2 Petro 1

1 Simoni Petro mtumishi na mtume wa Yesu Kristo:

Kwa wale ambao kwa njia ya haki ya Mungu na Mwokozi wetu Yesu Kristo mmepokea imani iliyo na thamani kama yetu:

2 Neema na amani iwe kwenu kwa wingi katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.

Wito Wa Mkristo Na Uteule

3 Uweza wake wa uungu umetupatia mambo yote tunayohitaji kwa ajili ya uzima na uchaji wa Mungu, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.

4 Kwa sababu hiyo, ametukirimia ahadi zake kuu na za thamani kupitia mambo haya, ili kwa kupitia hayo mpate kuwa washiriki wa asili ya Kiungu na kuokoka kutoka katika upotovu ulioko duniani kwa sababu ya tamaa mbaya.

5 Kwa sababu hii hasa, jitahidini sana katika imani yenu kuongeza wema na katika wema wenu maarifa,

6 katika maarifa yenu kiasi, katika kiasi, saburi, katika saburi yenu, utauwa,

7 katika utauwa wenu upendano wa kidugu, katika upendano wa kidugu, upendo.

8 Kwa maana haya yakiwa ndani yenu kwa wingi na kuzidi kuongezeka yanawafanya kuwa wenye bidii na wenye kuzaa matunda katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.

9 Lakini mtu ye yote asipokuwa na mambo haya haoni mbali, pia ni kipofu, naye amesahau kule kutakaswa kwa dhambi zake za zamani.

10 Kwa hiyo, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuuthibitisha wito wenu na uteule wenu, kwa maana mkifanya hivyo, hamtajikwaa kamwe.

11 Kwa njia hii, mtajaliwa kwa ukarimu mwingi kuingia katika ufalme wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Unabii Wa Maandiko

12 Hivyo nitawakumbusha mambo haya siku zote, hata ingawa mnayajua na yamethibitishwa katika kweli mliyo nayo.

13 Naona ni vyema kuwaamsha kwa kuwakumbusha mambo haya wakati wote niwapo katika hema hili ambalo ni mwili wangu.

14 Kwa sababu najua ya kwamba hivi karibuni nitaliweka kando, kama vile Bwana wetu Yesu Kristo alivyoliweka wazi kwangu.

15 Nami nitafanya kila juhudi kuona kwamba baada ya kuondoka kwangu mtaweza kuyakumbuka mambo haya siku zote.

16 Tulipowafahamisha juu ya uweza na kuja kwa Bwana wetu Yesu Kristo, hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, bali tulishuhudia kwa macho yetu ukuu wake.

17 Maana alipewa heshima na utukufu kutoka kwa Mungu Baba, sauti ilipomjia katika Utukufu Mkuu ikisema, “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye.”

18 Sisi wenyewe tuliisikia sauti hii ambayo ilitoka mbinguni, wakati tulipokuwa pamoja naye kwenye ule mlima mtakatifu.

19 Nasi tunalo pia neno la hakika zaidi la unabii, ambalo mtafanya vyema mkiliangalia kwa bidii, kama vile nuru inayong’aa gizani, hadi kupambazuka na nyota ya asubuhi itokee mioyoni mwenu.

20 Awali ya yote, yawapasa mjue kwamba hakuna unabii katika Maandiko uliofasiriwa kama alivyopenda nabii mwenyewe.

21 Kwa maana unabii haukuja kamwe kwa mapenzi ya mwanadamu, bali watu walinena yaliyotoka kwa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2PE/1-5cd93fe399ba4d62e244968fd0db0e50.mp3?version_id=1627—

2 Petro 2

Walimu Wa Uongo Na Uangamivu Wao

1 Lakini pia waliinuka manabii wa uongo miongoni mwa watu, kama vile watakavyokuwako walimu wa uongo miongoni mwenu, ambao kwa siri, wataingiza mafundisho yasiyopatana na kweli hata kumkana Bwana wa pekee aliyewanunua na kujiletea juu yao maangamizi ya haraka.

2 Hata hivyo, wengi watafuata njia zao za ufisadi ambao kwa ajili yao njia ya kweli itatukanwa.

3 Nao katika tamaa zao mbaya, watajipatia faida kwenu kwa maneno ya madanganyo waliyotunga wenyewe. Lakini hukumu imekwisha kutangazwa dhidi yao tangu zamani, ambayo haikawii wala uangamivu wao haujalala usingizi.

4 Kwa maana kama Mungu hakuwasamehe malaika walipotenda dhambi, bali aliwatupa kuzimu, katika vifungo vya giza wakae humo mpaka ije hukumu;

5 kama hakuusamehe ulimwengu wa kale alipoleta gharika juu ya watu wale wasiomcha Mungu, akamhifadhi Noa, mhubiri wa haki, pamoja na watu wengine saba;

6 kama aliihukumu miji ya Sodoma na Gomora kwa kuiteketeza kwa moto ikawa majivu na kuifanya kuwa kielelezo kwa yale yatakayowapata wale wasiomcha Mungu

7 na kama alimwokoa Loti, mtu mwenye haki, ambaye alihuzunishwa na maisha machafu ya watu wapotovu

8 (kwa sababu yale matendo mapotovu aliyoyaona na kuyasikia huyo mtu mwenye haki alipoishi miongoni mwao yalimhuzunisha siku baada ya siku),

9 ikiwa hivyo ndivyo, basi Bwana anajua jinsi ya kuwaokoa wacha Mungu kutoka katika majaribu na kuwaweka waasi katika adhabu hadi siku ya hukumu.

10 Hii ni hakika hasa kwa wale wanaofuata tamaa mbaya za mwili na kudharau mamlaka.

Kwa ushupavu na kwa kiburi watu hawa hawaogopi kunena mabaya dhidi ya viumbe vya mbinguni,

11 lakini hata malaika, ingawa wana nguvu na uwezo zaidi, hawaleti mashtaka dhidi ya viumbe kama hao mbele za Bwana.

12 Lakini watu hawa hukufuru katika mambo wasiyoyafahamu. Wao ni kama wanyama wasio na akili, viumbe wanaotawaliwa na hisia za mwili, waliozaliwa ili wakamatwe na kuchinjwa. Hawa nao kama wanyama wataangamizwa pia.

13 Watalipwa madhara kwa ajili ya madhara waliyowatendea wengine. Huhesabu kuwa ni fahari kufanya karamu za ulevi na ulafi mchana peupe. Wao ni mawaa na dosari, wakijifurahisha katika anasa zao wanaposhiriki katika karamu zenu.

14 Wakiwa na macho yaliyojaa uzinzi, kamwe hawaachi kutenda dhambi. Huwashawishi wale wasio imara, wao ni hodari kwa kutamani, wana wa laana!

15 Wameiacha njia iliyonyoka, wakapotoka na kuifuata njia ya Balaamu mwana wa Beori aliyependa mshahara wa uovu.

16 Lakini Balaamu kwa ajili ya uovu wake, alikemewa na punda, mnyama asiyejua kusema, akaongea akitumia sauti ya mwanadamu na kuzuia wazimu wa huyo nabii.

17 Watu hawa ni chemchemi zisizo na maji na ukungu upeperushwao na tufani, ambao giza nene limewekwa tayari kwa ajili yao.

18 Kwa maana wao hunena maneno makuu mno ya upumbavu na kwa tamaa mbaya za uasherati huwashawishi watu ambao ndipo tu wamejiondoa miongoni mwa wale wanaoishi katika ufisadi.

19 Huwaahidi uhuru hao waliowanasa, wakati wao wenyewe ni watumwa wa ufisadi. Kwa maana mtu ni mtumwa wa kitu cho chote kinachomtawala.

20 Kwa kuwa kama wameukimbia upotovu wa dunia kwa kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo, kisha wakanaswa tena humo na kushindwa, hali yao ya mwisho ni mbaya zaidi kuliko ile ya kwanza.

21 Ingelikuwa afadhali kwao kama wasingeliijua kamwe njia ya haki, kuliko kuijua kisha wakaiacha ile amri takatifu waliyokabidhiwa.

22 Imetukia kwao sawasawa na ile mithali ya kweli isemayo: “Mbwa ameyarudia matapishi yake mwenyewe,” tena nyingine yasema, “Nguruwe aliyeoshwa amerudi kugaagaa matopeni.”

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2PE/2-65ea23a992cbf57b7e114cf8cb1ea166.mp3?version_id=1627—

2 Petro 3

Ahadi Ya Kuja Kwa Bwana

1 Wapenzi, huu ndio waraka wangu wa pili ninaowaandikia. Katika nyaraka hizi mbili ninajaribu kuziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha kwamba,

2 nataka ninyi mkumbuke maneno yaliyosemwa zamani na manabii watakatifu na ile amri ya Bwana na Mwokozi mliyopewa kupitia kwa mitume wenu.

3 Kwanza kabisa, ni lazima mfahamu ya kwamba siku za mwisho watakuja watu wenye dhihaka wakidhihaki na kuzifuata tamaa zao mbaya,

4 wakisema, “Iko wapi ile ahadi ya kuja kwake? Tangu baba zetu walipokufa, kila kitu kinaendelea kama kilivyokuwa tangu mwanzo wa kuumbwa.”

5 Wao kwa makusudi hupuuza ukweli huu, ya kwamba kwa neno la Mungu mbingu zilikuwepo tangu zamani nayo dunia ilifanyizwa kutoka ndani ya maji na kwa hayo maji,

6 ulimwengu wa wakati ule uligharikishwa na kuangamia.

7 Lakini kwa neno lilo hilo mbingu za sasa na dunia, zimewekwa akiba kwa ajili ya moto, zikihifadhiwa hadi siku ile ya hukumu na ya kuangamizwa kwa watu wasiomcha Mungu.

8 Lakini wapenzi, msisahau neno hili, kwamba kwa Bwana, siku moja ni kama miaka elfu na miaka elfu ni kama siku moja.

9 Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake kama watu wengine wanavyodhani kukawia. Yeye anawavumilia, maana hataki mtu ye yote aangamie, bali kila mmoja afikilie toba.

10 Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi. Ndipo mbingu zitatoweka kwa kishindo kikuu na vitu vya asili vitateketezwa kwa moto, nayo dunia na kila kitu kilichomo ndani yake kitaunguzwa.

11 Kwa kuwa vitu vyote vitaharibiwa namna hii, ninyi je, imewapasa kuwa watu wa namna gani? Inawapasa kuishi maisha matakatifu na ya kumcha Mungu,

12 mkingojea na kuhimiza kuja kwa hiyo siku ya Mungu, ambayo siku hiyo mbingu zitachomwa moto na kutoweka na vitu vya asili vitayeyuka kwa moto.

13 Lakini kufuatana na ahadi yake, sisi tunatazamia kwa furaha mbingu mpya na dunia mpya, ambayo haki hukaa ndani yake.

14 Kwa sababu hii, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia kwa furaha mambo haya, fanyeni bidii ili awakute katika amani, bila mawaa wala dosari.

15 Nanyi hesabuni uvumilivu wa Bwana kuwa ni wokovu, kama vile ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima ile aliyopewa na Mungu.

16 Huandika vivyo hivyo katika nyaraka zake zote akizungumzia ndani yake mambo haya. Katika nyaraka zake kuna mambo mengine ambayo ni vigumu kuyaelewa, ambayo watu wajinga na wasio thabiti huyapotosha kwa maangamizi yao wenyewe, kama wapotoshavyo pia Maandiko mengine.

17 Basi, ninyi wapenzi, kwa kuwa mmekwisha kujua mambo haya, jilindeni msije mkachukuliwa na kosa la watu hao waasi na kuanguka kutoka kwenye uthabiti wenu.

18 Bali kueni katika neema na katika kumjua Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na milele! Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/2PE/3-53020c30f3ed70ee9ca17ac1560b72c3.mp3?version_id=1627—

1 Petro 1

Salamu

1 Petro, mtume wa Yesu Kristo:

Kwa wateule wa Mungu, wageni katika ulimwengu, waliotawanyika kote katika Ponto, Galatia, Kapadokia, Asia na Bithinia.

2 Ninawaandikia ninyi ambao mlichaguliwa tangu mwanzo na Mungu Baba kulingana na alivyotangulia kuwajua, kwa kazi ya utakaso wa Roho, katika utii na kunyunyizwa damu ya Yesu Kristo:

Neema iwe nanyi na amani iongezwe kwenu.

Tumaini Lenye Uzima

3 Ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo! Kwa rehema zake kuu ametuzaa sisi mara ya pili katika tumaini lenye uzima kwa kufufuka kwa Yesu Kristo kutoka kwa wafu,

4 ili tuupate urithi usioharibika, usio na uchafu, ule usionyauka, uliotunzwa mbinguni kwa ajili yenu,

5 ninyi ambao mnalindwa na nguvu za Mungu kwa njia ya imani hadi uje ule wokovu ulio tayari kufunuliwa nyakati za mwisho.

6 Katika hili mnafurahi sana, ingawa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna nyingi.

7 Haya yamewajia ili kwamba uhalisi wa imani yenu (yenye thamani kuliko dhahabu ipoteayo, ingawa hujaribiwa kwa moto) ionekane kuwa katika sifa, utukufu na heshima wakati Yesu Kristo atakapodhihirishwa.

8 Ambaye, ingawa hamjamwona, mnampenda, tena ingawa sasa hamumwoni, mnamwamini na kujawa na furaha isiyoneneka yenye utukufu usioelezeka.

9 Maana mnaupokea wokovu wa roho zenu, ambao ndio lengo la imani yenu.

10 Kwa habari ya wokovu huu, wale manabii waliosema kuhusu neema ambayo ingewajia ninyi, walitafuta kwa bidii na kwa uangalifu mkubwa,

11 wakijaribu kujua ni wakati upi na katika mazingira gani ambayo Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao alionyesha alipotabiri kuhusu mateso ya Kristo na utukufu ule ambao ungefuata.

12 Mitume walidhihirishiwa kwamba walikuwa hawajihudumii wao wenyewe, bali walihudumu kwa ajili yenu katika mambo hayo ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo ambayo hata malaika wanatamani kuyafahamu.

Mwito Wa Kuishi Maisha Matakatifu

13 Kwa hiyo, vifungeni viuno vya nia zenu, mwe na kiasi, mkitumainia kikamilifu ile neema mtakayopewa, Yesu Kristo atakapodhihirishwa.

14 Kama watoto watiifu, msifuate tamaa zenu mbaya za kwanza za wakati wa ujinga.

15 Bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote,

16 kwa maana imeandikwa: “Mtakuwa watakatifu, kwa kuwa Mimi ni mtakatifu.”

17 Nanyi kama mnamwita Baba yeye ahukumuye kila mtu kulingana na matendo yake pasipo upendeleo, enendeni kwa hofu ya kumcha Mungu wakati wenu wa kukaa hapa duniani kama wageni.

18 Kwa maana mnafahamu kwamba mlikombolewa kutoka katika mwenendo wenu usiofaa ambao mliurithi kutoka kwa baba zenu, si kwa vitu viharibikavyo, yaani, kwa fedha na dhahabu,

19 bali kwa damu ya thamani ya Kristo, kama ile ya Mwana-Kondoo asiye na dosari wala doa.

20 Yeye aliwekewa hayo kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu, lakini akadhihirishwa katika siku hizi za mwisho kwa ajili yenu,

21 ambaye kwa yeye mmemwamini Mungu aliyemfufua kutoka kwa wafu akampa utukufu, ili imani yenu na tumaini lenu liwe kwa Mungu.

22 Basi kwa kuwa mmejitakasa nafsi zenu kwa kuitii ile kweli kwa njia ya Roho kwa kuwapenda ndugu zenu kwa upendo wa kweli, pendaneni kwa dhati kutoka moyoni.

23 Kwa maana mmezaliwa upya, si kwa mbegu ile iharibikayo, bali kwa ile isiyoharibika, kwa neno la Mungu lililo hai na linalodumu hata milele.

24 Maana,

“Watu wote ni kama majani,

na utukufu wao ni kama ua la shambani;

majani hunyauka na ua lake hupukutika,

25 lakini neno la Mungu ladumu milele.”

Hili ndilo neno lililohubiriwa kwenu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1PE/1-bb41903f01d07fc3c47798d12aa10f20.mp3?version_id=1627—

1 Petro 2

Jiwe Lililo Hai Na Watu Waliochaguliwa

1 Kwa hiyo, wekeni mbali nanyi uovu wote na udanganyifu wote, unafiki, wivu na masingizio ya kila namna.

2 Kama watoto wachanga, waliozaliwa sasa, yatamanini maziwa ya kiroho yasiyochanganywa na kitu kingine cho chote, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu,

3 ikiwa kweli mmeonja ya kwamba Bwana ni mwema.

4 Mwendeeni yeye aliye Jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu bali kwa Mungu ni teule na la thamani kwake.

5 Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa kuwa nyumba ya Roho, mpate kuwa ukuhani mtakatifu, mkitoa dhabihu za kiroho zinazokubaliwa na Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.

6 Kwa maana Andiko lasema:

“Tazama, naweka katika Sayuni,

Jiwe Kuu la pembeni,

teule lenye thamani,

na kila amwaminiye

hataaibika.”

7 Kwenu ninyi mnaoamini, yeye ni wa thamani. Lakini kwao wasioamini,

“Jiwe lile walilolikataa waashi

limekuwa Jiwe Kuu la pembeni,”

8 tena,

“Jiwe lenye kuwafanya watu wajikwae,

mwamba wa kuwafanya waanguke.”

Wanajikwaa kwa sababu hawakulitii lile neno: kama walivyowekewa tangu zamani.

9 Lakini ninyi ni taifa teule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu la Mungu, mlioitwa ili kutangaza sifa zake yeye aliyewaita kutoka gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu.

10 Mwanzo ninyi mlikuwa si taifa, lakini sasa ninyi ni taifa la Mungu. Mwanzo mlikuwa hamkupata rehema, lakini sasa mmepata rehema.

11 Wapenzi, ninawasihi, mkiwa kama wageni na wapitaji hapa ulimwenguni, epukeni tamaa mbaya za mwili ambazo hupigana vita na roho zenu.

12 Mwe na mwenendo mzuri mbele ya watu wasiomjua Mungu, ili kama wanawasema kuwa ninyi ni watenda mabaya, wayaone matendo yenu mema wamtukuze Mungu siku atakapokuja kuhukumu.

Kuwatii Wenye Mamlaka

13 Tiini kila mamlaka iliyowekwa na wanadamu kwa ajili ya Bwana: Mfalme akiwa ndiye aliye na mamlaka ya juu zaidi,

14 pamoja na maafisa aliowaweka. Kwa kuwa mfalme amewatuma ili kuwaadhibu wale wanaokosa na kuwasifu wale watendao mema.

15 Kwa maana ni mapenzi ya Mungu kwamba kwa kutenda mema mnyamazishe maneno ya kijinga ya watu wapumbavu.

16 Ishini kama watu huru, lakini msitumie uhuru wenu kama kisingizio cha kutenda uovu, bali ishini kama watumishi wa Mungu.

17 Mheshimuni kila mtu. Wapendeni jamaa ya waaminio. Mcheni Mungu. Mpeni heshima mfalme.

18 Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu kwa heshima yote, si wale mabwana walio wema na wapole peke yao, bali pia wale walio wakali.

19 Kwa maana ni jambo la sifa kama mtu akivumilia anapoteswa kwa uonevu kwa ajili ya kumkumbuka Mungu.

20 Kwani ni faida gani kwa mtu kustahimili anapopigwa kwa sababu ya makosa yake? Lakini kama mkiteswa kwa sababu ya kutenda mema, nanyi mkastahimili, hili ni jambo la sifa mbele za Mungu.

Mfano Wa Mateso Ya Kristo

21 Kwa kuwa ninyi mliitwa kwa ajili ya hayo, kwa sababu Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akiwaachia kielelezo, ili mzifuate nyayo zake.

22 “Yeye hakutenda dhambi,

wala udanganyifu haukuonekana

kinywani mwake.”

23 Yeye alipotukanwa, hakurudisha matukano, alipoteswa, hakutishia, bali alijikabidhi kwa yeye ahukumuye kwa haki.

24 Yeye mwenyewe alizichukua dhambi zetu katika mwili wake juu ya mti, ili kwamba tukiwa wafu kwa mambo ya dhambi, tupate kuishi katika haki. Kwa kupigwa kwake, ninyi mmeponywa.

25 Kwa maana mlikuwa mmepotea kama kondoo, lakini sasa mmerudi kwa Mchungaji na Mwangalizi wa roho zenu.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1PE/2-0f9e508820f9c225944c1ee1ac1486ef.mp3?version_id=1627—

1 Petro 3

Mafundisho Kwa Wake Na Waume

1 Kadhalika enyi wake, watiini waume zenu, ili kama wako wasioamini lile neno, wapate kuvutwa na mwenendo wa wake zao pasipo neno,

2 kwa kuuona utakatifu na uchaji wa Mungu katika maisha yenu.

3 Kujipamba kwenu kusiwe kwa nje tu, kama vile kusuka nywele, kuvalia vitu vilivyofanyizwa kwa dhahabu na kwa mavazi.

4 Badala yake kujipamba kwenu kuwe katika utu wenu wa ndani, kwa uzuri usioharibika, wa roho ya upole na utulivu, ambako ni kwa thamani sana machoni pa Mungu.

5 Kwa kuwa hivi ndivyo walivyokuwa wakijipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu. Wao walikuwa ni watiifu kwa waume zao,

6 kama Sara alivyomtii mumewe Abrahamu, akamwita bwana. Ninyi ni watoto wa Sara kama mkitenda yaliyo mema na bila kuogopa jambo lo lote.

7 Vivyo hivyo ninyi waume, kaeni na wake zenu kwa akili, nanyi wapeni heshima mkitambua ya kuwa wao ni wenzi walio dhaifu na kama warithi pamoja nanyi wa kipawa cha thamani cha uzima, ili kusiwepo na cho chote cha kuzuia maombi yenu.

Kuteseka Kwa Kutenda Mema

8 Hatimaye, ninyi nyote iweni na nia moja, wenye kuhurumiana, mkipendana kama ndugu, wasikitivu na wanyenyekevu.

9 Msilipe ovu kwa ovu, au jeuri kwa jeuri, bali barikini, kwa maana hili ndilo mliloitiwa ili mpate kurithi baraka.

10 Kwa maana,

“Ye yote apendaye uzima

na kuona siku njema,

basi auzuie ulimi wake usinene mabaya

na midomo yake isiseme hila.

11 Mtu huyo lazima aache ubaya, akatende mema;

atafute amani na kuifuatilia sana.

12 Kwa maana macho ya Bwana

huwaelekea wenye haki,

na masikio yake

husikiliza maombi yao,

bali uso wa Bwana ni dhidi yao

watendao maovu.”

Kuvumilia Mateso

13 Basi, ni nani atakayewadhuru mkiwa wenye bidii katika kutenda mema?

14 Lakini mmebarikiwa hata kama ikiwalazimu kuteseka kwa ajili ya haki. “Msiogope vitisho vyao wala msiwe na wasiwasi.”

15 Bali mtakaseni Kristo kuwa Bwana mioyoni mwenu. Siku zote mwe tayari kumjibu mtu ye yote atakayewauliza kuhusu tumaini lililomo ndani yenu. Lakini fanyeni hivyo kwa upole na kwa heshima,

16 mkizitunza dhamiri zenu ziwe safi, ili wale wasemao mabaya dhidi ya mwenendo wenu mzuri katika Kristo, waaibike kwa ajili ya masingizio yao.

17 Kwa maana ni afadhali kupata mateso kwa ajili ya kutenda mema kama kuteseka huko ndiyo mapenzi ya Mungu, kuliko kuteseka kwa kutenda maovu.

18 Kwa kuwa Kristo naye aliteswa mara moja tu, mwenye haki kwa ajili ya wasio na haki, ili awalete ninyi kwa Mungu. Mwili wake ukauawa, lakini akafanywa hai katika Roho,

19 ambayo kwa hiyo alikwenda na kuzihubiria roho zilizokuwa kifungoni.

20 Roho hizo ambazo zamani hazikutii, wakati ule uvumilivu wa Mungu ulipokuwa ukingoja katika siku za Noa, wakati wa kujenga safina, ambako watu wachache tu, yaani, watu wanane waliokolewa wasiangamie kwa gharika.

21 Nayo maji hayo ni kielelezo cha ubatizo ambao sasa unawaokoa ninyi pia, si kwa kuondoa uchafu kwenye mwili, bali kama ahadi ya dhamiri safi kwa Mungu, kwa njia ya ufufuo wa Yesu Kristo,

22 ambaye ameingia mbinguni na amekaa mkono wa kuume wa Mungu: pamoja na malaika, mamlaka na nguvu zote vikiwa vimetiishwa chini yake.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1PE/3-98b8757cacb1561b46c7e02a2255272a.mp3?version_id=1627—

1 Petro 4

Kuishi Kwa Ajili Ya Mungu

1 Kwa hiyo, kwa kuwa Kristo aliteswa katika mwili wake, ninyi nanyi jivikeni nia iyo hiyo kwa maana mtu aliyekwisha kuteswa katika mwili ameachana na dhambi.

2 Matokeo yake, maisha yake yaliyobaki ya kuishi hapa duniani, haishi tena kwa kufuata tamaa mbaya za wanadamu, bali anaishi kwa kufuata mapenzi ya Mungu.

3 Maana wakati uliopita mmekwisha kutumia muda wa kutosha katika maisha yenu mkifanya yale ambayo watu wasiomjua Mungu hupenda kutenda, wakiishi katika uasherati, tamaa mbaya, ulevi, karamu za ulafi, vileo, ngoma mbaya na ibada za sanamu ambazo ni chukizo.

4 Wao huona kuwa ni ajabu ninyi kutokujiingiza tena pamoja nao katika huo wingi wa ufisadi, nao huwatukana ninyi.

5 Lakini itawapasa wao kutoa hesabu mbele zake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.

6 Kwa kuwa hii ndiyo sababu Injili ilihubiriwa hata kwa wale waliokufa, ili kwamba wahukumiwe sawasawa na wanadamu wengine katika mwili, lakini katika roho waishi sawasawa na Mungu aishivyo.

Kuja Kwa Kristo Kumekaribia

7 Mwisho wa mambo yote umekaribia. Kwa hiyo iweni na akili pia mwe na kiasi mkikesha katika kuomba.

8 Zaidi ya yote, dumuni katika upendo kwa maana upendo husitiri wingi wa dhambi.

9 Iweni wakarimu kila mtu na mwenzake pasipo manung’uniko.

10 Kila mmoja na atumie kipawa cho chote alichopewa kuwahudumia wengine, kama mawakili waaminifu wa neema mbalimbali za Mungu.

11 Ye yote asemaye hana budi kusema kama mtu asemaye maneno ya Mungu mwenyewe. Ye yote ahudumuye hana budi kuhudumu kwa nguvu zile apewazo na Mungu, ili Mungu apate kutukuzwa katika mambo yote kwa njia ya Yesu Kristo. Utukufu na uweza una yeye milele na milele. Amen.

Kuteseka Kwa Kuwa Mkristo

12 Wapenzi, msione ajabu katika yale mateso yanayotukia miongoni mwenu, kana kwamba ni kitu kigeni kinachowapata.

13 Bali furahini kuwa mnashiriki katika mateso ya Kristo, ili kwamba mpate kufurahi zaidi na kushangilia wakati utukufu wake utakapofunuliwa.

14 Kama mkilaumiwa kwa ajili ya Jina la Kristo, mmebarikiwa, kwa sababu Roho wa utukufu, yaani Roho wa Mungu, anakaa juu yenu.

15 Lakini asiwepo mtu ye yote miongoni mwenu anayeteswa kwa kuwa ni mwuaji, au mwivi, au mhalifu au anayejishughulisha na mambo ya watu wengine, ili kuwagombanisha.

16 Lakini kama mtu ye yote akiteseka kwa kuwa ni mkristo, asihesabu jambo hilo kuwa ni aibu, bali amtukuze Mungu kwa sababu ameitwa kwa jina hilo.

17 Kwa maana wakati umewadia wa hukumu kuanza katika nyumba ya Mungu. Basi kama ikianza kwetu sisi, mwisho wa hao wasiotii Injili ya Mungu utakuwaje?

18 Basi,

“Ikiwa ni vigumu kwa mwenye haki kuokoka,

itakuwaje kwa mtu asiyemcha Mungu

na mwenye dhambi?”

19 Kwa hiyo, wale wanaoteswa sawasawa na mapenzi ya Mungu, wajikabidhi kwa Muumba wao aliye mwaminifu, huku wakizidi kutenda mema.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1PE/4-6dbdf3f4e67313aa4b8225862d5bb17b.mp3?version_id=1627—

1 Petro 5

Kulichunga Kundi La Mungu

1 Kwa wazee waliomo miongoni mwenu, nawasihi mimi nikiwa mzee mwenzenu, shahidi wa mateso ya Kristo na mshiriki katika utukufu utakaofunuliwa,

2 lichungeni kundi la Mungu mlilokabidhiwa, mkitumika kama waangalizi, si kwa kulazimishwa bali kwa hiari, kama Mungu anavyowataka mwe, si kwa tamaa ya fedha, bali mlio na bidii katika kutumika.

3 Msijifanye mabwana juu ya wale walio chini ya uangalizi wenu, bali iweni vielelezo kwa hilo kundi.

4 Naye Mchungaji Mkuu atakapodhihirishwa mtapokea taji ya utukufu isiyoharibika.

5 Vivyo hivyo ninyi mlio vijana hamna budi kuwatii wazee. Nanyi nyote imewapasa kujivika unyenyekevu katika kuhudumiana, kila mtu na mwenzake, kwa kuwa,

“Mungu huwapinga wenye kiburi

bali huwapa wanyenyekevu neema.”

6 Basi, nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, ili awakweze kwa wakati wake.

7 Mtwikeni yeye fadhaa zenu zote kwa maana hujishughulisha sana na mambo yenu.

8 Mwe na kiasi na kukesha, maana adui yenu ibilisi, kama simba angurumaye huzungukazunguka akitafuta mtu ili apate kummeza.

9 Mpingeni huyo mkiwa thabiti katika imani, mkijua ya kwamba mateso yayo hayo yanawapata ndugu zenu pote duniani.

10 Nanyi mkiisha kuteswa kwa kitambo kidogo, Mungu wa neema yote aliyewaita kuingia katika utukufu wake wa milele ndani ya Kristo, yeye mwenyewe atawatengeneza upya, atawasaidia, atawatia nguvu na kuwathibitisha.

11 Uweza una yeye milele na milele. Amen.

Salamu Za Mwisho

12 Kwa msaada wa Silvano, yeye ambaye ninamhesabu kuwa ndugu mwaminifu, nimewaandikia waraka huu mfupi ili kuwatia moyo na kushuhudia kwamba hii ni neema halisi ya Mungu. Simameni imara katika neema hiyo.

13 Kanisa lililoko Babeli, lililochaguliwa pamoja nanyi, wanawasalimu; vivyo hivyo mwanangu Marko anawasalimu.

14 Salimianeni kwa busu la upendo.

Amani iwe nanyi nyote mlio katika Kristo. Amen.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/1PE/5-b774f816aa939fce279531236a4db09f.mp3?version_id=1627—

Yakobo 1

1 Yakobo, mtumwa wa Mungu na wa Bwana Yesu Kristo:

Kwa makabila kumi na mawili yaliyotawanyika ulimwenguni:

Salamu.

Imani Na Hekima

2 Ndugu zangu, hesabuni kuwa ni furaha tupu mnapopatwa na majaribu mbalimbali,

3 kwa sababu mnajua ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi.

4 Saburi na iwe na kazi timilifu, ili mpate kuwa wakamilifu, mmekamilishwa, bila kupungukiwa na kitu cho chote.

5 Kama mtu ye yote miongoni mwenu amepungukiwa na hekima na amwombe Mungu, yeye awapaye watu wote kwa ukarimu wala hana kinyongo, naye atapewa.

6 Lakini anapoomba, lazima aamini wala asiwe na shaka, kwa sababu mtu aliye na shaka ni kama wimbi la bahari, lililochukuliwa na upepo na kutupwa huku na huku.

7 Mtu kama huyo asidhani ya kuwa atapata kitu cho chote kutoka kwa Bwana.

8 Yeye ni mtu mwenye nia mbili, mwenye kusitasita katika njia zake zote.

Umaskini Na Utajiri

9 Ndugu asiye na cheo kikubwa yampasa ajivunie hali hiyo maana ametukuzwa.

10 Lakini yeye aliye tajiri afurahi kwa kuwa ameshushwa, kwa sababu atatoweka kama ua la shambani.

11 Kwa maana jua kali lenye kuchoma huchomoza na kuliunguza, likayakausha majani na ua lake likapukutika nao uzuri wake huharibika. Vivyo hivyo tajiri naye atanyauka akiwa anaendelea na shughuli zake.

Kujaribiwa

12 Heri mtu anayevumilia wakati wa majaribu, kwa sababu akiisha kushinda hilo jaribio atapewa taji ya uzima Mungu aliyowaahidia wale wampendao.

13 Mtu anapojaribiwa asiseme, “Ninajaribiwa na Mungu.” Kwa maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu wala yeye hamjaribu mtu ye yote.

14 Lakini kila mtu hujaribiwa wakati anapovutwa na kudanganywa na tamaa zake mwenyewe zilizo mbaya.

15 Basi ile tamaa mbaya ikishachukua mimba, huzaa dhambi, ile dhambi ikikomaa, huzaa mauti.

16 Ndugu zangu, msidanganyike.

17 Kila kitolewacho kilicho chema na kilicho kamili, hutoka juu, hushuka kutoka kwa Baba wa mianga, ambaye kwake hakuna kubadilika, wala kivuli cha kugeukageuka.

18 Kwa mapenzi yake mwenyewe alituzaa kwa neno la kweli, kusudi tuwe kama mazao ya kwanza katika viumbe vyake vyote.

Kusikia Na Kutenda

19 Ndugu zangu wapendwa, fahamuni jambo hili: Kila mtu awe mwepesi wa kusikiliza, lakini asiwe mwepesi wa kusema wala wa kukasirika.

20 Kwa maana hasira ya mwanadamu haitendi haki ya Mungu.

21 Kwa hiyo, ondoleeni mbali uchafu wote na uovu ambao umezidi kuwa mwingi, mkalipokee kwa unyenyekevu lile Neno lililopandwa ndani yenu ambalo laweza kuokoa nafsi zenu.

22 Basi iweni watendaji wa Neno wala msiwe wasikiaji tu, huku mkijidanganya nafsi zenu.

23 Kwa maana kama mtu ni msikiaji tu wa Neno wala hatendi kile linachosema, yeye ni kama mtu ajitazamaye uso wake kwenye kioo

24 na baada ya kujiona alivyo, huenda zake na mara husahau jinsi alivyo.

25 Lakini yeye anayeangalia kwa bidii katika sheria kamilifu, ile iletayo uhuru, naye akaendelea kufanya hivyo bila kusahau alichosikia, bali akalitenda, atabarikiwa katika kile anachofanya.

26 Kama mtu akidhani ya kuwa anayo dini lakini hauzuii ulimi wake kwa hatamu, hujidanganya moyoni mwake, wala dini yake mtu huyo haifai kitu.

27 Dini iliyo safi, isiyo na uchafu, inayokubalika mbele za Mungu Baba yetu, ndiyo hii: Kuwasaidia yatima na wajane katika dhiki zao na kujilinda usitiwe madoa na dunia.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JAS/1-dc57ab125d6d7b342d8dc00dc2141cd6.mp3?version_id=1627—

Yakobo 2

Onyo Kuhusu Upendeleo

1 Ndugu zangu, kama waaminio katika imani ya Bwana wetu Yesu Kristo, Bwana wa utukufu, msiwe na upendeleo kwa watu.

2 Kwa maana kama akija mtu katika kusanyiko lenu akiwa amevaa pete ya dhahabu na mavazi mazuri, pia akaingia mtu maskini mwenye mavazi yaliyochakaa,

3 nanyi mkampa heshima yule aliyevaa mavazi mazuri na kumwambia, “Keti hapa mahali pazuri,” lakini yule maskini mkamwambia, “Wewe simama pale,” au “Keti hapa sakafuni karibu na miguu yangu,”

4 je, hamjawabagua na kuwa mahakimu mioyoni mwenu mkihukumu kwa mawazo yenu maovu?

5 Ndugu zangu, sikilizeni: Je, Mungu hakuwachagua wale walio maskini machoni pa ulimwengu kuwa matajiri katika imani na kuurithi Ufalme aliowaahidi wale wampendao?

6 Lakini ninyi mmemdharau yule aliye maskini. Je, hao matajiri si ndio wanaowadhulumu na kuwaburuta mahakamani?

7 Je, si wao wanaolikufuru Jina lile lililo bora sana mliloitiwa?

8 Kama kweli mnaitimiza ile sheria ya kifalme inayopatikana katika Maandiko isemayo, “Mpende jirani yako kama unavyoipenda nafsi yako,” mnafanya vyema.

9 Lakini kama mnakuwa na upendeleo kwa watu, mnatenda dhambi na sheria inawahukumu kuwa ninyi ni wakosaji.

10 Kwa maana mtu ye yote anayeishika sheria yote lakini akajikwaa katika kipengele kimoja tu, ana hatia ya kuivunja sheria yote.

11 Kwa sababu yeye aliyesema, “Usizini,” alisema pia, “Usiue.” Basi kama huzini lakini unaua, umekuwa mvunjaji wa sheria.

12 Hivyo semeni na kutenda kama watu watakaohukumiwa kwa sheria ile iletayo uhuru.

13 Kwa kuwa hukumu bila huruma itatolewa kwa mtu ye yote asiyekuwa na huruma. Huruma huishinda hukumu.

Imani Na Matendo

14 Ndugu zangu, yafaa nini ikiwa mtu atadai kuwa anayo imani lakini hana matendo? Je, imani kama hiyo yaweza kumwokoa?

15 Ikiwa ndugu yako au dada hana mavazi wala chakula,

16 mmoja wenu akamwambia, “Enenda zako kwa amani, ukaote moto na kushiba,” pasipo kumpatia yale mahitaji ya mwili aliyopungukiwa, yafaa nini?

17 Vivyo hivyo, imani peke yake kama haikuambatana na matendo, imekufa.

18 Lakini mtu mwingine atasema, “Wewe unayo imani; mimi ninayo matendo.”

Nionyeshe imani yako pasipo matendo nami nitakuonyesha imani yangu kwa matendo.

19 Unaamini kwamba kuna Mungu mmoja. Vyema! Hata mashetani yanaamini hivyo na kutetemeka.

20 Ewe mpumbavu! Je, wataka kujua kwamba imani bila matendo haifai kitu?

21 Je, Abrahamu baba yetu hakuhesabiwa haki kwa kile alichotenda, alipomtoa mwanawe Isaki madhabahuni?

22 Unaona jinsi ambavyo imani yake na matendo yake vilikuwa vinatenda kazi pamoja, nayo imani yake ikakamilishwa na kile alichotenda.

23 Kwa njia hiyo yakatimizwa yale Maandiko yasemayo, “Abrahamu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki,” naye akaitwa rafiki wa Mungu.

24 Mnaona ya kwamba mtu huhesabiwa haki kwa yale anayotenda wala si kwa imani peke yake.

25 Vivyo hivyo, hata Rahabu, yule kahaba, hakuhesabiwa haki kwa yale aliyotenda alipowapokea wale wapelelezi na kuwaambia waende njia nyingine?

26 Kama vile ambavyo mwili pasipo roho umekufa, kadhalika nayo imani pasipo matendo imekufa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JAS/2-ea3ccb7081e841fefdcd1a43ded228e5.mp3?version_id=1627—