu kumaliza kusema haya yote watu wakiwa wanamsikiliza, akaingia Kapernaumu.

2 Mtumishi wa jemadari mmoja wa Kirumi, ambaye bwana wake alimthamini sana, alikuwa mgonjwa sana karibu ya kufa.

3 Jemadari huyo aliposikia habari za Yesu, aliwatuma wazee wa Kiyahudi kwake, wakamwomba aje kumponya mtumishi wa huyo jemadari.

4 Wale wazee walipofika kwa Yesu, wakamsihi sana amsaidie yule jemadari wakisema, “Mtu huyu anastahili wewe umfanyie jambo hili,

5 kwa sababu analipenda taifa letu tena ametujengea sinagogi.”

6 Hivyo Yesu akaongozana nao, lakini alipokuwa hayuko mbali na nyumbani, yule jemadari akatuma rafiki zake kumwambia Yesu, “Bwana, usijisumbue kwani mimi sistahili wewe kuingia chini ya dari yangu.

7 Ndiyo maana sikujiona ninastahili hata kuja kwako. Lakini sema neno tu, naye mtumishi wangu atapona.

8 Kwa kuwa mimi mwenyewe ni mtu niliyewekwa chini ya mamlaka, nikiwa na askari chini yangu. Nikimwambia huyu, ‘Nenda,’ yeye huenda; na huyu, ‘Njoo,’ yeye huja. Nikimwambia mtumishi wangu, ‘Fanya hili,’ yeye hufanya.”

9 Yesu aliposikia maneno haya alimshangaa sana, akaugeukia ule umati wa watu uliokuwa unamfuata, akawaambia, “Sijaona imani kubwa namna hii hata katika Israeli.”

10 Nao wale watu waliokuwa wametumwa kwa Yesu waliporudi nyumbani walimkuta yule mtumishi amepona.

Yesu Amfufua Mwana Wa Mjane

11 Baadaye kidogo, Yesu alikwenda katika mji mmoja ulioitwa Naini. Nao wanafunzi wake na umati mkubwa wa watu walikwenda pamoja naye.

12 Alipokaribia lango la mji, alikutana na watu waliokuwa wamebeba maiti wakitoka nje ya mji. Huyu aliyekufa alikuwa mwana pekee wa mwanamke mjane. Umati mkubwa wa watu wa mji ule ulikuwa pamoja na huyo mwanamke.

13 Bwana Yesu alipomwona yule mjane, moyo wake ulimhurumia, akamwambia, “Usilie.”

14 Kisha akasogea mbele akaligusa lile jeneza na wale waliokuwa wamelibeba wakasimama kimya. Akasema, “Kijana, nakuambia inuka.”

15 Yule aliyekuwa amekufa akaketi akaanza kuongea, naye Yesu akamkabidhi kwa mama yake.

16 Watu wote wakajawa na hofu ya Mungu, nao wakamtukuza Mungu wakisema, “Nabii mkuu ametokea miongoni mwetu, Mungu amekuja kuwakomboa watu wake.”

17 Habari hizi za mambo aliyofanya Yesu zikaenea Uyahudi wote na sehemu zote za jirani.

Yesu Na Yohana Mbatizaji

18 Wanafunzi wa Yohana Mbatizaji wakamweleza Yohana mambo haya yote. Hivyo Yohana akawaita wanafunzi wake wawili

19 na kuwatuma kwa Bwana ili kumwuliza, “Je, wewe ndiye yule ajaye, au tumtazamie mwingine?”

20 Wale watu walipofika kwa Yesu wakamwambia, “Yohana Mbatizaji ametutuma tukuulize, ‘Je, wewe ndiye yule ajaye au tumtazamie mwingine?’ ”

21 Wakati huo huo, Yesu aliwaponya wengi waliokuwa na magonjwa, maradhi na pepo wachafu, pia akawafungua vipofu wengi macho wakaona.

22 Hivyo akawajibu wale wajumbe, “Rudini mkamwambie Yohana yote mliyoyaona na kuyasikia. Vipofu wanaona, viwete wanatembea, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa na maskini wahubiriwa Habari Njema.

23 Amebarikiwa mtu yule asiyechukizwa nami.”

24 Wanafunzi wa Yohana walipoondoka, Yesu akaanza kuuambia ule umati wa watu kuhusu Yohana: “Mlipokwenda nyikani mlikwenda kuona nini? Je, ni unyasi ukipeperushwa na upepo?

25 Kama sivyo, mlikwenda kuona nini basi? Mtu aliyevaa mavazi ya fahari? La hasha, watu wanaovaa mavazi ya fahari na kuishi maisha ya anasa hukaa katika majumba ya kifalme.

26 Lakini mlikwenda kuona nini? Mlikwenda kumwona nabii? Naam! Nawaambia, tena zaidi ya nabii.

27 Huyu ndiye ambaye habari zake zimeandikwa:

“ ‘Tazama, namtuma mjumbe wangu akutangulie,

atakayeandaa njia mbele yako.’

28 Nawaambia, miongoni mwa wale waliozaliwa na mwanamke, hakuna aliye mkuu kuliko Yohana; lakini yeye aliye mdogo kabisa katika Ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana.”

29 (Watu wote hata watoza ushuru waliposikia maneno ya Yesu, walikubali kwamba mpango wa Mungu ni mwema, maana walikuwa wamebatizwa na Yohana.

30 Lakini Mafarisayo na wataalamu wa sheria walikataa mpango wa Mungu kwao kwa kutokukubali kubatizwa na Yohana.)

31 Yesu akawauliza, “Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Wanafanana na nini?

32 Wao ni kama watoto waliokaa sokoni wakiitana wao kwa wao wakisema:

“ ‘Tuliwapigia filimbi,

lakini hamkucheza,

tuliwaimbia nyimbo za maombolezo,

lakini hamkulia.’

33 Kwa maana Yohana Mbatizaji alikuwa hali mkate wala hanywi divai, ninyi mkasema, ‘Ana pepo mchafu,’

34 Mwana wa Adamu alikuja akila na kunywa, nanyi mnasema: ‘Mtazameni huyu mlafi na mlevi, rafiki wa watoza ushuru na “wenye dhambi.” ’

35 Nayo hekima imethibitishwa kuwa kweli na watoto wake wote.”

Yesu Apakwa Mafuta Na Mwanamke Mwenye Dhambi

36 Basi Farisayo mmoja alimwalika Yesu nyumbani kwake kwa chakula. Hivyo Yesu akaenda nyumbani mwa yule Farisayo na kukaa katika nafasi yake mezani.

37 Naye mwanamke mmoja kwenye ule mji, ambaye alikuwa mwenye dhambi, alipojua kwamba Yesu alikuwa akila chakula nyumbani kwa yule Farisayo, akaleta chupa ya marmar yenye manukato.

38 Yule mwanamke akiwa amesimama nyuma ya miguu ya Yesu akilia. Akailowanisha miguu yake kwa machozi yake, kisha akaifuta kwa nywele zake akaibusu na kuimiminia manukato.

39 Yule Farisayo aliyemwalika Yesu alipoona yanayotendeka, akawaza moyoni mwake, “Kama huyu mtu angekuwa nabii, angejua kwamba ni nani anayemgusa na kwamba yeye ni mwanamke wa namna gani na ya kuwa huyu mwanamke ni mwenye dhambi.”

40 Yesu akanena akamwambia, “Simoni, nina jambo la kukuambia.”

Simoni akajibu, “Mwalimu, sema.”

41 “Palikuwa na mtu mmoja aliyewakopesha watu wawili fedha: Mmoja alidaiwa dinari 500na mwingine dinari hamsini.

42 Wote wawili walipokuwa hawawezi kulipa, aliyafuta madeni yao wote wawili. Sasa ni yupi kati yao atakayempenda yule aliyewasamehe zaidi?”

43 Simoni akajibu, “Nadhani ni yule aliyesamehewa deni kubwa zaidi.”

Naye Yesu akamwambia, “Umehukumu kwa usahihi.”

44 Kisha akamgeukia yule mwanamke akamwambia Simoni, “Je, unamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani mwako, hukunipa maji ya kunawa miguu yangu, lakini huyu ameninawisha miguu kwa machozi yake na kunifuta kwa nywele zake.

45 Hukunisalimu kwa busu, lakini huyu mwanamke hajaacha kuibusu miguu yangu tangu nilipoingia.

46 Hukunipaka mafuta kichwani mwangu, lakini yeye ameipaka miguu yangu manukato.

47 Kwa hiyo, nakuambia, dhambi zake zilizokuwa nyingi zimesamehewa, kwani ameonyesha upendo mwingi. Lakini yule aliyesamehewa kidogo, hupenda kidogo.”

48 Kisha akamwambia yule mwanamke, “Dhambi zako simesamehewa.”

49 Lakini wale waliokuwa wameketi pamoja naye chakulani wakaanza kusemezana wao kwa wao, “Huyu ni nani ambaye hata anasamehe dhambi?”

50 Yesu akamwambia yule mwanamke, “Imani yako imekuokoa; nenda kwa amani.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/7-e68891695445d36e3d157be85994235a.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

sixteen − 14 =