Luka 8

Mfano Wa Mpanzi

1 Baada ya haya Yesu alikwenda akawa anazunguka katika miji na vijiji akihubiri habari njema za Ufalme wa Mungu. Wale wanafunzi wake kumi na wawili walikuwa pamoja naye,

2 pia baadhi ya wanawake waliokuwa wametolewa pepo wachafu na kuponywa magonjwa miongoni mwao alikuwepo Maria Magdalene, aliyetolewa pepo wachafu saba,

3 Yoana mkewe Kuza, msimamizi wa nyumba ya watu wa nyumbani mwa Herode, Susana na wengine wengi waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao.

4 Wakati umati mkubwa wa watu ulipokuwa ukija kwa Yesu kutoka mji hadi mji, akawaambia mfano huu:

5 “Mpanzi alitoka kwenda kusia mbegu zake. Alipokuwa akitawanya mbegu, nyingine zilianguka kando ya njia, zikakanyagwakanyagwa na ndege wa angani wakazila.

6 Mbegu nyingine zilianguka penye miamba, nazo zilipoota, hiyo mimea ikakauka kwa kukosa unyevu.

7 Nazo mbegu nyingine zilianguka kwenye miiba, ile miiba ikakua pamoja nazo na kusonga hiyo mimea ikafa.

8 Mbegu nyingine zilianguka penye udongo mzuri. Zikaota na kuzaa mara mia zaidi ya mbegu alizopanda.”

Baada ya kusema haya, Yesu akapaza sauti akasema, “Mwenye masikio ya kusikia na asikie.”

9 Wanafunzi wake wakamwuliza maana ya mfano huu.

10 Naye akasema, “Ninyi mmejaliwa kufahamu siri za Ufalme wa Mungu, lakini kwa wengine nazungumza kwa mifano, ili,

“ ‘ingawa wanaona, wasione;

ingawa wanasikia, wasielewe.’

11 “Maana ya mfano huu ni hii: Mbegu ni neno la Mungu.

12 Zile zilizoanguka kando ya njia, ni wale ambao husikia neno na ibilisi huja na kuliondoa kutoka mioyoni mwao, ili wasije wakaamini na kuokoka.

13 Zile za kwenye mwamba ni wale ambao hulipokea neno kwa furaha wanapolisikia, lakini hawana mizizi. Wanaamini kwa kitambo kidogo, lakini wakati wa kujaribiwa huiacha imani.

14 Zile mbegu zilizoanguka kwenye miiba ni mfano wa wale wanaosikia, lakini wanapoendelea husongwa na masumbufu ya maisha haya, utajiri na anasa, nao hawakui.

15 Lakini zile mbegu kwenye udongo mzuri ni mfano wa wale ambao hulisikia neno la Mungu na kulishika kwa moyo mnyofu na wa utii, nao kwa kuvumilia kwingi huzaa matunda.

Mfano Wa Taa

16 “Hakuna mtu awashaye taa na kuificha ndani ya gudulia au kuiweka mvunguni mwa kitanda. Badala yake, huiweka juu ya kinara, ili wale waingiao ndani waone mwanga.

17 Kwa maana hakuna jambo lo lote lililofichika ambalo halitafichuliwa, wala lo lote lililositirika ambalo halitajulikana na kuwekwa wazi.

18 Kwa hiyo, iweni waangalifu mnavyosikia. Kwa maana ye yote aliye na kitu atazidishiwa na ye yote asiye nacho, hata kile anachodhani anacho atanyang’anywa.”

Mama Yake Yesu Na Ndugu Zake

19 Wakati mmoja mama yake Yesu na ndugu zake walikuja kumwona, lakini hawakuweza kumfikia kwa sababu ya msongamano wa watu.

20 Mtu mmoja akamwambia, “Mama yako na ndugu zako wako nje wanataka kukuona.”

21 Yesu akamjibu, “Mama yangu na ndugu zangu ni wale wote wanaolisikia neno la Mungu na kulitii.”

Yesu Atuliza Dhoruba

22 Siku moja Yesu alipanda ndani ya mashua pamoja na wanafunzi wake, akawaambia, “Twendeni tuvuke mpaka ng’ambo ya ziwa.”

23 Hivyo walipokuwa wakienda, akalala usingizi. Dhoruba kali ikatokea mle ziwani, hata mashua ikawa inajaa maji, nao walikuwa katika hatari kubwa.

24 Wanafunzi wake wakamwendea na kumwamsha, wakipiga kelele, wakisema, “Bwana, Bwana, tunaangamia!”

Yeye akaamka akaukemea ule upepo na yale mawimbi, vikakoma, pakawa shwari.

25 Akawauliza wanafunzi wake, “Imani yenu iko wapi?”

Kwa woga na mshangao wakaulizana, “Huyu ni mtu wa namna gani ambaye anaamuru hata upepo na maji navyo vikamtii?”

Yesu Amponya Mtu Mwenye Pepo Mchafu

26 Basi wakafika katika nchi ya Wagerasi, ambayo iko upande wa pili wa ziwa kutoka Galilaya,

27 Yesu aliposhuka katika mashua na kukanyaga pwani, alikutana na mtu mmoja wa mji ule aliyekuwa amepagawa na pepo mchafu, naye kwa muda mrefu alikuwa havai nguo wala kuishi nyumbani, bali makaburini.

28 Alipomwona Yesu alipiga kelele, akajitupa chini mbele yake na kusema kwa sauti kuu, “Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu Aliye Juu Sana? Nakuomba, usinitese!”

29 Wakati huo Yesu alikuwa amemwamuru yule pepo mchafu amtoke huyo mtu. Mara nyingi huyo pepo mchafu alimpagaa na hata alipofungwa kwa minyororo mikono na miguu na kuwekwa chini ya ulinzi alikata hiyo minyororo na kupelekwa na huyo pepo mchafu kwenda nyikani.

30 Yesu akamwuliza, “Jina lako ni nani?”

# Akamjibu, “Legioni,”kwa kuwa alikuwa ameingiwa na pepo wachafu wengi mno.

31 Wale pepo wachafu wakamsihi sana asiwaamuru kwenda Shimoni.

32 Palikuwa na kundi kubwa la nguruwe hapo karibu wakilisha kandokando ya kilima. Wale pepo wachafu wakamsihi Yesu awaruhusu wawaingie hao nguruwe, naye akawaruhusu.

33 Wale pepo wachafu walipomtoka yule mtu, wakawaingia wale nguruwe, nalo kundi lote likatelemkia gengeni likatumbukia ziwani na kuzama.

34 Wale watu waliokuwa wakichunga lile kundi la nguruwe walipoona yaliyotukia, wakakimbia, wakaeneza habari hizi mjini na mashambani.

35 Nao watu wakatoka kwenda kujionea wenyewe yaliyotukia. Walipofika hapo alipokuwa Yesu wakamkuta yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu amekaa karibu na Yesu, akiwa amevaa nguo na mwenye akili timamu! Wakaogopa sana.

36 Wale walioona mambo hayo wakawaeleza wenzao jinsi yule mtu aliyekuwa amepagawa na pepo wachafu alivyoponywa.

37 Ndipo watu wote wa nchi ile ya Wagerasi wakamwomba Yesu aondoke kwao, kwa sababu walikuwa wamejawa na hofu. Basi akaingia katika mashua akaondoka zake.

38 Yule mtu aliyetokwa na pepo wachafu akamsihi Yesu afuatane naye, lakini Yesu akamuaga, akamwambia:

39 “Rudi nyumbani ukawaeleze mambo makuu Mungu aliyokutendea.” Kwa hiyo yule mtu akaenda, akatangaza katika mji wote mambo makuu Yesu aliyomtendea.

Msichana Afufuliwa Na Mwanamke Aponywa

40 Basi Yesu aliporudi, umati mkubwa wa watu ukampokea kwa furaha, kwani walikuwa wakimngojea.

41 Kisha mtu mmoja jina lake Yairo, kiongozi wa sinagogi, akaja na kuanguka miguuni mwa Yesu, akimwomba afike nyumbani kwake,

42 kwa kuwa binti yake wa pekee, mwenye umri wa miaka kumi na miwili, alikuwa anakufa.

Yesu alipokuwa akienda, umati wa watu ukamsonga sana.

43 Katika umati huo alikuwepo mwanamke mmoja aliyekuwa anatokwa damu kwa muda wa miaka kumi na miwili, tena alikuwa amegharimia yote aliyokuwa nayo kwa ajili ya matibabu, wala hakuna ye yote aliyeweza kumponya.

44 Huyo mwanamke akaja kwa nyuma na kugusa upindo wa vazi la Yesu, mara kutokwa damu kwake kukakoma.

45 Yesu akauliza, “Ni nani aliyenigusa?”

Watu wote walipokana, Petro akasema, “Bwana, huu umati wa watu unakusonga na kukusukuma kila upande.”

46 Lakini Yesu akasema, “Kuna mtu aliyenigusa, kwa maana nimetambua kuwa nguvu zimenitoka.”

47 Yule mwanamke alipofahamu ya kuwa hawezi kuendelea kujificha, alikuja akitetemeka, akaanguka miguuni mwa Yesu, akaeleza mbele ya watu wote kwa nini alimgusa na jinsi alivyoponywa mara.

48 Basi Yesu akamwambia, “Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani.”

49 Yesu alipokuwa bado anasema, akaja mtumishi kutoka nyumbani kwa Yairo, yule kiongozi wa sinagogi, kumwambia, “Binti yako amekwisha kufa. Usiendelee kumsumbua Mwalimu.”

50 Yesu aliposikia jambo hili, akamwambia Yairo, “Usiogope, amini tu, naye binti yako atapona.”

51 Walipofika nyumbani kwa Yairo, hakumruhusu mtu ye yote aingie ndani pamoja naye isipokuwa Petro, Yakobo na Yohana, baba na mama wa yule binti.

52 Wakati ule ule watu wote walikuwa wakilia na kuomboleza kwa ajili ya huyo binti. Yesu akawaambia, “Acheni kulia. Huyu binti hajafa ila amelala.”

53 Wao wakamcheka kwa dharau, wakijua kuwa amekwisha kufa.

54 Yesu akamshika yule binti mkono na kuita, “Binti, amka!”

55 Roho yake ikamrudia, naye akainuka mara. Akaamuru apewe kitu cho chote cha kula.

56 Wazazi wake wakastaajabu sana, lakini Yesu akawakataza wasimwambie mtu ye yote juu ya yale yaliyotukia.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LUK/8-229bb434a8336977af1bb3901b8b96f4.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

13 + eighteen =