Obadia 1

1 Maono ya Obadia.

Hili ndilo asemaloBwanaMwenyezi kuhusu Edomu:

Tumesikia ujumbe kutoka kwaBwana:

Mjumbe alitumwa kwa mataifa kusema,

“Inukeni, na twendeni tukapigane vita dhidi ya Edomu.”

2 “Angalieni, nitawafanya wadogo miongoni mwa mataifa,

mtadharauliwa kabisa.

3 Kiburi cha moyo wako kimekudanganya,

wewe unayeishi kwenye nyufa za miamba

na kufanya makao yako juu,

wewe unayejiambia mwenyewe,

‘Ni nani awezaye kunishusha chini?’

4 Ingawa unapaa juu kama tai

na kufanya kiota chako kati ya nyota,

kutoka huko nitakushusha chini,”

asemaBwana.

5 “Ikiwa wevi wangekuja kwako,

ikiwa wanyang’anyi wangekujia usiku:

Lo! Tazama ni maafa kiasi gani yangekuwa yanakungojea:

je, si wangeiba tu kiasi kile wanachotaka?

Kama wachuma zabibu wangekuja kwako,

je, wasingebakiza zabibu chache?

6 Lakini tazama ni jinsi gani Esau atatekwa,

hazina zake zilizofichwa zitatekwa nyara!

7 Wote ulioungana nao watakufukuza hadi mpakani,

rafiki zako watakudanganya na kukushinda,

wale wanaokula mkate wako watakutegea mtego

lakini hutaweza kuugundua.

8 “Katika siku hiyo,” asemaBwana,

“je, sitaangamiza watu wenye hekima wa Edomu,

watu wenye ufahamu katika milima ya Esau?

9 Ee Temani, mashujaa wako watatiwa hofu,

kila mmoja katika milima ya Esau

ataangushwa chini kwa kuchinjwa.

10 Kwa sababu ya jeuri uliyofanya dhidi ya ndugu yako Yakobo,

aibu itakufunika;

utaangamizwa milele.

11 Siku ile ulisimama mbali ukiangalia

wakati wageni walipojichukulia utajiri wake

na watu wa nchi nyingine walipoingia malango yake

wakipiga kura kwa ajili ya Yerusalemu,

ulikuwa kama mmoja wao.

12 Usingemdharau ndugu yako

katika siku ya msiba wake,

wala kufurahia juu ya watu wa Yuda

katika siku ya maangamizi yao,

wala kujigamba sana

katika siku ya taabu yao.

13 Usingeingia katika malango ya watu wangu

katika siku ya maafa yao,

wala kuwadharau katika janga lao

katika siku ya maafa yao,

wala kunyang’anya mali zao

katika siku ya maafa yao.

14 Usingengoja kwenye njia panda

na kuwaua wakimbizi wao,

wala kuwatoa watu wake waliosalia

katika siku ya shida yao.

15 “Siku yaBwanai karibu

kwa mataifa yote.

Kama ulivyofanya, nawe utafanyiwa vivyo hivyo,

matendo yako yatakurudia juu ya kichwa chako.

16 Kama vile ulivyokunywa juu ya mlima wangu mtakatifu,

vivyo hivyo mataifa yote watakunywa mfululizo,

watakunywa na kunywa,

nao watatoweka kana kwamba hawajawahi kuwepo.

17 Lakini katika Mlima Sayuni kutakuwepo

na wale watakaookoka;

nao utakuwa mtakatifu,

nayo nyumba ya Yakobo

itamiliki urithi wake.

18 Nyumba ya Yakobo itakuwa moto,

na nyumba ya Yosefu itakuwa mwali wa moto;

nayo nyumba ya Esau itakuwa bua kavu,

nao wataiwasha moto na kuiteketeza.

Hakutakuwa na watakaosalimika

kutoka katika nyumba ya Esau.”

Bwanaamesema.

19 Watu kutoka nchi ya Negebu

wataikalia milima ya Esau,

na watu kutoka mitelemko ya vilima

watamiliki nchi ya Wafilisti.

Watayakalia mashamba ya Efraimu na Samaria,

naye Benyamini atamiliki Gileadi.

20 Kundi la Waisraeli walioko uhamishoni Kanaani

watarudi na kumiliki nchi mpaka Sarepta.

Walioko uhamishoni Sefaradi kutoka Yerusalemu

watamiliki miji ya Negebu.

21 Waokoaji watakwea juu ya Mlima Sayuni

kutawala milima ya Esau.

Nao ufalme utakuwa waBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/OBA/1-4e079caae500ce55bfd86928b26e6194.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

13 + twelve =