Yeremia 10

Mungu Na Sanamu

1 Sikieni lile ambaloBwana, anena nanyi Ee nyumba ya Israeli.

2 Hili ndilo asemaloBwana:

“Usijifunze njia za mataifa

wala usitishwe na ishara katika anga,

ingawa mataifa yanatishwa nazo.

3 Kwa maana desturi za mataifa hazina maana,

wanakata mti kutoka msituni

na fundi anauchonga kwa patasi.

4 Wanaparemba kwa fedha na dhahabu,

wanakikaza kwa nyundo

na misumari ili kisitikisike.

5 Sanamu zao ni kama sanamu

iliyowekwa shambani kutishia ndege

kwenye shamba la matango,

nazo haziwezi kuongea; sharti zibebwe

kwa sababu haziwezi kutembea.

Usiziogope; haziwezi kudhuru

wala kutenda lo lote jema.”

6 Hakuna aliye kama wewe, EeBwana;

wewe ni mkuu,

jina lako ni lenye nguvu katika uweza.

7 Ni nani ambaye haimpasi kukuheshimu wewe,

Ee mfalme wa mataifa?

Hii ni stahili yako.

Miongoni mwa watu wote wenye hekima

katika mataifa na katika falme zao zote,

hakuna aliye kama wewe.

8 Wote hawana akili tena ni wapumbavu,

wanafundishwa na sanamu za miti

zisizofaa lo lote.

9 Huleta fedha iliyofuliwa kutoka Tarshishi

na dhahabu kutoka Ufazi.

Kile ambacho fundi na sonara wametengeneza

huvikwa mavazi ya rangi

ya samawi na urujuani:

vyote vikiwa vimetengenezwa

na mafundi stadi.

10 LakiniBwanani Mungu wa kweli,

yeye ndiye Mungu aliye hai,

Mfalme wa milele.

Akiwa amekasirika, dunia hutetemeka,

mataifa hayawezi kustahimili hasira yake.

11 “Waambie hivi: ‘Miungu hii, ambayo haikuumba mbingu na dunia, itaangamia kutoka duniani na kutoka chini ya mbingu.’ ”

12 Lakini Mungu aliiumba dunia kwa uweza wake,

akaufanya ulimwengu kwa hekima yake

na kwa ufahamu wake akazitandaza mbingu.

13 Atoapo sauti yake, maji yaliyo katika mbingu hunguruma;

huyafanya mawingu yainuke

kutoka miisho ya dunia.

Hupeleka umeme wa radi pamoja na mvua

naye huleta upepo kutoka katika ghala zake.

14 Kila mmoja ni mjinga na hana maarifa,

kila sonara ameaibishwa na sanamu zake.

Vinyago vyake ni madanganyo,

wala havina pumzi ndani yake.

15 Havina maana, ni vitu vya mzaha tu,

hukumu yao itakapokuja, wataangamia.

16 Yeye aliye Fungu la Yakobo si kama hivi,

kwani ndiye Muumba wa vitu vyote,

pamoja na Israeli, kabila la urithi wake:

BwanaMwenye Nguvu Zote ndilo jina lake.

Maangamizi Yajayo

17 Kusanyeni mali na vitu vyenu muondoke katika nchi hii,

enyi mnaoishi katika hali ya kuzingirwa na jeshi.

18 Kwa kuwa hili ndilo asemaloBwana:

“Wakati huu, nitawatupa nje kwa nguvu

wote waishio katika nchi hii;

nitawataabisha ili waweze kutekwa.”

19 Ole wangu mimi kwa ajili ya kuumia kwangu!

Jeraha langu ni kubwa!

Lakini nilisema,

“Kweli hii ni adhabu yangu,

nami sharti nistahimili.”

20 Hema langu limeangamizwa;

kamba zake zote zimekatwa.

Wana wangu wametekwa

na hawapo tena;

hakuna hata mmoja aliyebaki

kulisimika hema langu

wala wa kusimamisha kibanda changu.

21 Wachungaji hawana akili

wala hawamuliziBwana,

hivyo hawastawi

na kundi lao lote la kondoo

na mbuzi limetawanyika.

22 Sikilizeni! Taarifa inakuja:

ghasia kubwa kutoka nchi ya kaskazini!

Hii itafanya miji ya Yuda kuwa ukiwa,

makao ya mbweha.

Maombi Ya Yeremia

23 Ninajua, EeBwana, kwamba maisha ya mwanadamu

si yake mwenyewe;

hawezi kuziongoza hatua zake mwenyewe.

24 Unirudi, EeBwana,

lakini kwa kipimo cha haki:

si katika hasira yako,

usije ukaniangamiza.

25 Umwage ghadhabu yako juu ya mataifa

yale wasiokujua wewe,

juu ya mataifa yale wasioliitia jina lako.

Kwa kuwa wamemwangamiza Yakobo;

wamemwangamiza kabisa

na kuiharibu nchi yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/10-9deb23e784a2afef2cdc83b7e2f888c3.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twelve + sixteen =