Mambo ya Walawi 16

Siku Ya Upatanisho

1 Bwanaakasema na Mose baada ya kifo cha wana wawili wa Aroni waliokufa walipokaribia mbele zaBwana.

2 Bwanaakamwambia Mose: “Mwambie ndugu yako Aroni asije wakati wo wote atakavyo yeye ndani ya Patakatifu pa Patakatifu nyuma ya pazia mbele ya kiti cha rehema kile kilichoko juu ya Sanduku la Agano, la sivyo atakufa, kwa sababu huwa ninatokea ndani ya wingu juu ya kile kiti cha rehema.

3 “Hivi ndivyo Aroni atakavyoingia katika mahali patakatifu: akiwa na fahali mchanga kwa ajili ya sadaka ya dhambi na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.

4 Atavaa koti takatifu la kitani, pamoja na nguo za ndani za kitani; atafunga mshipi wa kitani kiunoni, na kuvaa kilemba cha kitani. Haya ni mavazi matakatifu, kwa hiyo ni lazima aoge kwa maji kabla ya kuyavaa mavazi hayo.

5 Atachukua mbuzi dume wawili kutoka kwa jumuiya ya Kiisraeli kwa ajili ya sadaka ya dhambi na kondoo dume kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa.

6 “Aroni atamtoa huyo fahali kwa ajili ya sadaka yake ya dhambi ili afanye upatanisho kwa ajili yake mwenyewe na nyumba yake.

7 Kisha atawachukua wale mbuzi waume wawili na kuwaleta mbele zaBwanakwenye ingilio la Hema la Kukutania.

8 Atapiga kura kwa ajili ya hao mbuzi wawili, mmoja kwa ajili yaBwanana mwingine kwa ajili ya Azazeli.

9 Aroni atamleta yule mbuzi ambaye kura yaBwanaimemwangukia na kumtoa dhabihu kwa ajili ya sadaka ya dhambi.

10 Lakini mbuzi aliyechaguliwa kwa kura kuwa wa Azazeli atatolewa akiwa hai mbele zaBwanaatumike kwa kufanya upatanisho kwa kumwacha aende jangwani kama aliyebebeshwa dhambi.

11 “Aroni atamleta yule fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi yake mwenyewe ili kufanya upatanisho kwa ajili yake na nyumba yake, naye atamchinja huyo fahali kwa ajili ya sadaka ya dhambi yake mwenyewe.

12 Atachukua chetezo kilichojaa makaa yanayowaka kutoka madhabahuni mbele zaBwanana konzi mbili za uvumba laini uliosagwa vizuri wenye harufu na kuvipeleka nyuma ya pazia.

13 Ataweka uvumba juu ya moto mbele zaBwana, na moshi wa uvumba utafunika kile kiti cha rehema kilicho juu ya Ushuhuda, ili kwamba asife.

14 Atachukua sehemu ya damu ya fahali na kwa kidole chake atanyunyiza sehemu ya mbele ya kiti cha rehema; kisha atanyunyiza sehemu ya hiyo damu kwa kidole chake mara saba mbele ya kiti cha rehema.

15 “Kisha atamchinja mbuzi wa sadaka ya dhambi kwa ajili ya watu na kuichukua damu yake nyuma ya pazia aifanyie kama alivyofanya kwa damu ya fahali: Atanyunyiza juu ya kiti cha rehema na mbele yake.

16 Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu kwa sababu ya unajisi na uasi wa Waisraeli, kwa dhambi zao zo zote. Atafanya hivyo kwa ajili ya Hema la Kukutania ambalo liko miongoni mwao katikati ya unajisi wao.

17 Mtu ye yote haruhusiwi kuwa ndani ya Hema la Kukutania kuanzia wakati Aroni anapoingia kufanya upatanisho katika Patakatifu pa Patakatifu mpaka atakapotoka nje, baada ya kujifanyia upatanisho yeye mwenyewe, nyumba yake pamoja na jumuiya yote ya Israeli.

18 “Kisha atatoka kuja kwenye madhabahu ile iliyo mbele zaBwanana kufanya upatanisho kwa ajili yake. Atachukua sehemu ya damu ya fahali na sehemu ya damu ya mbuzi na kuiweka kwenye pembe za madhabahu.

19 Atanyunyiza baadhi ya hiyo damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba ili kuitakasa na kuiweka wakfu kutokana na unajisi wa Waisraeli.

20 “Aroni atakapokuwa amemaliza kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, atamleta mbele yule mbuzi aliye hai.

21 Ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha mbuzi aliye hai na kuungama juu yake uovu wote na uasi wa Waisraeli, yaani dhambi zao zote, kisha kuziweka juu ya kichwa cha huyo mbuzi. Atamwachia huyo mbuzi akimbilie jangwani kwa uangalizi wa mtu aliyepewa wajibu huo.

22 Yule mbuzi atachukua juu yake dhambi zao zote mpaka mahali pasipo na watu; naye yule mtu atamwachia akimbilie jangwani.

23 “Kisha Aroni atakwenda ndani ya Hema la Kukutania na kuvua yale mavazi ya kitani aliyoyavaa kabla ya kuingia katika Patakatifu pa Patakatifu, naye atayaacha pale.

24 Ataoga kwa maji mahali patakatifu na kuvaa mavazi yake ya kawaida. Kisha atatoka na kutoa dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa kwa ajili yake na sadaka ya kuteketezwa kwa ajili ya watu, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake na kwa ajili ya watu.

25 Pia atachoma mafuta ya mnyama wa sadaka ya dhambi juu ya madhabahu.

26 “Yule mtu anayemwachia yule mbuzi wa Azazeli ni lazima afue nguo zake na kuoga kwa maji; baadaye anaweza kuingia kambini.

27 Yule fahali na mbuzi aliyetolewa kwa ajili ya sadaka za dhambi, ambao damu yao ilikuwa imeletwa Patakatifu pa Patakatifu kwa ajili ya kufanya upatanisho, ni lazima watolewe nje ya kambi; ngozi zao, nyama, na matumbo yake pamoja na mavi vitateketezwa kwa moto.

28 Mtu atakayevichoma ni lazima afue nguo zake na aoge kwa maji; baadaye ataweza kuingia kambini.

29 “Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu: Katika siku ya kumi ya mwezi wa saba ni lazima mfunge wala msifanye kazi yo yote akiwa mzaliwa au mgeni anayeishi miongoni mwenu,

30 kwa sababu siku hii upatanisho utafanyika kwa ajili yenu ili kuwatakasa. Kisha, mbele zaBwana, mtakuwa safi kutokana na dhambi zenu zote.

31 Ni Sabato ya mapumziko, ni lazima mfunge; ni agizo la kudumu.

32 Kuhani ambaye ametiwa mafuta na kuwekwa wakfu ili kuingia mahali pa baba yake kama Kuhani Mkuu atafanya upatanisho. Atavaa mavazi matakatifu ya kitani,

33 na kufanya upatanisho kwa ajili ya Patakatifu pa Patakatifu, Hema la Kukutania na madhabahu, pia kwa ajili ya makuhani pamoja na jumuiya yote ya watu.

34 “Hili litakuwa agizo la kudumu kwa ajili yenu: Upatanisho utafanywa mara moja tu kwa mwaka kwa ajili ya dhambi zote za Waisraeli.”

Ndivyo ilivyofanyika, kama vileBwanaalivyomwamuru Mose.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/LEV/16-92910585a8733c242150f6080019d6ce.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

five × three =