Yeremia 16

Siku Ya Maafa

1 Kisha neno laBwanalikanijia:

2 “Kamwe usioe na kuwa na wana wala binti mahali hapa.”

3 Kwa maana hilo ndilo asemaloBwanakuhusu wana na binti wazaliwao katika nchi hii na kuhusu wale wanawake ambao ni mama zao na wale wanaume ambao ni baba zao:

4 “Watakufa kwa magonjwa ya kufisha. Hawataombolezewa wala kuzikwa lakini watakuwa kama mavi yaliyosambaa juu ya ardhi. Watakufa kwa upanga na kwa njaa, nazo maiti zao zitakuwa chakula cha ndege wa angani na cha wanyama wa nchi.”

5 Kwa kuwa hili ndilo asemaloBwana: “Usiingie katika nyumba ambayo kuna chakula cha matanga, usiende kuwaombolezea wala kuwahurumia, kwa sababu nimeziondoa baraka zangu, upendo wangu na huruma zangu kutoka kwa watu hawa,” asemaBwana.

6 “Wakubwa na wadogo watakufa katika nchi hii. Hawatazikwa wala kuombolezewa, hakuna atakayejikatakata au kunyoa nywele za kichwa chake kwa ajili yao.

7 Hakuna ye yote atakayewapa chakula ili kuwafariji wale waombolezao kwa ajili ya wale waliokufa, hata akiwa amefiwa na baba au mama, hakuna ye yote atakayewapa kinywaji ili kuwafariji.

8 “Usiingie katika nyumba ambayo kuna karamu na kuketi humo ili kula na kunywa.

9 Kwa kuwa hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote, aliye Mungu wa Israeli: ‘Mbele ya macho yako na katika siku zako nitakomesha sauti zote za shangwe na za furaha, nazo sauti za bibi arusi na bwana arusi mahali hapa.’

10 “Utakapowaambia watu hawa mambo haya yote na wakakuuliza, ‘Kwa niniBwanaameamuru maafa makubwa kama haya dhidi yetu? Tumefanya kosa gani? Tumetenda dhambi gani dhidi yaBwana, Mungu wetu?’

11 Basi waambie, ‘Ni kwa sababu baba zenu waliniacha mimi, wakafuata miungu mingine kuitumikia na kuiabudu. Waliniacha mimi na hawakuishika sheria yangu,’ asemaBwana.

12 ‘Lakini ninyi mmetenda kwa uovu zaidi kuliko baba zenu. Tazama jinsi ambavyo kila mmoja wenu anafuata ukaidi wa moyo wake mbaya badala ya kunitii mimi.

13 Kwa hiyo nitawaondoa katika nchi hii na kuwatupa katika nchi ambayo ninyi wala baba zenu hamkuijua, nako huko mtaitumikia miungu mingine usiku na mchana, kwa maana sitawapa fadhili zangu huko.’

14 “Hata hivyo, siku zinakuja,” asemaBwana, “wakati ambapo watu hawatasema tena, ‘Hakika kamaBwanaaishivyo, aliyewapandisha Waisraeli kutoka Misri,’

15 bali watasema, ‘Hakika kamaBwanaaishivyo, aliyewatoa wana wa Israeli kutoka katika nchi ya kaskazini na nchi zote ambako alikuwa amewafukuzia.’ Maana nitawarudisha katika nchi niliyowapa baba zao.

16 “Lakini sasa nitawaagiza wavuvi wengi,” asemaBwana, “nao watawavua. Baada ya hilo nitawaagizia wawindaji wengi, nao watawawinda kwenye kila mlima na kilima na katika nyufa za miamba.

17 Macho yangu yanaziona njia zao zote, hazikufichika kwangu, wala dhambi yao haikusitirika.

18 Nitawalipiza maradufu kwa ajili ya uovu wao na dhambi yao, kwa sababu wameinajisi nchi yangu kwa maumbo yasiyo na uhai ya vinyago vyao vibaya na kuujaza urithi wangu na sanamu za kuchukiza.”

19 EeBwana, nguvu zangu na ngome yangu,

kimbilio langu wakati wa taabu,

kwako mataifa yatakujia

kutoka miisho ya dunia na kusema,

“Baba zetu hawakuwa na cho chote zaidi ya miungu ya uongo,

sanamu zisizofaa kitu

ambazo hazikuwafaidia lo lote.

20 Je, watu hujitengenezea miungu yao wenyewe?

Naam, lakini hao si miungu!”

21 “Kwa hiyo nitawafundisha:

wakati huu nitawafundisha

nguvu zangu na uwezo wangu.

Ndipo watakapojua

kuwa Jina langu ndimiBwana.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/16-7520136cf9d9651718f03e54d7447a3e.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

thirteen + seventeen =