Ufunuo 21

Mbingu Mpya Na Nchi Mpya

1 Kisha nikaona mbingu mpya na nchi mpya, kwa maana mbingu za kwanza na nchi ya kwanza vimekwisha kupita, wala hapakuwepo na bahari tena.

2 Nikaona Mji Mtakatifu, Yerusalemu mpya, ukishuka kutoka mbinguni kwa Mungu, ukiwa umeandaliwa kama bibi arusi aliyepambwa kwa ajili ya mumewe.

3 Nami nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, “Sasa makao ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atakaa pamoja nao. Yeye atakuwa Mungu wao nao watakuwa watu wake, naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.

4 Atafuta kila chozi, kutoka katika macho yao. Mauti haitakuwepo tena, wala maombolezo, wala kilio, wala maumivu, kwa maana mambo ya kwanza yamekwisha kupita.”

5 Naye yule aliyeketi juu ya kile kiti cha enzi akasema, “Tazama, nayafanya mambo yote kuwa mapya!” Kisha akasema, “Andika haya, maana maneno haya ni ya kuaminika tena ni kweli.”

6 Akaniambia, “Imekwisha kuwa. Mimi ni Alfa na Omega, Mwanzo na Mwisho. Yeye aonaye kiu nitampa kunywa kutoka katika chemchemi ya maji ya uzima bila gharama yo yote.

7 Yeye atakayeshinda atayarithi haya yote, Nami nitakuwa Mungu wake, naye atakuwa mwanangu.

8 Lakini waoga, wasioamini, wachafu, wauaji, wazinzi, wachawi, waabudu sanamu, pamoja na waongo wote, mahali pao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili.”

9 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba ya hayo mapigo saba ya mwisho akaja akaniambia, “Njoo, nami nitakuonyesha bibi arusi, yaani, mke wa Mwana-Kondoo.”

10 Naye akanichukua katika Roho hadi kwenye mlima mkubwa na mrefu, akanionyesha ule Mji Mtakatifu, Yerusalemu, likishuka kutoka mbinguni kwa Mungu.

11 Ulikuwa uking’aa kwa utukufu wa Mungu kama kito chenye thamani sana, kama yaspi, safi kama kioo.

12 Ulikuwa na ukuta mkubwa, mrefu wenye malango kumi na mawili, pakiwa na malaika kumi na wawili kwenye hayo malango. Kwenye malango hayo yaliandikwa majina ya yale makabila kumi na mawili ya Israeli.

13 Kulikuwa na malango matatu upande wa mashariki, matatu upande wa kaskazini, matatu upande wa kusini na matatu upande wa magharibi.

14 Ukuta wa huo mji ulikuwa na misingi kumi na miwili na juu yake yaliandikwa majina ya wale mitume kumi na wawili wa Mwana-Kondoo.

15 Huyo malaika aliyesema nami alikuwa na ufito wa dhahabu wa kupimia huo mji, malango yake na kuta zake.

16 Mji huo ulikuwa mraba, urefu wake ulikuwa sawa na upana wake. Akaupima huo mji kwa huo ufito akakuta una kama kilomita 2,400; urefu wake na upana wake na kwenda juu kwake vilikuwa sawa.

17 Akaupima ukuta wake, ulikuwa na unene wa dhiraa 144kwa kipimo cha kibinadamu ambacho huyo malaika alikuwa akikitumia.

18 Ukuta huo ulijengwa kwa yaspi hali mji wenyewe ulijengwa kwa dhahabu safi, iking’aa kama kioo.

19 Misingi ya kuta za mji huo zilipambwa kwa kila aina ya kito cha thamani. Msingi wa kwanza ulikuwa wa yaspi, wa pili yakuti samawi, wa tatu kalkedoni, wa nne zumaridi,

20 wa tano sardoniki, wa sita akiki, wa saba krisolitho, wa nane zabarajadi, wa tisa yakuti manjano, wa kumi krisopraso, wa kumi na moja hiakintho, wa kumi na mbili amethisto.

21 Yale malango kumi na mbili yalikuwa ni lulu kumi na mbili, kila lango lilikuwa limetengenezwa kwa lulu moja. Barabara za mji huo zilikuwa za dhahabu safi ing’aayo kama kioo.

22 Sikuona Hekalu ndani ya huo mji kwa sababu BWANA Mungu Mwenyezi na Mwana-Kondoo ndio Hekalu lake.

23 Ule mji hauhitaji jua wala mwezi kuuangazia, kwa sababu utukufu wa Mungu ndio nuru yake na Mwana-Kondoo ndiye taa yake.

24 Mataifa yatatembea yakiangaziwa na nuru yake na wafalme wa duniani wataleta fahari yao ndani yake.

25 Malango yake hayatafungwa kamwe, kwa maana hakutakuwa na usiku humo.

26 Utukufu na heshima za mataifa zitaletwa humo.

27 Lakini kitu kichafu hakitaingia humo kamwe, wala mtu ye yote atendaye mambo ya aibu au ya udanganyifu. Bali watakaoingia humo ni wale tu ambao majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/21-bd5b856884801cce591a109561f60709.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 22

Mto Wa Maji Ya Uzima

1 Kisha yule malaika akanionyesha mto wa maji ya uzima, maangavu kama kioo yakitiririka kutoka kwenye kile kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo,

2 kupitia katikati ya barabara kuu ya huo mji. Kwenye kila upande wa huo mto kulikuwa na mti wa uzima utoao matunda ya aina kumi na mbili, ukizaa matunda yake kila mwezi. Nayo majani ya mti huo ni kwa ajili ya uponyaji wa mataifa.

3 Katika mji huo hakutakuwa tena na kitu cho chote kilicholaaniwa, bali kiti cha enzi cha Mungu na cha Mwana-Kondoo kitakuwamo humo na watumishi wake watamtumikia,

4 nao watamwona uso wake na Jina lake litakuwa kwenye vipaji vya nyuso zao.

5 Usiku hautakuwako tena, wala hawatahitaji mwanga wa taa au wa jua, kwa maana BWANA Mungu atakuwa nuru yao, nao watatawala milele na milele.

6 Kisha yule malaika akaniambia, “Maneno haya ni ya kuaminika na kweli. BWANA, Mungu wa roho za manabii, alimtuma malaika wake kuwaonyesha watumishi wake yale ambayo hayana budi kutukia upesi.”

Bwana Yesu Anakuja

7 “Tazama, naja upesi! Amebarikiwa yeye ayashikaye maneno ya unabii wa kitabu hiki.”

8 Mimi, Yohana, ndiye niliyesikia na kuyaona mambo haya. Nami nilipokwisha kuyasikia na kuyaona, nilianguka chini nikasujudu miguuni pa yule malaika aliyekuwa akinionyesha mambo hayo.

9 Lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi ni mtumishi pamoja nawe na ndugu zako manabii na wote wanaoyashika maneno ya kitabu hiki. Msujudie Mungu!”

10 Kisha akaniambia, “Usiyafunge maneno ya unabii yaliyomo katika kitabu hiki, kwa sababu wakati umekaribia.

11 Atendaye mabaya na aendelee kutenda mabaya, aliye mchafu na aendelee kuwa mchafu, yeye atendaye haki na aendelee kutenda haki na yeye aliye mtakatifu na aendelee kuwa mtakatifu.”

12 “Tazama, naja upesi! Thawabu yangu i mkononi mwangu, nami nitampa kila mtu sawasawa na alivyotenda.

13 Mimi ni Alfa na Omega, wa Kwanza na wa Mwisho, Mwanzo na Mwisho.

14 “Wamebarikiwa wale wafuao mavazi yao, ili wapate haki ya kuuendea huo mti wa uzima na kuuingia huo mji kupitia kwenye malango yake.

15 Huko nje wako mbwa, wachawi, wazinzi, wauaji, waabuduo sanamu na kila mtu apendaye udanganyifu na kuufanya.

16 “Mimi, Yesu, nimemtuma malaika wangu kushuhudia mambo haya kwa ajili ya makanisa. Mimi ndimi Shina na Mzao wa Daudi, ile Nyota ya Asubuhi ing’aayo.”

17 Roho na bibi arusi wanasema, “Njoo!” Naye asikiaye na aseme, “Njoo!” Ye yote mwenye kiu na aje na kila anayetaka na anywe maji ya uzima bure.

18 Namwonya kila mtu asikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki: Mtu ye yote akiongeza humo cho chote, Mungu atamwongezea mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.

19 Kama mtu ye yote akipunguza humo cho chote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.

20 Yeye anayeshuhudia mambo haya asema, “Hakika, naja upesi!”

Amen. Njoo, Bwana Yesu.

21 Neema ya Bwana Yesu iwe na watakatifu wote. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/22-1909eb4f43e6fc880212503a7b022f29.mp3?version_id=1627—

Yuda 1

Salamu

1 Yuda, mtumwa wa Yesu Kristo na nduguye Yakobo:

Kwa wale walioitwa, wapendwa katika Mungu Baba na kuhifadhiwa salama ndani ya Yesu Kristo:

2 Rehema, amani na upendo viwe kwenu kwa wingi.

Dhambi Na Hukumu Ya Watu Wasiomcha Mungu

3 Wapenzi, ingawa nilikuwa ninatamani sana kuwaandikia kuhusu wokovu ambao tunaushiriki sisi sote, niliona imenipasa kuwaandikia na kuwasihi kwamba mwishindanie imani iliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu.

4 Kwa kuwa kuna watu waliojipenyeza kwa siri katikati yenu, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, waovu, wapotoshao neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi wakimkana yeye aliye Bwana wetu wa pekee, Bwana Yesu Kristo.

Hukumu Kwa Walimu Wa Uongo

5 Ingawa mmekwisha kujua haya yote, nataka niwakumbushe kuwa Bwana akiisha kuwaokoa watu wake kutoka Misri, baadaye aliwaangamiza wale ambao hawakuamini.

6 Nao malaika ambao hawakulinda nafasi zao, lakini wakayaacha makao yaliyokuwa yao hasa, hawa amewaweka katika giza, wakiwa wamefungwa kwa minyororo ya milele kwa ajili ya hukumu siku ile kuu.

7 Vivyo hivyo, Sodoma na Gomora na pia ile miji iliyokuwa kandokando, ambayo kwa jinsi moja na hao, walijifurahisha kwa uasherati na kufuata tamaa za mwili zisizo za asili, waliwekwa wawe mfano kwa kuadhibiwa katika moto wa milele.

8 Vivyo hivyo, hawa waotao ndoto huutia mwili unajisi, hukataa kuwa chini ya mamlaka na kunena mabaya juu ya wenye mamlaka.

9 Lakini hata Malaika Mkuu Mikaeli alipokuwa anashindana na ibilisi juu ya mwili wa Mose, hakuthubutu kumlaumu, bali alimwambia, “Bwana na akukemee!”

10 Lakini watu hawa hunena mabaya dhidi ya mambo wasiyoyafahamu na katika mambo yale wanayoyafahamu kwa hisia kama wanyama wasio na akili, hayo ndiyo hasa yanayowaharibu.

11 Ole wao! Kwa kuwa wanaifuata njia ya Kaini, wamekimbilia faida katika kosa la Balaamu na kuangamia katika uasi wa Kora.

12 Watu hawa ni dosari katika karamu zenu za upendo, wakila pamoja nanyi bila hofu, wakijilisha pasipo hofu. Wao ni mawingu yasiyokuwa na maji, yakichukuliwa na upepo, miti isiyo na matunda wakati wa mapukutiko, ambayo hunyauka, iliyokufa mara mbili na kung’olewa kabisa.

13 Wao ni mawimbi makali ya bahari, yakitoa povu la aibu yao wenyewe, ni nyota zipoteazo, ambao weusi wa giza ndio akiba yao waliowekewa milele.

14 Enoki, mtu wa saba kuanzia Adamu alitoa unabii kuhusu watu hawa, akisema: “Tazama, Bwana anakuja pamoja na maelfu kwa maelfu ya watakatifu wake,

15 ili kumhukumu kila mmoja na kuwapatiliza wote wasiomcha Mungu kwa matendo yao yote ya uasi waliyoyatenda, pamoja na maneno yote ya kuchukiza ambayo wenye dhambi wamesema dhidi yake.”

16 Watu hawa ni wenye kunung’unika na wenye kutafuta makosa; wao hufuata tamaa zao mbaya, hujisifu kwa maneno makuu kuhusu wao wenyewe na kuwasifu mno watu wenye vyeo kwa ajili ya kujipatia faida.

Maonyo Na Mausia

17 Lakini ninyi wapenzi, kumbukeni yale Mitume wa Bwana Yesu Kristo waliyotangulia kusema.

18 Kwa kuwa waliwaambia, “Siku za mwisho kutakuwa na watu wenye kudhihaki, watakaofuata tamaa zao wenyewe za upotovu.”

19 Hawa ndio watu wanaowagawa ninyi, wafuatao tamaa zao za asili, wala hawana Roho.

20 Lakini ninyi wapenzi, jijengeni katika imani yenu iliyo takatifu sana tena ombeni katika Roho Mtakatifu.

21 Jilindeni katika upendo wa Mungu mkitazamia kwa furaha rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo ili awalete katika uzima wa milele.

22 Wahurumieni wengine wale wenye shaka;

23 wengine waokoeni kwa kuwanyakua kutoka kwenye moto; nao wengine wahurumieni mkiwa na hofu, mkichukia hata vazi lenye mawaa na kutiwa unajisi na mwili.

Dua Ya Kutakia Heri

24 Kwake yeye awezaye kuwalinda ninyi msianguke na kuwaleta mbele za utukufu wake mkuu bila dosari na kwa furaha ipitayo kiasi:

25 kwake yeye Mungu pekee Mwokozi wetu, kwa Yesu Kristo Bwana wetu, utukufu, ukuu, uweza na mamlaka vina yeye tangu milele, sasa na hata milele! Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JUD/1-078a97e1a0bac433e445382647c30e22.mp3?version_id=1627—

3 Yohana 1

Salamu

1 Mzee:

Kwa Gayo mpenzi, nimpendaye katika kweli.

Gayo Anasifiwa Kwa Ajili Ya Ukarimu Wake

2 Mpenzi, naomba ufanikiwe katika mambo yote na kuwa na afya yako kama vile roho yako ifanikiwavyo.

3 Ilinifurahisha sana baadhi ya ndugu walipokuja na kutueleza juu ya uaminifu wako katika kweli na jinsi unavyoendelea kuenenda katika hiyo kweli.

4 Sina furaha kubwa kuliko hii, kusikia kwamba watoto wangu wanaenenda katika kweli.

5 Mpenzi, wewe ni mwaminifu kwa yale unayowatendea ndugu, ingawa wao ni wageni kwako.

6 Wameshuhudia kuhusu upendo wako mbele ya kanisa. Utafanya vyema ukiwasafirisha kama inavyostahili kwa Mungu.

7 Ilikuwa ni kwa ajili ya hilo Jina waliondoka, bila kukubali kupokea msaada wo wote kutoka kwa watu wasioamini.

8 Kwa hiyo imetupasa sisi kuonyesha ukarimu kwa watu kama hao ili tuweze kutenda kazi pamoja kwa ajili ya kweli.

Deotrefe

9 Nililiandikia kanisa, lakini Deotrefe, yeye apendaye kujifanya wa kwanza, hakubali mamlaka yetu.

10 Hivyo kama nikija, nitakumbuka matendo yake atendayo, akitusingizia kwa maneno ya hila. Wala hatosheki na hayo anayotusingizia, bali pia hukataa kuwakaribisha ndugu na hata huwazuia wale walio tayari kufanya hivyo na kuwafukuza watoke kanisani.

Demetrio

11 Mpenzi, usiige lile lililo baya bali lile lililo jema. Ye yote atendaye mema atoka kwa Mungu, atendaye mabaya hakumwona Mungu.

12 Kila mtu ameshuhudia mema kuhusu Demetrio, vivyo hivyo hata na hiyo kweli yenyewe. Sisi pia twashuhudia mema juu yake, nanyi mwajua kwamba ushuhuda wetu ni kweli.

Salamu Za Mwisho

13 Ninayo mambo mengi ya kukuandikia, lakini sipendi kuandika kwa kalamu na wino.

14 Badala yake, nataraji kukuona upesi, nasi tutaongea pamoja ana kwa ana.

Amani iwe kwako. Rafiki zetu walioko hapa wanakusalimu. Wasalimu hao rafiki zetu walioko huko, kila mmoja kwa jina lake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/3JN/1-4387cdc648dbd7fbbedcd1fbc89ff6c1.mp3?version_id=1627—

2 Yohana 1

Salamu

1 Mzee:

Kwa bibi mteule na watoto wake, niwapendao katika kweli, wala si mimi tu, bali na wale wote waijuayo kweli:

2 kwa sababu ya ile kweli ikaayo ndani yetu na ambayo itaendelea kukaa nasi milele:

3 Neema, rehema na amani itokayo kwa Mungu Baba na kwa Yesu Kristo, Mwanawe Baba, itakuwa pamoja nasi katika kweli na upendo.

Kweli Na Upendo

4 Imenipa furaha kuu kuona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile Baba alivyotuagiza.

5 Sasa, bibi mpendwa, nakuomba, si kwamba ninakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo. Sisi na tupendane kila mmoja na mwenzake.

6 Hili ndilo pendo, kwamba tuenende sawasawa na amri zake. Hii ndiyo amri yake kama vile mlivyosikia tangu mwanzo, kwamba mwenende katika upendo.

7 Wadanganyifu wengi, wasiokubali kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili, wametokea ulimwenguni. Mtu wa namna hiyo ni mdanganyifu na mpinga Kristo.

8 Jihadharini msije mkapoteza kile mlichokitenda, bali mpate kupewa thawabu kamilifu.

9 Mtu ye yote asiyedumu katika mafundisho ya Kristo, bali akayaacha, yeye hana Mungu. Ye yote anayedumu katika mafundisho ana Baba na Mwana pia.

10 Msimpokee mtu ye yote anayewajia ambaye hawaletei mafundisho haya, wala msimkaribishe nyumbani mwenu.

11 Ye yote amkaribishaye mtu wa namna hiyo anashiriki katika matendo maovu ya mtu huyo.

Salamu Za Mwisho

12 Ingawa ninayo mengi ya kuwaandikia, lakini sitaki kutumia karatasi na wino. Badala yake, nataraji kuja kwenu na kuongea nanyi ana kwa ana, ili furaha yetu ipate kuwa timilifu.

13 Watoto wa dada yako mteule wanakusalimu. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2JN/1-01922791e51083ee0d6d6cf6d4f3f655.mp3?version_id=1627—

1 Yohana 1

Neno La Uzima

1 Tunawajulisha lile lililokuwako tangu mwanzo, lile tulilosikia, ambalo tumeliona kwa macho yetu, ambalo tumelitazama na kuligusa kwa mikono yetu, kuhusu Neno la uzima.

2 Uzima huo ulidhihirishwa; nasi tumeuona na kuushuhudia, nasi twawatangazia uzima wa milele, ambao ulikuwa pamoja na Baba, nao ukadhihirishwa kwetu.

3 Twawatangazia lile tuliloliona na kulisikia, ili kwamba nanyi mwe na ushirika nasi. Na ushirika wetu hasa ni pamoja na Baba na Mwanawe, Yesu Kristo.

4 Tunaandika mambo haya ili furaha yetu ipate kuwa timilifu.

Kutembea Nuruni

5 Huu ndio ujumbe tuliosikia kutoka kwake na kuwatangazia ninyi: kwamba Mungu ni nuru na ndani yake hamna giza lo lote.

6 Kama tukisema kwamba twashirikiana naye huku tukienenda gizani, twasema uongo, wala hatutendi lililo kweli.

7 Lakini tukienenda nuruni, kama yeye alivyo nuruni, twashirikiana sisi kwa sisi na damu yake Yesu, Mwana wake yatusafisha dhambi yote.

8 Kama tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe wala kweli haimo ndani yetu.

9 Kama tukiziungama dhambi zetu, yeye ni mwaminifu na wa haki, atatusamehe dhambi zetu na kutusafisha toka kwenye udhalimu wote.

10 Kama tukisema hatukutenda dhambi, twamfanya yeye kuwa mwongo na neno lake halimo ndani yetu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1JN/1-317fa54eef7f42019b8b753b1bba5b7b.mp3?version_id=1627—

1 Yohana 2

Kristo Mwombezi Wetu

1 Watoto wangu wapendwa, nawaandikieni haya ili msitende dhambi. Lakini kama mtu ye yote akitenda dhambi, tunaye mwombezi kwa Baba: ndiye Yesu Kristo mwenye haki.

2 Yeye ndiye dhabihu ya upatanisho kwa ajili ya dhambi zetu, wala si kwa ajili ya dhambi zetu tu, bali pia kwa ajili ya dhambi za ulimwengu wote.

3 Basi katika hili twajua ya kuwa tumemjua kama tunazishika amri zake.

4 Mtu ye yote asemaye kuwa, “Ninamjua” lakini hazishiki amri zake, ni mwongo, wala ndani ya mtu huyo hamna kweli.

5 Lakini kama mtu ye yote analitii neno lake, upendo wa Mungu umekamilika ndani yake kweli kweli. Katika hili twajua kuwa tumo ndani yake.

6 Ye yote anayesema anakaa ndani yake hana budi kuenenda kama Yesu alivyoenenda.

Amri Mpya

7 Wapenzi, siwaandikii ninyi amri mpya bali ile ya zamani, ambayo mmekuwa nayo tangu mwanzo. Amri hii ya zamani ni lile neno mlilosikia.

8 Lakini ninawaandikia amri mpya, yaani, lile neno lililo kweli ndani yake na ndani yenu, kwa sababu giza linapita na ile nuru ya kweli tayari inang’aa.

9 Ye yote anayesema yumo nuruni lakini anamchukia ndugu yake bado yuko gizani.

10 Yeye ampendaye ndugu yake anakaa nuruni, wala hakuna kitu cho chote ndani yake cha kumkwaza.

11 Lakini ye yote amchukiaye ndugu yake, yuko gizani na anaenenda gizani, wala hajui anakokwenda, kwa sababu giza limempofusha macho.

12 Nawaandikia ninyi, watoto wadogo,

kwa sababu dhambi zenu

zimesamehewa kwa ajili ya Jina lake.

13 Nawaandikia ninyi, akina baba,

kwa sababu mmemjua

yeye aliye tangu mwanzo.

Nawaandikia ninyi vijana

kwa sababu mmemshinda yule mwovu.

Nawaandikia ninyi watoto wadogo,

kwa sababu mmemjua Baba.

14 Nawaandikia ninyi akina baba,

kwa sababu mmemjua

yeye aliye tangu mwanzo.

Nawaandikia ninyi vijana,

kwa sababu mna nguvu,

na neno la Mungu linakaa ndani yenu,

nanyi mmemshinda yule mwovu.

Msiupende Ulimwengu

15 Msiupende ulimwengu wala mambo yaliyoko ulimwenguni. Kama mtu ye yote akiupenda ulimwengu, upendo wa Baba haumo ndani yake.

16 Kwa maana kila kitu kilichomo ulimwenguni, yaani tamaa ya mwili, tamaa ya macho na kiburi cha uzima: havitokani na Baba bali hutokana na ulimwengu.

17 Nao ulimwengu unapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu milele.

Onyo Dhidi Ya Wapinga Kristo

18 Watoto wadogo, huu ni wakati wa mwisho! Kama mlivyosikia kwamba mpinga Kristo anakuja, hivyo basi wapinga Kristo wengi wamekwisha kuja. Kutokana na hili twajua kwamba huu ni wakati wa mwisho.

19 Walitoka kwetu, lakini hawakuwa wa kwetu hasa. Kwa maana kama wangelikuwa wa kwetu, wangelikaa pamoja nasi, lakini kutoka kwao kulionyesha kwamba hakuna hata mmoja wao aliyekuwa wa kwetu.

20 Lakini ninyi mmetiwa mafuta na yeye Aliye Mtakatifu, nanyi nyote mnaijua kweli.

21 Siwaandikii kwa sababu hamuijui kweli, bali kwa sababu mnaijua, nanyi mnajua hakuna uongo utokao katika kweli.

22 Je, mwongo ni nani? Mwongo ni mtu yule asemaye kwamba Yesu si Kristo. Mtu wa namna hiyo ndiye mpinga Kristo, yaani, yeye humkana Baba na Mwana.

23 Hakuna ye yote amkanaye Mwana aliye na Baba. Ye yote anayemkubali Mwana anaye na Baba pia.

24 Hakikisheni kwamba lile mlilosikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu. Kama lile mlilosikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana na ndani ya Baba.

25 Hii ndiyo ahadi yake kwetu, yaani, uzima wa milele.

26 Ninawaandikia mambo haya kuhusu wale watu ambao wanajaribu kuwapotosha.

27 Kwa habari yenu ninyi, upako ule mlioupata kutoka kwake unakaa ndani yenu, wala ninyi hamna haja ya mtu ye yote kuwafundisha. Lakini kama vile upako wake unavyowafundisha kuhusu mambo yote nayo ni kweli wala si uongo, basi kama ulivyowafundisha kaeni ndani yake.

Watoto Wa Mungu

28 Sasa basi, watoto wadogo, kaeni ndani yake, ili atakapofunuliwa, tuwe na ujasiri, wala tusiaibike mbele zake wakati wa kuja kwake.

29 Kama mkijua kuwa yeye ni mwenye haki, mwajua kwamba kila atendaye haki amezaliwa na yeye.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1JN/2-67c78abc9ba567e2ce6d22d40f617620.mp3?version_id=1627—

1 Yohana 3

1 Oneni ni pendo kuu namna gani alilotupa Baba, kwamba sisi tuitwe watoto wa Mungu! Nasi ndivyo tulivyo. Sababu kwa nini ulimwengu haututambui, ni kwa kuwa haukumtambua yeye.

2 Wapenzi, sasa tu watoto wa Mungu, lakini bado haijadhihirika tutakavyokuwa, lakini twajua ya kwamba yeye atakapodhihirishwa, tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo.

3 Kila mmoja mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama vile yeye alivyo mtakatifu.

4 Kila mtu atendaye dhambi afanya uasi, kwa kuwa dhambi ni uasi.

5 Lakini mwajua ya kuwa yeye alidhihirishwa ili aziondoe dhambi, wala ndani yake hamna dhambi.

6 Kila mtu akaaye ndani yake hatendi dhambi. Kila mtu atendaye dhambi hakumwona yeye wala hakumtambua.

7 Watoto wadogo, mtu ye yote asiwadanganye. Kila mtu atendaye haki ana haki, kama yeye alivyo na haki.

8 Yeye atendaye dhambi ni wa ibilisi, kwa sababu ibilisi amekuwa akitenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa ili aziangamize kazi za ibilisi.

9 Ye yote aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wa Mungu wakaa ndani yake, wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa na Mungu.

10 Kwa jinsi hii tunaweza kujua dhahiri watoto wa Mungu na pia watoto wa ibilisi. Ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.

Mpendane Ninyi Kwa Ninyi

11 Hili ndilo neno mlilolisikia tangu mwanzo: Kwamba imetupasa tupendane sisi kwa sisi.

12 Msiwe kama Kaini aliyekuwa wa yule mwovu akamwua ndugu yake. Basi kwa nini alimwua? Ni kwa sababu matendo yake Kaini yalikuwa mabaya na ya ndugu yake yalikuwa ya haki.

13 Ndugu zangu, ninyi msistaajabu kama ulimwengu ukiwachukia.

14 Sisi tunajua ya kwamba tumepita kutoka mautini kuingia uzimani, kwa sababu tunawapenda ndugu. Kila asiyempenda ndugu yake akaa mautini.

15 Ye yote amchukiaye ndugu yake ni mwuaji, nanyi mwajua ya kwamba mwuaji hana uzima wa milele ndani yake.

16 Kwa namna hii twaweza kulijua pendo la Mungu: Kwa sababu Yesu Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu. Nasi imetupasa kuutoa uhai kwa ajili ya hao ndugu.

17 Ikiwa mtu anavyo vitu vya ulimwengu huu na akamwona ndugu yake ni mhitaji lakini asimhurumie, upendo wa Mungu wakaaje ndani ya mtu huyo?

18 Watoto wangu wadogo, tusipende kwa maneno au kwa ulimi bali kwa tendo na katika kweli.

19 Basi hivi ndivyo tutakavyoweza kujua ya kuwa sisi tu wa kweli na hivyo twaithibitisha mioyo yetu mbele za Mungu

20 kila mara mioyo yetu inapotuhukumu. Kwa maana Mungu ni mkuu kuliko mioyo yetu, naye anajua kila kitu.

21 Wapenzi, kama mioyo yetu haituhukumu, tunao ujasiri mbele za Mungu,

22 lo lote tuombalo, twalipokea kutoka kwake, kwa sababu tumezitii amri zake na kutenda yale yanayompendeza.

23 Hii ndiyo amri yake: kwamba tuliamini Jina la Mwanawe, Yesu Kristo na kupendana sisi kwa sisi kama yeye alivyotuamuru.

24 Wale wote wanaozishika amri zake hukaa ndani yake na yeye ndani yao. Hivi ndivyo tunavyojua kwamba anakaa ndani yetu. Nasi twajua hili kwa njia ya Roho yule aliyetupatia.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1JN/3-11b25ab5b139a55b5c4e39c9b52fcd54.mp3?version_id=1627—

1 Yohana 4

Zijaribuni Hizo Roho

1 Wapenzi, msiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho mwone kama zimetoka kwa Mungu, kwa sababu manabii wengi wa uongo wametokea ulimwenguni.

2 Hivi ndivyo mnavyoweza kutambua Roho wa Mungu: Kila roho inayokubali kwamba Yesu Kristo amekuja katika mwili yatoka kwa Mungu.

3 Lakini kila roho ambayo haimkubali Yesu haitoki kwa Mungu. Hii ndiyo roho ya mpinga Kristo, ambayo mmesikia kwamba inakuja na sasa tayari iko ulimwenguni.

4 Watoto wadogo, ninyi mmetokana na Mungu, nanyi mmewashinda kwa sababu yeye aliye ndani yenu ni mkuu kuliko yeye aliye katika ulimwengu.

5 Wao wanatokana na ulimwengu na kwa hiyo hunena yaliyo ya ulimwengu, hivyo ulimwengu huwasikiliza.

6 Sisi twatokana na Mungu na ye yote anayemjua Mungu hutusikiliza, lakini asiyetokana na Mungu hatusikilizi. Hivi ndivyo tunavyoweza kutambua Roho wa Kweli na roho ya upotovu.

Mungu Ni Pendo

7 Wapenzi na tupendane, kwa kuwa pendo latoka kwa Mungu. Kila apendaye amezaliwa na Mungu naye anamjua Mungu.

8 Yeye asiyependa hamjui Mungu, kwa sababu Mungu ni pendo.

9 Hivi ndivyo Mungu alivyoonyesha pendo lake kwetu, kwa sababu Mungu alimtuma Mwanawe wa pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye.

10 Hili ndilo pendo, si kwamba tulimpenda Mungu, bali yeye alitupenda, akamtuma Mwanawe, ili yeye awe dhabihu ya kipatanisho kwa ajili ya dhambi zetu.

11 Wapenzi, kama Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana.

12 Hakuna mtu ye yote aliyemwona Mungu wakati wo wote. Kama tukipendana, Mungu anakaa ndani yetu na pendo lake limekamilika ndani yetu.

13 Tunajua kwamba twakaa ndani yake na yeye ndani yetu, kwa sababu ametupatia sisi sehemu ya Roho wake.

14 Nasi tumeona na kushuhudia kwamba Baba amemtuma Mwanawe ili awe Mwokozi wa ulimwengu.

15 Kila akiriye kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu.

16 Hivyo nasi twajua na kulitumainia pendo la Mungu alilo nalo kwa ajili yetu.

Mungu ni Upendo. Kila akaaye katika upendo hukaa ndani ya Mungu na Mungu hukaa ndani yake.

17 Kwa njia hii, pendo hukamilishwa miongoni mwetu ili tupate kuwa na ujasiri katika siku ya hukumu, kwa sababu kama alivyo ndivyo tulivyo sisi katika ulimwengu huu.

18 Katika pendo hakuna hofu. Lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa sababu hofu inahusika na adhabu. Kila mwenye hofu hakukamilika katika pendo.

19 Twampenda yeye kwa sababu yeye alitupenda kwanza.

20 Ikiwa mtu atasema, “Nampenda Mungu”, lakini anamchukia ndugu yake, yeye ni mwongo. Kwa maana kila mtu asiyempenda ndugu yake ambaye anamwona, atampendaje Mungu ambaye hamwoni?

21 Naye ametupa amri hii: Ye yote anayempenda Mungu lazima pia ampende ndugu yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1JN/4-da140fe4bea113ca38646cc429c73232.mp3?version_id=1627—

1 Yohana 5

Imani Katika Mwana Wa Mungu Huushinda Ulimwengu

1 Kila mtu anayeamini kwamba Yesu ndiye Kristo amezaliwa na Mungu na ye yote ampendaye Baba humpenda pia mtoto aliyezaliwa naye.

2 Hivi ndivyo tunavyojua kwamba tunawapenda watoto wa Mungu, kwa kumpenda Mungu na kuzitii amri zake.

3 Huku ndiko kumpenda Mungu, yaani, kuzitii amri zake. Nazo amri zake si nzito.

4 Kwa maana kila aliyezaliwa na Mungu huushinda ulimwengu. Huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, yaani, hiyo imani yetu.

5 Ni nani yule aushindaye ulimwengu? Ni yule tu aaminiye kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.

Ushuhuda Kuhusu Mwana Wa Mungu

6 Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, yaani, Yesu Kristo. Hakuja kwa maji peke yake, bali kwa maji na damu. Naye Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli.

7 Kwa maana wako watatu washuhudiao [mbinguni: hao ni Baba, Neno na Roho Mtakatifu. Hawa watatu ni wamoja.

8 Pia wako mashahidi watatu duniani], yaani Roho, Maji na Damu; wote hawa watatu wanakubaliana katika umoja.

9 Kama tunaukubali ushuhuda wa wanadamu, basi ushuhuda wa Mungu ni mkuu zaidi, kwa kuwa huu ndio ushuhuda wa Mungu kwamba amemshuhudia Mwanawe.

10 Kila mtu amwaminiye Mwana wa Mungu anao huu ushuhuda moyoni mwake. Kila mtu asiyemwamini Mungu amemfanya yeye kuwa mwongo, kwa sababu hakuamini ushuhuda Mungu alioutoa kuhusu Mwanawe.

11 Huu ndio ushuhuda: kwamba Mungu ametupa uzima wa milele, nao huo uzima umo katika Mwanawe.

12 Aliye naye Mwana wa Mungu anao uzima, yeye asiye na Mwana wa Mungu hana uzima.

Maneno Ya Mwisho

13 Nawaandikia mambo haya ninyi mnaoliamini Jina la Mwana wa Mungu ili mpate kujua ya kuwa mnao uzima wa milele.

14 Huu ndio ujasiri tulionao tunapomkaribia Mungu, kwamba kama tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia.

15 Nasi kama tunajua ya kuwa atusikia, lo lote tuombalo, tunajua ya kwamba tumekwisha kupata zile haja tulizomwomba.

16 Kama mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, inampasa aombe, naye Mungu atampa uzima mtu huyo, ninamaanisha, wale ambao dhambi yao si ya mauti. Iko dhambi ya mauti, sisemi kwamba utaomba kwa ajili ya hiyo.

17 Jambo lo lote lisilo la haki ni dhambi, lakini iko dhambi isiyo ya mauti.

18 Tunajua ya kuwa yeye aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, bali aliyezaliwa na Mungu hujilinda wala yule mwovu hawezi kumdhuru.

19 Sisi twajua kuwa tu watoto wa Mungu na ya kwamba ulimwengu wote uko chini ya utawala wa yule mwovu.

20 Nasi pia twajua ya kwamba Mwana wa Mungu amekuja, naye ametupa sisi ufahamu ili tupate kumjua yeye aliye Kweli. Nasi tumo ndani yake yeye aliye Kweli, yaani, ndani ya Yesu Kristo Mwanawe. Yeye ndiye Mungu wa kweli na uzima wa milele.

21 Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1JN/5-03bc27e19822e3a3ade9a564de5c9c05.mp3?version_id=1627—