Wimbo Ulio Bora 3

1 Usiku kucha kwenye kitanda changu

nilimtafuta yule moyo wangu umpendaye;

nilimtafuta huyo mwanaume lakini sikumpata.

2 Sasa nitaondoka na kuzunguka mjini,

kupitia katika barabara zake

na viwanjani;

nitamtafuta yule moyo wangu umpendaye.

Kwa hiyo nilimtafuta

lakini sikumpata huyo mwanaume.

3 Walinzi walinikuta

walipokuwa wakizunguka mji.

Nikawauliza, “Je, mmemwona

yule moyo wangu umpendaye?”

4 Kitambo kidogo tu baada ya kuwapita

nilimpata yule moyo wangu umpendaye.

Nilimshika na sikumwachia aende mpaka nilipomleta

katika nyumba ya mama yangu,

katika chumba cha yule aliyenichukua mimba.

5 Binti za Yerusalemu, ninawaagiza

kwa paa na kwa ayala wa shambani:

Msichochee wala kuamsha mapenzi

hata yatakapotaka yenyewe.

6 Ni nani huyu anayekuja kutoka jangwani

kama nguzo ya moshi,

anayenukia manemane na uvumba

iliyotengenezwa kwa vikolezo vyote

vya mfanyabiashara?

7 Tazama! Ni gari la Solomoni

lisindikizwalo na mashujaa sitini,

walio wakuu sana wa Israeli,

8 wote wamevaa panga,

wote wazoefu katika vita,

kila mmoja na upanga wake pajani,

wamejiandaa kwa ajili ya hofu za usiku.

9 Mfalme Solomoni alijitengenezea gari;

alitengeneza kwa mbao kutoka Lebanoni.

10 Nguzo zake alitengeneza za fedha,

kitako chake kwa dhahabu.

Kiti chake kilikuwa kimepambwa kwa zambarau,

gari lake limenakishiwa njumu,

kwa ndani limefunikwa kwa upendo

wa binti za Yerusalemu.

11 Tokeni nje, ninyi binti za Sayuni,

mumtazame Mfalme Solomoni

akiwa amevaa taji,

taji ambalo mama yake alimvika

siku ya arusi yake,

siku ambayo moyo wake ulishangilia.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/SNG/3-92b9f3c5a11759d9568a6fa395eeeddb.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

2 × two =