Ufunuo 11

Mashahidi Wawili

1 Ndipo nikapewa mwanzi wa kupimia ulio kama fimbo, nikaambiwa, “Nenda ukapime Hekalu la Mungu pamoja na madhabahu, nawe uwahesabu wale waabuduo humo.

2 Lakini usiupime ua wa nje wa Hekalu, uache, kwa sababu ua huo wamepewa watu Mataifa. Hao wataukanyagakanyaga mji mtakatifu kwa muda wa miezi arobaini na miwili.

3 Nami nitawapa mashahidi wangu wawili uwezo, nao watoe unabii kwa muda wa siku 1,260, wakiwa wamevaa nguo za gunia.”

4 Hawa ndio ile mizeituni miwili na vile vinara viwili vya taa visimamavyo mbele za Bwana Mungu wa dunia yote.

5 Kama mtu ye yote akitaka kuwadhuru, moto hutoka vinywani mwao na kuwateketeza adui zao. Hivi ndivyo impasavyo kufa mtu ye yote atakayetaka kuwadhuru.

6 Watu hawa wanao uwezo wa kufunga anga ili mvua isinyeshe wakati wote watakapokuwa wanatoa unabii wao. Nao watakuwa na uwezo wa kuyabadili maji kuwa damu na kuipiga dunia kwa kila aina ya mapigo mara kwa mara kama watakavyo.

7 Basi watakapokuwa wamemaliza ushuhuda wao, yule mnyama atokaye katika lile Shimo lisilo na mwisho atapigana nao vita, atawashinda na kuwaua.

8 Maiti zao zitabaki katika barabara ya mji mkubwa, ambao kwa fumbo unaitwa Sodoma na Misri, ambapo pia Bwana wao alisulibiwa.

9 Kwa muda wa siku tatu na nusu, watu wa kila kabila, jamaa, lugha na taifa wataziangalia hizo maiti zao na hawataruhusu wazikwe.

10 Watu waishio duniani watazitazama kwa furaha maiti za hao manabii wawili na kushangilia kwa kupeana zawadi kwa sababu hao manabii waliwatesa watu waishio duniani.

11 Lakini baada ya zile siku tatu na nusu, pumzi ya uhai kutoka kwa Mungu ikawaingia, nao wakasimama kwa miguu yao na wote waliowaona wakaingiwa na hofu kuu.

12 Kisha wale manabii wawili wakasikia sauti kuu kutoka mbinguni ikiwaambia, “Njoni huku juu!” Nao wakapaa mbinguni katika wingu, wakati adui zao wakiwa wanawatazama.

13 Saa iyo hiyo, kukatokea tetemeko kubwa la nchi na sehemu ya kumi ya mji ikaanguka. Watu elfu saba wakauawa katika tetemeko hilo, nao walionusurika wakaogopa sana, wakamtukuza Mungu wa mbinguni.

14 Ole ya pili imekwisha kupita, tazama ole ya tatu inakuja upesi.

Tarumbeta Ya Saba

15 Yule malaika wa saba akaipiga tarumbeta yake, pakawa na sauti kubwa mbinguni iliyosema:

“Ufalme wa ulimwengu umekuwa ufalme wa Bwana wetu na wa Kristo wake,

naye atatawala milele na milele.”

16 Nao wale wazee ishirini na wanne, waliokuwa wameketi mbele za Mungu, kwenye viti vyao vya enzi wakaanguka kifudifudi wakamwabudu Mungu,

17 wakisema:

“Tunakushukuru, BWANA Mungu Mwenyezi,

uliyeko na uliyekuwako,

kwa kuwa umetwaa uweza wako mkuu

na ukaanza kutawala.

18 Mataifa walikasirika kwa kuwa

wakati wa ghadhabu Yako umewadia.

Wakati umewadia wa kuwahukumu waliokufa

na kuwapa thawabu watumishi wako manabii

na watakatifu wako pamoja na wale wote

wanaoliheshimu Jina Lako,

wakubwa kwa wadogo:

na kuwaangamiza wale wanaoiangamiza dunia.”

19 Ndipo Hekalu la Mungu lililoko mbinguni likafunguliwa na Sanduku la Agano lake likaonekana humo ndani. Kukatokea mianga ya umeme wa radi, ngurumo, sauti za radi, tetemeko la nchi na mvua kubwa ya mawe.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/11-eab956d93de83483e6b6c4ee767577fd.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 12

Mwanamke Na Joka

1 Kukaonekana ishara kuu mbinguni: Palikuwa na mwanamke aliyevikwa jua na mwezi ukiwa chini ya miguu yake na taji ya nyota kumi na mbili ilikuwa kichwani mwake.

2 Alikuwa na mimba naye akilia kwa uchungu kwa kuwa alikuwa anakaribia kuzaa.

3 Kisha ishara nyingine ikaonekana mbinguni: Likaonekana joka kubwa jekundu lenye vichwa saba na pembe kumi na taji saba katika vichwa vyake.

4 Mkia wake ukakokota theluthi ya nyota zote angani na kuziangusha katika nchi. Ndipo lile joka likasimama mbele ya yule mwanamke aliyekuwa karibu kuzaa ili lipate kumla huyo mtoto mara tu atakapozaliwa.

5 Yule mwanamke akazaa mtoto mwanamume, atakayeyatawala mataifa yote kwa fimbo yake ya utawala ya chuma. Lakini huyo mtoto akanyakuliwa na kupelekwa kwa Mungu kwenye kiti chake cha enzi.

6 Yule mwanamke akakimbilia nyikani, ambako Mungu alikuwa amemtayarishia mahali ili apate kutunzwa huko kwa muda wa siku 1,260.

Malaika Mikaeli Amshinda Yule Joka

7 Basi palikuwa na vita mbinguni: Mikaeli na malaika zake wakapigana na hilo joka, nalo joka pamoja na malaika zake likapigana nao.

8 Lakini joka na malaika zake wakashindwa na hapakuwa tena na nafasi kwa ajili yao mbinguni.

9 Lile joka kuu likatupwa chini, yule nyoka wa zamani aitwaye ibilisi au Shetani, aupotoshaye ulimwenguni wote. Akatupwa chini duniani, yeye pamoja na malaika zake.

Ushindi Mbinguni Watangazwa

10 Kisha nikasikia sauti kuu mbinguni, ikisema:

“Sasa Wokovu na uweza na Ufalme wa Mungu wetu umekuja

na mamlaka ya Kristo wake.

Kwa kuwa ametupwa chini

mshtaki wa ndugu zetu,

anayewashtaki mbele za Mungu

usiku na mchana.

11 Nao wakamshinda

kwa damu ya Mwana-Kondoo

na kwa neno la ushuhuda wao.

Wala wao hawakuyapenda maisha yao

hata kufa.

12 Kwa hiyo, furahini ninyi mbingu

na wote wakaao humo!

Lakini ole wenu nchi na bahari,

kwa maana huyo Shetani ameshuka kwenu,

akiwa amejaa ghadhabu,

kwa sababu anajua ya kuwa

muda wake ni mfupi!”

13 Lile joka lilipoona kuwa limetupwa chini duniani, lilimfuatilia yule mwanamke aliyekuwa amezaa mtoto mwanamume.

14 Lakini huyo mwanamke akapewa mabawa mawili ya tai mkubwa, kusudi aweze kuruka mpaka mahali palipotayarishwa kwa ajili yake huko nyikani, ambako atatunzwa kwa wakati na nyakati na nusu, wakati ambako yule joka hawezi kufika.

15 Ndipo lile joka likamwaga maji kama mto kutoka kinywani mwake, ili kumfikia huyo mwanamke na kumkumba kama mafuriko.

16 Lakini nchi ikamsaidia huyo mwanamke kwa kufungua kinywa na kuumeza huo mto ambao huyo joka alikuwa ameutoa kinywani mwake.

17 Kisha lile joka likapatwa na hasira kali kwa ajili ya huyo mwanamke, likaondoka ili kupigana vita na watoto waliosalia wa huyo mwanamke, yaani, wale wanaozitii amri za Mungu na kuushika ushuhuda wa Yesu Kristo. Lile joka likasimama kwenye mchanga wa bahari.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/12-ac1302b27797bf067ba61a0c115d7adf.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 13

1 Yule joka akajikita katika mchanga ulioko ufuoni mwa bahari.

Mnyama Kutoka Baharini

Nami nikamwona mnyama akitoka ndani ya bahari. Mnyama huyo alikuwa na pembe kumi na vichwa saba, akiwa na taji kumi kwenye hizo pembe zake na juu ya kila kichwa kulikuwa na jina la kukufuru.

2 Mnyama yule niliyemwona alikuwa kama chui, miguu yake ilikuwa kama ya dubu na kichwa chake kama cha simba. Lile joka likampa huyo mnyama nguvu zake, kiti chake cha enzi na mamlaka makubwa.

3 Kimojawapo ya vichwa vya huyo mnyama kilikuwa kama kilichokwisha kupata jeraha la mauti, lakini jeraha hilo la mauti likapona. Ulimwengu wote ukashangaa ukamfuata huyo mnyama.

4 Watu wakaliabudu lile joka kwa sababu lilikuwa limempa huyo mnyama mamlaka yake, pia wakamwabudu huyo mnyama na kuuliza, “Ni nani aliye kama huyu mnyama? Ni nani awezaye kupigana vita naye?”

5 Huyo mnyama akapewa kusema maneno ya kujisifu na kukufuru na kutumia mamlaka yake kwa muda wa miezi arobaini na miwili.

6 Akafungua kinywa chake ili kumkufuru Mungu, akilitukana Jina lake na mahali aishipo na wale wakaao mbinguni.

7 Pia akaruhusiwa kufanya vita na watakatifu na kuwashinda. Akapewa uwezo juu ya watu wa kila kabila, jamaa, lugha na taifa.

8 Nao watu wote waishio duniani watamwabudu huyo mnyama, yaani, wale wote ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima cha Mwana-Kondoo aliyechinjwa tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

9 Yeye aliye na sikio na asikie.

10 Ikiwa mtu ni wa kuchukuliwa mateka,

atachukuliwa mateka.

Ikiwa mtu ni wa kuuawa kwa upanga,

atauawa kwa upanga.

Hapa ndipo penye wito kwa ajili ya saburi na imani ya watakatifu.

Mnyama Kutoka Katika Dunia

11 Kisha nikamwona mnyama mwingine, akipanda juu kutoka katika dunia. Alikuwa na pembe mbili kama mwana-kondoo, lakini akanena kama joka.

12 Akatumia mamlaka yote ya yule mnyama wa kwanza kwa niaba yake, naye akawafanya wote wakaao duniani kumwabudu yule mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona.

13 Naye akafanya ishara kuu na za ajabu, hata kusababisha moto kushuka toka mbinguni kuja duniani watu wakiona waziwazi.

14 Kwa sababu ya zile ishara alizokuwa amepewa uwezo wa kufanya kwa niaba ya yule mnyama wa kwanza, akawadanganya wakaao duniani. Akawaamuru wasimamishe sanamu kwa heshima ya yule mnyama aliyekuwa amejeruhiwa kwa upanga lakini akaishi.

15 Akapewa uwezo wa kuipa pumzi ile sanamu ya yule mnyama wa kwanza, ili iweze kusema na kuwasababisha wale wote waliokataa kuiabudu hiyo sanamu kuuawa.

16 Pia alimlazimisha kila mmoja, mdogo na mkubwa, tajiri na maskini, mtu huru na mtumwa, atiwe chapa kwenye mkono wake wa kuume au kwenye kipaji chake cha uso,

17 ili kwamba mtu ye yote asiweze kununua wala kuuza isipokuwa amekuwa na hiyo chapa, ambayo ni jina la huyo mnyama au tarakimu za jina lake.

18 Hapa ndipo penye hekima. Yeye aliye na ufahamu na ahesabu tarakimu za huyo mnyama, kwa maana ni tarakimu za kibinadamu. Tarakimu zake ni 666.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/13-f1139f2ea8b9e65e8d55840879066ddd.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 14

Mwana-Kondoo Na Wale 144,000

1 Kisha nikatazama na hapo mbele yangu alikuwepo Mwana-Kondoo, akiwa amesimama juu ya Mlima Sayuni. Pamoja naye walikuwa wale 144,000 wenye Jina la Mwana-Kondoo na Jina la Baba yake likiwa limeandikwa kwenye vipaji vya nyuso zao.

2 Nami nikasikia sauti kutoka mbinguni kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na sauti kama ngurumo ya radi. Sauti hiyo niliyoisikia ilikuwa kama sauti ya wapiga vinubi wakipiga vinubi vyao.

3 Nao wakaimba wimbo mpya mbele ya hicho kiti cha enzi na mbele ya wale viumbe wenye uhai wanne na wale wazee ishirini na wanne. Hakuna mtu ye yote aliyeweza kujifunza wimbo huo isipokuwa hao 144,000 waliokuwa wamekombolewa kutoka duniani.

4 Hawa ndio wale ambao hawakujitia unajisi kwa wanawake, kwa kuwa wao ni mabikira. Wao humfuata Mwana-Kondoo kila aendako. Hawa wamekombolewa kutoka miongoni mwa wanadamu wakawa malimbuko kwa Mungu na kwa Mwana-Kondoo.

5 Vinywani mwao hapakuonekana uongo, wala hawakuwa na hatia yo yote.

Malaika Watatu

6 Kisha nikamwona malaika mwingine akiruka juu angani, naye alikuwa na Injili ya milele ya kuwatangazia wale waishio duniani, yaani, kwa kila taifa, kabila, lugha na jamaa.

7 Akasema kwa sauti kubwa, “Mcheni Mungu na kumpa utukufu, kwa maana saa ya hukumu yake imewadia. Mwabuduni yeye aliyeziumba mbingu, dunia, bahari na chemchemi za maji.”

8 Malaika wa pili akafuata akisema, “Ameanguka! Ameanguka Babeli aliye mkuu, yeye aliyeyafanya mataifa yote kulewa kwa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake.”

9 Malaika wa tatu akawafuata hao wawili akisema kwa sauti kubwa, “Kama mtu ye yote anamwabudu huyo mnyama na sanamu yake na kutiwa chapa yake kwenye kipaji chake cha uso au kwenye mkono wake,

10 yeye naye, atakunywa mvinyo wa hasira kali ya Mungu ambayo imemiminwa katika kikombe cha ghadhabu yake pasipo kuchanganywa na maji. Naye atateswa kwa moto uwakao na kiberiti mbele ya malaika watakatifu na mbele za Mwana-Kondoo.

11 Nao moshi wa mateso yao hupanda juu milele na milele. Hakuna mapumziko, mchana wala usiku, kwa wale wamwabuduo huyo mnyama na sanamu yake, au kwa ye yote anayepokea chapa ya jina lake.”

12 Hapa ndipo penye subira na uvumilivu wa watakatifu, yaani, wale wanaozishika amri za Mungu na kudumu kuwa waaminifu kwa Yesu.

13 Kisha nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Andika: Wamebarikiwa wale wafao katika Bwana tangu sasa.”

“Naam,” asema Roho, “watapumzika kutoka katika taabu zao, kwa kuwa matendo yao yatawafuata.”

Kuvuna Mavuno Ya Dunia

14 Nikatazama, hapo mbele yangu palikuwa na wingu jeupe, na aliyekuwa ameketi juu ya hilo wingu alikuwa “kama Mwana wa Adamu” mwenye taji ya dhahabu kichwani mwake na mundu mkali mkononi mwake.

15 Kisha malaika mwingine akaja kutoka Hekaluni naye akamwita kwa sauti kubwa yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akasema, “Chukua mundu wako ukavune kwa kuwa wakati wa mavuno umewadia, kwa maana mavuno ya dunia yamekomaa.”

16 Hivyo yule aliyekuwa ameketi juu ya lile wingu akauzungusha mundu wake duniani, nayo dunia ikavunwa.

17 Malaika mwingine akatoka katika Hekalu lililoko mbinguni, naye pia alikuwa na mundu mkali.

18 Kisha malaika mwingine, aliyekuwa na mamlaka juu ya moto, akatoka kwenye madhabahu, naye akamwita yule malaika mwenye mundu mkali kwa sauti kubwa, akisema, “Chukua mundu wako mkali ukakusanye vichala vya mizabibu ya dunia, maana zabibu zake zimeiva.”

19 Hivyo yule malaika akauzungusha mundu wake duniani na kukusanya vichala vya zabibu za dunia na kuzitupa kwenye shinikizo kubwa la ghadhabu ya Mungu.

20 Lile shinikizo likakanyagwa nje ya mji, nayo damu ikatiririka kama mafuriko kutoka katika hilo shinikizo kufikia kimo cha hatamu za farasi, kwa umbali wa maili 200.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/14-3e645b069769645022c709ecdf94e8c6.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 15

Malaika Saba Na Mapigo Saba

1 Ndipo nikaona ishara nyingine kubwa ya ajabu mbinguni, malaika saba wenye yale mapigo saba ya mwisho, kwa sababu kwa mapigo hayo ghadhabu ya Mungu ilikuwa imekamilika.

2 Nikaona kile kilichoonekana kama bahari ya kioo iliyochanganyikana na moto. Kando ya hiyo bahari, walikuwa wamesimama wale watu waliomshinda yule mnyama na sanamu yake pamoja na tarakimu ya jina lake. Mikononi mwao walikuwa wameshika vinubi walivyopewa na Mungu.

3 Nao wakaimba wimbo wa Mose, mtumishi wa Mungu na wimbo wa Mwana-Kondoo wakisema:

“BWANA Mungu Mwenyezi,

matendo yako ni makuu na ya ajabu.

Njia zako wewe ni za haki na za kweli

Mfalme wa nyakati zote!

4 Ni nani ambaye hatakuogopa wewe Bwana

na kulitukuza jina lako?

Kwa kuwa wewe peke yako ndiwe mtakatifu.

Mataifa yote yatakuja

na kuabudu mbele zako,

kwa kuwa matendo yako ya haki

yamedhihirishwa.”

5 Baada ya haya nikatazama, nalo Hekalu la hema la Ushuhuda lilikuwa limefunguliwa mbinguni.

6 Ndani ya lile Hekalu wakatoka malaika saba wakiwa na mapigo saba. Walikuwa wamevaa nguo safi za kitani ing’aayo na kufungwa mikanda ya dhahabu vifuani mwao.

7 Ndipo mmoja wa wale wenye uhai wanne akawapa wale malaika saba mabakuli saba ya dhahabu yaliyojaa ghadhabu ya Mungu, yeye aishiye milele na milele.

8 Nalo lile Hekalu lilijawa na moshi uliotokana na utukufu wa Mungu na uweza wake, wala hakuna ye yote aliyeweza kuingia mle Hekaluni mpaka yale mapigo saba ya wale malaika saba yalipomalizika.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/15-3ec0b7ac9fb05e65ff21005342ee7cc5.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 16

Mabakuli Saba Ya Ghadhabu Ya Mungu

1 Kisha nikasikia sauti kubwa kutoka mle Hekaluni ikiwaambia wale malaika saba, “Nendeni, mkayamwage duniani hayo mabakuli saba ya ghadhabu ya Mungu.”

2 Malaika wa kwanza akaenda akalimwaga hilo bakuli lake juu ya nchi. Majipu mabaya yenye maumivu makali yakawapata wale watu wote waliokuwa na chapa ya yule mnyama na walioabudu sanamu yake.

3 Malaika wa pili akalimwaga bakuli lake baharini, nayo ikabadilika kuwa damu kama ya mtu aliyekufa na kila kiumbe hai kilichokuwa ndani ya bahari kikafa.

4 Malaika wa tatu akalimwaga bakuli lake katika mito na chemchemi za maji, nazo zikawa damu.

5 Ndipo nikamsikia malaika msimamizi wa maji akisema:

“Wewe una haki katika hukumu hizi ulizotoa,

wewe uliyeko, uliyekuwako, uliye Mtakatifu,

kwa sababu umehukumu hivyo;

6 kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu wako

na manabii wako,

nawe umewapa damu wanywe

kama walivyostahili.”

7 Nikasikia madhabahu ikiitikia,

“Naam, BWANA Mungu Mwenyezi,

hukumu zako ni kweli na haki.”

8 Malaika wa nne akamimina bakuli lake kwenye jua, nalo likapewa nguvu za kuwaunguza watu kwa moto.

9 Watu wakaunguzwa na hilo joto kali, wakalaani Jina la Mungu, aliyekuwa na uwezo juu ya mapigo haya, tena wakakataa kutubu na kumtukuza Mungu.

10 Malaika wa tano akamimina bakuli lake kwenye kiti cha enzi cha yule mnyama, nao ufalme wake ukagubikwa na giza. Watu wakatafuna ndimi zao kwa ajili ya maumivu

11 wakamlaani Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu na majeraha yao, wala hawakutubu kwa ajili ya matendo yao maovu.

12 Malaika wa sita akamimina bakuli lake kwenye mto mkubwa Eufrati, maji yake yakakauka ili kutayarisha njia kwa ajili ya wafalme watokao Mashariki.

13 Kisha nikaona roho wachafu watatu waliofanana na vyura wakitoka katika kinywa cha lile joka na katika kinywa cha yule mnyama na katika kinywa cha yule nabii wa uongo.

14 Hizo ndizo roho za pepo wachafu zitendazo miujiza. Nazo huwaendea wafalme wa ulimwengu wote na kuwakusanya tayari kwa ajili ya vita katika siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi.

15 “Tazama, naja kama mwivi! Amebarikiwa yeye akeshaye na kuziweka tayari nguo zake ili asiende uchi na kuonekana aibu yake.”

16 Ndipo wakawakusanya wafalme pamoja mahali paitwapo Armagedonikwa Kiebrania.

17 Malaika wa saba akamimina bakuli lake angani na sauti kubwa ikatoka mle Hekaluni katika kile kiti cha enzi, ikisema, “Imekwisha kuwa!”

18 Kukawa na mianga ya umeme wa radi, ngurumo, radi na tetemeko kubwa la ardhi. Hapajawa kamwe na tetemeko la ardhi kama hilo tangu mwanadamu awepo duniani, hivyo lilikuwa tetemeko kubwa ajabu.

19 Ule mji mkubwa ukagawanyika katika sehemu tatu, nayo miji ya mataifa ikaanguka. Mungu akaukumbuka Babeli ule uliokuwa mkuu na kuupa kikombe cha hasira na ghadhabu yake.

20 Kila kisiwa kikatoweka wala milima haikuonekana.

21 Mvua kubwa ya mawe, mawe yenye uzito wa talanta mojayakaanguka kutoka mbinguni, yakawaangukia wanadamu. Nao wanadamu wakamlaani Mungu kwa ajili ya hayo mapigo ya mvua ya mawe, kwa sababu pigo hilo lilikuwa la kutisha.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/16-cacbcd1969f59e1688038a0d7a81d5de.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 17

Kahaba Mkuu Na Mnyama

1 Mmoja wa wale malaika saba waliokuwa na yale mabakuli saba akaja akaniambia, “Njoo, nitakuonyesha adhabu ya yule kahaba mkuu, aketiye juu ya maji mengi.

2 Yule ambaye wafalme wa dunia walizini naye na watu wakaao duniani walilewa kwa mvinyo wa uzinzi wake.”

3 Kisha yule malaika akanichukua katika Roho akanipeleka nyikani. Huko nikamwona mwanamke mmoja ameketi juu ya mnyama mwekundu aliyejaa majina ya kumkufuru Mungu mwili mzima. Mnyama huyo alikuwa na vichwa saba na pembe kumi.

4 Huyo mwanamke alikuwa amevaa mavazi ya rangi ya zambarau na nyekundu, akimetameta kwa dhahabu, vito vya thamani na lulu. Mkononi mwake alikuwa ameshika kikombe cha dhahabu kilichojaa mambo ya machukizo na uchafu wa uzinzi wake.

5 Kwenye kipaji chake cha uso palikuwa pameandikwa jina:

“SIRI,

BABELI MKUU,

MAMA WA MAKAHABA

NA MACHUKIZO YA DUNIA.”

6 Nikaona kuwa huyo mwanamke alikuwa amelewa kwa damu ya watakatifu, yaani, damu ya wale watu waliouawa kwa ushuhuda wa Yesu.

Nilipomwona huyo mwanamke, nilistaajabu sana.

7 Ndipo yule malaika akaniambia, “Kwa nini unastaajabu? Nitakufafanulia siri ya huyo mwanamke na huyo mnyama aliyempanda, mwenye vichwa saba na pembe kumi.

8 Huyo mnyama, ambaye ulimwona, wakati fulani alikuwepo, lakini sasa hayupo, naye atapanda kutoka katika lile Shimo lisilo na mwisho na kwenda kwenye maangamizo yake. Watu waishio duniani ambao majina yao hayakuandikwa kwenye kitabu cha uzima tangu kuumbwa kwa ulimwengu watastaajabu kumwona huyo mnyama, kwa maana alikuwepo, wakati fulani na sasa hayupo, lakini atakuja.

9 “Hapa ndipo penye akili pamoja na hekima. Vile vichwa saba ni vilima saba ambavyo huyo mwanamke amevikalia.

10 Pia hivyo vichwa saba ni wafalme saba ambao miongoni mwao watano wamekwisha kuanguka, mwingine hajaja bado, lakini atakapokuja, atalazimika kukaa kwa muda mfupi.

11 Yule mnyama aliyekuwepo wakati fulani na ambaye sasa hayupo, yeye ni mfalme wa nane. Ni miongoni mwa wale saba, naye anakwenda kwenye maangamizi yake.

12 “Zile pembe kumi ulizoziona ni wafalme kumi ambao bado hawajapokea ufalme, lakini ambao watapokea mamlaka kuwa wafalme kwa saa moja pamoja na yule mnyama.

13 Hawa wana nia moja, nao watamwachia yule mnyama nguvu zao na mamlaka yao.

14 Watafanya vita na Mwana-Kondoo, lakini Mwana-Kondoo atawashinda kwa sababu yeye ni Bwana wa mabwana na Mfalme wa wafalme. Yeye atakuwa pamoja na watu wake walioitwa ambao ni wateule wake na wafuasi wake waaminifu.”

15 Kisha yule malaika akaniambia, “Yale maji uliyoyaona, yule kahaba akiwa ameketi juu yake ni jamaa za watu, makutano, mataifa na lugha.

16 Zile pembe kumi ulizoziona, pamoja na huyo mnyama, watamchukia huyo kahaba, watamfilisi na kumwacha uchi, watamla nyama yake na kumteketeza kwa moto.

17 Kwa maana Mungu ataweka mioyoni mwao kutimiza kusudi lake kwa kukubali kumpa yule mnyama mamlaka yao ya utawala mpaka maneno ya Mungu yatakapotimia.

18 Yule mwanamke uliyemwona ni ule mji mkubwa unaotawala juu ya wafalme wa dunia.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/17-8b6cb27aa61599aa7c16fc16f7a2a204.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 18

Kuanguka Kwa Babeli

1 Baada ya haya nikaona malaika mwingine akishuka kutoka mbinguni, akiwa na mamlaka makuu na dunia ikamulikiwa na mng’ao wake.

2 Naye akalia kwa nguvu kwa sauti kubwa, akisema:

“Umeanguka! Umeanguka Babeli uliye Mkuu!

Umekuwa makao ya mashetani

na makazi ya kila pepo mchafu,

makazi ya kila ndege na kila mnyama achukizaye.

3 Kwa maana mataifa yote yamekunywa

mvinyo wa uasherati wake.

Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi naye,

nao wafanya biashara wa dunia

wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.”

4 Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema:

“Tokeni katikati yake, enyi watu wangu,

ili msije mkashiriki dhambi zake,

ili msije mkapatwa na pigo lake lo lote;

5 kwa kuwa dhambi zake zimerundikana hadi mbinguni,

naye Mungu ameukumbuka uhalifu wake.

6 Mtendee kama yeye alivyotenda;

umlipe mara mbili kwa ajili ya yale aliyotenda.

Katika kikombe chake mchanganyie

mara mbili ya kile alichochanganya.

7 Mpatie mateso na huzuni nyingi sawa na

utukufu na anasa alizojipatia.

Kwa kuwa moyoni mwake hujivuna, akisema,

‘Mimi ninatawala kama malkia;

mimi si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.’

8 Kwa hiyo mapigo yatampata kwa siku moja:

mauti, maombolezo na njaa.

Naye atateketezwa kwa moto,

kwa maana amhukumuye

ni BWANA Mungu Mwenyezi.

9 “Wafalme wa dunia waliozini naye na kushiriki anasa zake watakapoona moshi wa kuungua kwake, watamlilia na kumwombolezea.

10 Watasimama mbali na kulia kwa hofu kutokana na mateso yake na kusema:

“ ‘Ole! Ole Ee mji mkubwa,

Ee Babeli mji wenye nguvu!

Hukumu yako imekuja katika saa moja!’

11 “Wafanyabiashara wa dunia watalia na kuomboleza kwa sababu hakuna anunuaye bidhaa zao tena:

12 Bidhaa za dhahabu, za fedha, za vito vya thamani na vya lulu, kitani safi, nguo za rangi ya zambarau, hariri, nguo nyekundu, aina zote za miti ya manukato, vifaa vyote vya pembe za ndovu, vifaa vyote vya miti yenye thamani kuliko yote, shaba nyeusi, chuma na marmar,

13 mdalasini, vikolezi, uvumba, manemane, uvumba wenye harufu nzuri, divai, mafuta ya zeituni, unga mzuri na ngano, ng’ombe na kondoo, farasi na magari, watumwa, pia na roho za wanadamu.

14 “Watasema, ‘Yale matunda ambayo roho yako iliyatamani yamekoma. Utajiri wako wote na fahari yako vimetoweka, wala haviwezi kupatikana tena kamwe!’

15 Wale wafanyabiashara waliotajirika kwa bidhaa hizo kutoka kwake watasimama mbali naye kwa hofu ya mateso yanayompata. Watalia na kuomboleza wakipiga kelele wakisema:

16 “ ‘Ole! Ole, Ee, mji mkubwa,

uliyekuwa umevikwa mavazi ya kitani safi,

ya rangi ya zambarau na nyekundu,

ukimetameta kwa dhahabu,

vito vya thamani na lulu!

17 Katika muda wa saa moja utajiri wote mkubwa

kama huu umeangamia!’

“Kila nahodha, mabaharia wote wasafirio baharini na wote wapatao kipato chao kutokana na bahari, watasimama mbali naye.

18 Watakapoona moshi wa kuungua kwake watalia wakisema, ‘Je, kulipata kuwako mji mkubwa kama huu?’

19 Nao watajirushia mavumbi vichwani mwao, huku wakilia na kuomboleza, wakisema:

“ ‘Ole! Ole, Ee mji mkubwa,

mji ambao wote wenye meli baharini

walitajirika kwa kupitia mali zake!

Katika saa moja tu ameangamizwa!

20 Furahia kwa ajili yake, Ee mbingu!

Furahini watakatifu, mitume na manabii!

Kwa kuwa Mungu amemhukumu

kwa vile alivyowatendea ninyi.’ ”

21 Kisha malaika mmoja mwenye nguvu akainua jiwe kubwa kama la kusagia akalitupa baharini akisema:

“Hivyo ndivyo mji mkubwa Babeli

utakavyotupwa chini kwa nguvu

wala hautaonekana tena.

22 Nyimbo za wapiga vinubi na waimbaji,

wapiga filimbi na sauti za wapiga tarumbeta

kamwe hazitasikika tena ndani yako.

Ndani yako kamwe hataonekana tena fundi

mwenye ujuzi wa aina yo yote.

Wala sauti ya jiwe la kusagia

kamwe haitasikika tena.

23 Mwanga wa taa

hautaangaza ndani yako tena.

Sauti ya bwana arusi na bibi arusi

kamwe haitasikiwa ndani yako tena.

Wafanyabiashara wako walikuwa watu maarufu wa dunia.

Mataifa yote yalipotoshwa kwa uchawi wako.

24 Ndani yake ilionekana damu ya manabii na ya watakatifu

na wote waliouawa duniani.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/18-5c6f9d4423132dd19237fa2f94162b51.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 19

Shangwe Huko Mbinguni

1 Baada ya haya nikasikia sauti kama ya umati mkubwa mbinguni wakipiga kelele wakisema:

“Haleluya!

Wokovu na utukufu na uweza ni vya Mungu wetu,

2 kwa maana hukumu zake

ni za kweli na za haki.

Amemhukumu yule kahaba mkuu

aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake.

Mungu amemlipiza kisasi

kwa ajili ya damu ya watumishi wake.”

3 Wakasema tena kwa nguvu:

“Haleluya!

Moshi wake huyo kahaba unapanda juu

milele na milele.”

4 Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wenye uhai wanne wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu:

“Amen, Haleluya!”

5 Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema:

“Msifuni Mungu wetu,

ninyi watumishi wake wote,

ninyi nyote mnaomcha,

wadogo kwa wakubwa!”

6 Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipiga kelele wakisema:

“Haleluya!

Kwa maana BWANA Mungu wetu Mwenyezi anatawala.

7 Tufurahi, tushangilie

na kumpa utukufu!

Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia

na bibi arusi wake amejiweka tayari.

8 Akapewa kitani safi, nyeupe

inayong’aa, ili avae.”

(Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.)

9 Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’ ” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.”

10 Ndipo nikaanguka kifudifudi miguuni pake ili kumwabudu, lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi pia ni mtumishi mwenzako pamoja na ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.”

Aliyepanda Farasi Mweupe

11 Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda huyo farasi aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita.

12 Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa chake kuna taji nyingi. Alikuwa na jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu ye yote anayelijua isipokuwa yeye mwenyewe.

13 Alikuwa amevaa joho lililochovywa kwenye damu na Jina lake ni “Neno la Mungu.”

14 Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani nzuri, nyeupe safi.

15 Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Atalikanyaga shinikizo la mvinyo wa ghadhabu ya Mungu Mwenyezi.

16 Kwenye joho lake na paja lake liliandikwa jina hili:

MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA.

Mnyama Na Majeshi Yake Yashindwa

17 Nami nikamwona malaika amesimama ndani kwenye jua, akaita ndege wote warukao angani kwa sauti kuu, “Njoni, kusanyikeni kwa ajili ya karamu kubwa ya Mungu,

18 ili mpate kula nyama ya wafalme na ya majemadari, ya mashujaa, ya farasi na ya wapanda farasi, nyama ya wanadamu, wote walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”

19 Kisha nikamwona yule mnyama na wafalme wa dunia pamoja na majeshi yao wakiwa wamekusanyika pamoja ili kufanya vita dhidi ya yule aliyempanda huyo farasi mweupe pamoja na jeshi lake.

20 Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo ambaye alikuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti.

21 Wale waliosalia waliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule aliyekuwa amempanda huyo farasi mweupe, nao ndege wote wakajishibisha kwa nyama yao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/19-f5a2e21f2e70e7332e5a0e96f03d9a05.mp3?version_id=1627—

Ufunuo 20

Utawala Wa Miaka Elfu Moja

1 Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, akiwa ameshika ufunguo wa lile Shimo lisilo na mwisho na mnyororo mkubwa mkononi mwake.

2 Akalishika lile joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ndiye ibilisi na Shetani, naye akamfunga kwa muda wa miaka 1,000.

3 Akamtupa katika lile Shimo lisilo na mwisho, akamfunga humo na kulitia lakiri, ili kumzuia asiendelee kudanganya mataifa mpaka hiyo miaka 1,000 itimie. Baada ya hayo lazima afunguliwe kwa muda mfupi.

4 Kisha nikaona viti vya enzi vilivyokuwa vimekaliwa na hao waliopewa mamlaka ya kuhukumu. Nami nikaona roho za wale waliokatwa vichwa kwa sababu ya ushuhuda wa Yesu na kwa sababu ya neno la Mungu. Hawakuwa wamemsujudia huyo mnyama wala sanamu yake wala hawakupokea ile chapa yake kwenye vipaji vya nyuso zao au kwenye mikono yao. Wakawa hai na kutawala pamoja na Kristo miaka 1,000.

5 (Wafu waliosalia hawakufufuka mpaka ilipotimia hiyo miaka 1,000.) Huu ndio ufufuo wa kwanza.

6 Waliobarikiwa na walio watakatifu ni wale walio na sehemu katika ufufuo wa kwanza. Hao mauti ya pili haina nguvu juu yao, bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye kwa muda wa miaka 1,000.

Kuhukumiwa Kwa Shetani

7 Hiyo miaka 1,000 itakapotimia, Shetani atafunguliwa kutoka kifungoni mwake,

8 naye atatoka ili kuyadanganya mataifa yaliyopo katika pembe nne za dunia, yaani, Gogu na Magogu apate kuwakusanya tayari kwa vita. Idadi yao ni kama mchanga ulioko Pwani.

9 Nao walitembea katika eneo lote la dunia, wakaizunguka kambi ya watakatifu na ule mji unaopendwa. Lakini moto ukashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza.

10 Naye ibilisi aliyewadanganya akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti walikokuwa wametupwa yule mnyama na yule nabii wa uongo. Watateswa humo mchana na usiku, milele na milele.

Wafu Wanahukumiwa

11 Kisha nikaona kiti kikubwa cheupe cha enzi pamoja na yeye aliyeketi juu yake. Dunia na mbingu zikaukimbia uso wake wala mahali pao hapakuonekana.

12 Nami nikawaona wafu wakubwa na wadogo, wakiwa wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi na vitabu vikafunguliwa. Pia kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni cha uzima. Hao wafu wakahukumiwa sawasawa na matendo yao kama yalivyoandikwa ndani ya hivyo vitabu.

13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake, nayo mauti na kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Kila mtu akahukumiwa kulingana na yale aliyotenda.

14 Kisha Mauti na Kuzimu zikatupwa katika ziwa la moto. Hii ndio Mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.

15 Iwapo mtu jina lake halikuonekana katika kile kitabu cha uzima, alitupwa ndani ya lile ziwa la moto.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/REV/20-a2dbaa73e8e7aa1a332b56554acf7b9f.mp3?version_id=1627—