Wimbo Ulio Bora 4

1 Tazama jinsi ulivyo mzuri, mpenzi wangu!

O, jinsi ulivyo mzuri!

Macho yako nyuma ya shela yako

ni kama ya hua.

Nywele zako ni kama kundi la mbuzi

zikishuka kutoka Mlima Gileadi.

2 Meno yako ni kama kundi la kondoo

waliokatwa manyoya sasa hivi,

watokao kuogeshwa.

Kila mmoja ana pacha lake,

hakuna hata mmoja aliye peke yake.

3 Midomo yako ni kama uzi mwekundu,

kinywa chako kinapendeza.

Mashavu yako nyuma ya shela yako

ni kama vipande viwili vya komamanga.

4 Shingo yako ni kama mnara wa Daudi,

uliojengwa kwa madaha,

juu yake zimetundikwa ngao elfu,

zote ni ngao za mashujaa.

5 Matiti yako mawili ni kama wana paa wawili,

kama mapacha ya wana paa

wale wajilishao katikati ya yungiyungi.

6 Hata papambazuke na vivuli vikimbie,

nitakwenda kwenye mlima wa manemane

na kwenye kilima cha uvumba.

7 Wewe ni mzuri kote, mpenzi wangu,

hakuna hitilafu ndani yako.

8 Twende pamoja nami kutoka Lebanoni,

bibi arusi wangu,

twende pamoja nami kutoka Lebanoni.

Shuka kutoka ncha ya Amana,

kutoka juu ya Seniri, kilele cha Hermoni,

kutoka mapango ya simba

na kutoka mlima wapendapo kukaa chui.

9 Umeiba moyo wangu, dada yangu,

bibi arusi wangu;

umeiba moyo wangu

kwa mtupo mmoja wa macho yako,

kwa kito kimoja cha thamani cha mkufu wako.

10 Tazama jinsi pendo lako linavyofurahisha,

dada yangu, bibi arusi wangu!

Ni mara ngapi zaidi pendo lako linafurahisha kuliko divai,

na harufu ya manukato yako zaidi

kuliko kikolezo cho chote!

11 Midomo yako inadondosha utamu kama sega la asali,

bibi arusi wangu;

maziwa na asali viko chini ya ulimi wako.

Harufu nzuri ya mavazi yako ni kama ile ya Lebanoni.

12 Wewe ni bustani iliyofungwa, dada yangu,

bibi arusi wangu;

wewe ni chanzo cha maji

kilichozungushiwa kabisa,

chemchemi yangu peke yangu.

13 Mimea yako ni bustani ya komamanga

yenye matunda mazuri sana,

yenye hina na nardo,

14 nardo na zafarani,

mchai na mdalasini,

pamoja na kila aina ya mti wa uvumba,

manemane na udi,

na aina zote za vikolezo bora kuliko vyote.

15 Wewe ni chemchemi ya bustani,

kisima cha maji yatiririkayo,

yatiririkayo kutoka Lebanoni.

16 Amka, upepo wa kaskazini,

na uje, upepo wa kusini!

Vuma juu ya bustani yangu,

ili harufu yake nzuri iweze kuenea mpaka ng’ambo.

Mpendwa wangu na aje bustanini mwake

na kuonja matunda mazuri sana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/SNG/4-b7bfa511541d24823c02d513c04318ac.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

12 + 3 =