Yakobo 3

Kuufuga Ulimi

1 Ndugu zangu, msiwe walimu wengi, kwa maana mnafahamu kwamba sisi tufundishao tutahukumiwa vikali zaidi.

2 Sisi sote tunajikwaa katika mambo mengi. Ikiwa mtu ye yote hakosei kamwe katika yale anayosema, yeye ni mkamilifu, naye anaweza kuuzuia pia na mwili wake wote.

3 Tunapotia lijamu kwenye vinywa vya farasi ni ili kuwafanya watutii, hivyo tunaweza kuigeuza miili yao yote.

4 Au angalia pia meli, ingawa ni kubwa sana, nazo huchukuliwa na upepo mkali, lakini hugeuzwa kwa usukani mdogo sana, ko kote anakotaka nahodha.

5 Vivyo hivyo ulimi ni kiungo kidogo sana katika mwili, lakini hujivuna majivuno makuu. Fikirini jinsi moto mdogo unavyoweza kuteketeza msitu mkubwa!

6 Ulimi pia ni moto, ndio ulimwengu wa uovu kati ya viungo vya mwili. Ulimi huutia mwili wote wa mtu unajisi na kuuwasha moto mfumo mzima wa maisha yake, nao wenyewe huchomwa moto wa jehanamu.

7 Kwa maana kila aina ya wanyama, ndege, wanyama watambaao na viumbe vya baharini vinafugika na vimefugwa na binadamu,

8 lakini hakuna mtu awezaye kuufuga ulimi. Ni uovu usiotulia, umejaa sumu iletayo mauti.

9 Kwa ulimi tunamhimidi Bwana, yaani, Baba yetu na kwa huo twawalaani watu walioumbwa kwa mfano wa Mungu.

10 Katika kinywa kile kile hutoka baraka na laana. Ndugu zangu, haistahili kuwa hivyo.

11 Je, chemchemi yaweza kutoa katika tundu moja maji matamu na maji ya chumvi?

12 Je, ndugu zangu, mtini waweza kuzaa zeituni, au mzabibu kuzaa tini? Wala chemchemi ya maji ya chumvi haiwezi kutoa maji matamu.

Aina Mbili Za Hekima

13 Ni nani aliye na hekima na ufahamu miongoni mwenu? Basi na aionyeshe hiyo kwa maisha yake mema na kwa matendo yake yaliyotendwa kwa unyenyekevu utokanao na hekima.

14 Lakini ikiwa mna wivu na ni wenye chuki na ugomvi mioyoni mwenu, msijisifu kwa ajili ya hayo wala msiikatae kweli.

15 Hekima ya namna hiyo haishuki kutoka mbinguni bali ni ya kidunia, tabia ya kibinadamu wala si ya kiroho bali ni ya kishetani.

16 Kwa maana panapokuwa na wivu na ubinafsi ndipo penye machafuko na uovu wa kila namna.

17 Lakini hekima itokayo mbinguni kwanza ni safi, kisha inapenda amani, ya upole, iliyo tayari kusikiliza maneno ya watu wengine, yenye unyenyekevu, iliyojaa huruma na matunda mema, isiyopendelea mtu, tena isiyokuwa na unafiki.

18 Mavuno ya haki hupandwa katika amani na wale wafanyao amani.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JAS/3-aef1b1ee18a004dbb86c8c0fdcd495cc.mp3?version_id=1627—

Yakobo 4

Jinyenyekezeni Kwa Mungu

1 Ni kitu gani kinachosababisha mapigano na ugomvi miongoni mwenu? Je, haya hayatokani na tamaa zenu zinazoshindana ndani yenu?

2 Mnatamani lakini hampati, kwa hiyo mwaua. Mwatamani kupata lakini hampati vile mnavyotaka, kwa hiyo mnajitia katika magomvi na mapigano. Mmepungukiwa kwa sababu hamumwombi Mungu.

3 Mnapoomba hampati kwa sababu mnaomba kwa nia mbaya, ili mpate kuvitumia hivyo mtakavyopata kwa tamaa zenu.

4 Ninyi wanaume na wanawake wazinzi, hamjui ya kwamba urafiki na dunia ni uadui na Mungu? Kwa hiyo mtu ye yote anayetaka kuwa rafiki wa dunia hufanyika adui wa Mungu.

5 Au mwadhani kwamba Andiko lasema bure kuwa, huyo Roho ambaye Mungu amemweka ndani yetu hututamani kiasi cha kuona wivu?

6 Lakini yeye hutupatia neema zaidi. Hii ndiyo sababu Andiko husema:

“Mungu huwapinga wenye kiburi,

lakini huwapa wanyenyekevu neema.”

7 Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia.

8 Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, ninyi wenye dhambi na kuisafisha mioyo yenu, ninyi wenye nia mbili.

9 Huzunikeni, ombolezeni na kulia. Kicheko chenu na kigeuzwe kuwa kuomboleza na furaha yenu kuwa huzuni.

10 Jinyenyekezeni mbele za Bwana, naye atawainua.

Onyo Kuhusu Kuhukumu Wengine

11 Ndugu, msineneane mabaya ninyi kwa ninyi. Mtu ye yote anayesema mabaya dhidi ya ndugu yake au kumhukumu anasema dhidi ya sheria na kuihukumu. Unapoihukumu sheria, basi huishiki sheria bali umekuwa hakimu wa kuihukumu hiyo sheria.

12 Yuko Mtoa-Sheria mmoja tu na yeye peke yake ndiye Hakimu, ndiye awezaye kuokoa au kuangamiza. Lakini wewe ni nani hata umhukumu jirani yako?

Kujivuna Kwa Ajili Ya Kesho

13 Basi sikilizeni ninyi msemao, “Leo au kesho tutakwenda katika mji huu ama ule tukae humo mwaka mmoja, tufanye biashara na kupata faida.”

14 Lakini hamjui hata litakalotukia kesho. Maisha yenu ni nini? Ninyi ni ukungu ambao huonekana kwa kitambo kidogo kisha hutoweka.

15 Badala yake, inawapasa kusema, “Kama Bwana akipenda, tutaishi na kufanya hili ama lile.”

16 Kama ilivyo sasa, mnajisifu na kujigamba. Kujisifu kwa namna hiyo ni uovu.

17 Basi mtu ye yote anayejua jema limpasalo kutenda, lakini asilitende, mtu huyo anatenda dhambi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JAS/4-57fa331fe2090682b85429b1bf547999.mp3?version_id=1627—

Yakobo 5

Onyo Kwa Matajiri

1 Basi sikilizeni, ninyi matajiri, lieni na kuomboleza kwa ajili ya hali mbaya sana inayowajia.

2 Utajiri wenu umeoza na mavazi yenu yameliwa na nondo.

3 Dhahabu yenu na fedha yenu vimeliwa na kutu. Kutu yake itashuhudia dhidi yenu nayo itaila miili yenu kama vile moto. Mmejiwekea hazina kwa ajili ya siku za mwisho.

4 Angalieni! Ule ujira wa vibarua waliolima mashamba yenu mliouzuia kwa hila unapiga kelele dhidi yenu na vilio vya wavunaji vimefika masikioni mwa Bwana Mwenye Nguvu Zote.

5 Mmeishi duniani kwa anasa na kwa starehe, mmejinenepesha tayari kwa siku ya kuchinjwa.

6 Mmewahukumu na kuwaua watu wenye haki, ambao walikuwa hawapingani nanyi.

Uvumilivu Katika Mateso

7 Kwa hiyo, ndugu zangu, vumilieni hadi kuja kwake Bwana. Angalieni jinsi mkulima angojavyo ardhi itoe mavuno yake yaliyo ya thamani na jinsi anavyovumilia kwa ajili ya kupata mvua za kwanza na za mwisho.

8 Ninyi nanyi vumilieni tena simameni imara, kwa sababu kuja kwa Bwana kumekaribia.

9 Ndugu zangu, msinung’unikiane msije mkahukumiwa. Hakimu amesimama mlangoni!

10 Ndugu zangu, waangalieni manabii walionena kwa Jina la Bwana, ili kuwa mfano wa uvumilivu katika kukabiliana na mateso.

11 Kama mnavyojua, tunawahesabu kuwa wamebarikiwa wale waliovumilia. Mmesikia habari za uvumilivu wake Ayubu na mmeona kile ambacho hatimaye Bwana alimtendea. Bwana ni mwingi wa huruma naye amejaa rehema.

12 Zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, ama kwa mbingu, au kwa dunia au kwa kitu kingine cho chote. “Ndiyo” yenu na iwe ndiyo, na “Hapana” yenu iwe hapana, la sivyo mtahukumiwa.

Maombi Ya Imani

13 Je, mtu ye yote miongoni mwenu amepatwa na taabu? Basi inampasa aombe. Je, kuna ye yote mwenye furaha? Basi na aimbe nyimbo za kusifu.

14 Je, kuna ye yote miongoni mwenu aliye mgonjwa? Basi inampasa awaite wazee wa kanisa wamwombee na kumpaka mafuta kwa Jina la Bwana.

15 Kule kuomba kwa imani kutamwokoa huyo mgonjwa, naye Bwana atamwinua na kama ametenda dhambi, atasamehewa.

16 Kwa hiyo ungamianeni makosa yenu ninyi kwa ninyi na kuombeana ili mpate kuponywa. Maombi ya mwenye haki yana nguvu tena yanafaa sana.

17 Eliya alikuwa mwanadamu kama sisi. Akaomba kwa bidii kwamba mvua isinyeshe nayo haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi sita.

18 Kisha akaomba tena, mbingu zikatoa mvua nayo ardhi ikatoa mazao yake.

19 Ndugu zangu, ye yote miongoni mwenu akipotoka na kuicha kweli, naye akarejezwa na mtu mwingine,

20 hamna budi kujua kwamba ye yote amrejezaye mwenye dhambi kutoka katika upotovu wake, ataiokoa roho ya huyo mwenye dhambi kutoka katika mauti na kusitiri wingi wa dhambi.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/JAS/5-7b59a2129497051ac52f034f89beaa71.mp3?version_id=1627—

Waebrania 1

Mwana Ni Mkuu Kuliko Malaika

1 Zamani Mungu alisema na baba zetu kwa njia ya manabii mara nyingi na kwa njia mbalimbali,

2 lakini katika siku hizi za mwisho anasema nasi kwa njia ya Mwanawe, ambaye amemweka kuwa mrithi wa vitu vyote, na ambaye kwa yeye aliuumba ulimwengu.

3 Mwana ni mng’ao wa utukufu wa Mungu na mfano halisi wa nafsi yake, akivihifadhi vitu vyote kwa neno lake lenye uweza. Akiisha kufanya utakaso kwa ajili ya dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Ukuu huko mbinguni.

4 Kwa hiyo alifanyika bora kuliko malaika, kama jina alilorithi lilivyo bora kuliko lao.

5 Kwa maana ni malaika yupi ambaye wakati wo wote Mungu alipata kumwambia,

“Wewe ni Mwanangu;

leo mimi nimekuzaa?”

Au tena,

“Mimi nitakuwa Baba yake,

naye atakuwa Mwanangu?”

6 Tena, Mungu amletapo mzaliwa wake wa kwanza ulimwenguni, husema,

“Malaika wote wa Mungu na wamsujudu.”

7 Anenapo kuhusu malaika husema,

“Huwafanya malaika zake kuwa upepo,

watumishi wake kuwa miali ya moto.”

8 Lakini kwa habari za Mwana asema,

“Kiti chako cha enzi, Ee Mungu,

kitadumu milele na milele,

nayo haki itakuwa fimbo ya utawala

ya ufalme wako.

9 Umependa haki na kuchukia uovu;

kwa hiyo Mungu, Mungu wako,

amekuweka juu ya wenzako

kwa kukupaka mafuta ya furaha.”

10 Pia asema,

“Hapo mwanzo, Ee Bwana, uliweka misingi ya dunia,

nazo mbingu ni kazi ya mikono yako.

11 Hizo zitaangamia, lakini wewe utadumu;

zote zitachakaa kama vazi.

12 Utazikung’utakung’uta kama joho,

kama vazi zitachakaa.

Bali wewe hubadiliki,

wala miaka yako kamwe haitakoma.”

13 Je, ni kwa malaika yupi ambaye Mungu amepata kumwambia wakati wo wote,

“Wewe keti mkono wangu wa kuume

mpaka nitakapowaweka adui zako

chini ya nyayo zako”?

14 Je, malaika wote si roho watumikao waliotumwa kuwahudumia wale watakaorithi wokovu?

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/1-477941132c7f821e41229c8efd63f530.mp3?version_id=1627—

Waebrania 2

Wokovu Mkuu

1 Kwa hiyo, imetupasa kuwa waangalifu sana kuhusu kile tulichosikia, ili tusije tukakiacha.

2 Kwa kuwa ujumbe ulionenwa na malaika ulikuwa imara na kila uasi na kutokutii kulipata adhabu ya haki,

3 je, sisi tutapaje kupona kama tusipojali wokovu mkuu namna hii? Wokovu huu, ambao mwanzo ulitangazwa na Bwana, kisha ulithibitishwa kwetu na wale waliomsikia.

4 Pia Mungu aliushuhudia kwa ishara, maajabu na kwa miujiza mbalimbali, na karama za Roho Mtakatifu alizozigawa kulingana na mapenzi yake.

Yesu Alifananishwa Na Ndugu Zake

5 Mungu hakuuweka ulimwengu ujao ambao tunanena habari zake chini ya malaika.

6 Lakini kuna mahali mtu fulani ameshuhudia akisema:

“Mwanadamu ni kitu gani hata umfikirie,

mwana wa mwanadamu ni nani hata umjali?

7 Umemfanya kuwa chini kidogo kuliko malaika;

umemvika taji ya utukufu na heshima,

8 nawe umeweka vitu vyote chini ya miguu yake.”

Kwa kuweka vitu vyote chini yake, Mungu hakuacha kitu cho chote ambacho hakukiweka chini ya mwanadamu. Lakini kwa sasa, hatuoni kwamba kila kitu kiko chini yake.

9 Lakini twamwona Yesu, aliyefanywa chini kidogo kuliko malaika, sasa akiwa amevikwa taji ya utukufu na heshima kwa sababu alistahimili mauti, ili kwamba kwa neema ya Mungu apate kuonja mauti kwa ajili ya kila mtu.

10 Ili kuwaleta wana wengi katika utukufu, ilimpendeza Mungu, kwa ajili yake na kwa kupitia yeye kila kitu kilichopo, kumkamilisha mwanzilishi wa wokovu wao kwa njia ya mateso.

11 Yeye awafanyaye watu kuwa watakatifu na wale ambao hufanywa watakatifu, wote hutoka katika jamaa moja. Hivyo Yesu haoni aibu kuwaita ndugu zake.

12 Yeye husema,

“Nitalitangaza jina lako kwa ndugu zangu;

mbele ya kusanyiko nitaimba sifa zako.”

13 Tena,

“Nitaweka tumaini langu kwake.”

Tena anasema,

“Niko hapa, mimi pamoja na watoto Mungu alionipa.”

14 Basi kwa kuwa watoto wana nyama na damu, yeye pia alishiriki katika ubinadamu wao, ili kwa kifo chake, apate kumwangamiza huyo mwenye nguvu za mauti, yaani, Shetani,

15 na kuwaweka huru wale waliokuwa utumwani maisha yao yote kwa sababu ya kuogopa mauti.

16 Kwa kuwa ni dhahiri kwamba hakuja kusaidia malaika, bali uzao wa Abrahamu.

17 Kwa sababu hii ilibidi afanane na ndugu zake kwa kila hali, ili apate kuwa Kuhani Mkuu mwenye huruma na mwaminifu katika kumtumikia Mungu, ili pia apate kufanya upatanisho kwa ajili ya dhambi za watu.

18 Kwa kuwa yeye mwenyewe aliteswa alipojaribiwa, aweza kuwasaidia wale wanaojaribiwa.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/2-78e98b66fd5465ac246ee7a9922b7933.mp3?version_id=1627—

Waebrania 3

Yesu Ni Mkuu Kuliko Mose

1 Kwa hiyo ndugu watakatifu, mnaoshiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini Yesu, mtume na Kuhani Mkuu wa ukiri wetu.

2 Alikuwa mwaminifu kwa yeye aliyemweka, kama vile Mose alivyokuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu.

3 Yesu ameonekana anastahili heshima kubwa kuliko Mose, kama vile mjenzi wa nyumba alivyo wa heshima kubwa kuliko nyumba yenyewe.

4 Kwa kuwa kila nyumba hujengwa na mtu fulani, lakini Mungu ni mjenzi wa kila kitu.

5 Basi Mose kama mtumishi alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu, akishuhudia kwa yale ambayo yangetamkwa baadaye.

6 Lakini Kristo yeye ni mwaminifu kama Mwana katika nyumba ya Mungu, sisi ndio nyumba yake, kama tutashikamana sana na ujasiri wetu na katika tumaini tunalojivunia.

Onyo Dhidi Ya Kutokuamini

7 Kwa hiyo, kama Roho Mtakatifu asemavyo:

“Leo, kama mkiisikia sauti yake,

8 msifanye mioyo yenu migumu,

kama mlivyofanya katika uasi,

wakati ule wa kujaribiwa jangwani,

9 pale baba zenu waliponijaribu na kunipima

ingawa kwa miaka arobaini

walikuwa wameona matendo yangu.

10 Hiyo ndiyo sababu nilikikasirikia kizazi kile,

nami nikasema, ‘Siku zote mioyo yao hupotoka,

nao hawajazijua njia zangu.’

11 Hivyo nikaapa kwa hasira yangu,

‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ”

12 Ndugu zangu, angalieni, asiwepo miongoni mwenu mtu mwenye moyo mwovu usioamini, unaojitenga na Mungu aliye hai.

13 Lakini mtiane moyo mtu na mwenzake kila siku, maadamu iitwapo Leo, ili asiwepo hata mmoja wenu mwenye kufanywa mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.

14 Kwa kuwa tumekuwa washiriki wa Kristo, kama tukishikamana tu kwa uthabiti na tumaini letu la kwanza hadi mwisho.

15 Kama ilivyonenwa:

“Leo, kama mtaisikia sauti yake,

msifanye mioyo yenu migumu

kama mlivyofanya wakati wa kuasi.”

16 Basi ni nani wale waliosikia lakini bado wakaasi? Je, si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Mose?

17 Lakini ni nani aliowakasirikia miaka arobaini? Je, si wale waliofanya dhambi ambao miili yao ilianguka jangwani?

18 Ni nani hao ambao Mungu aliapa kuwa kamwe hawataingia rahani mwake isipokuwa ni wale waliokataa kutii?

19 Hivyo tunaona kwamba hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/3-3c941f65ae9207abfe401f52a09facf3.mp3?version_id=1627—

Waebrania 4

Pumziko Lile Mungu Aliloahidi

1 Kwa hiyo, kwa kuwa bado ahadi ya kuingia rahani iko wazi, tujihadhari ili hata mmoja wenu asije akaikosa.

2 Kwa maana sisi pia tumesikia Injili iliyohubiriwa kwetu, kama nao walivyosikia, lakini ujumbe ule waliousikia haukuwa na maana kwao, kwa sababu wale waliousikia hawakuuchanganya na imani.

3 Sasa sisi ambao tumeamini tunaingia katika ile raha, kama vile Mungu alivyosema,

“Hivyo natangaza kwa kiapo katika hasira yangu,

‘Kamwe hawataingia rahani mwangu.’ ”

Lakini kazi yake ilikamilika tangu kuumbwa kwa ulimwengu.

4 Kwa maana mahali fulani amezungumza kuhusu siku ya saba, akisema: “Katika siku ya saba Mungu alipumzika katika kazi zake zote.”

5 Tena hapo juu asema, “Kamwe hawataingia rahani mwangu.”

6 Kwa hiyo kwa kuwa inabaki kuwa wazi kwa ajili ya wengine kuingia, nao wale wa kwanza waliopokea Injili walishindwa kuingia kwa sababu ya kutokutii,

7 kwa hiyo Mungu ameweka siku nyingine, akaiita Leo, akisema kwa kinywa cha Daudi baadaye sana, kwa maneno yaliyotangulia kunenwa:

“Leo, kama mkiisikia sauti yake,

msifanye migumu mioyo yenu.”

8 Kwa maana kama Yoshua alikuwa amewapa raha, Mungu hangelisema tena baadaye kuhusu siku nyingine.

9 Kwa hiyo basi, imebaki raha ya Sabato kwa ajili ya watu wa Mungu,

10 kwa kuwa kila mmoja aingiaye katika raha ya Mungu pia hupumzika kutoka kazi zake mwenyewe, kama vile naye Mungu alivyopumzika kutoka katika kazi zake.

11 Basi, na tufanye bidii kuingia katika raha hiyo, ili kwamba asiwepo ye yote atakayeanguka kwa kufuata mfano wao wa kutokutii.

12 Kwa maana Neno la Mungu li hai tena lina nguvu tena lina makali kuliko upanga uwao wote wenye makali kuwili, tena linachoma hata kuzigawanya nafsi na roho, viungo na mafuta yaliyo ndani yake, tena li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.

13 Wala hakuna kiumbe cho chote kilichofichika machoni pa Mungu. Kila kitu kimefunuliwa na kiko wazi machoni pake yeye ambaye kwake ni lazima tutatoa hesabu.

Yesu Kristo Kuhani Mkuu Kuliko Wote

14 Kwa kuwa tunaye Kuhani Mkuu kuliko wote ambaye ameingia mbinguni, Yesu Mwana wa Mungu, basi na tushikamane sana kwa uthabiti na ule ukiri wa imani yetu.

15 Kwa kuwa hatuna Kuhani Mkuu asiyeweza kuchukuliana na sisi katika udhaifu wetu, lakini tunaye mmoja ambaye alijaribiwa kwa kila namna, kama vile sisi tujaribiwavyo, lakini yeye hakutenda dhambi.

16 Basi na tukikaribie kiti cha rehema kwa ujasiri, ili tupewe rehema na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/4-bea9946e8920fbc208b7fa3ba515811a.mp3?version_id=1627—

Waebrania 5

1 Kwa maana kila Kuhani Mkuu anayechaguliwa miongoni mwa wanadamu anawekwa kuwawakilisha kwa mambo yanayomhusu Mungu, ili apate kutoa matoleo na dhabihu kwa ajili ya dhambi.

2 Kwa kuwa yeye mwenyewe ni dhaifu, aweza kuwachukulia kwa upole wale wasiojua na kupotoka.

3 Hii ndiyo sababu inampasa kutoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe na vivyo hivyo kwa ajili ya dhambi za watu.

4 Hakuna anayejitwalia heshima hii mwenyewe, ni lazima aitwe na Mungu, kama vile Aroni alivyoitwa.

5 Pia Kristo hakujitwalia utukufu yeye mwenyewe wa kuwa Kuhani Mkuu, bali Mungu alimwambia,

“Wewe ni Mwanangu,

mimi leo nimekuzaa.”

6 Pia mahali pengine asema,

“Wewe ndiwe kuhani milele,

kwa mfano wa Melkizedeki.”

7 Katika siku za maisha ya Yesu hapa duniani, alimtolea maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, yeye awezaye kumwokoa na mauti, naye Mungu akamsikia kwa sababu ya kutii kwake kwa unyenyekevu.

8 Ingawa alikuwa Mwana, alijifunza utii kutokana na mateso aliyoyapata,

9 akiisha kukamilishwa, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wote wanaomtii,

10 naye amewekwa na Mungu kuwa Kuhani Mkuu kwa mfano wa Melkizedeki.

Wito Wa Kukua Kiroho

11 Tunayo mengi ya kusema kuhusu habari ya ukuhani huu, lakini ni vigumu kuyaeleza, kwa sababu ninyi ni wazito wa kuelewa.

12 Kwa hakika, ingawa mpaka wakati huu ingewapasa kuwa walimu, lakini bado mnahitaji mtu wa kuwafundisha tena hatua za awali za kweli ya Neno la Mungu. Mnahitaji maziwa, wala si chakula kigumu!

13 Kwa maana ye yote aishiye kwa kunywa maziwa bado yeye ni mtoto mchanga, hana ujuzi katika mafundisho kuhusu neno la haki.

14 Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu wazima, ambao kwa kujizoeza wamejifunza kupambanua kati ya mema na mabaya.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/5-889f21e3462b55b0e6311925acdd954c.mp3?version_id=1627—

Waebrania 6

Hatari Ya Kuanguka

1 Kwa hiyo, tukiachana na mafundisho yale ya awali kuhusu Kristo na tusonge mbele ili tufikie utimilifu, si kuweka tena msingi wa mafundisho ya kuzitubia kazi zisizo na uhai na imani katika Mungu, yaani,

2 mafundisho kuhusu aina za ubatizo, kuwekea watu mikono, ufufuo wa wafu na hukumu ya milele.

3 Mungu akitujalia tutafanya hivyo.

4 Kwa kuwa ni vigumu kuwarejeza tena katika toba wale ambao wakati fulani walishapata nuru, ambao walishaonja kipawa cha mbinguni, ambao wamekwisha kushiriki katika Roho Mtakatifu,

5 wale ambao wameonja uzuri wa Neno la Mungu na nguvu za wakati ujao,

6 kisha wakaanguka, kwa kuwa kwa nafsi zao wanamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili na kumdhalilisha hadharani.

7 Ardhi ile ipokeayo mvua inyeshayo juu yake mara kwa mara hutoa mazao yanayowanufaisha wale ambao kwa ajili yao yalimwa, nayo nchi hiyo hupokea baraka kutoka kwa Mungu.

8 Lakini ardhi ile ikizaa miiba na mibaruti haina thamani na iko hatarini kulaaniwa. Mwisho wake ni kuchomwa moto.

9 Ingawa tunasema hivi, ndugu zangu wapendwa, kwa upande wenu tuna hakika ya mambo mema zaidi, mambo yale yahusuyo wokovu.

10 Mungu si dhalimu, hataisahau kazi yenu na upendo ule mlioonyesha kwa ajili yake katika kuwahudumia watakatifu na kama vile mnavyoendelea kuwahudumia.

11 Nasi twataka kila mmoja wenu aonyeshe bidii iyo hiyo ili mpate kujua uhakika kamili wa lile tumaini mpaka mwisho,

12 ili msije mkawa wavivu, bali mpate kuwaiga wale ambao kwa imani na saburi hurithi zile ahadi.

Uhakika Wa Ahadi Ya Mungu

13 Mungu alipompa Abrahamu ahadi yake, kwa kuwa hakuwepo mwingine aliyekuwa mkuu kuliko yeye ambaye angeweza kuapa kwa jina lake, aliapa kwa nafsi yake,

14 akisema, “Hakika nitakubariki na kukupa wazao wengi.”

15 Naye baada ya kungoja kwa saburi, Abrahamu alipokea kile kilichoahidiwa.

16 Wanadamu huapa kwa yeye aliye mkuu kuliko wao, nacho kiapo hicho huthibitisha kile kilichosemwa na kumaliza mabishano yote.

17 Kwa njia hii, Mungu alipotaka kuonyesha kwa udhahiri zaidi kwa warithi wa ile ahadi ile asili ya kutokubadilika kwa ahadi yake, aliithitibisha kwa kiapo.

18 Mungu alifanya hivyo, ili kwa vitu viwili visivyobadilika, yaani ahadi yake na kiapo chake, ambavyo kwa hivyo Mungu hawezi kusema uongo, sisi ambao tumemkimbilia, tuwe na moyo mkuu kulishika lile tumaini lililowekwa mbele yetu.

19 Tunalo tumaini hili lililo kama nanga ya roho, lililo imara na thabiti. Tumaini hili huingia katika patakatifu palipo nyuma ya pazia,

20 mahali ambapo Yesu mtangulizi wetu aliingia kwa niaba yetu. Yeye amekuwa Kuhani Mkuu milele, kwa mfano wa Melkizedeki.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/6-9c32152f6ae0491e330bc3ac47a5d53b.mp3?version_id=1627—

Waebrania 7

Kuhani Melkizedeki

1 Kwa kuwa huyu Melkizedeki alikuwa mfalme wa Salemu na Kuhani wa Mungu Aliye Juu Sana, aliyekutana na Abrahamu akirudi katika kuwashinda hao wafalme, naye Melkizedeki akambariki,

2 ambaye Abrahamu alimpa sehemu ya kumiya kila kitu. Kwanza, jina hilo Melkizedeki maana yake “mfalme wa haki”; pia “mfalme wa Salemu,” maana yake “mfalme wa amani.”

3 Hana Baba wala mama, hana ukoo, hana mwanzo wala mwisho wa siku zake, kama Mwana wa Mungu, yeye adumu kuhani milele.

4 Tazama jinsi alivyokuwa mkuu: Hata Abrahamu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara zake.

5 Basi sheria inawaagiza wana wa Lawi wale ambao hufanyika makuhani hupokea sehemu ya kumi kutoka watu, ambao ni ndugu zao, ingawa wao ni wazao wa Abrahamu.

6 Huyu Melkizedeki, ingawa hakufuatia ukoo wake kutoka kwa Lawi, lakini alipokea sehemu ya kumi kutoka kwa Abrahamu na kumbariki yeye aliyekuwa na zile ahadi.

7 Wala hakuna shaka kwamba mdogo hubarikiwa na aliye mkuu kuliko yeye.

8 Kwa upande mmoja, sehemu ya kumi hupokelewa na wale ambao hupatikana na kufa; lakini kwa upande mwingine hupokelewa na yeye ambaye hushuhudiwa kuwa yu hai.

9 Mtu anaweza hata kusema kwamba Lawi, ambaye hupokea sehemu ya kumi, alitoa hiyo sehemu ya kumi kupitia kwa Abrahamu,

10 kwa sababu Melkizedeki alipokutana na Abrahamu, Lawi alikuwa bado katika viuno vya baba yake wa zamani.

Yesu Mfano Wa Melkizedeki

11 Kama ukamilifu ungeweza kupatikana kwa njia ya ukuhani wa Walawi (kwa kuwa katika msingi huo sheria ilitolewa kwa watu) kwa nini basi imekuwapo haja ya kuja kuhani mwingine: kwa mfano wa Melkizedeki, wala si kwa mfano wa Aroni?

12 Kwa kuwa yanapotokea mabadiliko ya ukuhani, pia lazima yawepo mabadiliko ya sheria.

13 Yeye ambaye ndiye anayesemwa katika mambo haya, alikuwa wa kabila jingine na hakuna mtu wa kabila hilo aliyekuwa amehudumu katika madhabahu.

14 Kwa maana ni dhahiri kwamba Bwana wetu alitoka katika uzao wa Yuda, tena kuhusu kabila hilo Mose hakusema lo lote kwa habari za ukuhani.

15 Tena hayo tuliyosema yako wazi zaidi kama akitokea kuhani mwingine kama Melkizedeki,

16 yeye ambaye amefanyika kuhani si kwa misingi ya sheria kama ilivyokuwa kwa baba zake, bali kwa misingi ya uwezo wa uzima usioharibika.

17 Kwa maana imeshuhudiwa kwamba:

“Wewe ndiye kuhani milele,

kwa mfano wa Melkizedeki.”

18 Kwa upande mmoja, kubatilishwa kwa ile amri ya mwanzo isiyofaa

19 (kwa maana sheria haikufanya kitu cho chote kuwa kikamilifu), kwa upande mwingine, tumeletewa tumaini lililo bora zaidi ambalo kwalo linatuleta karibu na Mungu.

20 Nalo tumaini hilo halikutolewa pasipo kiapo! Wengine walikuwa makuhani pasipo kiapo cho chote,

21 lakini Yesu alikuwa Kuhani kwa kiapo wakati Mungu alipomwambia:

“BWANA ameapa

naye hatabadili nia yake:

‘Wewe ndiwe Kuhani milele.’ ”

22 Kwa ajili ya kiapo hiki, Yesu amekuwa mdhamini wa Agano lililo bora zaidi.

23 Basi pamekuwepo na makuhani wengi wa aina hiyo, kwa kuwa kifo kiliwazuia kuendelea na huduma yao ya ukuhani,

24 lakini kwa sababu Yesu anaishi milele, anao ukuhani wa kudumu.

25 Kwa hiyo anaweza kuwaokoa kabisa wale wanaomjia Mungu kupitia kwake, kwa sababu yeye adumu daima kuomba kwa ajili yao.

26 Kwa kuwa ilitupasa tuwe na Kuhani Mkuu wa namna hii, yaani, aliye mtakatifu, asiye na lawama, asiye na dosari, aliyetengwa na wenye dhambi na kuinuliwa juu ya mbingu.

27 Yeye hahitaji kutoa dhabihu siku kwa siku kwa ajili ya dhambi, kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, kisha kwa ajili ya dhambi za watu kama wale makuhani wakuu wengine. Yeye alitoa dhabihu kwa ajili ya dhambi zao mara moja tu, alipojitoa mwenyewe.

28 Kwa kuwa sheria huwaweka makuhani wakuu watu ambao ni dhaifu, lakini lile neno la kiapo, lililokuja baada ya sheria, lilimweka Mwana, ambaye amefanywa kuwa mkamilifu milele.

—https://d1b84921e69nmq.cloudfront.net/337/32k/HEB/7-f144e85acd4bddbb9e7842805e3327e0.mp3?version_id=1627—