Yeremia 9

1 Laiti kichwa changu kingekuwa chemchemi ya maji

na macho yangu yangekuwa kisima cha machozi!

Ningelia mchana na usiku

kwa kuuawa kwa watu wangu.

2 Laiti ningekuwa na nyumba

ya kukaa wasafiri katika jangwa,

ningewaacha watu wangu

na kwenda mbali nao,

kwa kuwa wote ni wazinzi,

kundi la watu wasio waaminifu.

3 “Huweka tayari ndimi zao kama upinde,

ili kurusha uongo;

wamekuwa na nguvu katika nchi

kwa ajili ya uongo,

wala si katika kweli.

Wanatoka dhambi moja hadi nyingine,

hawanitambui mimi,”

asemaBwana.

4 “Jihadhari na rafiki zako;

usiwaamini ndugu zako.

Kwa kuwa kila ndugu ni mdanganyifu,

na kila rafiki ni msingiziaji.

5 Rafiki humdanganya rafiki,

hakuna ye yote asemaye kweli.

Wamefundisha ndimi zao kudanganya,

wanajichosha wenyewe katika kutenda dhambi.

6 Unakaa katikati ya udanganyifu;

katika udanganyifu wao

wanakataa kunitambua mimi,”

asemaBwana.

7 Kwa hiyo hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote:

“Tazama, nitawasafisha na kuwajaribu,

kwani ni nini kingine niwezacho kufanya

kwa sababu ya dhambi ya watu wangu?

8 Ndimi zao ni mshale wenye sumu,

hunena kwa udanganyifu.

Kwa kinywa chake kila mmoja huzungumza maneno mazuri na jirani yake,

lakini moyoni mwake humtegea mtego.

9 Je, nisiwaadhibu kwa ajili ya jambo hili?”

AsemaBwana.

“Je, nisijilipizie kisasi

kwa taifa kama hili?”

10 Nitalia na kuomboleza kwa ajili ya milima na kuomboleza kuhusu malisho ya jangwani.

Yamekuwa ukiwa na wala hakuna apitaye humo,

milio ya ng’ombe haisikiki.

Ndege wa angani wameruka

na wanyama wameondoka.

11 “Nitaifanya Yerusalemu lundo la magofu,

makao ya mbweha;

nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa

ili asiwepo atakayeishi humo.”

12 Ni mtu yupi aliye na hekima ya kutosha ayaelewe haya? Ni nani aliyefundishwa naBwanaawezaye kuyaeleza haya? Kwa nini nchi imeharibiwa na kufanywa ukiwa kama jangwa ambapo hakuna awezaye kupita?

13 Bwanaakasema, “Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu, niliyoiweka mbele yao: hawajaniheshimu mimi wala kufuata sheria yangu.

14 Badala yake wamefuata ukaidi wa mioyo yao, wamefuata mabaali, kama vile baba zao walivyowafundisha.”

15 Kwa hiyo, hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: “Tazama, nitawafanya watu hawa wale chakula kichungu na kunywa maji yenye sumu.

16 Nitawatawanya katika mataifa ambayo wao hawakuwajua wala baba zao, nitawafuatia kwa upanga mpaka niwe nimewaangamiza kabisa.”

17 Hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenye Nguvu Zote:

“Fikiri sasa! Waite wanawake waombolezao waje,

waite wale walio na ustadi kuliko wote.

18 Nao waje upesi

kutuombolezea

mpaka macho yetu yafurike machozi

na vijito vya maji vitoke kwenye kope zetu.

19 Sauti ya kuomboleza imesikika kutoka Sayuni:

‘Tazama jinsi tulivyoangamizwa!

Tazama jinsi aibu yetu ilivyo kubwa!

Ni lazima tuihame nchi yetu

kwa sababu nyumba zetu

zimekuwa magofu.’ ”

20 Basi, enyi wanawake, sikieni neno laBwana;

fungueni masikio yenu

msikie maneno ya kinywa chake.

Wafundisheni binti zenu jinsi ya kuomboleza;

fundishaneni kila mmoja na mwenzake kuomboleza.

21 Mauti imeingia ndani kupitia madirishani

na imeingia kwenye majumba yetu ya fahari;

imewakatilia mbali watoto katika barabara

na vijana waume kutoka katika viwanja vya miji.

22 Sema, “Hili ndilo asemaloBwana:

“ ‘Maiti za wanaume zitalala

kama mavi katika mashamba,

kama malundo ya nafaka yaliyokatwa

yalalavyo nyuma ya mvunaji,

wala hakuna anayekusanya.’ ”

23 Hili ndilo asemaloBwana:

“Mwenye hekima asijisifu katika hekima yake

au mwenye nguvu asijisifu katika nguvu zake

au tajiri asijisifu katika utajiri wake,

24 lakini yeye ajisifuye na ajisifu kwa sababu hili:

kwamba ananifahamu na kunijua mimi,

kwamba mimi ndimiBwana, nitendaye wema,

hukumu na haki duniani,

kwa kuwa napendezwa na haya,”

asemaBwana.

25 “Siku zinakuja, nitakapowaadhibu wale wote ambao wametahiriwa kimwili tu, asemaBwana,

26 yaani Misri, Yuda, Edomu, Amoni, Moabu na wote wanaoishi jangwani sehemu za mbali. Kwa maana mataifa haya yote hayakutahiriwa mioyo yao, nayo nyumba yote ya Israeli haikutahiriwa.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/9-2849268e2ce5e5921009817933f8b1bf.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

13 − 10 =