Wimbo Ulio Bora 5

1 Nimekuja kwenye bustani yangu, dada yangu,

bibi arusi wangu;

nimekusanya manemane yangu pamoja

na kikolezo changu.

Nimekula sega langu la asali na asali yangu;

nimekunywa divai yangu na maziwa yangu.

Kuleni, enyi marafiki, mnywe;

kunyweni ya kutosha, Ee wapenzi.

2 Nililala lakini moyo wangu ulikuwa macho.

Sikiliza! Mpenzi wangu anabisha:

“Nifungulie, dada yangu, mpenzi wangu,

hua wangu, asiye na hitilafu.

Kichwa changu kimeloa umande,

na nywele zangu manyunyu ya usiku.”

3 Nimevua joho langu:

je, ni lazima nivae tena?

Nimenawa miguu yangu:

je, ni lazima niichafue tena?

4 Mpenzi wangu aliweka mkono wake kwenye tundu la komeo;

moyo wangu ulianza kugonga kwa ajili yake.

5 Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu,

mikono yangu ilidondosha manemane,

vidole vyangu vikitiririka manemane,

penye vipini vya komeo.

6 Nilimfungulia mpenzi wangu,

lakini mpenzi wangu alishaondoka;

alikuwa amekwenda zake.

Moyo wangu ulishuka kwa kuondoka kwake.

Nilimtafuta lakini sikumpata.

Nilimwita lakini hakunijibu.

7 Walinzi walinikuta

walipokuwa wakifanya zamu za ulinzi mjini.

Walinipiga, walinijeruhi,

walininyang’anya joho langu,

hao walinzi wa kuta!

8 Enyi binti za Yerusalemu, ninawaagiza:

kama mkimpata mpenzi wangu,

mtamwambia nini?

Mwambieni ninazimia kwa mapenzi.

9 Je, mpendwa wako ni bora kuliko wengine namna gani,

ni mzuri sana kupita wanawake wote?

Je, mpendwa wako ni mzuri kuliko wengine,

kwa namna gani,

hata unatuagiza hivyo?

10 Mpenzi wangu anang’aa tena mwekundu kwa afya,

wakuvutia miongoni mwa wanaume kumi elfu.

11 Kichwa chake ni dhahabu safi kuliko zote,

nywele zake ni za mawimbi

na ni nyeusi kama kunguru.

12 Macho yake ni kama ya hua

kandokando ya vijito vya maji,

aliyeogeshwa kwenye maziwa,

yamepangwa kama vito vya thamani.

13 Mashavu yake ni kama matuta ya vikolezo

yakitoa manukato.

Midomo yake ni kama yungiyungi

inayodondosha manemane.

14 Mikono yake ni fimbo za dhahabu

iliyopambwa kwa Krisolitho.

Mwili wake ni kama pembe ya ndovu iliyong’arishwa

iliyopambwa na yakuti samawi.

15 Miguu yake ni nguzo za marmar

zilizosimikwa katika vitako vya dhahabu safi.

Sura yake ni kama Lebanoni,

mzuri kama miti yake ya mierezi.

16 Kinywa chake chenyewe ni utamu,

kwa ujumla yeye ni wa kupendeza.

Huyu ndiye mpenzi wangu, huyu ndiye rafiki yangu,

Ee binti za Yerusalemu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/SNG/5-ecc48cc679f9d87d8ca6243ded71bc45.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

seventeen − 8 =