Yeremia 7

Dini Za Uongo Hazina Maana

1 Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwaBwana:

2 “Simama kwenye lango la nyumba yaBwanana huko upige mbiu ya ujumbe huu:

“ ‘Sikieni neno laBwana, enyi watu wote wa Yuda mliokuja kupitia malango haya ili kumwabuduBwana.

3 Hili ndilo asemaloBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Tengenezeni njia zenu na matendo yenu, nami nitawaacha mkae mahali hapa.

4 Msitumainie maneno ya udanganyifu na kusema, “Hili ni Hekalu laBwana, hili ni Hekalu laBwana, Hekalu laBwana!”

5 Kama kweli mkibadili njia zenu na matendo yenu mkitendeana haki kila mmoja na mwenzake,

6 kama msipomwonea mgeni, yatima wala mjane na kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, nanyi kama msipofuata miungu mingine kwa madhara yenu wenyewe,

7 ndipo nitawaacha mkae mahali hapa, katika nchi niliyowapa baba zenu milele na milele.

8 Lakini tazama, mnatumainia maneno ya udanganyifu yasiyo na maana.

9 “ ‘Je, mtaiba na kuua, mtazini na kuapa kwa uongo na kufukiza uvumba kwa Baali na kufuata miungu mingine ambayo hamkuijua,

10 kisha mje na kusimama mbele yangu katika nyumba hii, inayoitwa kwa Jina langu, mkisema, “Tuko salama.” Salama kwa kufanya mambo haya yote ya kuchukiza?

11 Je, nyumba hii, iitwayo kwa Jina langu, imekuwa pango la wanyang’anyi kwenu? Lakini nimekuwa nikiona yanayotendeka! AsemaBwana.

12 “ ‘Nendeni sasa mahali pangu palipokuwa huko Shilo, mahali ambapo nilipafanya pa kwanza kuwa makao ya Jina langu, nanyi mwone lile nililopafanyia kwa ajili ya uovu wa watu wangu Israeli.

13 Mlipokuwa mnafanya yote haya, asemaBwana, nilisema nanyi tena na tena, lakini hamkusikiliza, niliwaita, lakini hamkujibu.

14 Kwa hiyo, nililolifanyia Shilo, nitalifanya sasa kwa nyumba hii iitwayo kwa Jina langu, Hekalu mnalolitumainia, mahali nilipowapa ninyi na baba zenu.

15 Nitawafukuza mbele yangu, kama nilivyowafanyia ndugu zenu, watu wa Efraimu.’

16 “Kwa hiyo usiombe kwa ajili ya watu hawa, usinililie, usifanye maombi kwa ajili yao, wala usinisihi kwa sababu sitakusikiliza.

17 Je, huyaoni hayo wanayoyatenda katika miji ya Yuda na katika barabara za Yerusalemu?

18 Watoto wanakusanya kuni, baba zao wanawasha moto na wanawake wanakanda unga na kuoka mikate kwa ajili ya Malkia wa Mbinguni. Wanamimina sadaka za vinywaji kwa miungu mingine ili kunikasirisha.

19 Lakini je, mimi ndiye wanayenikasirisha? asemaBwana. Je, hawajiumizi wenyewe kwa aibu yao?

20 “ ‘Kwa hiyo hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenyezi: Hasira yangu na ghadhabu yangu itamwagwa mahali hapa, juu ya mwanadamu na mnyama, juu ya miti ya shambani na juu ya matunda ya ardhini, nayo itaungua pasipo kuzimwa.

21 “ ‘Hivi ndivyo asemavyoBwanaMwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli: Endeleeni, ongezeni sadaka zenu za kuteketezwa juu ya dhabihu zenu nyingine, mle nyama hiyo wenyewe!

22 Kwa kuwa nilipowaleta baba zenu kutoka Misri na kusema nao, sikuwapa amri kuhusu sadaka za kuteketezwa na dhabihu tu,

23 lakini niliwapa amri hii nikisema: Mtanitii mimi, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu. Enendeni katika njia zote ninazowaamuru ili mpate kufanikiwa.

24 Lakini hawakusikiliza wala kujali, badala yake, walifuata ukaidi wa mioyo yao miovu. Wakarudi nyuma badala ya kusonga mbele.

25 Tangu wakati ule baba zenu walipotoka Misri hadi sasa, siku baada ya siku, tena na tena nimewatumia watumishi wangu manabii.

26 Lakini hawakunisikiliza wala hawakujali. Walikuwa na shingo ngumu na kufanya maovu kuliko baba zao.’

27 “Utakapowaambia haya yote, hawatakusikiliza, utakapowaita, hawatajibu.

28 Kwa hiyo waambie, ‘Hili ni taifa ambalo halimtiiBwana, Mungu wao wala kukubali kurudiwa. Kweli imekufa, imetoweka midomoni mwao.

29 Nyoeni nywele zenu na kuzitupa, ombolezeni juu ya miinuko iliyo kame, kwa kuwaBwanaamekikataa na kukiacha kizazi hiki kilichomkasirisha.

Bonde La Machinjo

30 “ ‘Watu wa Yuda wamefanya maovu machoni pangu, asemaBwana. Wameziweka sanamu zao za machukizo ndani ya nyumba iitwayo kwa Jina langu na wameitia unajisi.

31 Wamejenga mahali pa juu pa kuabudia sanamu pa Tofethi kwenye Bonde la Ben-Hinomu ili kuwateketeza wana wao na binti zao kwenye moto, kitu ambacho sikuamuru, wala hakikuingia akilini mwangu.

32 Kwa hiyo mjihadhari, siku zinakuja, asemaBwana, wakati watu watakapokuwa hawapaiti Tofethi au Bonde la Ben-Hinomu, lakini watapaita Bonde la Machinjo, kwa sababu watawazika wafu huko Tofethi mpaka pasiwe tena nafasi.

33 Ndipo mizoga ya watu hawa itakuwa chakula cha ndege wa angani na wanyama wa nchi, wala hapatakuwepo na ye yote wa kuwafukuza.

34 Nitazikomesha sauti za shangwe na furaha na sauti za bwana arusi na bibi arusi katikati ya miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu, kwa sababu nchi itakuwa ukiwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/7-33a1b99e0bdfada4376ac4250541752a.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

3 × 4 =