Yeremia 8

1 “ ‘Wakati huo, asemaBwana, mifupa ya Wafalme na maafisa wa Yuda, mifupa ya makuhani na manabii, nayo mifupa ya watu wa Yerusalemu itaondolewa kutoka katika makaburi yao.

2 Itawekwa wazi juani na kwenye mwezi na nyota zote za mbingu, ambazo walizipenda na kuzitumikia na ambazo wamezifuata kutafuta ushauri na kuziabudu. Hawatakusanywa pamoja au kuzikwa, lakini watakuwa kama mavi yaliyotapakaa juu ya ardhi.

3 Po pote nitakapowafukuzia, mabaki wote wa kizazi hiki kiovu watatamani kufa kuliko kuishi, asemaBwanaMwenye Nguvu Zote.’

Dhambi Na Adhabu

4 “Waambie, ‘Hivi ndivyo asemavyoBwana:

“ ‘Je, watu wanapoanguka hawainuki?

Je, mtu anapopotea harudi?

5 Kwa nini basi watu hawa walipotea?

Kwa nini Yerusalemu inapotea kila mara?

Wanang’ang’ania udanganyifu

na wanakataa kurudi.

6 Nimewasikiliza kwa makini,

lakini hawataki kusema lililo sawa.

Hakuna anayetubia makosa yake

akisema, “Nimefanya nini?”

Kila mmoja hufuata njia yake mwenyewe

kama farasi anayekwenda vitani.

7 Hata korongo aliyeko angani

anayajua majira yake yaliyoamriwa,

nao njiwa, mbayuwayu na koikoi

hufuata majira yao ya kurudi.

Lakini watu wangu hawajui

Bwanaanachotaka kwao.

8 “ ‘Mwawezaje kusema, “Sisi tuna busara

kwa sababu tunayo sheria yaBwana,”

wakati ambapo kwa hakika kalamu ya uongo ya waandishi

imeandika kwa udanganyifu?

9 Wenye hekima wataaibika,

watafadhaika na kunaswa.

Kwa kuwa wamelikataa neno laBwana,

hiyo hekima waliyo nayo ni ya namna gani?

10 Kwa hiyo nitawapa watu wengine wake zao

na mashamba yao wamiliki wengine.

Kuanzia aliye mdogo kabisa hadi aliye mkubwa kabisa,

wana tamaa ya kupata zaidi,

manabii na makuhani vivyo hivyo,

wote wanafanya udanganyifu.

11 Wanafunga majeraha ya watu wangu

bila uangalifu.

Wanasema, “Amani, amani,”

wakati hakuna amani.

12 Je, wanaona aibu kwa ajili ya tabia yao inayochukiza mno?

Hapana, hawana aibu hata kidogo,

hawajui hata kuona haya.

Kwa hiyo wataanguka miongoni mwa hao walioanguka,

watashushwa chini watakapoadhibiwa,

asemaBwana.

13 “ ‘Nitayaondoa mavuno yao,

asemaBwana.

Hapatakuwepo zabibu kwenye mzabibu.

Hapatakuwepo na tini kwenye mtini,

majani yake yatanyauka.

Kile nilichowapa

watanyang’anywa.’ ”

14 “Kwa nini tunaketi hapa?

Kusanyikeni pamoja!

Tukimbilie kwenye miji yenye maboma

na tukaangamie huko!

Kwa kuwaBwana, Mungu wetu

ametuhukumu kuangamia,

na kutupa maji yenye sumu tunywe,

kwa sababu tumemtenda dhambi.

15 Tulitegemea amani,

lakini hakuna jema lililokuja,

tulitegemea wakati wa kupona,

lakini kulikuwa hofu tu.

16 Mkoromo wa farasi za adui

umesikika kuanzia Dani,

kwa mlio wa madume yao ya farasi,

nchi yote inatetemeka.

Wamekuja kuangamiza nchi na vyote vilivyomo,

mji na wote waishio ndani yake.”

17 “Tazama, nitatuma nyoka wenye sumu kali katikati yenu,

nyoka wenye sumu ambao hawawezi kulogwa,

nao watawauma,”

asemaBwana.

18 Ee mfariji wangu katika huzuni,

moyo wangu umezimia ndani mwangu.

19 Sikia kilio cha watu wangu

kutoka nchi ya mbali:

“Je,Bwanahayuko Sayuni?

Je, mfalme wake hayuko tena huko?”

“Kwa nini wamenikasirisha kwa vinyago vyao,

kwa sanamu zao za kigeni zisizofaa?”

20 “Mavuno yamepita,

kiangazi kimekwisha,

nasi hatujaokolewa.”

21 Kwa kuwa watu wangu wamepondwa,

nami nimepondeka pia;

ninaomboleza, nayo hofu kuu imenishika.

22 Je, hakuna zeri ya kuponya katika Gileadi?

Je, hakuna tabibu huko?

Kwa nini basi hakuna uponyaji

wa majeraha ya watu wangu?

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JER/8-e933fd5efcea2bc05863648d23243122.mp3?version_id=1627—

Leave a comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

twenty + 5 =