Yeremia 18

Katika Nyumba Ya Mfinyanzi

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwaBwana:

2 “Shuka uende mpaka kwenye nyumba ya mfinyanzi, nami huko nitakupa ujumbe wangu.”

3 Kwa hiyo nikashuka mpaka kwenye nyumba ya mfinyanzi, nikamkuta akifinyanga kwa gurudumu lake.

4 Lakini chombo alichokuwa akikifinyanga kutokana na udongo kilivunjika mikononi mwake, hivyo mfinyanzi akakifanya kuwa chombo kingine, umbo jingine kama vile ilivyoonekana vyema kwake yeye.

5 Kisha neno laBwanalikanijia kusema:

6 “Ee nyumba ya Israeli, je, siwezi kuwafanyia kama huyu mfinyanzi afanyavyo?” AsemaBwana. “Kama vile udongo ulivyo katika mikono ya mfinyanzi, ndivyo mlivyo katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli.

7 Ikiwa wakati wo wote nikitangaza kuwa taifa au ufalme utang’olewa, utaangushwa na kuangamizwa,

8 ikiwa lile taifa nililolionya litatubia uovu wake, ndipo nitakapokuwa na huruma wala sitawapiga kwa maafa niliyokuwa nimekusudia kwa ajili yao.

9 Ikiwa wakati mwingine nitatangaza kuwa taifa ama utawala ujengwe na kusimikwa,

10 ikiwa utafanya maovu mbele zangu na hukunitii, ndipo nitakapoghairi makusudio yangu mema niliyokuwa nimeyakusudia kwa ajili yake.

11 “Basi kwa hiyo waambie watu wa Yuda na wale waishio Yerusalemu, ‘Hili ndilo asemaloBwana: Tazama! Ninaandaa maafa kwa ajili yenu nami ninabuni mabaya dhidi yenu. Kwa hiyo geukeni kutoka katika njia zenu mbaya, kila mmoja wenu, tengenezeni njia zenu na matendo yenu.’

12 Lakini wao watajibu, ‘Hakuna faida. Tutaendelea na mipango yetu wenyewe, kila mmoja wetu atafuata ukaidi wa moyo wake mbaya.’ ”

13 Kwa hiyo hili ndilo asemaloBwana:

“Ulizia miongoni mwa mataifa:

Ni nani alishasikia jambo kama hili?

Jambo la kutisha sana limefanywa

na Bikira Israeli.

14 Je, barafu ya Lebanoni iliwahi kutoweka

kwenye mitelemko yake ya mawe

wakati wo wote?

Je, maji yake baridi yatokayo katika vyanzo vilivyo mbali

yaliwahi kukoma kutiririka wakati wo wote?

15 Lakini watu wangu wamenisahau mimi,

wanafukizia uvumba sanamu zisizofaa kitu,

zilizowafanya wajikwae katika njia zao

na katika mapito ya zamani.

Zimewafanya wapite kwenye vichochoro

na kwenye barabara ambazo hazikujengwa.

16 Nchi yao itaharibiwa,

itakuwa kitu cha kudharauliwa daima;

wote wapitao karibu nayo watashangaa

na kutikisa vichwa vyao.

17 Kama upepo utokao mashariki,

nitawatawanya mbele ya adui zao;

nitawapa kisogo wala sio uso,

katika siku ya maafa yao.”

18 Wakasema, “Njoni, tutunge hila dhidi ya Yeremia; kwa kuwa kufundisha sheria kwa kuhani hakutapotea, wala shauri litokalo kwa mwenye hekima, wala neno la manabii. Hivyo njoni, tumshambulie kwa ndimi zetu na tusijali cho chote asemacho.”

19 Nisikilize, EeBwana,

sikia wanayosema washitaki wangu!

20 Je, mema yalipwe kwa mabaya?

Lakini wao wamenichimbia shimo.

Kumbuka kwamba nilisimama mbele yako

na kunena mema kwa ajili yao

ili wewe ugeuze hasira yako kali mbali nao.

21 Kwa hiyo uwaache watoto wao waone njaa;

uwaache wauawe kwa makali ya upanga.

Wake zao na wasiwe na watoto, na wawe wajane;

waume wao na wauawe,

nao vijana wao waume

wachinjwe kwa upanga vitani.

22 Kilio na kisikike kutoka kwenye nyumba zao

ghafula uwaletapo adui dhidi yao,

kwa kuwa wamechimba shimo ili kunikamata

na wameitegea miguu yangu mitego.

23 Lakini unajua, EeBwana,

hila zao zote za kuniua.

Usiyasamehe makosa yao

wala usifute dhambi zao

mbele za macho yako.

Wao na waangamizwe mbele zako;

uwashughulikie wakati wa hasira yako.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/18-27ca7468582c0c018208e2a71f9f5661.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

seventeen + twelve =